Kwanini Trump anaitaka Greenland, inamaanisha nini kwa wanachama wa Nato?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, James FitzGerald
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ikulu ya Marekani imedokeza kuwa Donald Trump na washauri wake wa karibu wanajadili uwezekano wa Marekani kuchukua udhibiti wa Greenland, huku rais huyo akiendelea kusisitiza kuwa hatua hiyo ingekuwa na manufaa makubwa kwa usalama wa taifa lake.
Madai hayo yamekataliwa vikali na viongozi wa Greenland pamoja na Denmark, mwanachama wa Nato, ambayo Greenland ni eneo lake lenye mamlaka ya kujitawala kwa kiasi.
Greenland iko wapi, na kwa nini ni muhimu kwa Trump?
Greenland ni kisiwa kikubwa zaidi duniani ambacho si bara, na kinapatikana katika eneo la Aktiki.
Ni miongoni mwa maeneo yenye watu wachache zaidi kwa ukubwa wake, ikiwa na takribani wakazi 56,000, wengi wao wakiwa ni wenyeji wa asili wa jamii ya Inuit.
Takribani asilimia 80 ya eneo la Greenland limefunikwa na barafu, hali inayosababisha idadi kubwa ya watu kuishi katika ukanda wa kusini-magharibi, hususan karibu na mji mkuu, Nuuk.
Uchumi wa Greenland unategemea zaidi uvuvi, huku ukipokea ruzuku kubwa kutoka serikali ya Denmark.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, kumekuwepo na ongezeko la mvuto kuhusu rasilimali zake za asili, ikiwemo madini adimu ya ardhini, urani na chuma.
Rasilimali hizi zinaweza kupatikana kwa urahisi zaidi kadri mabadiliko ya tabianchi yanavyoendelea kuyeyusha barafu kubwa linalofunika kisiwa hicho.
Rasilimali za madini zimekuwa sehemu ya mkazo wa sera za Trump katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo katika mahusiano yake na Ukraine. Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa lengo lake si madini bali usalama wa Marekani, akisema:
"Tunahitaji Greenland kwa ajili ya usalama wa Marekani, si kwa ajili ya madini."
Aidha, amedai kuwa ''Greenland imezungukwa na shughuli za kijeshi za Urusi na China'', kauli ambayo imeungwa mkono na wabunge wengi wa Republican wanaoona mataifa hayo mawili kama tishio kwa usalama wa Marekani.
Trump amesema nini kuhusu udhibiti wa Marekani juu ya Greenland?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump alihuisha tena wito wake wa Marekani kuchukua Greenland kufuatia operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela, ambapo rais Nicolás Maduro na mkewe walikamatwa na kupelekwa New York.
Waziri Mkuu wa Greenland, Jens Frederik Nielsen, alijibu kwa kusema kuwa "imetosha," akielezea wazo la Marekani kuichukua Greenland kuwa ni ndoto isiyo na uhalisia.
Hata hivyo, Trump na washirika wake waliendelea kusisitiza msimamo wao. Rais Trump alisema kuwa alikuwa ''makini sana'' kuhusu mpango huo, akiongeza kuwa Greenland ni muhimu si tu kwa usalama wa Marekani bali pia wa Ulaya.
Mshauri wake waandamizi, Stephen Miller, alidai kuwa ''hakuna taifa litakalopambana na Marekani kuhusu mustakabali wa Greenland''.
Serikali ya Marekani haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi. Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, alieleza mbele ya bunge kuwa Pentagon ina ''mipango ya dharura kwa hali kama hiyo''.
Baada ya operesheni ya Venezuela, Ikulu ilithibitisha kuwa Trump na timu yake walikuwa wakichunguza njia mbalimbali za kuipata Greenland, ikiwemo ''matumizi ya jeshi la Marekani''.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2019, Trump aliwahi kutoa pendekezo la kununua Greenland, lakini alikataliwa kwa sababu kisiwa hicho hakikuwa kinauzwa.
Baada ya kurejea Ikulu mwezi Januari 2025, Trump alihuisha tena nia yake, bila kuondoa kabisa uwezekano wa kutumia nguvu.
Ziara za ngazi ya juu pia zimezua utata.
Makamu wa Rais JD Vance alitembelea Greenland mwezi Machi na kuikosoa Denmark kwa kile alichodai kuwa ni kushindwa kuwekeza vya kutosha katika ulinzi wa eneo hilo.
Mvutano uliongezeka zaidi mwishoni mwa mwaka 2025 baada ya Trump kumteua Jeff Landry kuwa mjumbe maalum wa Greenland, ambaye amezungumza waziwazi kuhusu kuifanya Greenland kuwa sehemu ya Marekani.
Denmark na washirika wengine wa Nato wamesemaje?
Msimamo wa Trump umeishtua Denmark, ambayo kwa muda mrefu imekuwa na uhusiano wa karibu na Washington, kwa mujibu wa mwanadiplomasia wa BBC James Landale.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alionya kuwa jaribio lolote la kuichukua Greenland lingeweza kusababisha kuvunjika kwa muungano wa Nato.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, alipohojiwa iwapo angemwambia Trump aachane na Greenland, alijibu moja kwa moja: "Ndiyo."
Starmer alisaini tamko la pamoja na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Hispania na Denmark, likisisitiza kuwa:
"Greenland ni ya watu wake, na ni Denmark na Greenland pekee wana mamlaka ya kuamua masuala yanayohusu uhusiano wao."
Kwa nini Denmark inadhibiti Greenland?
Ingawa ni sehemu ya bara la Amerika Kaskazini, Greenland imekuwa ikidhibitiwa na Denmark - karibu kilomita 3,000 (maili 1,860) - kwa takriban miaka 300.
Lakini maslahi ya usalama ya Marekani kwa Greenland pia yalianza muda mrefu, na tawala mbili za Marekani kabla ya Trump kufanya jitihada zisizofanikiwa za kuipata.
Kisiwa hicho kilitawaliwa kama koloni hadi katikati ya Karne ya 20. Kwa muda mwingi wa wakati huu, ilibaki kutengwa na maskini.
Baada ya Ujerumani ya Nazi kuiteka Denmark bara wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Marekani ilivamia kisiwa hicho, na kuanzisha vituo vya kijeshi na stesheni za redio.
Baada ya vita, vikosi vya Marekani vilibaki Greenland.
Kambi ya Pituffik Space, ambayo zamani ilijulikana kama kambi ya Thule Air, imekuwa ikiendeshwa na Marekani tangu wakati huo.
Mnamo 1951, makubaliano ya ulinzi na Denmark yaliipatia Marekani jukumu kubwa katika ulinzi wa eneo hilo, pamoja na haki ya kujenga na kudumisha kambi za kijeshi.
Mnamo 1953, kisiwa hicho kilifanywa kuwa sehemu ya Ufalme wa Denmark na Greenlanders wakawa raia wa Denmark.
Mnamo 1979, kura ya maoni juu ya sheria ya nyumbani iliipa Greenland udhibiti wa sera nyingi ndani ya eneo hilo, huku Denmark ikishikilia udhibiti wa mambo ya nje na ulinzi.
Greenland ni makazi ya vituo vya kijeshi vya Denmark na vile vile vya Marekani.

Chanzo cha picha, Reuters
Watu wa Greenland wana maoni gani?
Akijibu vitisho vya Trump mapema mwaka wa 2026, Waziri Mkuu wa Greenland Nielsen alisema: "Hakuna shinikizo tena. Hakuna kisingizio zaidi. Hakuna mawazo zaidi ya kunyakua.
"Tuko wazi kwa mazungumzo. Tuko wazi kwa majadiliano. Lakini hili lazima lifanyike kupitia njia zinazofaa na kwa kuheshimu sheria za kimataifa."
Mwandishi wa BBC Fergal Keane alipotembelea kisiwa hicho mwaka wa 2025, alisikia msemo mmoja tena na tena: "Greenland ni mali ya Greenland. Kwa hivyo, Trump anaweza kutembelea lakini ndivyo hivyo."
Suala hilo lilichukua nafasi kubwa wakati wa uchaguzi mkuu wa eneo hilo mwaka huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kura ya maoni inapendekeza kwamba watu wengi wa Greenland wanaunga mkono kusimamiwa na Denmark, lakini kwamba wengi wao pia wanakataa wazo la kuwa sehemu ya Marekani.
Wakati Trump alitoa wazo la kununua Greenland kwa mara ya kwanza mnamo 2019, wenyeji wengi walisema walipinga pendekezo hilo.
"Hili ni wazo hatari sana," Dines Mikaelsen, mwelekezi wa watalii alisema.
"Anatuweka katika fungu la kama bidhaa nzuri anaweza kununua," alisema Aleqa Hammond, waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Greenland.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












