Jaribio la kumuua kiongozi wa Burkina Faso latibuliwa, yasema serikali ya kijeshi
Tangu alipochukua madaraka, Kapteni Traoré amekabiliwa na majaribio mawili ya mapinduzi na pia anakabiliwa na ongezeko la vurugu za wanajihadi.
Muhtasari
- Nchi za Ulaya zajiandaa ikiwa Marekani itaivamia Greenland
- Marekani yakamata meli mbili za mafuta zinazohusishwa na Venezuela
- Kiongozi wa upinzani Machado asema muungano wake ndio unapaswa kuiongoza Venezuela
- Jaribio la kumuua kiongozi wa Burkina Faso latibuliwa, yasema serikali ya kijeshi
- Watu sita wamefariki na mamia ya safari za ndege zafutwa kutokana na theluji Ulaya
- Mfanyakazi wa shirika la nyuklia la Japani apoteza simu yenye taarifa za siri China
- Watu 36 wameuawa katika maandamano Iran
- Wanajeshi wa Venezuela waripotiwa kupekua simu za raia na waandishi wa habari
- Urusi yatoa ulinzi kwa meli ya mafuta inayofuatiliwa na vikosi Marekani
- AFCON 2025: Amad aipeleka Ivory Coast robo fainali, sasa macho kwa vigogo Misri
- Uingereza na Ufaransa kuwapeleka wanajeshi Ukraine mkataba wa amani ukifikiwa
- Venezuela 'itaikabidhi' Marekani hadi mapipa 50m ya mafuta
- Marekani inajadili mbinu ya kuinyakua Greenland
Moja kwa moja
Ambia Hirsi & Rashid Abdallah
Nchi za Ulaya zajiandaa ikiwa Marekani itaivamia Greenland

Washirika wa Ulaya wakiwemo Ufaransa na Ujerumani wanafanyia kazi mpango jinsi ya kujibu iwapo Marekani itachukulia hatua ya kuichukua Greenland.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema mada hiyo itazungumziwa katika mkutano na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Poland.
"Tunataka kuchukua hatua, lakini tunataka kufanya hivyo pamoja na washirika wetu wa Ulaya," amesema kwenye redio ya France Inter.
Viongozi kutoka mataifa makubwa ya Ulaya na Canada wameiunga mkono Greenland wiki hii, wakisema kisiwa hicho cha Aktiki ni cha Denmark, kufuatia tishio jipya la Trump la kulichukua eneo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yakamata meli mbili za mafuta zinazohusishwa na Venezuela

Chanzo cha picha, Reuters
Marekani inasema imezikamata meli za mafuta baada ya kuikamata meli ya kwanza yenye bendera ya Urusi inayohusishwa na mafuta ya Venezuela huko Atlantiki Kaskazini na meli ya pili imekamatwa karibu an visiwa vya Caribbean.
Waziri wa usalama wa ndani wa Marekani anasema Walinzi wa Pwani wa Marekani wamezishikilia meli mbili.
Noem anasema meli moja ilikuwa katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini huku nyingine ikiwa katika maji ya kimataifa karibu na Caribea. Operesheni hizo zilifanyika ndani ya saa chache tu, amesema.
Meli za mafuta, Marinera na Sophia—“zilikuwa zilkitoka Venezuela au zikiwa njiani kuelekea huko,” Noem ameongeza.
Pia unaweza kusoma:
Kiongozi wa upinzani Machado asema muungano wake ndio unapaswa kuiongoza Venezuela

Chanzo cha picha, AFP
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela María Corina Machado amesema muungano wake wa upinzani unapaswa kuongoza nchi, kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Nicolás Maduro na Marekani wiki iliyopita.
"Tuko tayari na tuko tayari kuwahudumia watu wetu kama tunavyotakikana," Machado alisema katika mahojiano na CBS ya Marekani.
Amemshukuru Rais wa Marekani Donald Trump kwa "uongozi na ujasiri" wake baada ya vikosi vya Marekani kuvamia Caracas na kumkamata Maduro, lakini akasema hakuna mtu anayemwamini mshirika wa rais aliyeondolewa madarakani, ambaye ameteuliwa kuwa rais wa mpito.
Machado na harakati zake za upinzani walidai ushindi katika uchaguzi wa 2024 uliopingwa vikali, lakini Trump amekataa kumuunga mkono, akisema hana uungwaji mkono na watu wengi.
Mbunge huyo wa zamani, ambaye alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka jana, alielezea hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela mwishoni mwa wiki kama "hatua kubwa kuelekea kurejesha ustawi na utawala wa sheria na demokrasia nchini Venezuela".
Amesema hajazungumza na Trump mwaka huu, lakini amemshukuru kwa kumng'oa madarakani Maduro.
Rais wa Marekani amekataa hadharani Machado kuwa mrithi wa Maduro.
"Nadhani itakuwa vigumu sana kwake kuwa kiongozi," Trump aliuambia mkutano na waandishi wa habari siku chache zilizopita, akimrejelea Machado.
"Hana usaidizi ndani au heshima ndani ya nchi. Ni mwanamke mzuri sana, lakini hana nguvu hiyo."
Machado, ambaye amekuwa mafichoni kwa miezi kadhaa baada ya kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa rais wa 2024 nchini Venezuela, hapo awali ametoa wito kwa Edmundo González kiongozi wa upinzani kuchukua madaraka baada ya kukamatwa kwa Maduro.
Machado alimuunga mkono González katika uchaguzi huo, na hesabu za kura zilizotolewa na chama chake zinaonyesha alishinda kwa kishindo.
Hata hivyo, Maduro alitangazwa kuwa rais na baraza la uchaguzi la Venezuela (CNE), chombo kinachotawaliwa na wafuasi wa serikali.
Licha ya haya, Marekani na nchi nyingine nyingi zilimtambua González kama rais mteule.
Pia unaweza kusoma:
Jaribio la kumuua kiongozi wa Burkina Faso latibuliwa, yasema serikali ya kijeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kapteni Traoré alichukua madaraka Septemba 2022 Njama ya kumuua kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, imezuiwa, limetangaza taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mpango huo ulikuwa umepangwa na Luteni Kanali Paul Henri Damiba, afisa wa kijeshi aliyeondolewa madarakani na Traoré Septemba 2022, amesema waziri wa usalama katika taarifa ya usiku wa manane.
"Shirika letu la kijasusi limezuia operesheni hii katika saa za mwisho. Walikuwa wamepanga kumuua mkuu wa nchi na kisha kushambulia taasisi zingine muhimu, wakiwemo watu mashuhuri," amesema Mahamadou Sana, akidai njama hiyo imeandaliwa nchi jirani ya Ivory Coast.
Hakuna taarifa yoyote kutoka kwa Kanali Damiba au Ivory Coast.
Tangu alipochukua madaraka, Kapteni Traoré amekabiliwa na majaribio mawili ya mapinduzi na pia anakabiliwa na ongezeko la vurugu za wanajihadi ambazo zimewalazimisha mamilioni ya watu kukimbia makwao.
Licha ya changamoto hizi, kiongozi huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 37 ana uungwaji mkono mkubwa na amepata wafuasi kote Afrika kwa maono yake ya umajumui wa Kiafrika na ukosoaji wake wa nchi za Magharibi.
Kulingana na waziri wa usalama, serikali iligundua video iliyovuja ikiwaonyesha wapangaji wakijadili mipango yao.
Katika picha hizo, inadaiwa walizungumzia jinsi walivyokusudia kumuua rais - iwe karibu au kwa kuweka vilipuzi nyumbani kwake – siku ya Jumamosi tarehe 3 Januari.
Baadaye inadaiwa walipanga kuwalenga maafisa wengine wakuu wa kijeshi na raia.
Sana amedai Damiba amekusanya wanajeshi na wafuasi wa kiraia, akapata ufadhili wa kigeni - zaidi ya faranga milioni 70 za CFA ($125,000; £92,000) zilizotolewa kutoka Ivory Coast - na alipanga kuangamiza kambi ya ndege zisizo na rubani nchini humo kabla ya vikosi vya kigeni kuingilia kati.
"Tunafanya uchunguzi na tumewakamata watu kadhaa. Watu hawa watafikishwa mahakamani hivi karibuni," waziri huyo amesema kwenye televisheni ya taifa.
Haijulikani ni watu wangapi wamekamatwa.
Kanali Damiba alihudumu kama kiongozi wa Burkina Faso kuanzia Januari-Septemba 2022 baada ya kunyakua madaraka kutoka kwa serikali iliyochaguliwa kiraia.
Baada ya kufukuzwa alikwenda uhamishoni katika nchi jirani ya Togo na akasema katika ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba anamtakia mrithi wake kila la heri.
Pia unaweza kusoma:
Watu sita wamefariki na mamia ya safari za ndege zafutwa kutokana na theluji Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images
Mvua kubwa ya theluji na hali ya hewa ya barafu imesababisha usumbufu mkubwa wa usafiri kote Ulaya, huku watu sita wakiripotiwa kufariki katika matukio yanayohusiana na hali ya hewa hiyo barani humo.
Watu watano walifariki katika maeneo mawili tofauti ya Ufaransa kutokana na hali mbaya ya hewa wakati wakiendesha gari, mamlaka zimesema, huku mwanamke mmoja pia akifariki katika mji mkuu wa Bosnia, Sarajevo, baada ya theluji ya inchi 16 (sentimita 40) kumuangukia.
Mamia ya safari za ndege zimefutwa kote Ulaya, huku maelfu wakiwa wamekwama katika viwanja vya ndege vya Paris na Amsterdam.
Usumbufu unatarajiwa kuendelea hadi Jumatano.
Nchini Ufaransa, watu wengine watatu walifariki katika matukio mawili tofauti huko Landes, kusini-magharibi, kutokana na barafu, mamlaka zinasema.
Pia unaweza kusoma:
Mfanyakazi wa shirika la nyuklia la Japani apoteza simu yenye taarifa za siri China

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mfanyakazi huyo alipoteza simu yake katika uwanja wa ndege jijini Shanghai alipokuwa kwenye safari binafsi. Mfanyakazi katika shirika la usalama wa nyuklia la Japani amepoteza simu yake ya kazini ambayo ina taarifa nyeti, wakati wa ziara binafsi nchini China, vimeripoti vyombo vya habari vya Japani.
Simu hiyo ina taarifa za siri juu ya mawasiliano ya wafanyakazi wanaohusika katika kazi za usalama wa nyuklia katika Mamlaka ya Kudhibiti Nyuklia (NRA). Shirika hilo halijasema kama kuna taarifa zilizovuja, ripoti zinasema.
Tukio hili linakuja huku Japani ikijaribu kufufua mpango wake wa nishati ya atomiki, ambao umesimama kwa zaidi ya muongo mmoja.
Japani iliamuru mitambo yake yote ya nyuklia kufungwa mwaka 2011 baada ya tetemeko la ardhi la ukubwa wa 9 na tsunami kubwa kusababisha uharibifu wa kiwanda cha nyuklia cha Fukushima.
NRA liliundwa baada ya janga la nyuklia la Fukushima ili kusimamia usalama wa nyuklia, ikiwa ni pamoja na kuanzisha upya vinu vya nyuklia vya nchi hiyo.
Inaaminika kwamba mfanyakazi huyo wa NRA alipoteza simu yake ya kazini Novemba 3 alipokuwa akifanyiwa ukaguzi wa usalama katika uwanja wa ndege wa Shanghai akiwa safarini.
Aligundua kuwa simu imepotea siku tatu baadaye, na licha ya kuwasiliana na uwanja wa ndege, hakuipata.
Gazeti la Asahi liliripoti kwamba NRA hutoa simu janja kwa wafanyakazi fulani ili waweze kukabiliana na dharura kwa haraka ikihitajika.
NRA iliripoti tukio hilo kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya nchi hiyo na imewaonya wafanyakazi dhidi ya kutembea na simu za kazini nje ya nchi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa nyuklia wa Japani kugonga vichwa vya habari kuhusu mambo ya usalama.
2023, mfanyakazi katika Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Kashiwazaki-Kariwa—kituo kikubwa zaidi cha nyuklia duniani—alipoteza rundo la hati baada ya kuziweka juu ya gari lake na kuliendesha.
Novemba iliyopita, mfanyakazi mwingine katika kiwanda cha Kashiwazaki-Kariwa alipatikana akifanya uzembe kwa kuchapishwa nakala za siri na kuzifungia kwenye dawati.
Pia unaweza kusoma:
Watu 36 wameuawa katika maandamano Iran

Maelezo ya picha, Video inaonyesha polisi wa kutuliza ghasia wakifyatua gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano huko Grand Bazaar, Tehran Takribani watu 36 wameuawa katika siku 10 zilizopita za maandamano nchini Iran, linasema kundi la haki za binadamu.
Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake makuu nje ya nchi limeripoti kwamba 34 kati ya wale waliothibitishwa kuuawa ni waandamanaji na wawili ni maafisa wa usalama.
Serikali ya Iran haijachapisha idadi rasmi ya vifo lakini imesema maafisa watatu wa usalama wameuawa. BBC Persian hadi sasa imethibitisha vifo na utambulisho wa watu 20.
HRANA pia imesema zaidi ya waandamanaji 60 wamejeruhiwa na 2,076 wamekamatwa wakati wa machafuko, ambayo yalisababishwa na mgogoro wa kiuchumi na yameenea katika majimbo 27 kati ya 31.
Maandamano haya yalianza tarehe 28 Desemba, wakati wafanyabiashara wa maduka walipoingia mitaani mwa mji mkuu kuelezea hasira zao kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Iran dhidi ya dola ya Marekani katika soko huria.
Rial imeshuka hadi kiwango cha chini kabisa katika mwaka uliopita na mfumuko wa bei umepanda hadi 40% huku vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran vikikandamiza uchumi ambao pia umedhoofika kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi.
Wanafunzi wa vyuo vikuu walijiunga na maandamano hayo na yakaanza kusambaa hadi miji mingine.
Siku ya Ijumaa, Rais Donald Trump alitishia kuingilia kati ikiwa vikosi vya usalama vya Iran vitawaua waandamanaji akisema: "Tuko tayari kuingia."
Siku iliyofuata, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei - alisema "wafanya fujo wanapaswa kushughulikiwa" na akaapa "hatosalimu amri mbele ya adui."
Pia unaweza kusoma:
Wanajeshi wa Venezuela waripotiwa kupekua simu za raia na waandishi wa habari

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Polisi walilinda Bunge la taifa ambapo Delcy Rodríguez aliapishwa Jumatatu Takribani waandishi wa habari 14 walikamatwa nchini Venezuela siku ya Jumatatu walipokuwa wakiripoti kuhusu mgogoro uliosababishwa na operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyomkamata kiongozi wa nchi hiyo, Nicolás Maduro.
Muungano wa wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini humo ulieleza kuwa karibu wote waliokamatwa, isipokuwa mmoja, walikuwa wakifanya kazi kwa mashirika ya habari ya kimataifa.
Wengi wao waliachiliwa huru baadaye siku hiyo, huku mwandishi mmoja akifukuzwa nje ya nchi.
Vyombo vya habari vya kigeni kwa muda mrefu vimekuwa vikikabiliwa na vikwazo vikali nchini Venezuela, na ni idadi ndogo tu ya waandishi wa habari wanaopata viza za kufanya kazi nchini humo.
Kukamatwa kwa waandishi hao kulijiri wakati Delcy Rodríguez aliapishwa kuwa rais wa mpito, muda mfupi baada ya kutangaza kuwa yuko tayari kushirikiana na utawala wa Rais Donald Trump, ambao alidai ungekuwa na nafasi ya kuisimamia Venezuela.
Kwa mujibu wa muungano huo, waandishi wa habari walikamatwa na vikosi vya usalama katika na pembezoni mwa jengo la Bunge la Taifa, pamoja na katika eneo la Altamira, ndani ya mji mkuu, Caracas.
Angalau wawili walikamatwa na maafisa wa idara ya ujasusi wa kijeshi, huku wengine wakishikiliwa na vyombo vya ujasusi wa kiraia.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa vifaa vyao vilichunguzwa, simu zao zilifanyiwa upekuzi, na jumbe zao za maandishi pamoja na mawasiliano yao ya mitandao ya kijamii zilisomwa bila idhini.
Mwandishi wa habari kutoka Colombia na mwandishi mwingine kutoka Hispania pia walikamatwa katika mpaka wa Venezuela na Colombia, karibu na mji wa Cúcuta.
Matukio hayo yametokea katika kipindi cha mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Venezuela, kufuatia kukamatwa kwa Nicolás Maduro na mkewe na vikosi vya Marekani katika uvamizi wa alfajiri uliosababisha vifo vya makumi ya walinzi wake na askari wa usalama.
Ingawa tukio hilo lilishangiliwa na baadhi ya Wavenezuela waliompinga Maduro, hususan walioko nje ya nchi, hali ya tahadhari na ukimya ilitawala miongoni mwa raia waliobaki ndani ya Venezuela.
Kwa muda mrefu, upinzani wa Venezuela umekuwa ukilalamikia vitisho na mashinikizo wanayokumbana nayo wanapotoa maoni yanayoukosoa utawala wa Maduro.
Zaidi ya watu 2,000 wamekamatwa katika maandamano yaliyoibuka kufuatia uchaguzi wa urais wa mwaka 2024.
Soma pia:
Urusi yaanza kulinda meli ya mafuta inayofuatiliwa na vikosi Marekani

Chanzo cha picha, EPA
Urusi imepeleka jeshi la wanamaji kuweka ulinzi kwa meli ya mafuta ambayo pia inafuatiliwa na majeshi ya Marekani katika Atlantic, kulingana na CBS, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani,
Meli hiyo, ambayo kwa sasa haijabeba chochote, imekuwa ikisafirisha mafuta ghafi ya Venezuela na inasadikiwa kuwa kati ya Scotland na Iceland siku ya Jumanne.
Mwezi uliopita Rais Donald Trump alisema kuwa ametoa amri ya "kuzuiliwa" kwa meli za mafuta za Venezuela zilizowekewa vikwazo kuingia nchini humo katika hatua ambayo serikali ya Venezela ilitaja kuwa "wizi".
Kabla ya Marekani kumkamata kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Nicolás Maduro siku ya Jumamosi, Trump mara kwa mara aliishutumu serikali ya Venezuela kwa kutumia meli hizo kuingiza dawa za kulevya Marekani.
Walinzi wa Pwani ya Marekani walijaribu kuabiri Bella 1 mwezi uliopita katika visiwa vya Caribbean wakati iliaminika kuelekea Venezuela.
Walikuwa na kibali cha kukamata meli hiyo, ambayo ilishutumiwa kwa kukiuka vikwazo vya Marekani na kusafirisha mafuta ya Iran.
Maelezo zaidi:
AFCON 2025: Amad aipeleka Ivory Coast robo fainali, sasa macho kwa vigogo Misri

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Amad Diallo hakuwa sehemu ya kikosi cha Ivory Coast ambacho kilishinda Afcon 2023 kwa utulivu lakini sasa ana mabao matatu kwenye michuano hii. Amad Diallo aliibuka shujaa wa usiku wa kuamkia leo baada ya kuiongoza Ivory Coast kuichapa Burkina Faso kwa kishindo na kufuzu robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 linaloendelea Morocco.
Winga wa Manchester United aliifungia Ivory Coast bao la kwanza dakika ya 20, akiwapita mabeki wawili kwa ustadi kabla ya kuinua mpira kwa akili na kumshinda kipa Herve Koffi kutoka umbali wa karibu.
Dakika 12 baadaye, Amad aliendelea kung’ara kwa kutoa pasi ya bao la pili. Aliwachanganya mabeki kabla ya kumtengenezea Yan Diomande nafasi, naye akapiga shuti la kupinda lililomshinda Koffi aliyekuwa ameenda upande tofauti.
Burkina Faso walijaribu kujibu mapema kabla ya mapumziko kupitia Dango Ouattara, lakini shuti lake kali la mguu wa kulia kutoka kona finyu liligonga chini ya mwamba wa goli upande wa kushoto na kurudi mikononi mwa kipa Yahia Fofana.
Baada ya mapumziko, Fofana aliendelea kuokoa kwa ustadi, akimzuia tena Ouattara kwa mguu wa kulia dakika chache baada ya saa moja ya mchezo, huku Amad naye akikosa kuongeza bao lake la pili baada ya Koffi kufanya uokoaji mzuri.
Hatimaye, kijana Bazoumana Toure aliimalizia Burkina Faso kwa bao la tatu la kuvutia, akianza mbio kutoka nusu ya uwanja wake, akiwapita wapinzani na kumalizia kwa shuti la uhakika lililotinga ndani ya nguzo ya kushoto.
Sasa kikosi cha kocha Emerse Fae kitavaana na vigogo wa Afrika, Misri, mabingwa mara saba wa Afcon, waliopata ushindi wa 3-1 dhidi ya Benin baada ya muda wa ziada.
Pambano hilo la robo fainali litapigwa Agadir Jumamosi saa 7:00 usiku kwa saa ya GMT.
Ivory Coast wamezoea kuokoa heshima kwa makeke na mirejesho ya kichokozi kama ilivyokuwa walipotwaa taji lao la tatu nyumbani mwaka 2023.
Hata safari yao ya Morocco ilianza kwa tabu, wakilazimika kufunga bao la dakika za majeruhi ili kuifunga Gabon 3-2 na kuongoza kundi. Hata hivyo, mjini Marrakesh walionyesha nia mapema.
Bao la Diomande lilizidi kuonyesha ubora wa Tembo, huku nafasi zikiendelea kuundwa.
Diomande mwenyewe alizuiwa shuti lake, na beki wa kulia Guela Doue alipiga kichwa kilichopita lango kabla ya mapumziko, Ivory Coast wakionekana kutaka mabao zaidi.
Kocha wa Burkina Faso, Brama Traore, alifanya mabadiliko kadhaa akiwemo kumuingiza nahodha Bertrand Traore ili kuipa timu nguvu mpya, lakini jaribio la karibu zaidi lilikuwa shuti la chini la Ouattara lililodhibitiwa na Fofana.
Licha ya kukosa nyota wake Simon Adingra na Sebastien Haller, Ivory Coast wameandika historia kwa kuwa mabingwa watetezi wa kwanza kufika robo fainali ya Afcon tangu Misri mwaka 2010.
Misri walikuwa timu ya mwisho kulibakiza taji hilo walipokamilisha rekodi ya mataji matatu mfululizo miaka 16 iliyopita, na sasa Mohamed Salah na wenzake wanatazamiwa kujaribu kuumaliza utawala wa Tembo katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa Jumamosi.
Soma pia:
Uingereza na Ufaransa kuwapeleka wanajeshi Ukraine mkataba wa amani ukifikiwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza na Ufaransa zimetia saini azimio la kupeleka wanajeshi nchini Ukraine ikiwa makubaliano ya amani yatafikiwa kumaliza vita vya Urusi, Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ametangaza.
Baada ya mazungumzo na washirika wa Ukraine mjini Paris, alisema Uingereza na Ufaransa "zitaanzisha kambi za kijeshi kote Ukraine" ili kuzuia uvamizi wa siku zijazo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa upande wake amesema maelfu ya wanajeshi wanaweza kupelekwa Ukraine.
Washirika hao pia walikubali kwa kauli moja dhamana ya usalama kwa Ukraine na kupendekeza kuwa Marekani itaongoza itafuatilia utekelezaji wa mkataba wa amani.
Lakini suala kuu linalohusiana na umiliki wa maeneo bado linajadiliwa.
Urusi imeonya mara kwa mara kwamba wanajeshi wowote wa kigeni watakaoingia nchini Ukraine 'watakabiliwa" vilivyo.
Pia unaweza kusoma:
Trump asema Venezuela 'itaikabidhi' Marekani hadi mapipa milioni 50 ya mafuta

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Venezuela "itawasilisha" hadi mapipa 50m ya mafuta kwa Marekani, baada ya operesheni ya kushtukiza ya kijeshi iliyomuondoa Rais Nicolás Maduro mamlakani.
Mafuta hayo yatauzwa kwa bei ya soko, Trump aliandikwa kwenye mitandao wake wa kijamii wa Truth Sociala na kuongeza kuwa fedha hizo zitasimamiwa na yeye binafsi na zitatumika kuwanufaisha watu wa Venezuela na Marekani.
Tamko hilo linakuja baada ya Trump kudokeza kuwa sekta ya mafuta ya Marekani itakuwa tayari "kufanya kazi" nchini Venezuela ndani ya miezi 18 na kwamba anatarajia uwekezaji mkubwa nchini humo.
Wachambuzi awali waliiambia BBC inaweza kugharimu mabilioni ya dola, na uwezekano wa muongo mmoja, kurejesha pato la zamani la Venezuela.
Kwenye ujumbe wake wa Truth Social siku ya Jumanne Trampa aliandika: "Ninafuraha kutangaza kwamba Mamlaka ya mpito nchini Venezuela itawasilisha kati ya Mapipa MILIONI 30 na 50 ya mafuta yaliyo na Ubora wa hali ya Juu kwa Marekani.
"Mafuta haya yatauzwa kwa Bei yake ya Soko, na fedha hizo zitadhibitiwa na mimi kama Rais wa Marekani, ili kuhakikisha zinatumika kuwanufaisha watu wa Venezuela na Marekani!"
Kauli yake imekuja siku moja baada ya Delcy Rodríguez, aliyekuwa makamu wa rais wa Venezuela, kuapishwa kama rais wake wa muda.
Maduro amefikishwa Marekani kujibu mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya na umiliki wa silaha.
Pia unaweza kusoma:
Marekani inajadili mbinu ya kuinyakua Greenland

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa tathmini "mbinu tofauti" zitakazosaidia kuchukua eneo la Greenland, ikiwa ni pamoja na matumizi ya kijeshi, White House ilisema.
Ikulu ya White House iliiambia BBC kwamba kupata Greenland - eneo linalojitawala linalosimamiwa na nchi mwanachama mwenzao wa Nato Denmark - lilikuwa "kipaumbele cha usalama wa kitaifa".
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya viongozi wa Ulaya kutoa tamko la pamoja la kuiunga mkono Denmark, ambayo imekuwa ikipinga mpango wa Trump kunyakua kisiwa hicho cha Arctic.
Mwishoni mwa wiki Trump alirejelea kauli ya kwamba Marekani "inahitaji" Greenland kwa sababu za usalama, na kumfanya Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen kuonya kwamba shambulio lolote la Marekani litamaanisha mwisho wa Nato.
Ikulu ya White House ilisema Jumanne: "Rais na timu yake wanajadili chaguzi mbalimbali ili kutekeleza lengo hili muhimu la sera ya kigeni, na bila shaka, kutumia jeshi la Marekani daima ni chaguo kwa Amiri Jeshi Mkuu."
Nato ni muungano wa kijeshi wa mataifa ya Ulaya ambapo washirika wanatarajiwa kusaidiana kudhibiti mashambulizi ya nje.
Siku ya Jumanne, washirika sita wa Ulaya walionyesha mshikamano wao na Denmark.
"Greenland ni mali ya watu wake, na Denmark na Greenland pekee ndizo zinazoweza kuamua juu ya mambo yanayohusu uhusiano wao," viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Denmark walisema katika taarifa ya pamoja.
Soma pia:
Natumai hujambo
Karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Jumatano 07/01/2026.
