Namna Ulaya inavyojiandaa na mashambulizi ya Urusi mpakani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Natasha Lindstaedt
- Nafasi, The Conversation*
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mnamo 1946, Winston Churchill, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na kiongozi mashuhuri wa dunia, alielezea mgawanyiko wa kisiasa kati ya nchi za Magharibi na zile zilizo chini ya ushawishi wa Umoja wa Kisovyeti kama "Iron Curtain," au kizuizi cha kisiasa na kijeshi. Sasa, miaka kadhaa baadaye, ni nchi za Ulaya zinazojenga vizuizi vya kisasa kando ya mipaka yao ili kujilinda dhidi ya uwezekano wa mashambulio ya Urusi.
Kila taifa linalopakana na Urusi au mshirika wake Belarus lina harakisha mipango ya kujenga vizuizi vya mamia ya kilomita ili kulinda wananchi wake. Muundo wa usalama wa Ulaya uliokuwa ukitegemea NATO, mashirika ya kimataifa, na ulinzi wa Marekani unaonekana kudhoofika, na hivyo kila nchi zinajilinda zaidi kwa njia za moja kwa moja.
Finlandi
Finland, yenye mpaka wa kilomita 1,340 na Urusi, ilipendekeza kujenga ukuta unaofunika sehemu ya mpaka wake kwa gharama ya zaidi ya Dola za Marekani 400 milioni, na kukamilisha mradi ifikapo 2026. Sababu ni pamoja na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022 na ongezeko la Warusi wanaokimbia kwenda Finland kuepuka mashambulizi ya kijeshi.
Serikali ya Finland ilipitisha sheria mpya mnamo 2023 kujenga vizuizi virefu na imara, kwani vizuizi vya zamani vilikuwa vya mbao tu vilivyoundwa kuzuia mifugo kuvuka. Vituo nane vya mipaka vimejengwa, ikiwemo kimoja kaskazini, pamoja na vizuizi vikubwa kusini mwa nchi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata katika maeneo ya mbali kaskazini-mashariki, vizuizi sasa vimejengwa, huku hapo awali Warusi na raia wengine walivuka mpaka mara kwa mara bila vizuizi vikubwa.
Estonia, Latvia, Lithuania na Poland
Estonia ilitangaza mnamo 2015 kujenga uzio kwenye mpaka wake wa mashariki na Urusi, kufuatia ujumuishaji wa Crimea. Mnamo 2024, mataifa ya Baltiki (Estonia, Latvia, Lithuania) na Poland yalipendekeza kuimarisha mipaka yao zaidi kwa ukuta wa ulinzi unaofunika karibu kilomita 700, kwa gharama ya Dola za Marekani 2.7 bilioni.
Mipango hii imeharakishwa, huku viongozi wa Baltiki wakihofia kuwa iwapo kutakuwa na mapumziko ya vita kati ya Ukraine na Urusi, Moscow inaweza kuhamisha vikosi vyake karibu na mipaka yao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Latvia inakusudia kutumia Dola za Marekani 350 milioni kuimarisha mpaka wake wa kilomita 386 na Urusi. Lithuania yenyewe inapanga ukuta wa ulinzi wa kilomita 48.
Poland tayari imeanza kujenga uzio wa kudumu kwenye mpaka wake na Belarus, kama sehemu ya mipango yake ya kujilinda.
Vizuizi hivi vinajumuisha: Mahandaki, Mashimo na viziuzi vikubwa vya saruji kukabiliana na mashambulizi. Viziuizi vya barabara na madaraja yaliyofungwa, ili kuzuia jeshi la Urusi kufikia maeneo yao ya mipaka kwa urahisi na kwa haraka.
Baltiki pia inajenga zaidi ya maeneo 1,000, hifadhi za risasi, na makazi ya vifaa, kila moja ikiwa na ukubwa wa angalau mita za mraba 35 zenye uwezo wa kubeba wanajeshi 10, ili kustahimili shambulio la mabomu.
Mnamo 2025, mataifa haya, pamoja na Finland na Poland, yalitangaza kujiondoa kwenye mikataba ya kimataifa inayozuia madini ya antipersonnel na silaha, huku Poland ikiongeza maeneo ya madini kwenye mipango yake ya "Eastern Shield."

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujenzi wa Ukuta wa Droni
Vizuizi hivi pia vitashirikiana na teknolojia za kisasa, mifumo ya onyo la mapema, na vitengo vya silaha. Lithuania, Latvia, Estonia, Poland, Ufinlandi, na Norway walikutana Riga mwaka 2024 kuanzisha mpango wa "ukuta wa droni" wa kilomita 2,977.
Ukuta huu utakuwa na mtandao wa rada na vifaa vya kielektroniki kutambua na kuharibu droni za Kirusi. Mara tu kitisho kitakapogunduliwa, droni wa karibu watatumwa kudhibiti hali. Kampuni za Estonia tayari zinaunda droni zinazoweza kugundua na kuondoa vitisho kwenye mito, misitu, na maswamps kando ya mipaka ya Baltiki na Urusi.
Historia inavyojirudia
Ushirikiano wa nchi zote zinazopakana na Urusi na uelewa wa jiografia ni muhimu kuzuia kushindwa kama ilivyotokea kwenye Maginot Line ya Ufaransa wakati wa Vita kuu ya pili ya dunia. Ingawa handaki lililojengwa la Maginot Line ililazimisha Wajerumani kubadilisha mpango wao, Ubelgiji uliendelea kuwa hatarini.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sasa, mataifa ya Ulaya yamegundua kuwa hawawezi kuzuia kabisa shambulio la warusi, lakini wanaweza kubadilisha namna ya uvamizi. Lengo la vizuizi hivi siyo tu kuzuia, bali pia kudhibiti nafasi za uvamizi wowote.
Viongozi wa Baltiki wanahofia kwamba iwapo kutatangazwa kusitishwa kwa vita kati ya Ukraine na Urusi, Kremlin inaweza kuhamisha vikosi vyake karibu na mipaka yao.
Mataifa yanayopakana na Urusi yanajiandaa kuwa tayari kwa lolote ambalo Vladimir Putin anaweza kufanya.














