Baada ya Ukraine, Urusi kuishambulia nchi hii? nchi tatu zinahaha kujilinda dhidi ya Putin

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Katya Adler
- Nafasi, Mhariri mkuu Ulaya
- Muda wa kusoma: Dakika 8
''Nilijiunga na Jeshi la Wanaanga miaka 35 iliyopita, nikiwa na umri wa miaka 18, na nikaenda moja kwa moja hadi Ujerumani, nikiwa nimepelekwa kwa ndege ya Tornado," anasema Kapteni wa Jeshi la Anga la Uingereza Andy Turk, ambaye sasa ni Naibu Kamanda wa Kikosi cha NATO cha Airborne Early Warning and Control (AWACS).
"Hii ilikuwa kuelekea mwisho wa Vita baridi, na tulikuwa na jukumu la nyuklia wakati huo."
"Baada ya vita, tulitarajia faida za amani, kuendeleza kijiografia, lakini ni wazi kwamba hilo sio jambo ambalo Urusi inataka kufanya. Na sasa mwanangu mkubwa anapanga kujiunga na Jeshi la Wanaangaa, akitaka pia kuleta mabadiliko..."
Tuko takribani futi 30,000 juu ya Bahari ya Baltic, ndani ya ndege ya uchunguzi ya NATO iliyo na rada kubwa (chombo kitumiwacho na marubani kuonyesha vitu kwenye skrini, vitu vinavyowakaribia), inayong'aa na inawaruhusu wahudumu kukagua eneo hilo kwa mamia ya maili, wakitafuta iwapo kuna shughuli iliyojificha ambazo Urusi inafanya.
Misheni za uchunguzi wa angani kama hii na uanachama wa NATO kwa upana zaidi na kwa muda mrefu umefanya mataifa madogo ya Baltic ya Lithuania, Latvia, na Estonia (majirani wa Urusi) kujisikia salama.
Lakini Rais wa Marekani Donald Trump anabadilisha hilo, kutokana na uhusiano wake na Vladimir Putin, ambao umedhihirika tangu muhula wake wa kwanza.

Trump amewaambia wazi Ulaya msimamo wake: kwa mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia, bara hili haliwezi tena kutegemea msaada wa kijeshi kutoka Marekani kama ilivyokuwa kawaida.
Hali hii inaziacha nchi za Baltic kuwa katika wasiwasi, zikiishi kwa hofu.
Walitumia miaka 40 wakiwa chini ya Umoja wa Sovieti hadi ulipovunjika mwishoni mwa Vita vya Baridi.
Sasa ni wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) na NATO, lakini Putin bado anaamini wazi kwamba nchi za Baltic lazima zirudi katika eneo la ushawishi la Urusi.
Na ikiwa Rais Putin atashinda nchini Ukraine, je, atawageukia wao, iwapo kama atahisi kwamba Trump hana nia ya kuingilia kati?
"Urusi inaendelea kuimarisha uchumi wa ulinzi"
Ian Bond, Naibu mkurugenzi wa Kituo cha Mageuzi ya Ulaya, anaamini kwamba ikiwa mapatano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano yatapatikana nchini Ukraine, Putin huenda asikome hapo.
Hakuna mtu mwenye akili timamu anayetaka kufikiria kwamba vita vya Ulaya vinakaribia tena.
Lakini ukweli ni kwamba idadi inayoongezeka ya maafisa wa ujasusi wa Ulaya wanatuambia: "Iwe inatokea baada ya miaka mitatu, mitano, au kumi, wanachosema ni kwamba wazo la amani ya kudumu barani Ulaya sasa ni jambo la kale."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pamoja na hayo, uchumi wa Urusi kwa sasa uko zaidi vitani, bajeti yake kubwa ikielekezwa huko.
Karibu asilimia 40% ya bajeti ya serikali kuu inatumika kwa ulinzi na usalama wa ndani.
Gharama inaongezeka kwa uzalishaji wa vifaa vya kivita.
"Tunaona jinsi uchumi wa Urusi unavyojielekeza. Na si amani," anasema Bond.
"Vitimbi na mbinu" mpakani Estonia
Unapotembelea eneo la Narva, mji uliokaskazini mwa Estonia , utagundua ni kwanini nchi hiyo inahisi iko na wasiwasi na ni rahisi kushambuliwa.
Urusi imepakana na Estonia kuanzia kaskazini hadi Kusini.
Narva imetenganishwa na Urusi na mto ambao umepatiwa jina na mataifa hayo mawili.
Ngome yenye sura ya enzi za kati iko pande zote mbili, moja ikipeperusha bendera ya Urusi na nyingine ya Kiestonia.
Kati ya hizi mbili kuna daraja, mojawapo ya vivuko vya mwisho vya watu wanaotembea kwa miguu huko Ulaya bado iko wazi kwa Urusi.
"Tumezoea hila na mbinu zao," mkuu wa polisi wa mpaka wa Estonia Egert Belitsev aliniambia.

"Tishio la Urusi si jambo geni kwetu. Hivi sasa," alisema, "kuna uchochezi na mivutano ya mara kwa mara [mpakani]."
Polisi wa mpakani wamerekodi picha za maboya katika Mto Narva, ambayo huweka mpaka kati ya nchi hizo mbili. Zilichukuliwa na walinzi wa Urusi ...
"Tunatumia vifaa vya angani - ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege za kawaida, zote zikitumia mawimbi ya GPS na kuna msongamano wa mara kwa mara wa GPS. Kwa hivyo, [mtazamo] wa Urusi unaathiri uwezo wetu wa kutekeleza majukumu yetu."

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadaye, nikiwa tu katika upande wa Estonia, nilivuka daraja ambalo limefunikwa na theluji inayoelekea upande wa Urusi na nikiwa hapo niliona walinzi wa Urusi wakiniangalia.
Tulikuwa mita chache na mahali walipokuwa wakishika doria.
Mwaka jana, Estonia ilikarabati daraja hilo kwa kuweka vizuizi vya zege.
Sijasikia mtu yeyote akipendekeza kwamba Urusi ingetuma tani za mizinga kwani hawana haja na hilo.
Hata askari wachache wa Urusi wanaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu nchini Estonia.
Takriban asilimia 96% ya wakaazi wa Narva huzungumza Kirusi kama lugha yao ya asili.
Wengi wana uraia wa nchi mbili.
Estonia inahofia kwamba Vladimir Putin anayejiamini atatumia jamii kubwa ya kabila la Kirusi ndani na karibu na Narva kama kisingizio cha uvamizi.
Huu ni mpangilio wa matukio ya baadaye ambayo tayari ashawahi kufanya katika eneo la Georgia na Ukraine.
Katika dalili kubwa ya kuongezeka kwa wasiwasi, Estonia, Lithuania, na Poland zilitangaza kwa pamoja wiki hii kwamba zinaomba mabunge yao yaidhinishe kujiondoa kwenye mkataba wa kimataifa wa mabomu ya ardhini, ambayo yanapiga marufuku matumizi yao.
Imetiwa saini na nchi 160.
Hii ilikuwa kuwaruhusu "kubadilika zaidi" katika kulinda mipaka yao, walisema.
Lithuania ilikuwa tayari imejiondoa kwenye mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku mabomu ya vifungu mapema mwezi huu.
Je, mataifa yasiyo wanachama wa NATO yako hatarini kuliko mengine?
Camille Grand, kutoka Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Nje, anasema kuwa baada ya Ukraine, Putin ana uwezekano mkubwa wa kulenga nchi zisizo wanachama wa NATO, kama Moldova, badala ya kutishia mataifa ya NATO kutokana na hatari ndogo ya athari za kimataifa.
Aliongeza kuwa mataifa ya Baltic yalikuwa hatarini kwa sababu ya kijiografia, lakini hali hiyo imebadilika baada ya Sweden na Finland kujiunga na NATO.
Dkt. Marion Messmer, kutoka Chatham House, anasisitiza kwamba vita na Urusi yanaweza kuwa ni upotoshaji, na sio makusudi.

Chanzo cha picha, Kremlin Press Office handout via Getty Images
Ikiwa amani itapatikana nchini Ukraine, Dkt. Messmer anatarajia kuwa Urusi itaendelea na kampeni za uongo, vita vya mtandao barani Ulaya, pamoja na uharibifu na ujasusi katika Bahari ya Baltic.
Anasema kwamba shughuli za kutishia uthabiti zinaweza kuendelea, hata kama amani itapatikana kwa Ukraine.
Dkt. Messmer pia anahofia ajali isiyokusudiwa katika Bahari ya Baltic, inayoweza kusababishwa na shughuli za Urusi au sera ya mwisho ya Urusi.
Hali hii inaweza kusababisha mzozo kati ya nchi za NATO na Urusi, ambao unaweza kuongezeka.
Lakini Grand ni mwangalifu kutopunguza kabisa hatari kwamba Putin atalenga Baltic.
Je, wanachama wa NATO wana umoja?
Grand anasema kuwa Putin atazingatia uwezekano wa washirika wa NATO kujibu mashambulizi.
Ikiwa Urusi itaendelea kuingilia Estonia, ni vigumu kusema kama NATO itachukua hatua, hasa ikiwa Urusi itatumia mbinu za kukataa uwajibikaji kama ilivyofanyika Donbass mwaka 2014.
Kama NATO haitachukua hatua, Putin huenda akafaidika kwa kudhoofisha umoja wa NATO, na kuzua kutokuwepo kwa uthabiti katika nchi za Baltiki.
Hali hii inaweza pia kutisha wawekezaji wa kigeni.
Pia, kuna wasiwasi kwamba Rais Donald Trump huenda akapunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani barani Ulaya, jambo linaloweza kuathiri usalama wa kanda hiyo.

Kujilinda dhidi ya Putin
Hali ya kutokuwa na usalama katika nchi za Baltic na Poland, karibu na Urusi, inadhihirika kupitia sheria mpya za kijeshi.
Poland imetangaza kwamba kila mwanaume mzima atapaswa kuwa tayari kwa vita, na mpango wa mafunzo ya kijeshi utaanza mwaka huu.
Waziri Mkuu Donald Tusk pia ameonyesha nia ya kukubali pendekezo la Ufaransa la kushirikiana katika mchakato wake wa nyuklia na washirika wake wa Ulaya, ikiwa Marekani itajiondoa katika ulinzi wa nyuklia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Estonia na Lithuania pia zimeongeza matumizi kwa ulinzi, huku Poland ikikusudia kutumia asilimia 4.7% ya Pato lake la Taifa kwa ulinzi.
Uingereza imeahidi kuimarisha uwepo wake katika Estonia kwa kupeleka wanajeshi 900.
Haya yanajiri baada ya Rais Trump kusisitiza msimamo wake aliousema awali: "Ikiwa [nchi za NATO] hazitalipa, sitawalinda. Hapana, sitawalinda."
Kuhusu kiwango cha matumizi ya kila mwaka kinachohesabiwa kuwa "kinatosha" kwa utawala wa Trump, Matthew Whitaker, mgombea wa Trump kwa nafasi ya balozi wa Marekani katika NATO, alisema: "Kiwango cha chini cha matumizi ya ulinzi kinachohitajika ni asilimia 5, hivyo kuhakikisha kwamba NATO inakuwa muungano wa kijeshi wenye mafanikio zaidi katika historia."
Mpango mbadala wa Estonia
Kwa ujumbe tofauti unaotoka Washington, Estonia inazidi kutegemea washirika wake wa Ulaya kwa msaada usiosuasua hasa Uingereza.
Uingereza ina jukumu muhimu katika kuimarisha ulinzi wake katika mkoa huu na imeahidi kuimarisha uwepo wake.

Alipoulizwa kuhusu ombi la Estonia kwa Uingereza kuongeza uwepo wake kutokana na tishio la Urusi, alijibu kwamba NATO kwa ujumla inajihisi hatarini, hasa upande wa mashariki.
Estonia na nchi za Baltiki wanahisi tishio kutoka kwa Urusi, ingawa wanapinga vita.
Hata hivyo, kama vita vitatokea, Estonia iko tayari kujihami.
Estonia inafanya majaribio ya kimbunga za kijeshi kwenye mpaka wake na Urusi na kuwekeza katika teknolojia ya ndege zisizo na rubani.
Ingawa vikosi vyake haviwezi kukabiliana na shambulio la Urusi peke yao, wanajifunza kutoka kwa uvamizi wa Ukraine, hali wanayotumaini kuwa hawatalazimika kukutana nayo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












