Kwa nini Kenya kuwa mshirika wa NATO ni muhimu kwa usalama wa kikanda?

Rais wa Marekani Joe Biden (kulia) na Rais wa Kenya William Ruto (kushoto) Mei 23, 2024.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kama mshirika asiyekuwa mwanachama wa NATO, Kenya itakuwa na fursa ya kupata vifaa vya kisasa vya kijeshi na mafunzo kutoka Marekani
    • Author, Beverly Ochieng
    • Nafasi, BBC Monitoring, Nairobi

Kuteuliwa kwa Kenya kama mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato kunainua hadhi yake katika usalama wa kikanda na kimataifa wakati ambapo maafisa wake 1,000 wa polisi wanajiandaa kupambana na magenge katika mji mkuu wa Port-au-Prince unaozingirwa nchini Haiti.

Tangazo hilo lilitolewa wakati Rais wa Kenya William Ruto alipoanza ziara ya kihistoria nchini Marekani ili kujadiliana na Rais Joe Biden kuhusu kutumwa kwa wanajeshi hao katika taifa hilo la Caribbea na masuala mengine kuhusu pande hizo mbili.

Kenya inakuwa taifa la nne la Afrika kupata hadhi hiyo, na la kwanza katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kuimarisha hadhi ya Kenya kama mojawapo ya washirika wa karibu wa Marekani katika bara hilo.

Pia unaweza kusoma:

Washington iliahidi $200m kwa Nairobi katika misheni ya Haiti inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, na hivyo kupata imani kutoka kwenye historia ndefu ya Kenya ya kuunga mkono mipango ya amani ya kikanda, na kufanikiwa kiasi.

Kwa sasa Kenya inasimamia mpango wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Bw.Ruto pia amekuwa mpatanishi kati ya mataifa katika eneo la Maziwa Makuu yaliyogawanyika pakubwa na uasi wa muda mrefu wa waasi mashariki mwa DR Congo.

Tangu 2011, jeshi la Kenya limekuwa likipambana na kundi la kigaidi la al-Shabab katika nchi jirani ya Somalia. Kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko katika kaunti ya Lamu pwani ya Kenya imekuwa uti wa mgongo wa operesheni hizo za kukabiliana na waasi.

Kuegemea huku ni muhimu kwa Marekani, ambayo inazingirwa na Urusi na China, hasa katika sehemu za Afrika Magharibi, ambako majeshi ya Magharibi yamelazimika kupunguza uwepo wao.

Italeta tofauti gani?

Kama mshirika asiyekuwa mwanachama wa Nato, Kenya itakuwa na fursa ya kupata vifaa vya kisasa vya kijeshi, mafunzo na mikopo ili kuongeza matumizi ya ulinzi.

Hata hivyo, Marekani haina wajibu wa kuipatia msaada wa kijeshi wa moja kwa moja na Kenya haina mamlaka ya kutuma wanajeshi kwa ajili ya operesheni za Nato.

Licha ya tishio kutoka kwa kundi la al-Shabab, ambalo limefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Kenya, matumizi yake ya kijeshi mara nyingi yamekuwa ya wastani ikilinganishwa na majirani zake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Graph showing military spending by different East African countries

Uvamizi mdogo wa hapa na pale ya kawaida kwenye mpaka wa kilomita 680 kati ya Somalia na Kenya.

Kundi la Al-Shabab pia limedai kutekeleza mashambulio kadhaa mabaya na ya hali ya juu nchini Kenya, likiwemo shambulio la mwaka 2013 katika jumba la Westgate katika mji mkuu wa Nairobi ambapo zaidi ya watu 70 waliuawa.

Tangu mwanzoni mwa 2024, al-Shabab imedai takribani mashambulizi 30 nchini Kenya, kulingana na data iliyokusanywa na BBC Monitoring kutoka kwenye vyombo vya habari vya kundi hilo la wanamgambo.

Mashambulizi hayo yamefanyika zaidi katika kaunti za mpakani za Lamu, Garissa, Wajir na Mandera. Waliopoteza maisha zaidi wamekuwa maafisa wa vikosi vya usalama vya Kenya.

Graph showing al-Shabab attacks in Kenya

Wakati walinda amani wa Umoja wa Afrika wakiondoka Somalia mwishoni mwa mwaka huu, Kenya inapanga kuimarisha uwepo wake mpakani.

Hali ya juu ya usalama inaweza kuboresha mwelekeo wa Kenya katika kukusanya taarifa za kijasusi na ili kuchukua hatua za kimkakati.

Kujihusisha kwa Kenya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa mtihani wa nguvu ya kijeshi ya jeshi la kikanda la nchi wanachama wa EAC.

Mpango huo ulionekana kutofaulu kwani wanajeshi waliondoka chini ya miezi tisa baada ya kuingia katika taifa hilo la Afrika ya kati, na waasi waliendeleana mashambulizi yao.

Misheni ya Haiti

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati Kenya ina uzoefu mkubwa katika ulinzi wa amani wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone na Liberia, Haiti ni eneo lisilojulikana.

TakribanI magenge 100 yameifanya mji wa Port-au-Prince kuwa ngome yao vita kufuatia kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka wa 2021. Ghasia zimefanya zaidi ya watu 300,000 kutoroka makwao na hatimaye kumlazimu Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu mwaka huu.

Wanapotafuta udhibiti wa eneo, magenge ya Haiti pia yameshiriki yamekuwa yakijihami kwa silaha za kisasa. Silaha zao nyingi huingizwa kinyemela kutoka Marekani, Jamhuri ya Dominica, Jamaica na Colombia.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu iligundua mapema mwaka huu kwamba magenge yana silaha aina ya AK47 za Urusi, AR-15 zinazotengenezwa Marekani na Israel.

Ufadhili wa Marekani unaweza kuwawezesha polisi wa Kenya, ambao wanatatizwa kwa muda mrefu na vifaa duni na mafunzo, kupata bunduki, magari ya kivita na risasi za kutosha kukabiliana na magenge.

Je, nchi nyingine za Afrika zimenufaika vipi na uteuzi huo?

Hadhi ya kywa mshirika wa NATO asiye mwanachama iliboresha kwa kiwango kikubwa wanajeshi wa Tunisia, Morocco na Misri.

Nguvu ya kijeshi ya Tunisia ilibadilika sana mara tu ilipopata hadhi hiyo mwaka 2015, sambamba na mageuzi ya bajeti na uendeshaji.

Misri, ambayo ina moja ya majeshi yanayoheshimika zaidi duniani, imekuwa na hadhi hiyo tangu 1989 ikiwa ndio msingi wa mazungumzo ya kidiplomasia ya Marekani katika Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Morocco imepata uzoefu mkubwa katika kukabiliana na ugaidi huku wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS) wakitafuta kujikita katika maeneo ya Afrika Kaskazini.

Ufalme huo umekuwa mwenyeji wa mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi katika bara hilo tangu 2007 iliyopewa jina la "Simba wa Afrika".

Toleo la mwaka huu linajumuisha wanajeshi 7,000 kutoka mataifa 20 ya Afrika na Nato wakipokea mafunzo ya mbinu.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi