Ariel Henry: Kupanda na kuporomoka kwa Waziri Mkuu wa Haiti

Chanzo cha picha, Getty Images
Ariel Henry, waziri mkuu wa Haiti tangu Julai 2021, alitangaza Jumatatu kwamba atajiuzulu punde tu baraza la mpito litakapoundwa kuchukua nafasi yake.
Kujiuzulu kwake kulitarajiwa kwani wimbi la ghasia za magenge limeikumba mji mkuu, na kufanya isiwezekane kwake kurejea kutoka safarini nje ya nchi.
Henry, daktari mtaalamu wa upasuaji wa neva, aliteuliwa kuwa waziri mkuu mwanzoni mwa mwezi Julai 2021 na rais wa wakati huo, Jovenel Moïse.
Waandamanaji walikuwa wakimtaka rais ajiuzulu, wakisema amekaa muda mrefu madarakani. Kisha akauawa kikatili na kundi la mamluki wa Colombia.
Baada ya mauaji hayo, utata ulitawala kuhusu nani ataongoze nchi.
Henry hakuwa ameapishwa. Ilichukua siku 13 nafasi ya Waziri Mkuu ikiongozwa na mtangulizi wake, Claude Joseph, kabla ya Henry kuapishwa.
Hali haikuimarika. Akizungumza baada ya sherehe ya kuapishwa tarehe 20 Julai 2021, waziri mkuu huyo mpya aliahidi kurejesha utulivu na uchaguzi mpya wa rais "haraka iwezekanavyo."
Wakati huo haukufika - katika kipindi chake cha miezi 32 madarakani hakuna uchaguzi uliofanyika.
Henry alisema kuwa hali ya usalama imezorota kiasi kwamba uchaguzi huru na wa haki haukuwezekana.
Wakati huo, Wahaiti walizidi kukosa subira huku ghasia za magenge zikiongezeka na kukosekana nguvu za kisiasa.
Tarehe 7 Februari mwaka huu, siku ambayo kikawaida marais wapya wanachukua madaraka nchini Haiti, waandamanaji waliingia katika mitaa ya mji mkuu kumtaka Henry ajiuzulu.
Henry alijibu kwa kusema anapanga kufanya uchaguzi Agosti 2025. Hilo lilionekana kuwakasirisha zaidi Wahaiti.
Mpango wa mwaka mwingine na nusu Henry kuwa mamlakani ulionekana na baadhi ya wachambuzi kuwa mpango utakao ongeza matatizo.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wengine wanataja ziara yake nchini Kenya mwishoni mwa Februari kama kichochezi cha wimbi la hivi punde la ghasia.
Kenya ilikuwa imekubali kuongoza kikosi cha polisi wa kimataifa kutumwa Haiti kusaidia kupambana na magenge ambayo yanaendesha wimbi la utekaji nyara na mauaji ambayo yameathiri mji mkuu.
Lakini mpango huo umegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kuzuia.
Henry alisafiri hadi Nairobi mwishoni mwa mwezi Februari kwa mazungumzo na Rais wa Kenya, William Ruto kujaribu kufufua kikosi hicho.
Wapinzani wa Henry walihofia angetumia maafisa wa polisi wa kigeni kujilinda na kuendelea kuimarisha mamlaka yake.
Wimbi la mashambulizi ya magenge yameikumba mji mkuu wakati Henry alipokutana na Rais Ruto.
Magenge hayo yalivamia uwanja wa ndege wa Toussaint Louverture ili kumzuia Henry asirudi, na amekwama Puerto Rico tangu wakati huo.
Kwa siku 10, hakuzungumza hadharani. Hatimaye alijitokeza siku ya Jumatatu na kutangaza kuwa ataachia ngazi "mara tu baada ya kusimikwa kwa baraza la mpito.
Ingawa bado haijulikani ni lini hilo litafanyika, lakini itakuwa vigumu kwa Henry kuwa na ushawishi wowote akiwa uhamishoni nchini Puerto Rico.














