Kwa nini NATO haijaipa Ukraine uwanachama?

tgyrf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna kauli kinzani kuhusu Ukraine kujiunga na Nato

NATO itaikubali Ukraine, pindi washirika watakapoamua na nchi inakidhi vigezo vitakiwavyo. Huu ndio ujumbe uliotolewa na muungano wa kijeshi wa Atlantiki katika taarifa yake ya siku ya Jumanne, siku ya kwanza kati ya siku mbili za mkutano wao wa kila mwaka huko Vilnius, mji mkuu wa Lithuania.

Mkurugenzi mkuu NATO, Jens Stoltenberg, aliahidi kuharakisha kujiunga kwa Ukraine "kutoka mchakato wa hatua mbili hadi mchakato wa hatua moja," kutegemeana na uamuzi wa kisiasa.

Pia, alitangaza kuundwa kwa Baraza jipya la NATO-Ukraine, ambalo litafanya mkutano wake wa kwanza siku ya Jumatano na kuipa Kyiv haki ya kuitisha mikutano ya muungano mzima.

Hata hivyo, maendeleo haya hayaonyeshi kwamba NATO itaikubali Ukraine katika muda mfupi kwani haijaonyesha hata tarehe ya kuanza kwa mchakato huo.

Kwa hakika, rais wa Ukrain, Volodymyr Zelensky, alielezea ni "upuuzi" kwamba hakuna ratiba maalum na anahuzunika wito wa serikali yake haujazingatiwa katika mpango wa kuwa mwanachama hadi sasa.

"Inaonekana hakuna nia ya kualika Ukraine katika NATO au kuwa mwanachama wa muungano. Kwa Urusi, hii ni kichocheo cha kuendeleza ugaidi wake, "alisema.

Vita

fddf

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukraine iliomba kujiunga na NATO mwaka 2008, ingawa miaka miwili baadaye ilitupilia mbali azma yake kwa kupitisha sheria ya kupiga marufuku uanachama wa kambi yoyote ya kijeshi.

Hata hivyo, baada ya Urusi kunyakua Crimea mwaka 2014, Kyiv ilibatilisha sheria hii, na kuthibitisha nia yake ya kujiunga na NATO na ushirikiano wa karibu na muungano huo. Hata wakati huo, mzozo juu ya Crimea ilikuwa ni kikwazo kikubwa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nchi inapojiunga na NATO, inajiunga na ulinzi wa Pamoja, ambapo kifungu cha 5 cha Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini, kinasema - shambulio dhidi ya mwanachama mmoja linachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya wote.

Kwa maneno mengine, ikiwa Kyiv itajiunga na NATO wakati wa mzozo unaoendelea inaweza kusababisha kifungu hicho kufanya kazi na kuzitia nchi zote wanachama wa muungano katika vita.

"Iwapo vita vinaendelea, sote tutakuwa vitani. Tutakuwa katika vita na Urusi," alisema Rais wa Marekani Joe Biden, alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Ukraine kujiunga na muungano huo katika mahojiano na CNN siku ya Jumatatu, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo.

Makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi na Urusi ni jamba ambalo washirika wote wanataka kuepuka kwa gharama zote, kutokana na hatari kubwa ya matokeo mabaya ya vita vya nyuklia vinavyoweza kutokea

Ni lazima ikumbukwe Urusi ina nguvu kubwa ya atomiki na ina idadi kubwa zaidi ya vichwa vya nyuklia kwenye sayari. Muungano huo kukumkubali mwanachama mpya aliye katika mgogoro wa kimataifa kunaweza kutafsiriwa kama uchochezi.

NATO inaweza kuipa Ukraine tarehe ya kuwa mwanachama iwapo vita vitaisha, lakini wataalam wanaamini hilo halitakuwa na tija, na litaipa Kremlin sababu nyingine ya kurefusha mzozo huo kwa muda usiojulikana.

Vilevile hilo lingetilia nguvu moja kwa moja hoja iliyotumiwa na Rais Vladmir Putin kuhalalisha uvamizi huo; kwamba nchi za Magharibi ndizo zilizoanzisha vita hivyo ili kupanua nguvu zake za kijeshi.

Kukosekana kauli moja

rererere

Chanzo cha picha, Getty Images

Kuikubali Ukraine kutahitaji idhini ya pamoja ya wanachama wote 31 wa NATO. Ikiwa mchakato wa kujumuisha Uswidi - nchi isiyo na migogoro ya wazi – ulikwama kwa miezi kadhaa kutokana na kusita kutoka kwa Uturuki, kwa upande wa Ukraine mtu anaweza kutarajia upinzani mkubwa zaidi.

Katika mkutano wa kilele wa Kilithuania ilikuwa wazi kuwa sio wanachama wote wanaounga mkono kujumuishwa kwa Ukraine.

Kwa upande mmoja, nchi za Ulaya Mashariki, zikiongozwa na Ufaransa na Uingereza, zimejionyesha kuwa tayari kuikubali Ukraine katika NATO. Kundi hili lilishawishi neno "mwaliko" lijumuishwe katika taarifa, na kuwezesha mwendo wa haraka wa uanachama kupitia uamuzi wa kisiasa.

Kinyume chake, Marekani na Ujerumani zimekuwa na kusitasita kuhusu kuongeza kasi ya kujumuishwa Ukraine. Biden alikuwa wazi, "sidhani kama kuna umoja katika NATO juu ya kukubali au kutokubali Ukraine katika familia ya muungano wakati huu wa vita."

Wakati baadhi ya wanachama wanaamini kuwa kualika Ukraine ni ishara ya mshikamano katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi, wengine wanaona kuwa ni kuongeza mivutano na Moscow ambayo inaweza kuweka usalama na utulivu wa Ulaya katika hatari.

Kwa hivyo, pamoja na ukweli kwamba muungano huo umethibitisha kwamba "mustakabali wa Ukraine upo katika NATO," kukosekana kwa maelewano kati ya wanachama wake juu ya lini na jinsi gani jambo hili linapaswa kutokea kunaleta kikwazo kikubwa kwa nchi hiyo kujiunga.

Demokrasia na majeshi

Hata kama kungekuwa na umoja kati ya wanachama na kuijumuisha Ukraine, na ukiacha tatizo la nchi kuwa vitani, pia kuna vikwazo vinavyoifanya kuwa ngumu kwa nchi hiyo kujiunga na NATO.

Hata kabla ya uvamizi wa Urusi, Ukraine ilikuwa na kasoro fulani ambazo ziliifanya kutokuwa na hadhi ya kujiunga na muungano huo, hasa kiwango chake cha uimarishaji wa kidemokrasia.

Biden alisema saa chache kabla ya mkutano huo ulioanza Jumanne kwamba kutakuwa na mahitaji mengine ambayo lazima yatimizwe, ikiwa ni pamoja na demokrasia kuikubali Ukraine kama nchi mwanachama.

NATO inatarajia kutoka kwa wanachama wake kujitolea kuimarisha kidemokrasia, kulinda utawala wa sheria, kanuni za utawala bora, na viwango vinavyokubalika vya uwazi na vita dhidi ya rushwa. Kabla ya kuanza kwa uvamizi Februari mwaka jana, NATO ilieleza kuwa Ukraine haikufikia viwango vinavyohitajika.