Ukraine itajiunga lini na muungano wa kijeshi wa NATO?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mkuu wa muungano wa kijeshi wa Nato, Jens Stoltenberg, alikosoa maneno ya Donald Trump kwamba ataichajihisha Urusi kushambulia wanachama wa NATO ambao wanashindwa kulipa ada zao za ulinzi.
Stoltenberg alisema maneno ya Trump yanaviweka vikosi vya Ulaya na Marekani hatarini.
NATO, inajumuisha nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini, imeongeza wanachama wake na kuimarisha hatua za ulinzi baada ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Nato ni nini na ilianzishwa lini?
Nato - ni shirika lililoanzishwa mwaka 1949 na nchi 12, zikiwemo Marekani, Uingereza, Canada na Ufaransa. Lengo lilikuwa ni kuzuia upanuzi wa Umoja wa Kisovieti wa wakati huo - kundi la nchi zilizojumuisha Urusi.
Wanachama hao wameingia makubaliano; ikiwa mmoja wao atashambuliwa, nchi zingine zote zitasaidia - msaada unaoweza kujumuisha matumizi ya silaha.
Nato haina vikosi vyake vya kijeshi, lakini nchi wanachama wanaweza kuchukua hatua ya pamoja ya kijeshi kutatua mizozo. Pia huratibu mipango ya kijeshi na kufanya mazoezi ya pamoja.
Kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari 2022, Nato ilisema "uvamizi huo ni tishio kubwa zaidi na la moja kwa moja kwa usalama wa washirika wake."
Ni nchi gani wanachama wa Nato?
Nato ina wanachama 31 kote Ulaya na Amerika Kaskazini. Baada ya kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mwaka 1991, nchi nyingi za Ulaya Mashariki zilijiunga na umoja huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchi hizo ni pamoja na Albania, Bulgaria, Hungary, Poland, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Romania, Lithuania, Latvia na Estonia.
Sweden na Finland zilituma maombi ya kujiunga Mei 2022, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Nchi zote mbili zina wasiwasi kuhusu usalama wao.
Finland ambayo inapakana na Urusi katika mpaka wa ardhi wa kilomita 1,340 (maili 832), ilipata uwanachama wa NATO mwezi Aprili 2023.
Sweden sasa inahitaji tu bunge la Hungary kuidhinisha uanachama wake. Bosnia na Herzegovina na Georgia pia wanataka kujiunga na Nato.
Nato ilizitaka nchi wanachama kutumia angalau asilimia 2 ya mapato yao katika ulinzi. Uingereza inatumia zaidi ya asilimia 2.
Marekani inatumia zaidi ya asilimia 3 na nchi zinazopakana na Urusi - kama vile Poland na Jamhuri za Baltic - zinatumia zaidi ya asilimia 2 kwa jeshi lao.
Polandi - 3.9%, Marekani - 3.49, Estonia - 2.7%. Lithuania - 2.54%, Uingereza - 2.07, Ufaransa - 1.9%, Ujerumani - 1.57%, Italia - 1.46%, Uhispania - 1.26%, Luxemburg - 0.72%.
Ukraine itajiunga lini na Nato?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Nato ilisema Ukraine inaweza kuwa mwanachama, lakini haikuthibitisha ni lini hilo litafanyika. Shirika hilo lilikataa ombi la Rais wa Ukraine Zelensky kuwa mwanachama Septemba 2022.
Urusi inapinga wazo la Ukraine la kujiunga na kundi la usalama la NATO, kwa sababu ya hofu kwamba majeshi ya washirika yatakaribia eneo lake.
Kyiv imekubali kwamba haiwezi kujiunga na Nato wakati iko vitani na Urusi, lakini inataka kujiunga mara tu mzozo huo utakapomalizika. Kwa sasa NATO na Ukraine zinafanya kazi pamoja ili kuisaidia Ukraine kujilinda dhidi ya Urusi.
Nato kama shirika halijatuma silaha kwa Ukraine, lakini nchi nyingi wanachama zimetuma silaha. Marekani, Uingereza, Ujerumani na Uturuki zimetoa silaha, makombora, vifaru, mifumo ya kujilinda dhidi ya makombora na ndege zisizo na rubani.
Marekani imeziruhusu nchi za NATO kuipatia Ukraine ndege za kivita, kama vile F-16, na kutoa mafunzo kwa marubani jinsi ya kuziendesha. Uholanzi inasema hivi karibuni itaweza kusafirisha ndege 18 za kivita za F-16.
Hata hivyo, nchi za Nato hazipeleki wanajeshi wake Ukraine, au kutumia jeshi la anga kushambulia, kwa sababu hilo linaweza kusababisha mzozo wa moja kwa moja na Urusi.
NATO inafanya nini dhidi ya Urusi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mwaka 2023, makamanda wa Nato walikubaliana kujiandaa na uwezekano wa mashambulizi ya Urusi huko Arctic na Atlantiki ya Kaskazini, Ulaya ya Kati, au eneo la Mediterania.
Mwezi Februari 2024, Nato itafanya mojawapo ya mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi tangu kumalizika kwa Vita Baridi.
Zoezi hilo litakalofanyika Ulaya Mashariki litahusisha maafisa 90,000 kutoka nchi zote 31 za Nato na Sweden.
Katika siku za nyuma, NATO ilitangaza mipango ya kuongeza idadi ya vikosi barani Ulaya kutoka 40,000 hadi 300,000. Pia, iliimarisha hatua za ulinzi katika maeneo yanayopakana na Urusi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












