Mkutano wa Urusi -Afrika 2023: Afrika ‘inavyojichimbia’ katikati mwa Urusi na NATO
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkutano wa pili wa kilele kati ya Urusi na Afrika unafanyika huko St. Petersburg, Urusi. Mkutano huo wa siku mbili umeanza Alhamisi ya Julai 26, 2023 na utamalizika Ijumaa hii ya Julai 27,2023.
Mkutano huu umelenga kuunganisha juhudi za kuleta amani, maendeleo na mustakabali wenye mafanikio, ambapo Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa Comoro, Azali Assoumani, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) wanaendesha mkutano huo kwa pamoja.
Viongozi wakuu 49 kati ya 54 wa serikali za Afrika walihudhuria mkutano wa kwanza uliofanyika Sochi, Urusi mwaka 2019, kama ambavyo ilitarajiwa ni viongozi 17 wakuu wa nchi ndiyo wanaoshiriki mkutano wa mwaka huu, idadi ambayo haifiki hata nusu ya walioshiriki mkutano uliopita, uliofanyika kabla ya Urusi kuivamia Ukraine Februari 24, 2022.
Hapo Jumatano Urusi imezilaumu nchi za Magharibi, washirika wao na Jumuia yao ya kujihami, NATO kwa kusababisha viongozi wachache wa Afrika kuhudhuria.
Swali kubwa je bara hili litaweza kutoegemea upande wowote? na ni rahisi kuhudumia 'mabwana' hawa wawili bila kuwaudhi?
Afrika ilivyo njia panda

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkutano wa sasa kati ya Urusi na Afrika unafuatiliwa zaidi na nchi za Magharibi hasa zinazounda Muungano wa NATO. Ni kama macho yao yote yako huko kujua nini kitakubaliwa na kitakuwa na maana gani kwao.
'NATO inataka Urusi isalie kisiwani, itengwe na kila mtu, na Urusi inataka uungwaji mkono na yeyote kutoka Afrika, ikifahamu kabisa, hilo litaisaidia kwenye uamuzi wowote hasa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine', alisema Seif Shangali, mchambuzi wa siasa za Afrika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mtihani unaowaweka viongozi wa Afrika njia panda ni kwamba, wasipohudhuria kabisa mkutano huo, tafsiri yake ni kuunga mkono Magharibi wanaoipinga Urusi kuivamia Ukraine. Lakini pia itakuwa ni kuipinga Urusi kwa uvamizi wake Ukraine, hata kama si hivyo moja kwa moja.
Na kuhudhuria kwao mkutano huo maana yake ni kuunga mkono kinachoendelea Ukraine na kuzipinga nchi za Magharibi ambazo nyingi zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya zimekuwa na mchango mkubwa wa kiuchumi kwa Afrika.
Nchi za magharibi hasa za Ulaya kupitia Umoja wa Ulaya (EU) zimekuwa na mchango kwenye uchumi wa Afrika. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ufadhili wa umoja huo kwa Afrika umefikia Euro bilioni 26.6, huku utoaji wa mikopo kwa Afrika ukiongezeka kwa 50% hadi takribani Euro bilioni 5 katika sekta mbalimbali.
Urafiki wa nchi moja moja za Umoja huo pia zimekuwa na mchango wake kwa Afrika, kama ilivyo Marekani ambayo nayo kama sehemu ya nchi za Magharibi na mwanachama mwenye nguvu kwenye Umoja wa NATO imekuwa ikiwekeza fedha nyingi Afrika.
Kwa miongo miwili imekuwa ikiisadia Afrika kwenye elimu, afya, teknolojia, kilimo, miungo mbinu na biashara. Kwenye mkutano wa Disemba, 2022 kati ya Marekani na viongozi wa Afrika, taifa hilo lilihaidi kuipa Afrika dola bilioni $55 ili kusaidia uchumi, afya na kuimarisha usalama katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Aidha Rais Joe Biden wa taifa hilo kupitia Mkutano huo akahaidi kupitia Agenda 2063 ambayo inalenga kuifanya Afrika kuwa bara lenye nguvu zaidi miaka 40 ijayo kwamba Marekani itaendelea kulisaidia bara hilo ili kuweza kujitegemea kufikia wakati huo.
Haya yote yanaifanya Afrika kusalia njia panda. Wakuu wa nchi za Afrika wangetamani kuhudhuria ili kujenga misingi ya ushirika ambayo Urusi inataka kuongeza nguvu zake katika ukanda huu, lakini kufanya hivyo kunawaweka njia panda dhidi ya nchi za Magharibi.
Haishangazi kuona ni wakuu 17 tu kati ya 54 ndiyo wanaohudhuria mkutano na Urusi, wengine wengi wanawakilishwa na viongozi ama maafisa wengine wa juu wa serikali.
Urusi inaitaka Afrika zaidi kuliko Afrika inavyoitaka Urusi
Likiwa linaundwa na nchi 54 na idadi ya watu wapatao bilioni 1.3, Afrika ni bara muhimu kwenye suala la mzozo wa Urusi na Ukraine. Ndiyo ukanda wenye kura nyingi kwenye Mkutano Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Pengine Urusi inatambua hilo, na ndiyo maana imeamua kutafuta uungwaji mkono kutoka Afrika.
Hata hivyo, Urusi haina mchango mkubwa sana kiuchumi kwa nchi za Afrika. Ukiacha Putin mwenyewe kutembelea Afrika upande wa Kusini mwa jangwa la Sahara mara moja tu katika kipindi cha miongo miwili, uwekezaji wa kigeni wa taifa hilo kwa Afrika ni 1% tu.
Kisiasa mchango wake unaonekana kugawa mitazamo mingi. Nchi kadhaa za Afrika zinanunua silaha kwa wingi kutoka Urusi kukabiliana na waasi ama kujilinda zenyewe. Karibu nusu ya nchi hizo za Afrika zinazonunua silaha za Urusi ama kupewa msaada wa kiusalama na Urusi, kutokana na kukabiliwa na migogoro. Wapo wanaoona Urusi inasaidia Usalama na wapo wanaoona msaada wake unazidi kuleta mzozo na kusababbisha vifo vya waafrika.
Taasisi ya kimataifa huduma za habari za amani (International Peace Information Service) IPIC Inaonesha kupitia mtandao wake kuwa katika kipindi cha miaka mitano kati ya mwaka 2017-2021 Urusi ambayo inashika nafasi ya pili kwa uuzaji wa silaha duniani, iliuza asilimia 44 ya silaha zote zilizoingizwa Afrika kutoka nje na hivyo kuwa kinara waa uuzaji silaha barani humo. Taasisi hiyo inaonesha kuwa asilimia 56 ya silaha zilizoingia Afrika katika kipindi hicho kwa kiwango kikubwa zilitoka katika mataifa ya Ulaya, Marekani na China.
Aidha Rais Putin alitoa ahadi ya kuongeza mara tano zaidi biashara baina ya taifa lake na Afrika kutoka kiwa ngo cha sasa cha dola za Marekani bilioni 18 hadi kufikia dola bilioni 40. Hata hivyo, robo tatu ya biashara hizo, Urusi inafanya na nchi nne tu za Algeria, Misri, Morocco na Afrika Kusini.
Ingawa wengi hawaoni kama Urusi itafanikiwa sana kupitia mkutano wa mwaka huu lakini itakuwa imepata pa kuanzia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alexandra Prokopenko, msomi katika Kituo cha Carnegie Russia Eurasia huko Berlin, ameliambia gazeti la The Guardian kuwa hatarajii mafanikio ya Kremlin katika mkutano huo.
"Nchini Urusi hakuna mkakati wa wazi kuhusu Afrika au kuzungumza kwa upana zaidi kuelekea kusini mwa ulimwengu. Ni hali ilivyo zaidi: sisi si marafiki wa magharibi tena, kwa hiyo tutaangalia mashariki," alisema, na kuongeza: "Na kuna hali mbaya sana kwa sababu ya mpango wa nafaka."
Labda hili la mazao ya kilimo na mafuta, huenda ni jambo linaloweza kuizuzua Afrika. Kuna utegemezi wa Afrika katika eneo hilo. Taifa hilo limehaidi kutoa nafaka za bure kwa nchi masikini za Afrika.
“Nataka kuwahakikishia kwamba nchi yetu ina uwezo wa kuziba pengo la nafaka za Ukraine kibiashara na bure,” alisema Putin katika taarifa aliyoitoa Jumatatu kuhusu mkutano huu.
Tayari Urusi imeshapeleka Afrika takriban tani milioni 10 za nafaka katika nusu ya kwanza tu ya mwaka huu. Kwenye Mkutano wa mwaka huu, huenda Putin akajaribu kutoa ahadi nyingi zaidi pengine kuliko wakati wowote ili ipate uungwaji mkono kutoka Afrika. Kwa ufupi Urusi inaitaka Afrika wakati huu pengine kuliko wakati mwingine wowote. Afrika yenyewe ikimuona mshirika mwema lakini anayeweza kuwaletea matatizo mbele ya macho ya nchi za Magharibi.
Je Afrika itaweza kutoegemea katika pande hizi mbili?

Chanzo cha picha, Getty Images
'Huu ni mtihani mkubwa iliyonao Afrika', anasema Shangali na kuongeza: 'Inapaswa kuukubali'.
Mkutano huu unafanyika ikiwa ni wiki moja na nusu tu imepita tangu badhi ya viongozi wa Afrika kushiriki mkutano wa kilele wa Marekani na Afrika kuhusu biashara (U.S.-Africa Business Summit) uliofanyika Julai 12, 2023, Gaborone, Botswana.
Ni miezi nane tangu Marekani kupitia Rais Joe Biden ikutane na viongozi takribani 50 wa Afrika pale Washington DC, katika mkutano wa siku tatu. Na ni takribani mwaka mmoja mmoja na nusu tangu kufanyika mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya – Februari 17 -18 2022.
Mikutano hii ina faida kwa Afrika lakini inaiweka njia panda Afrika, hasa kwa wakati huu wa vita ya Ukraine, wapi pa kuegemea: Je ni nchi za NATO ambazo Marekani na nchi nyingi za Ulaya ni wanachama au upande wa Urusi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa hatua yoyote Afrika kuendelea kutoegemea upande wowote kwenye mzozo wa Ukraine haitadumu sana. Kama mzozo utaendelea, kidogokidogo tutashuhudia sura na upande wa nchi nyingi za Afrika kwenye mzozo huo.
Kutokupiga kura kwa baadhi ya nchi za Afrika wakati wa kura ya Umoja wa Mtaifa kulaani uvamizi huo ulioanza Februari 2022, ilikuwa hatua ya mwanzo. Mkutano huu ni hatua ya pili.
Baadhi ya viongozi wakuu wa Afrika wanahudhuria Mkutano huu wa Urusi wakiwa na fikra mbili. Kutoiudhi Urusi na kutowakwaza Magharibi au kuwafurahisha Magharibi na kuwaburudisha Urusi.
Nchi za Magharibi kupitia NATO zinaitenga Urusi, ndugu zake na mambo yake. Kwa mantiki hiyo hata mkutano huu ni kama umetengwa nao, hauwafurahishi NATO. Inajua unafaida kwa Urusi kidiplomasia.
Lakini Afrika inautaka mkutano huu na Urusi inaitaka Afrika. Na hicho kinaifanya Afrika kusalia kuwa njia panda na kujichimbia zaidi katikati mwa pande hizi mbili.












