Putin aweka masharti kwa Marekani ili kusitisha vita Ukraine

Chanzo cha picha, REUTERS
Rais wa Urusi hajafanya mahojiano na waandishi wa habari wa Magharibi tangu kufanya uvamizi Ukraine Februari 2022.
Hatimaye Vladimir Putin alifanya mahojiano na mwandishi wa habari maarufu wa Marekani, Tucker Carlson na kupeperushwa Alhamisi iliyopita.
Katika mahojiano hayo Putin aljibu maswali kuhusu Ukraine na kuhalalisha "hatua yake ya kijeshi" dhidi ya Kiev. Sababu yake ni upanuzi wa NATO ambao anasema unatishia Urusi.
Hata hivyo, alitoa uhakika kwamba hana nia ya kuishambulia Poland au nchi yoyote mwanachama wa NATO.
Mambo sita muhimu katika mahojiano ya Putin.
'Hatutoshambulia nchi za Nato'

Chanzo cha picha, REUTERS
Rais Putin alisema 'hakuna mpango wa kuishambulia Lithuania, Poland au nchi yoyote ya NATO.'
Uvamizi dhidi ya Ukraine umezua hofu katika mataifa ya Baltic, Poland na mataifa mengine ya Ulaya kwamba Urusi inaweza kufanya uvamizi huo pia.
Kwa sababu ya hofu hiyo, Finland na Sweden, ambazo hazikuegemea upande wowote katika mvutano wa Moscow na Magharibi, ziliomba uanachama wa NATO.
Katika mahojiano hayo, Putin aliondoa uwezekano wa shambulio dhidi ya Poland, "isipokuwa ikiwa Poland itaishambulia Urusi."
Wakati rais wa Urusi akiondoa uwezekano wa shambulio dhidi ya nchi yoyote ya NATO, amesema muungano huo utalazimika kukubali kwamba eneo linaloshikiliwa na Urusi huko Ukraine litabakia kuwa la Urusi.
'Marekani iache kutoa silaha'

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Carlson alimuuliza rais wa Urusi ikiwa mazungumzo ya moja kwa moja na Rais wa Merekani, Joe Biden yanaweza kumaliza vita nchini Ukraine.
Putin amesema kuna mazungumzo kati ya mashirika ya Urusi na Marekani, lakini hadi 'Marekani itakapoacha kutuma silaha kwa Ukraine, hakuna cha kuzungumza.'
Alielezea kuipa Ukraine silaha ni 'kosa la kimkakati'.
"Nikwambie ukweli kuhusu ujumbe wetu kwa uongozi wa Marekani. Ikiwa unataka kumaliza vita, unapaswa kuacha usambazaji wa silaha. Vita vitaisha baada ya wiki chache tu.”
Maoni ya Putin yanakuja wakati Seneti ya Marekani imepitisha msaada wa dola bilioni 61 kwa Ukraine, lakini Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Republican linapinga.
Kwa upande mwingine, wale wanaounga mkono Ukraine wanasema, "ikiwa Urusi itaacha mashambulizi, vita vitaisha. Lakini ikiwa Ukraine itaacha kujilinda, itamalizwa."
'Hawawezi Kuishinda Urusi'
Kiongozi wa Urusi alitaja maendeleo ya silaha nchini Urusi.
Amesema viwanda vya kijeshi vya Urusi vimewekeza zaidi katika silaha za haipasoniki kuliko nchi nyingine.
Na kusema kuwa watawala wa Magharibi wanaelewa vyema kuwa "hawawezi kuishinda Urusi kimkakati."
'Ukraine iliundwa kwa matakwa ya Stalin'

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Katika mahojiano hayo, Putin amezungumza juu ya historia ya Umoja wa Kisovieti (USSR) kabla ya Vita vya pili vya Dunia.
''Ukraine ilikuwa sehemu ya USSR. Ukraine ni taifa ghushi, lililoundwa kwa amri ya Stalin," Putin alisema.
''Ingawa ni kweli kwamba Ukraine haina historia kabla ya 1918, lakini sasa limekuwa taifa na mchakato wa umoja wa kitamaduni na lugha ulianza katikati ya karne ya 19,'' anasema mwanahistoria wa Chuo Kikuu cha Rochester, Matthew Lenoy.
'Kuachiliwa mwandishi wa Marekani'

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kuhusu kuachiliwa kwa mwandishi wa habari wa The Wall Street Journal, Ivan Gershkovich (32), anayeshikiliwa nchini Urusi kwa tuhuma za ujasusi, Putin alisema 'kama washirika wetu watashirikiana, kungekuwa na makubaliano ya kuachiliwa.'
"Mazungumzo yanaendelea katika ngazi maalumu. Nadhani makubaliano yanaweza kufikiwa," alisema.
Gershkovich alikamatwa Machi 29 mwaka jana. Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kufungwa jela hadi miaka 20.
Carlson alimuuliza Putin "kama atamwachia mwandishi wa habari" na akasema, "Tutamrudisha Marekani lakini hilo litafanyika ikiwa kutakuwa na kubadilishana wafungwa.''
'Marekani iliahidi kutoipanua NATO'

Chanzo cha picha, REUTERS
Kulingana na rais wa Urusi, viongozi kadhaa waliahidi kwamba NATO haitapanuliwa. Putin anasema shirika kama hilo halihitajiki tena baada ya kufutwa USSR.
Mtangulizi wa Putin, Boris Yeltsin, alidai mwaka 1993 kwamba upanuzi wa NATO kuelekea mashariki ni "haramu".
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Urusi, Yevgeny Primkov alitoa hoja sawa na hiyo."
'Maswali ambayo Putin hakuulizwa'
Tucker Carlson hakumhoji Putin kuhusu uhalifu wa kivita unaofanywa na vikosi vya Urusi nchini Ukraine, uhamisho wa kulazimishwa wa watoto wa Ukraine hadi Urusi (ambapo ICC ilitoa hati ya kukamatwa Putin).
Pia hakumuuliza kuhusu mauaji ya wapinzani wa kisiasa au kiongozi wa upinzani aliyefungwa jela Alexei Navalny.















