Mtoto wa Ukraine aliyetoweka apatikana kwa mshirika wa Putin

Na Hilary Andersson

BBC Panorama

f

Chanzo cha picha, IGOR KASTYUKEVICH

Maelezo ya picha, Mmoja wa watoto 48 waliofurushwa katika Makao ya Watoto ya Mkoa wa Kherson mnamo 2022

Mshirika mkuu wa kisiasa wa Vladimir Putin amemchukua mtoto aliyetekwa kutoka kwa nyumba ya watoto ya Ukraine, kulingana na hati zilizofichuliwa na BBC Panorama.

Sergey Mironov, kiongozi mwenye umri wa miaka 70 wa chama cha kisiasa cha Urusi, ametajwa kwenye rekodi ya kuasili ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka miwili ambaye alichukuliwa mwaka 2022 na mwanamke ambaye sasa ameolewa na Mironov.

Rekodi zinaonyesha utambulisho wa msichana huyo ulibadilishwa nchini Urusi.

Bw Mironov hajajibu ombi la BBC kutoa maoni kuhusu hilo.

Mtoto huyo, ambaye awali aliitwa Margarita, alikuwa mmoja wa watoto 48 waliotoweka katika Makao ya Watoto ya Mkoa wa Kherson wakati majeshi ya Urusi yalipoudhibiti mji huo.

Ni miongoni mwa watoto wapatao 20,000 ambao, kulingana na serikali ya Ukraine, wamechukuliwa na vikosi vya Urusi tangu kuanza kwa uvamizi kamili mnamo 2022.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mapema mwaka huu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin na Kamishna wake wa Haki za Watoto, Maria Lvova-Belova, kwa madai ya kuwawahamisha watoto wa Ukraine kinyume cha sheria na kuwapeleka katika eneo linalodhibitiwa na Urusi, kwa nia ya kuwaondoa kabisa kutoka nchi yao ya asili.

Serikali ya Urusi inasema inawahamisha watoto wa Ukraine ili kuwapa ulinzi dhidi ya vita.

BBC ilishirikiana na mpelelezi wa haki za binadamu wa Ukraine Victoria Novikova ili kujua kilichomsibu Margarita na watoto wengine. Bi Novikova ametayarisha ripoti ya ushahidi mpya kwa ajili ya ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine, ambayo ataikabidhi kwa ICC.

Siri inayomzunguka Margarita ilianza wakati mwanamke aliyevalia vazi la rangi ya kijivu alipofika katika hospitali ya watoto ya Kherson, ambapo mtoto huyo wa miezi 10 alikuwa akitibiwa mnamo Agosti 2022.

Margarita ndiye mtoto mdogo zaidi katika nyumba ya watoto ya eneo hilo, ambayo iliwatunza watoto waliokuwa na matatizo ya kiafya, au ambao wazazi wao walikuwa wamepoteza haki ya kuwalea au wamefariki.

Mama yake Margarita alikuwa ameacha kumlea muda mfupi baada ya kuzaliwa, na baba yake hakujulikana aliko.

Dk Nataliya Lyutikova, ambaye aliongoza matibabu ya watoto wachanga katika hospitali hiyo, alisema alikuwa mtoto mwenye tabasamu ambaye alipenda kuwakumbatia watu.

g
Maelezo ya picha, Margarita alikuwa na miezi 10 tu alipochukuliwa kutoka katika nyumba ya malezi

Mwanamke aliyemchukua alijitambulisha kama "mkuu wa maswala ya watoto kutoka Moscow", Dk Lyutikova anakumbuka.

Kherson - sasa imerejea chini ya udhibiti wa Ukraine- wakati huo ilikuwa imekuwa chini ya udhibiti wa Urusi kwa miezi sita.

Mara tu baada ya mwanamke huyo kuondoka, Dk Lyutikova anasema alipokea simu mara kwa mara kutoka kwa afisa aliyeteuliwa na Urusi, ambaye hivi karibuni alikuwa amepewa jukumu la kusimamia nyumba ya watoto. Afisa huyo alidai Margarita arudishwe nyumbani kwao mara moja.

Ndani ya wiki moja, Margarita aliruhusiwa kutoka hospitalini. Asubuhi iliyofuata, wafanyakazi katika nyumba ya watoto waliombwa wamtayarishe kwa ajili ya safari.

"Tuliogopa, kila mtu aliogopa," Lyubov Sayko, muuguzi wa nyumba ya watoto alisema.

Alieleza jinsi wanaume Warusi - baadhi wakiwa wamevaa mavazi ya kijeshi yaliyoficha nyuso zao mmoja wao akiwa amevaa miwani myeusi na aliyeshikilia mkoba - walivyofika kumchukua msichana huyo.

"Ilikuwa kama filamu," alisema.

Lakini huu ulikuwa ni mwanzo tu.

g

Chanzo cha picha, GOR KASTYUKEVICH

Maelezo ya picha, Mbunge wa Urusi Igor Kastyukevich (kushoto) alipanga usafirisha wa watoto kwenye basi

Wiki saba baadaye, Igor Kastyukevich, mbunge wa Urusi aliyevalia mavazi ya kijeshi, alifika nyumbani na, pamoja na maafisa wengine, wakaanza kuandaa uhamisho wa watoto waliobaki, akiwemo kaka wa kambo wa Margarita, Maxym.

"Walizichukua kutoka mikononi mwetu na kwenda nazo nje," Bi Sayko alisema.

Kanda za video - zilizowekwa kwenye Telegram na Bw Kastyukevich - zilionyesha watoto, wakibebwa ndani ya mabasi na magari ya kubebea wagonjwa, na kutoroshwa.

"Watoto hao watapelekwa katika mazingira salama huko Crimea," Bw Kastyukevich alisema, huku watoto hao wakipakiwa. Crimea ilitwaliwa na Urusi kutoka chini ya mamlaka ya Ukraine mwaka wa 2014. Bw Kastyukevich alionyesha tukio hilo kama tukio la kibinadamu.

Treni ya usiku wa manane

Kwa muda wa miezi mitano, BBC imekuwa ikijaribu kuwatafuta Margarita na watoto wengine 47, kwa ushirikiano na Victoria Novikova.

Kupata watoto waliopotea katika eneo kubwa kama Urusi, nchi yenye zaidi ya kilomita za mraba milioni 17 (maili za mraba milioni 6.6), si kazi rahisi.

Kazi ya kwanza ilikuwa ni kumtambua mwanamke wa ajabu aliyekuwa amevalia gauni la rangi ya zambarau iliyopauka katika ambaye alimtembelea kwa mara ya kwanza Margarita katika hospitali Agosti iliyopita.

h
Maelezo ya picha, "Mwanamke mwenye gauni la zambarau iliyopauka" (katikati) baadaye alitambuliwa kama Inna Varlamova

Victoria aligundua hati ya Kirusi ambayo iliidhinisha uhamisho wa Margarita katika hospitali ya Moscow kwa ajili ya vipimo vya afya. Mwanamke aliitwa kwenye hati: Inna Varlamova. Utafutaji kwenye mitandao ya kijamii ulithibitisha kuwa ndiye aliyekuwa mwanamke wa ajabu aliyevalia gauni la zambarau iliyopauka.

Kisha tukamwonyesha Dk Lyutikova picha ya Bi Varlamova na akamtambulisha kama mwanamke yule yule aliyemtembelea Margarita kwenye wodi ya watoto.

Baada ya upekuzi zaidi, tuligundua kuwa Bi Varlamova anafanya kazi katika bunge la Urusi, ingawa haijabainika katika nafasi gani, na anamiliki mali huko Podolsk, karibu na Moscow.

Tulikuwa tumetatua sehemu ya fumbo. Lakini maswali yalibaki.

"Margarita hakuhitaji uchunguzi maalum," Dk Lyutikova alisema, akizungumzia usiku ambao mtoto alichukuliwa. "Kwanini umpeleke mtoto mdogo sana?"

BBC Panorama inachunguza kilichotokea kwa zaidi ya watoto 40 waliochukuliwa na vikosi vya Urusi kutoka kwenye nyumba ya watoto huko Kherson.

Watayarishaji wa filamu, wakifanya kazi na waandishi wa habari nchini Ukraine, walifichua vyeti vya kuzaliwa ghushi, kuidhinishwa kwa siri na msururu wa ushahidi unaowaongoza hadi kwenye bunge la Urusi.

Ikiwa na jina la Inna Varlamova mkononi Panorama ilipata rekodi za treni kutoka vyanzo vya ndani ya Urusi. Rekodi hizo zilionyesha kwamba alifika katika eneo hilo la Ukraine lililokaliwa na Urusi siku ileile ambayo mashahidi wanasema Margarita alichukuliwa kutoka kwenye nyumba malezi ya watoto.

Baadaye usiku huo, saa sita na dakika 20, Bi Varlamova alichukua gari moshi kurudi Moscow, akiwa na tikiti za ziada za kurudi.

Lakini ni kwa nini?

Chanzo cha habari cha Urusi kiliwasilisha habari nyingine muhimu: hati inayoonyesha Bi Varlamova alikuwa amefunga ndoa hivi karibuni na kiongozi wa chama cha siasa Sergey Mironov.

w

Chanzo cha picha, A JUST RUSSIA

Maelezo ya picha, Mpelelezi wa haki za binadamu Victoria Novikova amekuwa akifanya kazi na BBC kugundua kilichowapata watoto hao

Bw Mironov, askari wa zamani wa kikosi cha miavuli, ni kiongozi wa Chama cha Just Russia - sehemu ya upinzani ulioidhinishwa na serikali ya Urusi - na anamuunga mkono Rais Putin. Amewekewa vikwazo na nchi kadhaa za Magharibi, zikiwemo Uingereza na Muungano wa Ulaya (EU).

Kisha ukaja ufunuo muhimu.

Tuliipata rekodi ya kuzaliwa, iliyoundwa Disemba iliyopita, ya msichana wa miezi 14 anayeitwa "Marina". Wazazi wa mtoto huyo waliitwa Inna Varlamova na Sergey Mironov. Rekodi hiyo hatahivyo haikuwa ya kawaida kwani haikuonyesha asili ya kuzaliwa kwa mtoto.

Siku ya kuzaliwa ya "Marina" iliorodheshwa kama 31 Oktoba 2021 - siku hiyo halisi ya kuzaliwa ya mtoto Margarita. "Nilipoona siku ya kuzaliwa ya Marina ni sawa na ya Margarita, niligundua kuwa ulikuwa ni 'mchezo wa bingo'," Victoria alisema.

Kupitia vyanzo vya Urusi visivyojulikana, timu yetu sasa imepewa rekodi ya kuasili ya Margarita. Margarita Prokopenko amepewa jina la Marina Mironova, ambalo ni la baba yake mlezi Sergey Mironov. Mahali pa kuzaliwa kwake pameorodheshwa kama Podolsk.

Serikali ya Urusi ilisema haina ufahamu wowote kuhusu kesi ya Margarita na haikuweza kutoa maoni yoyote.

Sheria za kuasili

Mkataba wa Geneva, ambao unafafanua kile kinachojumuisha uhalifu wa kivita, unasema ni kinyume cha sheria kuwahamisha raia wakati wa vita, isipokuwa pale inapokuwa ni muhimu kwa usalama au sababu za lazima za kijeshi na ni za muda. Mkataba pia unapiga marufuku kubadilisha hali halisi ya familia ya mtoto.

g

Chanzo cha picha, ROBIN BARNWEL

Maelezo ya picha, Mpelelezi wa haki za binadamu Victoria Novikova amekuwa akifanya kazi na BBC kugundua kilichowapata watoto hao

Wakati Rais Putin na kamishna wake wa masuala ya watoto Maria Lvova-Belova walipofunguliwa mashtaka na ICC mapema mwaka huu, mahakama hiyo ilidai kuwa kuhamishwa kinyume cha sheria kwa mamia ya watoto wa Ukraine kutoka katika vituo vya kulelea watoto yatima na nyumba za malezi ya watoto kulifanyika kwa nia ya "kuwaondoa kabisa watoto hao kutoka katika nchi yao ya asili."

Hii ilifuatia uamuzi wa Rais Putin wa kutoa amri ambazo zilikuwa na athari ya kurahisishia Warusi kuasili watoto wa Ukraine.

Bi Lvova-Belova amesema kuwa Urusi inawapeleka watoto katika malezi pekee."Hatuna watoto wa kuasili," alisema mwezi uliopita. "Huu ni ukweli muhimu sana kwa sababu kuasili kunamaanisha kwamba mtoto anakuwa mzaliwa kamili. Unaweza kubadilisha jina lake la mwisho, jina la kwanza, patronymic [jina la kati], unaweza kubadilisha mahali pa kuzaliwa."

Lakini katika majibu yake kwa uchunguzi wetu, serikali ya Urusi ilisema haikuwa "sahihi" kusema kwamba Urusi haiidhinishi kupitishwa kwa watoto wa Kiukreni kutoka kwa mikoa iliyotangazwa hivi karibuni ya Urusi. Ilisema sasa inachukulia sehemu kubwa za Ukraine kuwa za Urusi na watu wanaoishi huko ni raia wake, pamoja na watoto.

Mtoto mmoja alirejeshwa

Tumewaandikia Sergey Mironov na Inna Varlamova, tukiuliza Margarita yuko wapi sasa, lakini hawajajibu.

Takriban watoto wengine wote waliochukuliwa kutoka nyumba za malezi wanaaminika kubaki mikononi mwa Warusi. Takriban 17 wako Crimea, kulingana na mamlaka ya Urusi. Wote wana jamaa nchini Ukraine, Victoria Novikova anasema.

Ukraine inasema imewatambua watoto 19,546 ambao wamepelekwa Urusi. Inadai kuwa ni chini ya watoto 400 pekee wamerudi. Urusi inapinga takwimu hizi.

Moscow inasema itawaunganisha watoto na familia au marafiki ikiwa dai halali litatolewa. Lakini wazazi wengi hawajui ni wapi watoto wao wako, na mchakato wa kuwapata ni ngumu.

Tunamfahamu mtoto mmoja tu kutoka Makao ya Watoto ya Kherson ambaye amerejeshwa Ukraine.

Mwezi uliopita, Viktor Puzik mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye alikuwa katika kituo hicho akisubiri upasuaji kwa ajili ya hali ya afya, alirejeshwa kutoka Crimea na mama yake, Olha.

Alisema alikuwa na uchungu sana alipokuwa akisubiri kujua iwapo alikuwa salama:

"Niliendelea kuwaza, yuko wapi, yukoje? Yupo hai au? Kila kitu kilinipitia akilini."

Victoria anataka kuwatafuta watoto wengine wote waliotoweka kutoka katika makao ya watoto ya Kherson lakini anahofia kuwa hivi karibuni wanaweza kuwa wasioweza kutambulika.

"Wakati hauko upande wetu," anasema. "Tatizo ni [mamlaka ya Urusi] kujaribu na kufuta utambulisho wa watoto wanapotoa vyeti vya kuzaliwa vya Kirusi au hata pasi."

Kwa sasa, hajakata tamaa ya kumrudisha Margarita Ukraine.

Bado hajapata jamaa ambao wanaweza kumchukua Margarita kwa hivyo yeye mwenyewe ameteuliwa kuwa mlezi wa kisheria wa msichana mdogo na serikali ya Ukraine, na ana mipango ya kutuma maombi kwa mamlaka ya Urusi kumrudisha.

"Ulimwengu unahitaji kujua kuhusu uwepo kwa Margarita. Walitaka kumfuta. Tunahitaji kumrudisha."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah