Mzozo wa Ukraine: 'Sikuruhusiwa kusema kwaheri'

Sasha akiwa amevalia shati la kitamaduni la Kiukraine

Chanzo cha picha, Orphans Feeding Foundation

Maelezo ya picha, Sasha akiwa amevalia shati la kitamaduni la Kiukraine

Ukraine inasema karibu watoto 19,500 wamepelekwa Urusi au eneo linalokaliwa na Urusi tangu nchi hiyo ilipoanzisha uvamizi dhidi yake.

Ni watoto 400 pekee ndio wamefanikiwa kurudi nyumbani kufikia sasa kwani ni safari ya hatari.

Sasha, Veronika, Ilya, Maxim, Kira na Ivan ni kundi la watoto sita walionusurika.

Wamesafiri hadi Uholanzi kukutana na wanasiasa wa Uholanzi, kama sehemu ya kampeni ya serikali ya Ukraine ya kuongeza ufahamu barani Ulaya.

Watoto hao sita wanasimama na waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi

Chanzo cha picha, Ukraine Ombudsman Office

Maelezo ya picha, Ivan, Veronika, Kira, Ilya, Maxim, Sasha (kutoka kushoto kwenda kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Hanke Bruins Slot katikati

Sasha alimuona mama yake mara ya mwisho mwaka mmoja na nusu uliopita. "Warusi walisema mama yangu hakunitaka," anasema.

Ilikuwa majira ya vuli ya mwaka 2022. Urusi ilikuwa imevamia Ukraine na ilikuwa ikishambulia kwa makombora mji wa bandari Mariupol kusini mwa nchi.

Sasha na mama yake Snizhana walijua hawana budi kuondoka lakini njia pekee ya kutoka ilikuwa kupitia kituo cha ukaguzi cha jeshi la Urusi.

"Tuliwekwa kwenye lori kama wanyama na kupelekwa kwenye kambi ya ukaguzi," anasema Sasha, ambaye sasa ana umri wa miaka 12.

Wanajeshi wa Urusi na wafuasi wa eneo hilo walikagua kila mtu anayeondoka.

Ukraine na Umoja wa Mataifa zimeishutumu Urusi kwa kuwahamisha watu kwa nguvu pamoja na kuwahoji vikali katika kambi hizi.

Mama yake Sasha alichukuliwa kuhojiwa.

"Nilimsubiru mama yangu kwa saa kadhaa. Walimrudisha lakini sikuruhusiwa kumuaga."

Sasha, ambaye jicho lake lilikuwa limejeruhiwa katika shambulio hilo la makombora, alipelekwa katika hospitali ya Donetsk mashariki mwa Ukraine, ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa waasi wanaounga mkono Urusi tangu 2014.

tt

Chanzo cha picha, Orphans Feeding Foundation

Maelezo ya picha, Ilya, ambaye sasa ana umri wa miaka 11, anataka masaibu ya watoto wa Ukraine walionaswa nchini Urusi kugonga vichwa vya habari

Ilya pia ni sehemu ya kikundi kinachozuru The Hague. Alipokuwa na umri wa miaka tisa, mama yake alifaki mikononi mwake huko Mariupol.

"Mama yangu aliuawa na mimi nikatekwa, wanajeshi wa Urusi," anasema, sauti yake imetulia lakini macho yake yamejaa maumivu.

Alifanyiwa upasuaji kwenye mguu wake uliojeruhiwa na hakuruhusiwa kupiga simu kwa familia yake.

Lakini bibi yake alimwona kwenye video iliyorekodiwa na mwanajeshi wa Urusi na kumuokoa kutoka Donetsk.

Ilya, sasa 11, anataka kuongeza ufahamu.

"Ningependa kupaza sauti kuhusu kile kilichotokea huko, kilichowakumbawatoto. Kuna vita nchini Ukraine," anasema.

Sasha pia ana hamu kubwa.

"Jina la mama yangu ni Kozlova Snizhana. Ninajaribu kumtafuta," anawaambia wanasiasa wote waliopo.

Uamuzi mbaya

Ogla
Maelezo ya picha, Olga anajuta kuruhusu mwanawe kupelekwa kwenye kambi nchini Urusi wakati wa mashambulizi makali ya makombora

Moscow inakanusha kuwateka nyara watoto na inasema walichukuliwa kwa usalama wao wenyewe.

Machafuko ya vita yalimaanisha wazazi wakabiliane na maamuzi mabaya.

Olga Usyk anatoka Balaklia, jiji linalokaliwa na Urusi mashariki mwa Ukraine.

Kulikuwa na mapigano makali na mnamo Agosti 2022, aliamua kumtuma mwanawe Bogdan kwenye kambi huko Urusi kwa wiki chache.

"Hatua ya kumpeleka Urusi ilikuwa kosa kubwa zaidi maishani mwangu," anasema Olga.

Jeshi la Ukraine lilimkomboa Balaklia na Warusi walikataa kuwarudisha watoto.

"Nilihuzunika sana. Niliikumbuka sana familia yangu," anasema Bogdan.

Alihofia huenda akapelekwa kwenye kituo cha watoto yatima huko Urusi na kumsihi mama yake amrudishe nyumbani.

Ni pale tu alipotoa mamlaka ya wakili kwa mama mwingine aliyekuwa akisafiri kwenda kumwokoa mtoto wake mwenyewe ambapo 'mgeni' huyu aliweza kurudi na Bogdan -- na kuhitimisha masaibu ya miezi saba.

tt
Maelezo ya picha, Bogdan na mama yake Olga wakiwa nyumbani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Familia haziwezi kuvuka moja kwa moja kutoka Ukrainia hadi Urusi au eneo linalokaliwa na Warusi ili kuwaokoa watoto wao.

Lazima zipitie majimbo ya Baltic, Poland, Belarus au hata Uturuki. Ni safari ya maelfu ya kilomita kwa gharama kubwa.

Wanawake wengi hufanya hivyo kwani wanaume walio katika umri wa kupigana hawaruhusiwi kuondoka Ukraine.

"Operesheni zingine huchukua miezi kadhaa ya maandalizi ya kumrejesha nyumbani mtoto mmoja," anasema Myroslava Kharchenko, wakili wa Save Ukraine, shirika lisilo la kiserikali, ambalo husaidia kuandaa uokoaji.

"Mama au wawakilishi wengine wanaweza kutumia kati ya siku 10-12 barabarani. FSB (huduma ya Kijasusi ya Urusi) huwahoji akina mama kwenye mpaka. Mama mmoja alihojiwa kwa siku tatu, mwingine kwa saa 13."

Shirika hilo limesaidia kuokoa watoto 118 kutoka Urusi na 120 kutoka maeneo yanayokaliwa na Warusi nchini Ukraine.

Ni jitihada za siri ambapo ufichuzi wa njia moja ya uokoaji unaweza kuwa hatari kwa wengine.

“Safari ya kuwarudisha watoto nyumbani ni hatari sana na inatisha lakini akina mama na mabibi wanaelewa wanachopigania,” asema Bi Kharchenko.

Ukaidi wa Urusi

Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema taarifa za vyombo vya habari kuhusu watoto 'waliotekwa nyara' wa Ukraine "zimetiwa chumvi".

"Hakuna matatizo ya kuwarudisha watoto kwa jamaa zao [nchini Ukraine]," alisema, katika matamshi yaliyonukuliwa na shirika la habari la Urusi Tass mnamo Julai 2023.

Lakini makumi ya familia na watoto wameiambia BBC jinsi ilivyo ngumu.

Hivi majuzi Moscow ilifanya iwe rahisi kwa watoto wa Kiukrene nchini Urusi kupata pasi za kusafiria za Urusi - jambo ambalo linafanya iwe vigumu zaidi kuwarudisha nyumbani.

"Wanataka kutenganisha watoto na familia zao halisi, kuwafanya watoto hawa kuwa Warusi, kuwaficha watoto hawa na kuwahamishia katika kabila lingine," anasema Daria Gerasymchuk, mshauri wa rais wa Ukrainie wa Haki za Watoto.

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua haya kama mauaji ya kimbari."

tt

Chanzo cha picha, Ukraine Ombudsman Office

Mnamo Machi 2023, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rais Putin na Kamishna wa Haki za Watoto wa Urusi, Maria Lvova-Belova, ikiwashutumu kwa kuwondoa kwa nguvu mamia ya watoto kutoka Ukraine.

Watoto hao sita walisafiri hadi Uholanzi kama sehemu ya kampeni ya 'Bring Kids Back UA' ambayo inaungwa mkono na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

"Inavunja moyo kusikia hadithi zao. Ni unyama kile ambacho Warusi wamewafanyia," anasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Hanke Bruins Slot.

"Nadhani watoto wana nguvu za ajabu, wana ustahimilivu, na ujasiri kwa kusimulia hadithi zao. Ni muhimu sana kwamba watu wengi wasikie hadithi zao ili tukomeshe hili."