Raia wa Ukraine 'wanavyotoweka' kutoka magereza ya Urusi

Na Olga Prosvirova & Zhanna Bezpyatchuk

BBC World Service

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mykyta alitoweka baada ya kukamatwa na wanajeshi wa Urusi, kwa mujibu wa familia yake, ambao wanasema hakufanya kosa lolote.

Volodymyr Buzynov amekuwa akimtafuta kaka yake Mykyta kwa karibu miaka miwili. Mykyta ni moja ya maelfu ya raia wa Ukraine wanaoshikiliwa katika magereza nchini Urusi na maeneo yaliyokaliwa kwa kupinga vita. Lakini kwa kuwa hawana mashtaka, uchunguzi rasmi, kesi, au tarehe ya kukuachiliwa kwao ni siri , na tofauti na wafungwa wa vita, hakuna utaratibu rasmi wa kuwawezesha kuwa huru.

Tahadhari: Taarifa hii hii ina maelezo ya mateso

Wakati Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022, ndugu wa Buzynov, mama yao, na mpenzi wa Mykyta walikimbilia katika mji wa nyumbani kwao wa Chernihiv kaskazini mwa nchi ili kuepuka mgogoro. Walikwenda katika kijiji cha Mykhailo-Kotsiubynske, lakini mapema mwezi Machi, wanajeshi wa Urusi walifika huko pia. "Tumekuja kuwakomboa kutoka kwa serikali yako. Putin ni mtu wa ajabu," wanajeshi hao walisema.

Volodymyr anasema wanajeshi hao walifanya upekuzi katika kijiji hicho, wakawanyang'anya simu na kuituhumu familia yake kwa kushirikiana na jeshi la Urusi - jambo ambalo wote wanalikana. Kisha, Volodymr anasema, askari walianzisha kile kilichosikika kama mauaji bandia.

"Walimchukua kaka yangu Mykyta na wengine nyuma ya miti na kuwaambia wajipange karibu na ukuta, huku wakipiga kelele: 'Jitayarishe! Lengo!' Kisha wakamchukua mpenzi wa Mykyta Kateryna, na kumwambia apige magoti karibu naye. Wakilenga bunduki kichwani mwake, walimwambia kaka yangu: 'Ikiwa hukiri, tutampiga risasi.'"

Volodymyr anasema hiyo ilikuwa mara ya mwisho kumuona Mykyta. "Huenda alikiri kumuokoa mpenzi wake kwa sababu walimruhusu aende. Walituambia: "Alikubali kila kitu. Anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa serikali ya Ukraine, kufikia Novemba 2023 kulikuwa na Waukraine 4,337 waliokamatwa na Urusi. Wengi wao walikuwa wanajeshi lakini 763 walikuwa ni raia. Hata hivyo, hakuna orodha rasmi ya majina yao na mamlaka ya Ukraine hutegemea data kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu.

Shirika la Msalaba Mwekundu haliwezi kuyafikia kila wakati maeneo ambayo Waukraine wanashikiliwa nchini Urusi, isipokuwa katika maeneo yaliyokaliwa ambapo vituo visivyo rasmi vya kizuizini vinaweza kujumuisha vyumba vya chini vya hoteli na majengo yaliyoachwa. Kamishna wa Haki za Binadamu wa Ukraine Dmytro Lubinets anasema idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi, na idadi ya raia waliotoweka inakadiriwa kuwa 25,000.

BBC imeitaka wizara ya ulinzi ya Urusi kufichua ni raia wangapi wa Ukraine wanaozuiliwa na wanashikiliwa wapi lakini hatujapata jibu.

Chini ya sheria ya Urusi, mtu anaweza kuzuiliwa kwa saa 48 tu bila amri ya mahakama na rekodi lazima kuhifadhiwa. Mwaka jana Rais Putin aliongeza muda wa siku 30 katika maeneo yaliyokaliwa na Ukraine kwa makosa makubwa au ukiukaji wa marufuku ya wakati wa vita au vikwazo.

Lakini mara nyingi muda, mahali na sababu za kuwekwa kizuizini hazirekodiwi, hakuna kesi za uhalifu au utawala zinazofunguliwa, na hakuna uchunguzi unaofanywa, kulingana na nyaraka za mahakama zilizopitiwa na BBC.

Anastasia Panteleyeva kutoka Shirika la Vyombo vya Habari vya Haki za Binadamu (MIHR) anasema Urusi inahalalisha kukamatwa kwa raia wa Ukraine chini ya muda mrefu wa "kupinga operesheni maalum ya kijeshi".

"Mtu anaweza kukamatwa kwasababu tu madirisha katika nyumba yake yanakaribiana na eneo lenye umuhimu kwa jeshi la Urusi. Na kama askari watapigwa risasi, mtu anayeishi karibu analaumiwa," anaeleza.

g
Maelezo ya picha, Wafungwa wa Ukraine wameiambia BBC kuwa wameshuhudia matukio ya kunyongwa kwa watu katika mahabusu za Urusi

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema kuwa raia wa Ukraine waliotekwa "wanashikiliwa kulingana na Mkataba wa Geneva juu ya matibabu ya wafungwa wa vita".

Mkataba wa Geneva unapiga marufuku kuwateka watu lakini hausemi chochote kuhusu kuwafunga raia, ni wanajeshi tu.

Wanasema raia wanaweza tu kuwekwa kizuizini "kwa mujibu wa sheria za maeneo ya Ukraine yaliyokaliwa kimabavu na Urusi " na kwa dhamana ya mchakato wa mahakama.

Wakili Polina Murygina, ambaye anawasaidia wafungwa kupitia mradi wake, Every Human Being anasema: "Mbali na kumtoa, hata kumtafuta mtua aliyeshikiliwa na Urusi ni vigumu sana katika mfumo uliowekwa. hata, ni bora kama wanafikiri wewe ni mhalifu."

Mtu anaposhtakiwa huonekana katika mfumo na ana haki au kama ni wafungwa wa vita, anaweza kubadilishwa. Lakini raia waliokamatwa wanaishia kizuizini bila ya ulinzi, mashtaka, au kesi.

Kumfuatilia Mykyta nchini Urusi

Wakiwa na matamanio ya kumfuatilia Mykyta chini, marafiki na jamaa zake walianza kutumia huduma ya barua ya magereza, ambayo hukuruhusu kutuma ujumbe kwa baadhi ya vyumba vya adhabu na vitengo vya kutengwa kwa uchunguzi ndani ya Urusi.

Hatimaye walipokea jibu kuthibitisha kuwa alikuwa akizuiliwa katika kituo cha kizuizini cha kabla ya kesi kinachoitwa SIZO-3 huko Belgorod, karibu na mpaka wa Urusi. Lakini wakati mwanasheria alipokwenda kutembelea, gereza hilo aliambiwa asingepewa jibu lolote kumhusu.

Wakili mwingine, Leonid Solovyov, anasema hili ni tukio la kawaida: "Mara nyingi, mimi hufika na wananiambia mtu hayupo. Ama hawataniruhusu kuingia, au mtu huyo amehamishwa. Huwezi kwenda huko na kutarajia kuwa na uwezo wa kuangalia mahabusu zote. Lazima utegemee jibu unalopata mlangoni au, ukibahatika unaweza kupata jibu kutoka kwa ofisi ya mkuu wa gereza."

BBC pia ilijaribu kumfuatilia Mykyta. Tuliandika kwa SIZO-3, kitengo cha Penal Colony 4 ambacho pia kiko katika mkoa wa Belgorod, na taasisi zingine ambapo wanaharakati wa haki za binadamu wanaamini wafungwa wa Kiukreni wanashikiliwa.

Taasisi nyingi zilitujibu zikisema hazikuwa na mfungwa kama huyo. Hata hivyo, SIZO-3 ilisema ujumbe huo ulikuwa "umeweka wazi udhibiti na ulikabidhiwa kwa afisa anayehusika" - hii inapaswa kumaanisha Mykyta alikuwa huko, lakini siku moja baadaye tulipokea jibu sawa na hilo kutoka kwa Penal Colony 4.

Wakati msako wa muda mrefu na wa kukatisha tamaa kwa Mykyta ukiendelea, BBC imeweza kuzungumza na wafungwa wa zamani. Mara nyingi hadithi zao huchora picha mbaya, huku mmoja wao mmoja akisema Waukraine katika magereza ya Urusi wanachukuliwa "kama wanadamu wenye hadhi ya chini".

f
Maelezo ya picha, Anton Lomakin anasema alipigwa na kudhalilishwa katika utumwa wa Urusi

Afisa wa polisi katika jimbo la Kherson Anton Lomakin, hakuweza kuondoka wakati uvamizi wa Urusi ulipoanza kwa hivyo alijificha. Kisha katika majira ya joto ya 2022 pia alitoweka na familia yake haikuweza kumpata.

Katika kisa cha Anton ilisema alikuwa amekusanya taarifa ambazo alipeleka kwa jeshi la Ukraine. Anasema, baada ya kusalitiwa na mwenzake aliyekuwa akimletea vifaa, alikamatwa na jeshi la Urusi na kupelekwa katika kituo cha muda cha mahabusu cha Kherson.

"Wakati wa safari walinifunga kwa vyuma kwenye miguu yangu na sehemu nyingine za mwili wangu. Walinitesa na kunipeleka kwenye shimo chini. Walinipigisha magoti na kuniambia niombe.

"Walipakia bunduki zao na kufyatua risasi kwenye sikio langu la kushoto. Kulikuwa na michubuko mitatu au minne. Kisha simu ya mkononi ikalia, wakaiweka kwenye kipaza sauti na mtu mwingine akasema asinipige risasi."

Anton alipofika kituoni anasema alihojiwa, kupigwa, kutishwa, na kumwagiwa maji baridi. Maelezo yake yanafanana na ushuhuda wa wafungwa wengine uliotolewa katika taasisi hiyo wakati mji wa Kherson ulipokaliwa na vikosi vya Urusi.

"Wakati mmoja, waliniambia niinue miguu yangu kwa visigino vyangu juu. Nilikataa. Waliweka bunduki kwenye sehemu zangu za siri na kuniambia ni chague. Kwa kweli, nilichagua kuinua miguu yangu, " Anton anasema.

"Walichukua mijeredi miwili ya plastiki na kunipiga visigino kwa muda mrefu. Wakati wowote niliposhusha miguu yangu, nililazimishwa kuiinua tenavinginevyo ningepigwa kichwani na mgongoni," anakumbuka.

BBC imeiuliza Wizara ya Ulinzi ya Urusi kuhusu kisa cha Anton na inasubiri majibu. Urusi haitambui kuwashikilia raia kama mateka na hapo awali ilikanusha tuhuma za umashambulizi au uhalifu dhidi yao.

Anton anasema alikuwa katika mahabusu moja na wanaume wengine saba: mmoja alikuwa afisa wa zamani wa polisi wa Ukraine, na mwingine aliishi katikati ya Kherson, karibu na mahala ambapo kulikuwa na jengo la jeshi la Urusi . Wote wawili wanatuhumiwa kuwa maafisa wa ujasusi wa Ukraine. Wafungwa wengine hawakuweza kueleza ni kwa nini walikuwa wamefungwa.

Anton alihamishwa mara mbili na familia yake iliweza kumpata kwa msaada wa rafiki yake ambaye alikuwa na pasipoti ya Urusi.

Hatimaye aliachiliwa baada ya siku 104, bila ya kuwa na nyaraka.

g

Chanzo cha picha, Suspilne/Taras Ibragimov/BBC

Maelezo ya picha, Anton Lomakin asema picha hii inaonyesha hali katika mahabusu alikokuwa akishikiliwa.

Polisi wa Ukraine na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine wanachukulia kukamatwa kwa raia kama uhalifu wa kivita na huhusika katika kuwatafuta watu waliopotea au kutekwa.

Irina Didenko kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka anasema kuwa "90% ya wale waliokamatwa wanakabiliwa na mateso".

Katika sheria za kimataifa, hakuna utaratibu maalum wa kuwakomboa raia kutoka maeneo walikotekwa. Mkataba wa Geneva unasema kwamba mpiganaji anaweza tu kubadilishwa kwa mpiganaji - unaweza kumwachia raia, lakini sio kwa kubadilishana na mtu ambaye ni askari.

"Kwa kweli, njia bora ya kuwaachilia huru na kuwarudisha mateka raia inaweza kuwa kupitia taifa la tatu," anasema Didenko. Nchi za Mashariki ya Kati tayari zimejadiliana kubadilishana wafungwa wa vita, kurudi kwa watoto na raia waliofukuzwa na kuachiliwa huru kwa wageni kutoka mahabsu za Urusi.

Linapokuja suala la Umoja wa Mataifa (UN), wanaharakati wa haki za binadamu wanasema mifumo yake imepitwa na wakati, wakisema - nyaraka za Umoja wa Mataifa hazitambui aina hii ya "mfungwa".

Na kwa watu kama Volodymyr ambaye ana ndoto ya kuungana tena na kaka yake Mykyta tena, matumaini yanafifia haraka. "Hakuna mahali ambapo hatujaweza kwenda," alisema.

"Kwa kuanzia, tulijidanganywa kwamba tungepata msaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa. Lakini yote tuliyoyapata kutoka kwao yalikuwa: 'tumepokea ombi, tumelisajiri.' Hatujawahi kufika mbali zaidi ya hapo."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi