Mmarekani anayeshikiliwa Urusi anahisi nchi yake 'imemtelekeza'

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Sarah Rainsford
- Nafasi, BBC
Miaka mitano iliyopita, Paul Whelan alisafiri kwenda Moscow kwa likizo ya wiki mbili lakini safari yake ikamalizikia katika kambi gereza huko Urusi. Mmarekani huyo huenda akatumia Krismasi nyingine kizuizini, maelfu ya maili kutoka nyumbani.
Serikali ya Marekani inasema amezuiliwa isivyo haki kwa tuhuma za ujasusi.
Katika mahojiano ya nadra kwa njia ya simu kutoka katika gereza, Paul Whelan aliiambia BBC anahisi "kutelekezwa" na nchi yake, ambayo ilibadilishana wafungwa wawili na Urusi mwaka uliopita.
Aliita uamuzi wa yeye kutobadilishwa ni "usaliti mkubwa."
Maoni ya Whelan yanakuja wakati mwandishi wa habari wa Marekani, Evan Gershkovich akijiandaa kwa mara ya kwanza kuupokea mwaka mpya akiwa jela kwa tuhuma sawa na za Whelan.
Gazeti lake la Wall Street Journal, na serikali ya Marekani - wote wanasema kesi ya Urusi dhidi yake ni ya uwongo. Mwandishi huyo wa habari, alikamatwa mwezi Machi akiwa katika majukumu yake.
Mwandishi mwingine wa habari, raia wa Marekani na Urusi, Alsu Kurmasheva, alizuiliwa mwezi Oktoba baada ya kusafiri kuiona familia yake. Anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela, kwa mashtaka ya kueneza "habari za uongo" kuhusu jeshi la Urusi.
Msemaji wa serikali ya Marekani ameiambia BBC - wametoa mapendekezo mengi kwa Urusi na wanajadili mara kwa mara kesi ya Whelan.
'Nimetelekezwa'

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Najua Marekani ina kila aina ya mapendekezo, lakini mapendekezo hayo sio Urusi inayoyataka. Kwa hiyo wanakwenda na kurudi. Tatizo ni kwamba, maisha yangu ndiyo yanaharibika wakati wao wanafanya wanakwenda na kurudi. Ni miaka mitano imepita."
Whelan anasema Urusi ilitaka kumrudisha kwa kubadilishana na mchuuzi wa silaha aliyepatikana na hatia, Viktor Bout. Lakini Donald Trump akiwa rais wa Marekani wakati huo "alisema hapana."
Miaka miwili baadaye, Viktor Bout alibadilishwa na nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani, Brittney Griner, ambaye alikiri kosa la kumiliki mikebe ya kuvutia bangi na mafuta ya bangi.
"Inatia mawazo sana kujua kwamba ningeweza kuwa nyumbani miaka iliyopita," aliniambia. "Inasikitisha sana kujua kwamba wamefanya makosa. Kwa hakika wameniacha hapa."
Whelan pia ana pasipoti za Uingereza, Ireland na Canada, na mabalozi wa nchi zote nne wamekuwa wakimtembelea.
Lakini nilipouliza Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza kuhusu juhudi za kumtoa, niliambiwa, "ubalozi unatoa usaidizi kwa raia wa Uingereza."
Ni kauli hiyo hiyo waliitoa miaka mitano iliyopita.
Mkasa wa Evan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haielezi kuhusu mazungumzo ya mapatano. Lakini msemaji wa serikali ya Marekani alielezea kuwa Waziri Blinken amejitolea kuhakikisha Whelan anaachiliwa.
Msemaji huyo amesema Urusi imekataa "mapendekezo kadhaa" lakini Marekani haitasitisha juhudi za kuwarudisha nyumbani raia wake.
Evan Gershkovich alikamatwa mwezi Machi, ni mara ya kwanza kwa mwandishi wa Magharibi kushtakiwa kwa ujasusi na Moscow tangu Vita Baridi.
"Evan si jasusi, ni mwandishi wa habari," anasema mwandishi wa Financial Times kutoka Moscow na rafiki wa Evan, Polina Ivanova.
Wawili hao walianza kuripoti kutoka Moscow kwa wakati mmoja. Polina anaelezea jioni ya kutisha Evan alipopoteza mawasiliano na gazeti lake wakati akiwa nje ya Moscow.
Kisha aliibuka kama mfungwa, akishutumiwa kwa ujasusi. "Ni shtaka la kuogofya kwa rafiki."
Polina na marafiki wengine hutumia muda wao mwingi kupitia barua za kuwaunga mkono zinazotumwa kutoka nje ya nchi. Kisha wanazitafsiri kwenda Kirusi ili ziweze kupitiwa na kupitishwa kwenye gereza ambalo Evan anazuiliwa na FSB.
Kabla ya kukamatwa kwake, Evan aliripoti kuhusu kubadilishana wafungwa wa Marekani na Urusi, Brittney Griner kwa Viktor Bout. Kabla ya hapo, Trevor Reed mwanajeshi wa zamani wa Marekani alibadilishwa na mlanguzi wa dawa za kulevya wa Urusi.
Masharti magumu ya Urusi

Paul Whelan aliniambia Moscow sasa inataka afisa wa shirika la kijasusi la FSB aliyehukumiwa - aachiwe kutoka Ujerumani kama sehemu ya kubadilishana.
Vadim Krasikov alipofikishwa mahakamani mjini Berlin, hakimu aliyaita mauaji aliyoyafanya katika bustani katikati mwa jiji - mchana kweupe - ni kitendo cha "ugaidi wa serikali." Muuaji huyo alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mwanasiasa wa Ujerumani Roderich Kiesewetter anasema, Washington ina usemi mkubwa mbele ya Berlin, kwani Ujerumani "inategemea sana" ujasusi wa Marekani - kwa kuwapa taarifa na ushauri".
Lakini Kiesewetter, mjumbe wa kamati ya bunge ya masuala ya kigeni, anapinga mpango wa Urusi: "Hatuwezi kutoa ishara kwa Urusi kwamba wanaweza kufanya uhalifu katika nchi nyingine na kisha, baada ya mazungumzo ya kidiplomasia ya miaka kadhaa, wakarudishiwa wauaji wao."
Wiki iliyopita, Vladimir Putin alisisitiza kwamba mpango wowote ambao Urusi itafanya kuwarudisha Wamarekani lazima "ukubalike pande zote."
Hilo linaweza kuwa ni dokezo kwamba mazungumzo yanaweza kufanyika. Au inaweza isiwe hivyo.
Hofu ya Whelan

"Sijui Kremlin inafikiria nini, najua rafiki yangu yuko jela, na hapaswi kuwa jela," Polina Ivanova aliniambia. "Anapaswa kuwa nyumbani na anapaswa kufanya kazi."
Whelan hutumia siku zake akishona sweta na kofia katika kiwanda cha magereza. Anasema maisha yake "yameharibika" tangu kukamatwa. Amepoteza uhuru wake, kazi yake, na nyumba yake, na hivi karibuni alishambuliwa na mfungwa mwingine.
Serikali ya Marekani inasema "hajasahaulika."
Lakini hofu yake kubwa ni kubadilishwa wafungwa na yeye kusahauliwa tena: "Nina wasiwasi sana. Kwa kila kesi, kesi yangu inaachwa nyuma. Wameniacha kwenye vumbi."
Ni Urusi ndiyo imemtia gerezani. Lakini Paul Whelan anasema anaitaka Marekani kufanya zaidi ili kumrudisha nyumbani.
"Ahadi zote zilizotolewa zimekuwa tupu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












