Kwanini ni vigumu kwa nchi za Ulaya kuachana na gesi ya Urusi?

Chanzo cha picha, VLADIMIR SMIRNOV/TASS
Umoja wa Ulaya unaagiza kiasi kikubwa cha gesi asilia (LNG) kutoka Urusi. Hayo yanajiri wakati umoja huo unapambana kuacha kufanya biashara na nchi iliyoanzisha vita nchini Ukraine.
Idhaa ya BBC ya Urusi inaelezea kwa nini sio rahisi kwa EU kupunguza ununuaji wa gesi ya Urusi wakati huu kukiwa na uhaba wa nishati hiyo.
Shirika la Global Witness linakadiria tangu kuanza kwa vita, uagizaji wa gesi asilia ya Urusi kwenda Ulaya bado ni mkubwa. Kuanzia Januari hadi Julai 2023, nchi za Ulaya zilinunua mita za ujazo milioni 22 kutoka Urusi. Kiasi cha uagizaji katika muda sawa na huo 2021, kilikuwa ni mita za ujazo milioni 15.
Kabla ya vita, Urusi ilikuwa muuzaji mkubwa zaidi wa gesi asilia barani Ulaya. Baada ya uvamizi wa Ukraine, Urusi imepunguza kwa kasi usambazaji wa gesi kwenda Uropa.
Mei 2022, usambazaji kupitia bomba la gesi la Yamal-Ulaya ulisimamishwa kabisa. Wakati huo huo, Urusi ilikuwa inapunguza mauzo ya nje kupitia bomba la Nord Stream. Septemba 2022, mlipuko uliopiga bomba hilo, ulipelekea usambazaji kusimamishwa.
Mwisho wa 2022, usafirishaji wa gesi ya Urusi kwenda Ulaya ulishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu kuanza kwa karne hii. Kupungua huko kumesababisha ukweli kwamba nchi za EU zinatafuta gesi kwingine.
Wanunuzi wakubwa wa gesi asili ya Urusi ulimwenguni baada ya China ni Uhispania na Ubelgiji. Katika miezi saba ya kwanza ya 2023, Uhispania ilifanya mauzo ya gesi kwa 18% ya jumla ya mauzo ya Urusi, na Ubelgiji 17%.
Waagizaji wengine wakuu ni pamoja na Ufaransa na Uholanzi, ambapo kupitia miundombinu ya nchi hizo, gesi ya Urusi inapelekwa katika nchi zingine za Ulaya.
Tume ya Ulaya sasa inatekeleza mpango wa REPowerEU, uliopitishwa Mei 2022 ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Lengo lake kuu ni kuondoa utegemezi wa Umoja wa Ulaya wa mafuta, gesi na makaa ya mawe ya Urusi.
EU inaamini rasilimali hizi ni kama "silaha ya kiuchumi na kisiasa." Hofu kuu ikiwa, Urusi chini ya shinikizo la vikwazo vya Ulaya, itakata ghafla usambazaji wake wa gesi kwa bara hilo.
Inatarajiwa kufikia 2027, hatua za REPowerEU zitasaidia Ulaya kuachana kabisa na Urusi. Kwa nini inaonekana mpango huu hautekelezeki kwa haraka?
Gesi asili kutoka Urusi

Chanzo cha picha, REUTERS/NACHO DOCE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sehemu kubwa ya gesi asili ya Urusi barani Ulaya inatoka katika kiwanda cha Yamal, kinachoendeshwa na serikali. Mwezi Septemba, Marekani iliweka vikwazo dhidi ya kiwanda hicho kinachozalisha gesi asilia
Zaidi ya tani milioni 16 za gesi asilia zilitumwa Ulaya 2022 - hii ni zaidi ya 75% ya kiasi cha uzalishaji wa kila mwaka wa biashara.
Miezi kadhaa baada ya kuanza vita huko Ukraine, kiasi cha uagizaji wa gesi asilia kutoka Urusi kilizidi kiwango cha mwaka 2020. Mfano, Machi (mita za ujazo milioni 1.987) na Novemba, 2022 (mita za ujazo milioni 1.851) ya 2022.
Kwa kulinganisha, Machi 2021, Ulaya iliagiza mita za ujazo milioni 1.579 na Novemba mwaka huo huo - mita za ujazo milioni 1.186.
Vikwazo vya Ulaya vimepunguza kwa kasi uagizaji wa mafuta ya Urusi na kuanzisha marufuku ya kuagiza aina zote za makaa ya mawe, lakini havijaathiri uagizaji wa gesi asilia.
Mapema Septemba, Waziri wa Nishati wa Uhispania Teresa Ribera aliiambia Reuters - EU kwa sasa haina mpango wa kuachana na gesi ya Urusi.
Kulingana na Shirika la Nishati la Kimataifa, mwishoni mwa 2022, usambazaji wa gesi ya Urusi kwenda Uropa ulipungua kwa mita za ujazo bilioni 90 ikilinganishwa na 2021. Lakini kuachana kabisa na gesi ya Urusi bado hakujawezekana.
[Mwaka 2023] Ulaya ilipoteza mita za ujazo bilioni 120 za gesi ya bomba la Urusi, na ilinunua mita za ujazo milioni 22 kutoka Urusi - hii ni sawa na takriban mita za ujazo bilioni 30 za gesi.
Ulaya itaachana na gesi ya Urusi?

Chanzo cha picha, REUTERS/NACHO DOCE
Ili kupunguza kununua gesi ya Urusi, Ulaya inatakiwa ifanye nini?
"Wekeza katika vyanzo vinavyopunguza matumizi ya gesi, au kujenga vituo vipya na kuingia katika kandarasi mpya za muda mrefu na ili kupata gesi,’’ anasema mtaalamu wa nishati hiyo, Andrey Bely.
‘’Shida nyingine ni kwamba soko la kimataifa la gesi lina uhaba na husababisha bei kuwa juu. Ni faida zaidi kwa Ulaya kununua gesi nchini Urusi. Ni nafuu kuagiza kutoka Urusi kuliko kutoka Marekani,” anaelezea Sergei Suverov, mtaalamu wa uwekezaji kutoka Kampuni ya Arikapital Management.
Wakati huo huo, mauzo ya nje ya gesi ya Marekani kwa EU pia yanakua. Mwisho wa 2022, kiasi cha gesi kiliongezeka hadi mita za ujazo milioni 117.4. Ukilinganishwa na mita za ujazo milioni 47.8 mwaka 2021.
Soko la Urusi ni rahisi zaidi kwa Ulaya kwa suala la gharama za usafiri. "Kwa Ulaya, haijalishi ni wapi unanunua gesi - suala ni gharama za usafiri tu. Usafiri kutoka Marekani au Qatar inamaanisha bima ghali zaidi na usafiri wa bei ghali zaidi,” anabainisha Suverov.
‘’Hatimaye, hakuna maana kuweka vikwazo kwa Urusi wakati baadhi ya nchi za Umoja huo zinaendelea kununua gesi yake,’’ anasisitiza Sergei Vakulenko.
Nchi zinazonunua gesi ya Urusi ni Italia, Austria, Hungary, Slovakia na Ugiriki. Kwa nchi hizi kupata rasilimali hiyo kwingine ni ngumu zaidi kwao, kwa sababu ya eneo lao.
Mafanikio ya Ulaya katika kupunguza uingizaji wa gesi ya Urusi inategemea mambo kadhaa, anabainisha Andrey Bely.
Je, Ulaya itaweza kuunda mikataba ya muda mrefu na wagavi mbadala? Je, kiasi cha mauzo ya gesi kutoka Marekani kwenda Ulaya kitaendelea? Je, ushindani wa EU na Asia kupata gesi utaongezeka ikiwa mahitaji ya gesi yataendelea kukua nchini China?
Majibu ya maswali haya yanaamua ikiwa Ulaya itaweza kujihakikisha usalama wake wa nishati bila gesi ya Urusi.












