Kumshabikia Putin: Waziri wa zamani wa Austria aliyehamia Urusi

Putin dances with Kneissl at her wedding, August 2018

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Vladimir Putin alicheza na Bi Kneissl kwenye harusi yake mnamo 2018, na akamletea shada la maua.
    • Author, Steve Rosenberg
    • Nafasi, Mhariri wa Urusi, St Petersburg

Yote ni kama ndoto.

Nimekaa katika jumba la kifahari la Karne ya 19 la St Petersburg. Aliyelala sakafuni karibu na kiti changu ni Winston Churchill. Amelala fofofo… na anakoroma.

"Labda ukimuamsha mara kwa mara ni vizuri."

Ushauri huu unatoka kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria Karin Kneissl ambaye ameketi mkabala nami. Winston Churchill ni mbwa wake. Miezi michache iliyopita walihamia Urusi, pamoja na paka na farasi wa Bi Kneissl.

"Tuliwahi kuwa na tukio kidogo la kidiplomasia na kukoroma kwake," anakumbuka. "Nilifanya mazungumzo ya simu na mwenzangu. [Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Ujerumani, Heiko] Maas alikuwa kwenye kipaza sauti na Winston Churchill alikoroma. Ilibidi tumwamshe ili tusiwaudhi Berlin. La sivyo, wangeweza kufikiri kwamba Vienna hulala usingizi wakati Berlin ikipiga simu."

Karin Kneissl amekuwa mambo mengi: mhadhiri, mwandishi wa habari wa kujitegemea, mchambuzi wa nishati. Yeye pia amekuwa mtu mwenye utata. Sio zaidi ya mwaka wa 2018 wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin alipohudhuria harusi yake.

Kwa muda mrefu wa miaka ya 1990 alifanya kazi katika wizara ya mambo ya nje ya Austria. Mwaka wa 2017 chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Freedom Party (ambacho hakuwa mwanachama) kilimteua kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali mpya ya muungano. Chama hicho kilikuwa kikikuza uhusiano wa karibu na Kremlin na kilikuwa kimetia saini makubaliano ya ushirikiano na chama tawala cha Urusi cha United Russia.

Mnamo 2019 serikali ilianguka, na Bi Kneissl akaondoka ofisini. Anadai kuwa "shinikizo la kisiasa" lilizuia majaribio yake ya kuanza tena taaluma na biashara kwa sababu alichukuliwa kuwa karibu sana na Urusi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulikuwa na mengi ambayo wakosoaji wake wangeweza kueleza. Mnamo 2020 Karin Kneissl alianza kuchangia maoni kwa chombo cha habari kinachodhibitiwa na serikali cha Urusi RT. Akawa profesa anayetembelea Taasisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya Jimbo la Moscow. Mnamo 2021, kampuni kubwa ya mafuta ya Urusi, Rosneft, ilimteua kwenye bodi yake (alijiuzulu mnamo Mei 2022).

Akilalamika kuhusu "hila dhidi yake" na kushindwa kupata kazi nyumbani, Karin Kneissl alihamia Ufaransa, kisha Lebanoni. Miezi michache iliyopita alikuwa safarini tena: wakati huu kuelekea Urusi kuongoza kituo cha uchambuzi katika Chuo Kikuu cha St Petersburg. Imejengwa katika jumba la kifahari ambalo nimekaa. Tovuti ya shirika hilo inasema kuwa dhamira yake ni "kutafuta suluhisho kwa changamoto za maendeleo ya kimataifa na majukumu ya sera ya Urusi".

Bi Kneissl kando na kuendesha kituo hicho ndiye aliyelipa jina .

"Niliunda jina G.O.R.K.I, ambalo ni kifupi cha Geo-Political Observatory for Russia's Key Issues," Bi Kneissl ananiambia.

"Unaelewa kuwa kuna utata mkubwa kwa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Austria kuhamia Urusi," ninamhoji, "wakati ambapo nchi hii imeanzisha uvamizi kamili wa Ukraine bila sababu? Je, hakuna hatari kwamba kwa kuwa hapa unahalalisha uvamizi, vita na ukandamizaji wa nyumbani unaofanyika hapa?"

"Kweli, hadi sasa sijaona aina yoyote ya ukandamizaji katika mazingira yangu ya karibu," anajibu. "Ninaweza kufanya kazi hapa katika aina ya uhuru wa kitaaluma ambao nilianza kukosa nilipokuwa bado nafundisha katika vyuo vikuu mbalimbali vya Umoja wa Ulaya."

Ninamkumbusha Bi Kneissl kwamba, siku chache tu zilizopita katika jiji hili hili, mwanamke mdogo - Sasha Skochilenko - alifungwa gerezani kwa miaka saba kwa kubadilisha vitambulisho vya bei katika duka kuu na kauli mbiu za kupinga vita. Mfano mmoja wa hivi karibuni wa wimbi la ukandamizaji linaloikumba Urusi.

"Kwa hiyo, ninahusiana vipi na hilo?" anajibu. "Nimeeleza kwa kirefu hali ambayo nimekuwa nikipitia. Wacha tuweke jambo zima kwa njia nyingine: kwa nini Karin Kneissl alikatazwa kufanya kazi? Uhalifu wangu ni upi? Ninashukuru sana kupata nafasi ya kufanya kazi [nchini Urusi .]"

Winston Churchill, the dog
Maelezo ya picha, Winston Churchill alikatiza mahojiano ya mmiliki wake na BBC

Kukoroma kwa Winston Churchill kunazidi kuongezeka. Ni sauti kubwa sana hivi kwamba maikrofoni yangu ya Runinga sasa inaipokea. Siwezi kuruhusu mbwa huyu anayelala alale. Kwa mara ya kwanza katika taaluma yangu, ninalazimika kukatiza mahojiano ili kuamsha mbwa.

Ilikuwa mnamo 2018 ambapo Karin Kneissl aligonga vichwa vya habari kote ulimwenguni.

Mnamo Machi mwaka huo, kemikali alikuwa imetumiwa katika mitaa ya Uingereza. Ajenti wa zamani wa Urusi Sergei Skripal na bintiye Yulia walikuwa wakilengwa na Novichok. Walinusurika katika shambulio la Salisbury.

Lakini mwananchi, Dawn Sturgess, alipewa sumu, pia, na baadaye akafa. Umoja wa Ulaya ulikuwa umekubaliana na tathmini ya serikali ya Uingereza "kwamba kuna uwezekano mkubwa Shirikisho la Urusi linahusika."

Wanadiplomasia wengi wa Urusi walifukuzwa kutoka Uropa. Moscow ilikana kuhusika kwa vyovyote na tukio hilo.

Miezi mitatu tu baadaye, Karin Kneissl alimwalika Rais Putin kuwa mgeni katika harusi yake iliyopangwa kwa majira ya joto.

Mnamo Agosti 2018, kiongozi wa Kremlin alifika na shada la maua, busu na zawadi nyingi kwa Bi Kneissl na bwana harusi wake, ikiwa ni pamoja na samovar (birika la kale linalotumiwa kuandaa chai nchini Urusi), mchoro na pete.

Rais wa Urusi na waziri wa mambo ya nje wa Austria walishiriki .Mwishoni mwa ngoma, Bi Kneissl alifanya ishara ya utiifu kwa Putin.

Katika mahojiano na kipindi cha HARDtalk cha BBC mapema mwaka huu, akiwa bado yuko Lebanon, Karin Kneissl aliulizwa iwapo angecheza na Rais Putin leo kwenye harusi, akijua kwamba kiongozi huyo wa Kremlin amefunguliwa mashtaka na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuwa ni mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita.

"Ndiyo," alijibu. "Je, kuna jingine la kufanya? Sitaingia katika mashitaka yote ya uhalifu wa kivita kwa sababu tuna wahalifu wengi wa kivita ndani ya duru za juu za kisiasa."

Ninapoibua mada ya harusi yake ya 2018, kuna kusitasita. Lakini sio kengele za harusi.

"Hii inachosha sana," anasema kwa hasira. "Jambo lote lilitokea karibu miaka sita iliyopita. Wakati huo nikiwa waziri wa mambo ya nje na nilicheza ngoma na Rais Putin.

Lakini nimefanya mambo mengine katika maisha yangu kabla na baada ya hapo. Kusema kweli, inachosha sana. Inachosha sana."

"Kuzungumza juu ya harusi?"

"Ndiyo. Kuna mada zaidi ya kuvutia tunaweza kujadili."

Putin and Kneissl attend Sochi summit 2019

Chanzo cha picha, Kremlin

Maelezo ya picha, Bi Kneissl alimtaja Rais Putin kama "bwana mwenye akili zaidi"

"Tutafanya hivyo. Lakini huna majuto?"

"Naona ni jambo la kuchosha. Na mbwa alilala tu na alikuwa akikoroma kwa sababu anajua mada."

Yuko sawa. Winston Churchill ametikisa kichwa tena. Nina shaka kuwa ni swali la harusi ya Putin ambalo limemrudisha kulala; ingawa nadhani hatutawahi kujua.

Lakini najua maoni ya Karin Kneissl kuhusu shinikizo la nchi za Magharibi kwa Urusi: anaamini kwamba viongozi wa Ulaya wanaanza kutambua kutofaulu kwa vikwazo.

"Ninachofikiria ni kusonga mbele ni kukiri kwa wengi kuwa vikwazo havifanyi kazi," ananiambia. "Wengi wanalazimika kukiri kwamba vikwazo dhidi ya Urusi havikuleta matokeo waliyotaka kupata.

"Na unapoangalia jinsi maafisa wote wa EU wamekuwa wakizungumza kwa miezi kumi na minane iliyopita - mabadiliko ya serikali nchini Urusi ndio wanauliza - ninamaanisha, unawezaje kama Urusi kisha kujadiliana na watu wanaouliza uvamizi wako, uharibifu wako? "

Ninaona picha kwenye baraza la mawaziri nyuma yake. Miongoni mwao ni picha ya Karin Kneissl akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov; na picha yake akiwa na Rais Putin.

"Kutoka kwa mikutano yako na Vladimir Putin," ninauliza, "unafikiri ni mtu wa aina gani?"

"Yeye ndiye bwana mwenye akili zaidi, anayezingatia ,muungwana - na nimekutana na wachache," Karin Kneissl anajibu. "Kwa maana ya kile Jane Austen aliandika katika Pride na Prejudice kuhusu bwana aliyekamilika, yeye ni sawa na kiwango hiki."

Karin Kneissl with Putin, in a photo in her home
Maelezo ya picha, Bi Kneissl ana picha zake na za rais wa Urusi ndani ya ofisi yake katika jumba la St Petersburg

"Tunaona wimbi la ukandamizaji ndani ya nchi na tumeona Urusi ikivamia Ukraine," ninadokeza. "Ni vigumu kuliona hili kama hatua ya kiungwana."

"Sawa," anajibu, "Tony Blair, David Cameron ... wote walihusika na serikali zao katika hatua za kijeshi."

Karin Kneissl anajijengea maisha mapya nchini Urusi. Lakini je, angeweza kufikiria kurudi Austria?

"Nchini Austria kuna sauti kadhaa zinazotaka uraia wangu uondolewe kwa sababu sasa ninafanya kazi katika chuo kikuu nchini Urusi," ananiambia. "Ninatuhumiwa kuwa mfisadi, mhaini , ambaye ametumikia KGB kwa miaka thelathini ,kulingana na Wikipedia. Uchafu wa aina hii na kashfa huharibu maisha. Na sitaki kurejea Austria hadi kesi hizi zisafishe jina langu

"Unasema kuna watu nchini Austria ambao wanakushtaki kwa uhaini mkubwa na kuwa ..."

"Jasusi wa Urusi."

"Lakini unaweza kuelewa, kwa kiasi ...?"

Bi Kneissl ananikatisha.

"Hapana, hata inchi moja. Sielewi," anasema. "Ni ndoto chafu tu."

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi