Mfahamu kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Maria Corina Machado

.
Maelezo ya picha, Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Corina Maria Machado
    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela Maria Corina Machado ameapa kuwa atarudi nyumbani haraka, huku akimsifu Rais wa Marekani Donald Trump kwa kumpindua adui yake Nicolas Maduro na kutangaza kuwa yuko tayari kwa uchaguzi huru.

"Napanga kurudi Venezuela haraka iwezekanavyo," amesema Machado, 58, wakili na mama wa watoto watatu ambaye alitoroka Venezuela akiwa mafichoni Oktoba kwenda kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.

Katika mahojiano na Fox News siku ya Jumatatu alisema, "tulishinda uchaguzi (mwaka 2024) kwa kishindo chini ya hali ngumu. Katika uchaguzi huru na wa haki, tutashinda zaidi ya 90% ya kura."

Machado amesema hajazungumza na Trump tangu Oktoba 10, wakati alipopokea tuzo ya Nobel. Amesema Marekani inapaswa kusaidia kushughulikia matatizo ya Venezuela kabla ya uchaguzi wowote mpya.

Ni mahojiano yake ya kwanza ya Machado tangu Maduro alipokamatwa na Marekani mwishoni mwa wiki.

Machado anatafutwa na serikali ya Chama cha Kisoshalisti kilichopo madarakani.

Utawala wa Marekani hadi sasa unaonekana huenda ukafanya kazi na Rais wa mpito Delcy Rodriguez, mshirika wa muda mrefu Maduro ambaye amekosoa "utekaji nyara" wa Maduro huku pia akitaka ushirikiano na uhusiano wa heshima na Washington.

Lakini Machado ni nani haswa?

María Corina Machado amezaliwa 7 Oktoba 1967 ni mwanasiasa wa Venezuela na mhandisi wa viwanda.

Machado ni kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Venezuela na aliwahi kuwa mbunge katika Bunge la Kitaifa la Venezuela kutoka 2011 hadi 2014.

Na leo, tarehe 10/10/2025, Machado ametunikiwa Tuzo ya Amani ya Nobel "kwa kazi yake ya kukuza na kuendeleza haki za kidemokrasia kwa watu wa Venezuela na kwa mapambano yake kufikia mabadiliko ya haki na ya amani kutoka kwa udikteta hadi demokrasia."

Machado aliingia katika siasa mnamo mwaka 2002 kama mwanzilishi wa shirika la ufuatiliaji wa kura la Súmate.

Mnamo mwaka wa 2012, alikuwa mgombea katika mchujo wa kumtafuta mgombea urais wa upinzaji lakini alishindwa na Henrique Capriles.

Wakati wa maandamano ya Venezuela ya 2014, Machado alikuwa kiongozi aliyeongoza maandalizi ya maandamano dhidi ya serikali ya Rais Nicolás Maduro.

Soma zaidi:
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kabla ya uchaguzi wa 2024, Bi Machado alikuwa mgombea urais wa upinzani, lakini serikali ilimzuia kuwania. Kisha akamuunga mkono mwakilishi wa chama tofauti, Edmundo Gonzalez Urrutia, katika uchaguzi huo.

Kulingana na tovuti ya Tuzo ya Amani ya Nobel, mamia ya maelfu ya watu walijitokeza na kupata mafunzo ya waangalizi wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa uwazi na wa haki. Licha ya hatari ya kunyanyaswa, kukamatwa na kuteswa, raia kote nchini humo walifuatilia kwa karibu vituo vya kupigia kura. Walihakikisha kuwa hesabu za mwisho zimerekodiwa.

"Juhudi za za pamoja za upinzani, kabla na wakati wa uchaguzi, zilikuwa za kiubunifu na za ujasiri, za amani na za kidemokrasia," Tovuti ya Amani ya Nobel imesema.

Upinzani ulipata uungwaji mkono wa kimataifa wakati viongozi wake walipotangaza hesabu ya kura zilizokuwa zimekusanywa kutoka kwa wilaya za uchaguzi nchini humo, na kuonyesha kwamba upinzani ulipata ushindi mkubwa.

Lakini serikali ilikataa kukubali matokeo ya uchaguzi, na kung'ang'ania madarakani.

Katika historia yake ndefu, Kamati ya Nobel ya Norway imewaheshimu wanawake na wanaume jasiri ambao wamesimama kukabiliana na ukandamizaji, ambao wamebeba matumaini ya uhuru katika seli za magereza, mitaani na katika viwanja vya umma, na ambao wameonyesha kwa matendo yao kwamba kupigania amani kunaweza kubadilisha ulimwengu.

.

Chanzo cha picha, AFP

Katika kipindi cha mwaka uliopita, Bi Machado amelazimika kuishi mafichoni. Licha ya vitisho vikali dhidi ya maisha yake amesalia nchini Venezuela, chaguo ambalo limewatia moyo mamilioni ya watu.

"Wakati madikteta wanaponyakua mamlaka, ni muhimu kutambua watetezi jasiri wa uhuru wanaoinuka na kupinga hatua hiyo. Demokrasia inategemea watu wanaokataa kukaa kimya, wanaothubutu kusonga mbele licha ya hatari kubwa, na ambao wanatukumbusha kwamba uhuru haupaswi kuchukuliwa kuwa wa kawaida, lakini lazima ulindwe kila wakati - kwa maneno, kwa ujasiri na kwa uamuzi," Tovuti ya Amani ya Nobel imesema.

Kulingana na Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Corina Machado anakidhi vigezo vyote vitatu vilivyotajwa katika wosia wa Alfred Nobel kwa uteuzi wa mshindi wa Tuzo ya Amani.

"Ameleta upinzani wa nchi yake pamoja. Hajawahi kuyumba katika kupinga jeshi la Venezuela. Amekuwa thabiti katika kuunga mkono mabadiliko ya amani kuelekea demokrasia," Tovuti ya Amani ya Nobel imesema.

Venezuela imebadilika kutoka nchi yenye demokrasia na ustawi hadi kuwa nchi ya kikatili, ya kimabavu ambayo sasa inakabiliwa na mgogoro wa kibinadamu na kiuchumi. Wananchi wengi wa Venezuela wanaishi katika umaskini mkubwa, hata kama wachache walio juu wanajitajirisha.

Takriban watu milioni 8 wameondoka nchini humo. Upinzani umekandamizwa kimfumo kwa njia ya wizi wa kura huku wapinzani kama Machado, wakifunguliwa mashitaka ya kisheria na kufungwa jela.

Kilichotokea katika chumba cha kumchagua mshindi

.

Chanzo cha picha, NRK

Kila mwaka tangu mwaka 1901 wanachama hukusanyika kwa siri, bila kufichua wakati wako pamoja, au kuruhusu waandishi wa habari kushuhudia mkutano wao wa mwisho - hadi sasa.

Wanachama wa kamati ya Nobel ya Norway – wanaosimamia mchakato wa utambuzi wa mshindi wa tuzo hiyo ya kifahari zaidi duniani - leo Ijumaa, tarehe 10/20/2025, wamemtuza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Na BBC, pamoja na shirika la utangazaji la taifa la Norway, walifanikiwa kuwa karibu wanachama walipokuwa wamekusanyika kufanya chaguo lao.

Ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 125 ya tuzo hiyo kwa vyombo vya habari kuruhusiwa kuona mchakato huo unaofanyika nyuma ya pazia.

Wajumbe hao watano na katibu wamekutana katika chumba cha Kamati ya taasisi ya Nobel ya Oslo, ambako kumepambwa kwa samani sawa na zilizokuwa tangu tuzo ya kwanza.

Kando ya kuta kuna picha za kila mshindi wa tuzo hiyo ya amani, na mwishoni kuna nafasi ya picha ya mshindi wa mwaka huu.

"Tunajadili, tunabishana, joto linapanda," mwenyekiti wa kamati ya Nobel ya Norway, Jorgen Watne Frydnes, alisema "lakini pia, bila shaka, sisi ni wastaarabu, na tunajaribu kufanya uamuzi kwa kufikia makubaliano kila mwaka."

Walisoma kwa sauti vigezo vya tuzo vilivyowekwa katika wosia wa Nobel kuanzia mwaka1895; kwamba itolewe kwa yeyote ambaye amefanya mengi kwa ajili ya udugu kati ya mataifa, kukomesha au kupunguzwa kwa majeshi, au kwa kufanya au kuendeleza makongamano ya amani.

Kisha wanahabari wakatoka nje na mlango ukafungwa wakabaki wenyewe kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.

Donald Trump pia alipigania nafasi ya kushinda Tuzo

.

Chanzo cha picha, Reuters

"Mimi nilizuia vita saba," alisema Rais wa Marekani, Donald Trump, alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni akirudia kauli ambayo ameitoa mara kadhaa hapo awali.

Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa vikali na watu wengi, huku kikosi maalum cha BBC kinachofuatilia ukweli kikichapisha makala yaliyouliza kama kweli Trump alihusika moja kwa moja kusitisha vita hivyo.

Usichojua ni kwamba, Trump alikuwa anajipigia debe kutwaaTuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu ambako pia kuliungwa mkono na baadhi ya viongozi mashuhuri wa kimataifa.

Siku chache kabla Kamati ya Nobel kutangaza mshindi wa mwaka huu, kundi moja linalopigania kuachiliwa kwa mateka waliokuwa wakishikiliwa na Hamas huko Gaza kwa miaka miwili, lilimpendekeza Trump apokee tuzo hiyo.

Uteuzi wa Trump ulianza nchini Pakistan.

Tarehe 21 Juni, serikali ya Pakistan ilitangaza kuwa inapanga kumteua Trump kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel, ikieleza kuwa alisaidia kusuluhisha mzozo wa muda mfupi kati ya India na Pakistan.

"Trump anastahili tuzo hiyo kwa kutambua uongozi wake wa kidiplomasia na mchango wake muhimu katika kutuliza mgogoro wa hivi karibuni kati ya India na Pakistan."

Hata hivyo, India ilikanusha kuwa Marekani ilihusika katika kusitisha mzozo huo wa kijeshi ulioibuka mwezi Mei.

Aidha, Pakistan haikufafanua kama iliwahi kuwasilisha rasmi uteuzi huo kwa Kamati ya Nobel.