Kiongozi wa upinzani Venezuela amshinda Trump katika tuzo ya amani ya Nobel

María Corina Machado ameshinda tuzo hiyo kwa kuendeleza haki za kidemokrasia nchini Venezuela.

Muhtasari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi, Mariam Mjahid & Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Burkina Faso yakataa kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa Marekani

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imekataa kuwachukua watu waliofukuzwa Marekani huku Washington ikisitisha kutoa viza kwa taifa hilo la Afrika Magharibi.

    Waziri wa Mambo ya Nje, Karamoko Jean-Marie Traoré amehoji ikiwa uamuzi wa ubalozi huo ni wa "kulipiza kisasi" baada ya kusema kuwa amekataa pendekezo la Marekani la kuchukua wahamiaji kutoka nchi ya tatu.

    Utawala wa Donald Trump umegeukia nchi za Kiafrika kama maeneo ya kuwapeleka wahamiaji kama sehemu ya mpango wake wa kuwafukuza wahamiaji.

    Kiongozi wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré anajionesha kama mwanamajumui wa Afrika, na anapinga ubeberu wa Magharibi.

    Serikali yake ya kijeshi ilichukua mamlaka katika mapinduzi miaka mitatu iliyopita, na imekuwa na uhusiano mbaya na mataifa ya Magharibi tangu wakati huo.

    Kwenye shirika la utangazaji la serikali RTB siku ya Alhamisi, waziri wa mambo ya nje aliuliza: "Je, hii ni njia ya kutuwekea shinikizo? Je, huku ni kulipiza kisasi? Vyovyote itakavyokuwa... Burkina Faso ni mahali pa hadhi, si mahali pa waliofukuzwa."

    Amesema alikuwa na mkutano na Ubalozi wa Marekani siku ya Jumatano ambapo alikataa pendekezo la kupokea waliofukuzwa - anasema pendekezo hilo limetolewa mara kwa mara.

    Siku ya Alhamisi, ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou ulisema kwenye tovuti yake kwamba unasitisha kwa muda kutoa viza za wahamiaji, watalii, wanafunzi na wasafiri wa biashara.

    Badala yake, wakaazi wa Burkina Faso watalazimika kusafiri hadi kwenye ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa nchi jirani ya Togo.

    Nchi kadhaa za Afrika - Eswatini, Ghana, Rwanda na Sudan Kusini - zote zimekubali kupokea watu kutoka nchi ya tatu waliofukuzwa Marekani katika miezi ya hivi karibuni.

    Nigeria imesema haitachukua raia yeyote aliyefukuzwa Marekani.

    Mpango wa Trump unalenga kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji nchini Marekani kinyume cha sheria.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Wapalestina waanza kurejea kaskazini mwa Gaza

    Hh

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wapalestina wanaanza kurejea kaskazini mwa Gaza huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akimshukuru rais Donald Trump wa Marekani, kwa kufanikisha usitishaji mmapigano.

    Vikosi vya Jeshi la Israel (IDF), vimerudi nyuma katika mstari uliokubaliwa chini ya mpango wa Trump, lakini IDF inasema, itaendelea "kuondoa tishio lolote."

    Hamas ina hadi Jumatatu kuwaachilia mateka wote wa Israel, na Israel itawaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

    Haya yanajiri baada ya serikali ya Israel kuidhinisha awamu ya kwanza ya mkataba wa kusitisha mapigano na kurejea kwa mateka.

    Chini ya makubaliano hayo, malori ya misaada yanatarajiwa kuanza kuingia kusaidia watu milioni mbili wa Gaza, ambao wengi wao wameyakimbia makazi yao.

    H

    Wakati huo huo, vikosi vya usalama vya Hamas vyenye silaha vimeonekana katika mitaa ya Gaza katika maeneo ambayo Israel imejiondoa.

  4. Mali yawatimua maafisa wa kijeshi kwa tuhuma za kupanga mapinduzi

    Nj

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya kijeshi nchini Mali imewafuta kazi maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu kumi na mmoja - wakiwemo majenerali wawili - wanaotuhumiwa kupanga njama ya kuyumbisha serikali.

    Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na kile ambacho baadhi wanasema, huenda ni mvutano unaoongezeka ndani ya serikali ya kijeshi ya Kanali Assimi Goïta.

    Amri iliyotiwa saini na Kanali Goïta inathibitisha kufukuzwa kazi kwa sababu za kinidhamu.

    Amri hiyo inafuatia kukamatwa takribani wanajeshi thelathini mwezi Agosti kwa madai ya kupanga njama ya kuipindua serikali.

    Miongoni mwa walioondolewa ni Jenerali Abass Dembélé, gavana wa zamani wa Mopti, na Néma Sagara - mmoja wa wanawake wachache kufikia cheo cha jenerali katika jeshi la anga la Mali.

    Inaelezwa kuwa wote wawili wanaheshimiwa sana ndani ya jeshi.

    Televisheni ya serikali, ORTM, ilionyesha picha za maafisa waliozuiliwa, na kusema jaribio la mapinduzi limezimwa. Lakini baadhi ya vyanzo vya usalama huko Bamako vinasema hatua hiyo inaakisi hali ya wasiwasi inayoongezeka ndani ya utawala na inaweza kuongeza mgawanyiko.

    Raia wa Ufaransa, Yann Vézilier - anayeripotiwa kuhusishwa na idara ya ujasusi ya nje ya Ufaransa, DGSE- pia alikamatwa kwa madai ya njama hiyo.

    Kuzuiliwa kwake kumeifanya Ufaransa kusitisha ushirikiano wake wa kiintelijensia na Mali dhidi ya ugaidi.

    Mkasa huu unakuja wakati jeshi likikabiliwa na mashambulizi yanayoongezeka ya wanajihadi kaskazini mwa nchi.

    Siku ya Alhamisi, wanamgambo walishambulia eneo lililo kilomita chache tu kutoka mji mkuu. Jeshi linasema lilizuia shambulio hilo na kuwauwa washambuliaji kadhaa.

    Doria za kijeshi tangu wakati huo zimeimarishwa katika maeneo ya Sikasso, Ségou, na Kidal.

    Mali imekuwa katika vita tangu mwaka 2012, huku makundi yenye silaha yanayohusishwa na al-Qaeda na Islamic State yakiendelea kuipinga serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mahakama yasogeza mbele uamuzi juu ya hatima ya Mpina

    DF

    Chanzo cha picha, ACT

    Mahakama kuu masjala kuu Dodoma imesema inahitaji muda zaidi wa kutoa uamuzi wa mwisho na usio wa mashaka katika shauri la Kikatiba lililofunguliwa na Mgombea Urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.

    Shauri hilo ni la kupinga kuondolewa kwake kuendelea na kampeni za kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwisho mwa mwezi huu.

    Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa hii leo oktoba 10 na kuweka mustakabali wa iwapo Luhaga Mpina ataendelea na mchakato wa Kampeni au la.

    Shauri hilo la Kikatiba la ACT WAZALENDO inayosikikizwa na Majaji watatu dhidi ya Tume ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa itaamuliwa Oktoba 15 mwaka huu kwa njia ya mtandao.

    Hata hivyo, hoja zote za shauri hilo la kikatiba zilishasikilizwa kwa hiyo kipengele kilichobaki ni uamuzi wa mwisho.

    Upande wa waleta maombi ukiongozwa na Wakili, John Seka unasema pande zote zilikuwa tayari kupokea uamuzi wa Mahakama Kuu.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Kesi ya Drake kuhusu kukashifiwa na Kendrick Lamar yatupiliwa mbali

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jaji mmoja nchini Marekani, ametupilia mbali kesi ya kashfa ya msanii Drake aliyoifungua dhidi ya kampuni ya Universal Music Group kuhusu wimbo wa Kendrick Lamar wa Not Like Us.

    Katika hukumu ya kurasa 38 Jaji Jeannette Vargas ametoa uamuzi kwamba mashairi ya Lamar, ambayo yanamshutumu Drake na washirika wake kuwa ni "mafataki wanaotambuliwa," ni "maoni yasiyoweza kuchukuliwa hatua" na hayangeweza kuchukuliwa kuwa ya kukashifu.

    Drake alifungua kesi hiyo mwezi Januari akiituhumu Universal Music Group (UMG), kampuni ya inayorikodi nyimbo za wasanii wote wawili, kwa kumkashifu kwa kuruhusu wimbo huo kuchapishwa, akisema ulieneza "taarifa za uongo na zenye nia mbaya.”

    Msemaji wa Drake amesema atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo. UMG imesema imefurahishwa na uamuzi huo na inatazamia kuendelea kufanya kazi na nyota huyo raia wa Canada.

    Not Like Us, ambayo ilitolewa Mei 2024, ilionekana kama pigo la mwisho katika vita vinavyoendelea kati ya wasanii hao wapinzani.

    Ni wimbo mkubwa zaidi miongoni mwa kazi za Lamar, baada ya kushinda tuzo tano za Grammy na kuufanya kuwa mojawapo ya wimbo uliozungumzwa zaidi.

    Lamar bado hajatoa maoni yake kuhusu kesi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mbunge wa upinzani afariki baada ya gari lake kumgonga tembo

    szx

    Chanzo cha picha, Desire Moyo/Facebook

    Maelezo ya picha, Mbunge huyo ndiye pekee aliyefariki katika ajali hiyo mapema Ijumaa asubuhi

    Mbunge wa upinzani nchini Zimbabwe Desire Moyo amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akisafiria kumgonga tembo, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.

    Ajali hiyo ilitokea alfajiri ya Ijumaa asubuhi wakati Moyo na wabunge wengine wanne walipokuwa wakisafiri katika barabara kuu ya Bulawayo-Gweru, kulingana na shirika la utangazaji la serikali ZBC.

    Alifariki papo hapo huku wabunge wenzake wakipata majeraha.

    Mbunge huyo ambaye pia ni mshairi, anayesifiwa kwa mchango wake katika sanaa, amefariki siku moja kabla ya kutimiza miaka 46.

    Alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC), kilichoongozwa na Nelson Chamisa.

    Jimbo la Nkulumane katika jiji la Bulawayo, ambalo aliliwakilisha, limethibitisha habari za kifo chake katika taarifa na kueleza "huzuni kubwa na mshtuko mkubwa."

    Moyo alikuwa mshairi aliyeshinda tuzo, mwalimu na msimamizi wa sanaa "ambaye alijitolea maisha yake katika kukuza sekta ya ubunifu ya Zimbabwe," kulingana na tovuti ya habari ya serikali ya Herald.

    Wabunge wengine waliohusika katika ajali ya Ijumaa wamepelekwa hospitalini.

  8. Marekani kutuma wanajeshi 200 Israel kufuatilia usitishaji mapigano Gaza

    D

    Chanzo cha picha, EPA

    Wanajeshi 200 wa Marekani ambao tayari wako Mashariki ya Kati watahamishwa na kupelekwa Israel ili kusaidia kufuatilia usitishaji mapigano Gaza, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani.

    Jeshi la Marekani litaanzisha kikosi kazi cha kimataifa nchini Israel, ambacho huenda kikajumuisha wanajeshi kutoka Misri, Qatar, Uturuki na UAE.

    Afisa mmoja amesema hakuna wanajeshi wa Marekani watakaoingia Gaza, na kusema jukumu la Marekani ni kuunda Kituo cha Pamoja cha Udhibiti ambacho "kitaunganisha" kikosi cha kimataifa kitakacho kwenda Gaza.

    Serikali ya Israel imeidhinisha awamu ya kwanza ya makubaliano ya amani, ambayo yamepelekea kusitishwa kwa mapigano na baadaye kuachiliwa kwa mateka na wafungwa.

    Kikosi kazi hicho kitaongozwa na Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) yenye makao yake Mashariki ya Kati, na kinanuiwa kusimamia makubaliano ya kusitisha mapigano na pia kusaidia kuratibu usaidizi wa kibinadamu.

    Jeshi la kimataifa litawajuulisha Israel na Hamas kupitia Misri na Qatar juu ya hali ilivyo na ukiukaji wowote wa makubaliano ya kusitisha mapigano, mmoja wa maafisa amesema.

    Kikosi hicho kinaanzishwa chini ya uongozi wa Adm Brad Cooper, mkuu wa Centcom, ambaye alijiunga na ujumbe wa Marekani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri mapema wiki hii, mmoja wa maafisa amesema.

    Mojawapo ya hoja katika mpango wa Trump wa Gaza ni Marekani kufanya kazi na washirika wa nchi za Kiarabu na kimataifa kuunda Kikosi cha muda cha Kimataifa cha Udhibiti wa Utulivu kitakachotumwa mara moja huko Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Kanisa Katoliki Kenya labadilisha mvinyo wa madhabahuni baada ya kuwa maarufu katika baa

    D
    Maelezo ya picha, Askofu Mkuu Maurice Muhatia Makumba anawataka MapadrI kutumia mvinyo mpya kutoka katika maduka yaliyoidhinishwa

    Kanisa Katoliki la Kenya limeanzisha matumizi ya aina mpya ya mvinyo wa madhabahuni kwa ajili ya Misa Takatifu baada ya ule wa awali kupatikana kwa wingi katika baa za mitaani.

    Kinywaji hicho kipya cha kisakramenti kinachoitwa Mass Wine, kinabeba nembo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) na kutiwa saini rasmi kuthibitisha uhalisi wake.

    "Mvinyo mpya ulioidhinishwa hauuzwi katika eneo lolote la biashara, huagizwa kutoka nje na kumilikiwa na KCCB, na kusambazwa kwa dayosisi," Askofu Mkuu wa Nyeri Anthony Muheria aliambia BBC.

    Hatua hiyo imekaribishwa na waumini wa Kikatoliki, ambao wanaamini kwamba chapa ya hapo awali ilikuwa imepoteza utakatifu wake kutokana na matumizi yake kuwa makubwa nje ya kanisa.

    Mvinyo hutumiwa kwenye Misa kuashiria damu ya Yesu Kristo na kwa kawaida hunywewa na kasisi. Katika baadhi ya nyakati, unatolewa kwa waumini pia.

    Mvinyo wa zamani ambao ulisambazwa na mtengenezaji wa pombe wa ndani, ulikuwa ukiuzwa kwa wingi katika maduka ya vileo, hoteli, baa na maduka makubwa.

    "Imekuwa kawaida kwa bahati mbaya, mvinyo wa zamani unapatikana kwa urahisi katika maduka na baa," Askofu Mkuu Muheria aliiambia BBC.

    Wakristo wengi wa Kenya ni Wakatoliki - takriban watu milioni 10, sawa na 20% ya watu wote, kulingana na takwimu za serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Habari za hivi punde, Maria Corina Machado ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maria Corina Machado kutoka Venezuela ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel 2025

    María Corina Machado ameshinda tuzo hiyo kwa kazi ya kukuza haki za kidemokrasia nchini Venezuela.

    Machado ashinda kwa 'kuendeleza haki za kidemokrasia' bila kukoma

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, kamati hiyo inasema imemtunuku Maria Corina Machado Tuzo ya Amani ya Nobel "kwa kazi yake bila kukoma ya kuendeleza haki za kidemokrasia kwa watu wa Venezuela na kwa mapambano yake ya kufikia mabadiliko ya haki na amani kutoka kwa udikteta hadi demokrasia".

    Machado 'amekuwa mtu muhimu wa kuunganisha'

    Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2025 inaenda kwa "mwanamke ambaye anaendeleza harakati za kupatikana kwa demokrasia, katikati ya giza linaloongezeka".

    Maria Corina Machado anapokea tuzo ya Amani ya Nobel kwa kuwa mmoja wa "kupigiwa mfano" kwa ujasiri katika Amerika ya Kusini siku za hivi karibuni.

    Machado amekuwa mtu muhimu wa kuunganisha watu, mwenyekiti wa kamati anaongeza.

    "Hii ndiyo hasa kiini cha demokrasia, nia yetu ya pamoja ya kutetea kanuni za utawala, ingawa hatukubaliani.

    "Wakati ambapo demokrasia inakabiliwa na tishio, ni muhimu zaidi kutetea msingi huu wa pamoja."

    Pia unaweza kusoma:

  11. Israel yaanza kujiondoa katika baadhi ya maeneo ya Gaza

    Ju

    Chanzo cha picha, Reuters

    Israel yaanza kujiondoa katika sehemu za Gaza baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka kupitishwa.

    Usitishaji vita unatarajiwa kuanza kutekelezwa huko Gaza, baada ya serikali ya Israel kuidhinisha makubaliano na Hamas ambayo pia yatashuhudia kuachiliwa kwa mateka.

    Wakaazi wanaiambia BBC kuwa wanajeshi wa Israel wameanza kuondoka katika sehemu za eneo hilo.

    Chini ya makubaliano hayo, jeshi la Israel lina saa 24 kuondoka kwa njia iliyokubaliwa.

    Hamas watakuwa na saa 72 kuwaachilia mateka wote wa Israel, wakati Israel itawaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

    Mara tu mpango huo utakapoanza, malori ya misaada yataongezeka kusaidia watu milioni mbili wa Gaza, ambao wengi wao wamelazimika kuyahama makazi yao.

  12. Rais wa Peru aenguliwa na bunge, mkuu wa bunge aapishwa

    Rais wa Peru aliyeenguliwa na bunge

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wabunge wa Peru wamemuapisha mkuu wa bunge Jose Jeri kuwa rais mpya wa nchi hiyo chini ya saa moja baada ya kupiga kura kwa kauli moja kumuondoa Rais Dina Boluarte, mmoja wa viongozi wasiojulikana sana duniani.

    Sherehe ya kupiga kura na kuapishwa ilifanyika muda mfupi baada ya saa sita usiku siku ya Ijumaa, saa chache tu baada ya kambi za kisiasa kutoka katika wigo wa kwanza kuwasilisha hoja ya kuondolewa kwa Boluarte kwa misingi ya ukosefu wa maadili.

    Jeri, ambaye anakuwa rais wa saba wa Peru tangu 2016, aliashiria kuwa atachukua mbinu ngumu juu ya kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, mojawapo ya shutuma kuu ambazo zilitolewa dhidi ya Boluarte.

    Alihutubia bunge akiwa amevalia ukanda wa bendera ya taifa.

    "Adui mkuu yuko huko nje mitaani: magenge ya wahalifu," alisema. "Lazima tutangaze vita dhidi ya uhalifu."

    Mwanachama huyo mwenye umri wa miaka 38 wa chama cha kihafidhina cha Somos Peru, ambaye alikua rais wa bunge mwezi Julai, anajiunga na safu ya baadhi ya wakuu wa nchi vijana zaidi duniani.

    Umati ulikuwa umekusanyika nje ya Bunge la Congress na ubalozi wa Ecuador, ambapo ilisemekana kwamba Boluarte angeweza kutafuta hifadhi, baadhi wakiwa katika hali ya sherehe wakipeperusha bendera, kucheza na kucheza ala.

    Soma pia:

  13. Mzozo wa Ukraine: Shambulizi la Urusi lalitumbukiza jiji la Kyiv gizani

    Vituo vya umeme vya Ukraine vimekumbwa na mashambulizi yaliyoongezeka katika wiki za hivi karibuni

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Vituo vya umeme vya Ukraine vimekumbwa na mashambulizi yaliyoongezeka katika wiki za hivi karibuni

    Mashambulizi makubwa ya Urusi katika eneo la kati la Kyiv yamesababisha moto katika jengo la ghorofa ya juu na kulenga maeneo ya nishati mapema ya leo Ijumaa, na kukata nguvu za umeme katika sehemu za mji mkuu, maafisa walisema.

    Katika mji wa kusini mashariki wa Zaporizhzhia, ndege zisizo na rubani na makombora ziliharibu majengo 12 ya ghorofa, na kumuua mtoto wa miaka saba na kuwajeruhi watu wanne, gavana wa eneo hilo amesema.

    Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema watu 12 wamejeruhiwa, na wanane kati yao kupelekwa hospitalini.

    Waziri wa Nishati Svitlana Grynchuk amesema vikosi vya Urusi vilishambulia miundo mbinu ya nishati.

    "Wataalamu wa nishati wanafany akila wawezalo kudhibiti athari za shambulizi hilo," Grynchuk alisema kwenye Facebook.

    "Mara tu hali ya usalama itakaporuhusu, wataalam wa nishati wataanza kutathmini athari ya shambulio hilo na kuanza shughuli ya ukarabati."

    Takriban familia 28,000 ziliachwa bila huduma za umeme kufikia Ijumaa asubuhi katika mkoa wa Kyiv, Gavana Mykola Kalashnyk amesema.

    Soma pia:

  14. Kim Jong Un asifia hadhi ya kimataifa ya Korea Kaskazini

    Li ni wa pili kutoka kwa rais wa China Xi Jinping, na mahudhurio yake yanaashiria ziara ya ngazi ya juu zaidi ya Beijing huko Pyongyang tangu 2019.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Li ni wa pili kutoka kwa rais wa China Xi Jinping, na mahudhurio yake yanaashiria ziara ya ngazi ya juu zaidi ya Beijing huko Pyongyang tangu 2019.

    Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amesifu hadhi ya kimataifa ya nchi yake kama “mshirika mwaminifu wa majeshi ya kisoshalisti”, katika kile alichokiita kipindi cha ongezeko la heshima ya taifa lake mbele ya jumuiya ya kimataifa.

    Kauli hiyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wafanyakazi wa Korea, chama kinachotawala taifa hilo la kiimla.

    Sherehe hizo zimefanyika kwa mbwembwe kubwa, zikiambatana na makaribisho rasmi kwa wageni wa ngazi ya juu kutoka mataifa rafiki.

    Miongoni mwao ni Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, na Rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev.

    Akihutubia wageni na wananchi, Kim alisema licha ya taifa lake kukumbwa na “shinikizo kali la kisiasa na kijeshi” kutoka kwa mahasimu wake, heshima ya Korea Kaskazini kama mshirika mwaminifu wa mataifa ya kisoshalisti inaendelea kuimarika kila uchao.

    “Ingawa tunakabiliwa na mashinikizo makali, hadhi yetu kimataifa inaendelea kukua kama taifa linaloshikilia misingi ya kisoshalisti kwa uaminifu,” alisema Kim.

    Picha za vyombo vya habari vya serikali zilimuonesha Kim akiwapokea kwa bashasha wageni wa kimataifa, huku fataki, ngoma za kitamaduni na dansi za kitaifa zikiashiria uzito wa sherehe hizo.

    Uwepo wa viongozi kutoka mataifa mengine ya kisoshalisti, akiwemo To Lam, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, na Thongloun Sisoulith, Rais wa Laos, umechukuliwa kama dalili ya kuimarika kwa mahusiano ya Kimataifa ya Pyongyang, licha ya vikwazo vikali vya kiuchumi na kisiasa vinavyoiandama nchi hiyo.

    Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wameeleza kuwa maadhimisho haya ni ishara ya kurejea kwa Korea Kaskazini kwenye jukwaa la kidiplomasia.

    Prof. Yang Moo-jin wa Chuo cha Masomo ya Korea Kaskazini mjini Seoul alinukuliwa akisema: “Uwepo wa Waziri Mkuu Li Qiang unaonesha nia njema ya China na kuashiria kurejeshwa kwa uhusiano wa karibu kati ya Beijing na Pyongyang.”

    Ziara ya Li, ambaye ni kiongozi wa pili kwa mamlaka nchini China baada ya Rais Xi Jinping, ndiyo ya juu zaidi kutoka Beijing kwenda Pyongyang tangu mwaka 2019.

    Mwezi uliopita, Kim alionekana bega kwa bega na Rais Xi Jinping wa China na Rais Vladimir Putin wa Urusi katika Gwaride la Taifa jijini Beijing, kuadhimisha miaka 80 tangu Japan isalimishe rasmi Vita vya Pili vya Dunia. Hili liliashiria mara ya kwanza kwa Kim kushiriki hadharani mkutano wa viongozi wa dunia. Mahusiano ya karibu kati ya Korea Kaskazini na Urusi yamezidi kudhihirika, hasa baada ya Pyongyang kupeleka wanajeshi wapatao 15,000 kuisaidia Urusi katika uvamizi wake dhidi ya Ukraine.

    Leo Ijumaa, taifa hilo linatarajiwa kufanya gwaride la kijeshi la usiku, ambalo litahusisha maonyesho ya silaha mpya, makombora ya masafa marefu na vifaa vingine vya kivita.

    Hatua hii inalenga kuonesha uwezo wa Korea Kaskazini katika kujilinda, huku ikituma ujumbe kwa mahasimu wake wa kimataifa.

    Kwa watazamaji wa ndani na nje, maadhimisho haya si tu kumbukizi ya kihistoria, bali pia ni maonyesho ya ushawishi wa kisiasa, uhalali wa utawala, na ishara ya Korea Kaskazini kujitangaza upya kama mchezaji wa maana katika siasa za kimataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Tshisekedi amtaka Kagame awaondoe waasi wa M23 Mashariki mwa Congo

    g

    Chanzo cha picha, X/Présidence RDC, Paul Kagame/Flickr

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amemtaka mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, kuwaamuru waasi wa M23 kuondoka mara moja mashariki mwa Congo.

    Tshisekedi alisema hayo katika Mkutano wa Global Gateway uliofanyika jijini Brussels.

    Kauli yake inakuja wakati kuna ongezeko la mvutano kati ya nchi hizo jirani, na huenda ikazua hofu mpya kuhusu mustakabali wa usalama katika eneo hilo la Maziwa Makuu.

    Tshisekedi aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila kumaliza kabisa uingiliaji wa mataifa ya nje na kusitishwa kwa mashambulizi ya mipakani.

    “Amani katika eneo hili inahitaji kusitishwa kwa uingiliaji wa kigeni na kumaliza mashambulizi yanayovuka mipaka,” alisema Rais Tshisekedi.

    Nao Mamlaka za Rwanda zimemjibu Tshisekedi kwa tuhuma nzito, zikidai kwamba yeye mwenyewe ndiye anayechochea migogoro kupitia vitisho, misaada kwa wanamgambo, na ukiukaji wa makubaliano ya amani.

    Rais Kagame, kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), aliibeza kauli ya Tshisekedi kwa kusema: “Ni kelele za ngoma tupu.”

    Rwanda imeendelea kushutumu DRC kwa kuhusishwa na kundi la waasi la FDLR, ambalo linatuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, na ambalo bado linaendesha harakati zake mashariki mwa Congo.

    Rwanda pia inaituhumu serikali ya Congo kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa Wazalendo, kutumia mamluki wa kigeni, na kufanya mashambulizi ya anga.

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, kupitia mtandao wa X, alisema: “Ili kumaliza mvutano huu, Rais Tshisekedi anapaswa kulivunja kundi la wanamgambo la Wazalendo alilolianzisha, kulihami na kulifadhili kundi ambalo sasa limekuwa chanzo cha chuki na utesaji dhidi ya Watutsi wa Congo.”

    Licha ya jitihada zinazoendelea kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na viongozi wa kikanda, uhusiano kati ya Rwanda na DRC umezorota kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni.

    Huku viongozi wa dunia wakikutana kujadili masuala ya uwekezaji, swali kubwa linabaki: Je, marais hao wawili wanaweza kuondoa tofauti zao na kurejesha mazungumzo ya amani baada ya miezi kadhaa ya ukimya?

    Soma pia:

  16. Ufilipino na Indonesia zatoa tahadhari kuhusu tsunami baada ya tetemeko la ukubwa wa 7.4

    Wanafunzi wakitaharuki baada ya matetemeko ya ardhi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la seismolojia la Ufilipino limeonya kuwa linatarajia mawimbi ya tsunami “hatari kwa maisha,” baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea karibu na pwani ya Mindanao, kusini mwa nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa onyo hilo, mawimbi ya tsunami yanaweza kufikia hadi mita 3 (sawa na futi 10) juu ya kiwango cha kawaida cha bahari katika maeneo ya Ufilipino.

    Nchini Indonesia, yanaweza kufikia hadi mita 1.

    Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr., ametoa wito wa kuhamishwa kwa wakazi katika baadhi ya mikoa ya pwani, ili kuepuka madhara ya mawimbi hayo.

    Amesema kuwa operesheni za uokoaji na utoaji misaada zitaanza mara tu hali itakapokuwa salama.

    Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Rais Marcos ameandika: “Tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa msaada unawafikia wote wanaouhitaji.”

    Mamlaka za Indonesia zimesema bado hawajapokea taarifa za uharibifu kutokana na tetemeko hilo, lakini bado wanafuatilia hali kwa karibu.

    Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani zinaonesha hali ya taharuki nje ya hospitali katika Jiji la Davao, lililo karibu na kiini cha tetemeko hilo.

    Mamlaka za usimamizi wa maafa katika mji wa Manay hazijaripoti vifo au majeruhi hadi sasa, lakini imethibitishwa kuwa baadhi ya wanafunzi walizimia kutokana na mshtuko wa tetemeko hilo.

    Richie Diuyen, mfanyakazi wa idara ya maafa, amesema bado anahisi kizunguzungu kufuatia tetemeko hilo lililodumu kwa karibu dakika moja.

    “Bado nina hofu na situlii. Hatukuamini jinsi lilivyokuwa na nguvu. Hii ndiyo mara ya kwanza nashuhudia tetemeko kali kiasi hiki,” ameiambia BBC.

    Soma pia:

  17. Simu janja na skrini ni chanzo cha janga la kutengana katika familia - Binti mfalme wa Wales

    Catherine alitembelea kituo cha kusaidia familia huko Oxford

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Catherine alitembelea kituo cha kusaidia familia huko Oxford

    Binti mfalme wa Wales, Catherine Middleton, ameonya kwamba matumizi kupita kiasi ya simu janja na skrini za kompyuta yamesababisha kile alichokiita “janga la kutengana” ambalo linavuruga maisha ya kifamilia.

    Kupitia tahariri aliyoiandika kwa ushirikiano na Profesa Robert Waldinger kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Harvard, Catherine anasema kuwa, “Ingawa vifaa vya kidijitali vinaahidi kutuweka karibu, mara nyingi hufanya kinyume chake.”

    Anabainisha kuwa simu janja na vifaa vingine vya teknolojia vimegeuka kuwa “mashine za kutuvuruga kila mara,” vinavyotatiza umakini wetu na kuharibu muda wa thamani unaotumika pamoja kama familia.

    “Tupo kimwili lakini kiakili hatupo hatuwezi kushiriki kikamilifu na wale walioko mbele yetu,” ameandika Catherine katika insha hiyo, ambayo ni sehemu ya kampeni yake ya kuhamasisha uelewa kuhusu umuhimu wa malezi katika miaka ya awali ya mtoto.

    Kwa mujibu wa tafiti, binti wa kifalme wa Wales anasisitiza kuwa mahusiano ya karibu, yenye afya na joto ndani ya familia huleta manufaa ya maisha ya muda mrefu kimwili na kiakili.

    Hata hivyo, anatahadharisha kwamba mwenendo wa sasa wa kijamii unakwenda kinyume, huku watu wengi wakiishi katika hali ya upweke na kutengwa, na familia zikishindwa kupeana umakini wa kutosha.

    “Tunaposhika simu wakati wa mazungumzo, kuburuta mitandao ya kijamii wakati wa chakula cha familia, au kujibu barua pepe huku tukicheza na watoto wetu hatupotezi tu umakini, bali pia tunapunguza upendo wa msingi unaohitajika katika mahusiano ya kibinadamu,” ameandika.

    Ameeleza kuwa tatizo hili ni kubwa zaidi kwa watoto wa kizazi cha sasa ambao wanakua katika “mazingira yaliyojaa teknolojia ya kidijitali.”

    Hali hii, anasema, inaweza kudhoofisha uwezo wao wa kuendeleza uhusiano wa karibu, kuwasiliana kwa ufanisi na kustawi kihisia.

    Mwaka 2021, Catherine alianzisha Royal Foundation Centre for Early Childhood, taasisi inayolenga kuongeza uelewa na kuchochea tafiti kuhusu umuhimu wa miaka ya awali katika maisha ya mtoto.

    Lengo ni kuhakikisha kwamba watoto wanapokea malezi bora ambayo yatawasaidia kustawi kwa afya bora kimwili, kiakili na kijamii kwa maisha yao yote.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Mpango huo umeidhinishwa - hiki ndicho kitakachofanyika katika siku zijazo

    Hatua ya Israel kutia saini m[ango wa kusitisha mapigano huko Gaza inatoa nafasi ya utekelezaji wa masuala kadhaa – katika kipindi cha muda mfupi na mrefu.

    Haya hapa ni mambo manne ambayo yanatarajiwa kufanyika mara moja baada ya makubaliano kukamilika:

    1. Kusitishwa kwa mapigano huko Gaza

    Baada ya makubaliano hayo kuidhinishwa rasmi na baraza la mawaziri la Israel, usitishaji mapigano unatarajiwa kuanza kutekelezwa.

    Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha kuwa hili litafanyika mara moja, msemaji wa ofisi ya waziri mkuu amesema hatua hiyo itaanza kutekelezwa ndani ya saa 24 baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri.

    2. Wanajeshi wa Israel wataondoka

    Jeshi la Israel litajiondoa vitani lakini itaendelea kudhibiti takriban 53% ya Ukanda huo, msemaji huyo alisema. Kulingana na ramani iliyosambazwa na Ikulu ya White House wiki iliyopita, hii ni hatua ya kwanza kati ya hatua tatu za kujiondoa kwa Israel.

    3. Kubadilishana mateka na miili ya waliofariki

    Baada ya hayo, Hamas inatarajiwa mkuwaachilia mateka wote 20 wanaoaminika kuwa hai ndani ya muda wa saa 72. Hatua hiyo pia itajumuisha kurejeshwa kwa miili ya mateka 28 waliofariki, ingawa haijabainika hilo litachukuwa muda gani.

    Israel itawaachilia wafungwa 250 wa Kipalestina wanaotumikia vifungo vya maisha katika jela za Israel na wafungwa 1,700 kutoka Gaza, chanzo kimoja cha Wapalestina kiliiambia BBC.

    Israel pia itarudisha miili 15 ya watu wa Gaza kwa mabaki ya kila mateka wa Israel, kulingana na mpango wa Trump.

    4. Msaada kuiingia Gaza

    Mamia ya malori yaliyobeba misaada pia yataanza kuingia Gaza, ambako njaa ilithibitishwa na wataalam wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwezi Agosti.

  19. Israel yaidhinisha mpango wa Trump wa usitishaji mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka

    Gaza City on 9 October

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Mji wa Gaza Oktoba tarehe 9

    Serikali ya Israel imethibitisha rasmi kuidhinisha mpango wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza pamoja na mpango wa kuwaachilia mateka, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    “Serikali imeidhinisha mfumo wa kuwaachilia mateka wote walio hai na waliopoteza maisha,” imesema taarifa hiyo. Hata hivyo msemaji wa serikali ya Israel amesema kwamba Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litajipanga upya katika mstari mpya mara baada ya kuanza kwa usitishaji mapigano, hatua itakayowaacha wakidhibiti takribani asilimia 53 ya Ukanda wa Gaza.

    Hatua hiyo hata hivyo imewakera wakosoaji wa mpango huo, akiwemo mjumbe mmoja wa siasa kali za mrengo wa kulia ambaye aliishutumu Marekani kwa "kufikia amani na Hitler".

    Hatua hii inafungua njia kwa usitishaji mapigano kuanza kutekelezwa. Pia na mwanzo wa mfululizo wa hatua zingine ambazo zitawezesha kuachiliwa kwa mateka katika siku chache zijazo.

    Hamas sasa inatarajiwa kuanza kuhamisha mateka, na inatayarisha miili ya mateka ambao wamekufa. Hamas pia inatafuta miili ya baadhi ya mateka hao, ambayo imefukiwa chini ya vifusi.

    Huku hayo yakijiri Israel inajiandaa kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina ambao kuachiliwa kwao kumekumbwa na utata mkubwa.

    Umoja wa Mataifa unatarajiwa kutoa msururu wa misaada ya kiutu kama sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa Trump wa kusitisha mapigano.

    Maelezo zaidi:

  20. Twatumai hujambo.

    Katika kipindi cha saa chache zilizopita, kumekuwa na harakati nyingi za kidiplomasia duniani.

    Kikao cha baraza la mawaziri la Israel, hotuba ya Donald Trump huko Washington DC, pamoja na mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Kiarabu na Ulaya uliofanyika Paris.

    Karibu kwa matangazo haya ya moja kwa moja leo Ijumaa 10.10.2025.