Mtoto aliyezaliwa dakika chache kabla ya tetemeko la ardhi nchini Morocco

h
Maelezo ya picha, Mtoto wa Khadija alizaliwa dakika chache kabla ya tetemeko kuu la ardhi kupiga Morocco

Mtoto wa Khadija hata hana jina bado, lakini nyumba yake ya kwanza ni hema lililowekwa kando ya barabara.

Alizaliwa dakika chache kabla ya tetemeko la ardhi la Morocco kutokea Ijumaa usiku.

Ingawa mama na binti yake hawakujeruhiwa, hospitali ya Marrakesh walimokuwa ilihamishwa.

Baada ya uchunguzi wa haraka, walitakiwa kuondoka saa tatu tu baada ya kuzaliwa.

"Walituambia tulilazimika kwenda kwa sababu ya hofu ya matetemeko ya baadaye," alisema.

Wakiwa na mtoto wao mchanga, Khadija na mumewe walijaribu kuchukua teksi mapema Jumamosi hadi nyumbani kwao Taddart katika Milima ya Atlas, kama kilomita 65 (maili 40) kutoka Marrakesh.

Lakini walipokuwa wakielekea huko walikuta barabara zimezibwa na maporomoko ya ardhi, wakafika tu mpaka kijiji cha Asni.

Familia hiyo imekuwa ikiishi ndani ya hema kando ya barabara kuu tangu wakati huo.

"Sijapata usaidizi wowote kutoka kwa mamlaka," alituambia, akiwa amemshika mtoto wake mchanga akiwa amejikinga na jua chini ya kipande cha turubai.

"Tuliomba baadhi ya watu katika kijiji hiki mablanketi ili tupate kitu cha kutufunika.""Tuna Mungu pekee," aliongeza.

Tangu wakati huo, wameweza kujenga hema la msingi. Khadija alituambia ana nguo mbili za kuvaa za mtoto .

Marafiki kutoka mji wa kwao wameiambia familia kwamba nyumba yao imeharibiwa vibaya, na hawajui ni lini wanaweza kuwa na mahali pazuri pa kuishi.

Kuongezeka kwa hasira

Katika maeneo jirani na Khadija wengi wameonyesha kukasirishwa na usaidizi mdogo wa kuifikia miji na vijiji katika maeneo ya vijijini ya milima kusini mwa Marrakesh.

Asni ni eneo lililopo kilomita 50 tu (maili 30) kutoka Marrakesh, lakini watu wanasema wanahitaji kupelekewa msaada wa haraka.

Kundi la watu wenye hasira walimzingira mwandishi wa habari wa eneo hilo, wakielezea masikitiko yao kwake.

"Hatuna chakula, hatuna mkate wala mboga. Hatuna chochote," alisema mtu mmoja katika umati huo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

"Hakuna mtu aliyekuja kwetu, hatuna chochote. Tuna Mungu tu na mfalme."

h
Maelezo ya picha, Umati wa watu wenye hasira waliokuwa wakisubiri msaada walimzunguka mwandishi wa habari wa eneo la Asni

Tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi amekuwa akiishi kando ya barabara kuu ya kijiji hicho na watoto wake wanne.

Nyumba yake bado imesimama, lakini kuta zote zimepasuka vibaya na anagopa sana kuishi hapo.

Wameweza kurudi na kuchukua mablanketi, ambayo sasa ndio wanalazimika kuyalalia.

Lori lilipokuwa likipita katikati ya umati wa watu wengine walijaribu kulishusha, wakitumaini kwamba lilikuwa limebeba vifaa. Lakini iliendelea tu, likafuatwa kwa kelele.

Mwandishi aliyekuwa katikati ya umati wa watu alisindikizwa na polisi, bado akifuatwa na watu waliokuwa na hamu ya kudhihirisha hasira zao.

Baadhi ya watu wanasema wamepokea mahema kutoka kwa mamlaka, lakini hakuna mahali karibu ambapo watu wote wanaoyahitaji wanaweza kuyapata.

Mbarka, ni mtu mwingine anayeishi katika hema. Alituongoza kupitia mitaa ya kando hadi nyumbani kwake ambako hawezi kuishi tena.

g
Maelezo ya picha, Nyumba ya Mbarka iliharibiwa na tetemeko la ardhi

"Sina njia ya kujenga upya nyumba," Mbarka alisema. "Kwa sasa, ni watu wa ndani tu ambao wanatusaidia."

Aliishi na binti zake wawili, mkwe na wajukuu watatu.

Nyumba yao ilipoanza kutetemeka wakati tetemeko la ardhi lilipotokea, walitoka nje kwa kasi na nusura waangukiwe na nyumba kubwa zaidi iliyoanza kuteremka mlima kuelekea kwao.

"Tunafikiri serikali itasaidia," mkwewe Abdelhadi alisema, "lakini kuna vijiji 120 katika eneo hilo."

Kukiwa na watu wengi wanaohitaji msaada, idadi kubwa ya watu italazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi kwa usaidizi.