Tetemeko la ardhi Morocco: Vifo vyafikia 2,122

Tetemeko hilo la kipimo cha 6.8 lilipiga Marrakesh na miji mingi Ijumaa usiku

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapo tumefikia mwisho wa habari zetu za moja kwa moja kwa siku ya leo, tukutane kesho majaliwa

  2. Watu 35 wauawa soko likishambuliwa huko Sudan

    Sudan

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 35 wameuawa baada ya soko lililofurika watu katika mji mkuu wa Sudan kushambuliwa kwa "silaha za milipuko", shirika la misaada la matibabu linasema.

    Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) lilieleza kuwa ni "mauaji", na kusema kuwa zaidi ya watu 60 pia wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

    Wafanyakazi wa kujitolea wa ndani wanasema ndege ya kijeshi ilishambulia soko la Qouro kusini mwa Khartoum siku ya Jumapili.

    Makundi hasimu ya kijeshi yamekuwa yakipigana tangu Aprili. Siku ya Jumapili mratibu wa dharura wa MSF Marie Burton alisema Khartoum "imekuwa kwenye vita kwa karibu miezi sita".

    "Lakini hata hivyo, wafanyakazi wa kujitolea na wafanyakazi wa matibabu katika hospitali ya Bashair wameshtushwa na kuzidiwa na ukubwa wa hofu iliyolikumba jiji hilo" siku ya Jumapili, aliongeza kwenye X, zamani Twitter.

    "Tunajaribu kuokoa maisha ya watu ambao viungo vyao vya mwili vimeng'olewa na mlipuko huo. Ilikuwa mauaji," MSF iliongeza.

    Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili, 2023 baada ya mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kutofautiana.

    Takriban watu milioni tano wamelazimika kuyakimbia makazi yao, na maelfu wameuawa. Khartoum na eneo la magharibi la Darfur zimeathiriwa zaidi na mzozo huo.

  3. Tetemeko Morocco: 'Waokoaji wanakabiliwa na changamoto kubwa kutoa watu kwenye vifusi'

    mOROCCO

    Kufikia vijiji vya mbali na kuvuta watu kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporpmoka ni "kipaumbele kikubwa", mfanyakazi wa misaada ameiambia BBC.

    Caroline Holt wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu aliongeza kuwa bado changamoto zinazowakabili waokoaji ni kubwa. Mashine nzito zinahitajika ili kusafisha njia kwa jamii zilizoathirika zaidi katika Milima ya Atlas, aliongeza.

    Bado kuna changamoto ya misaada kuwafikia waathiriwa. Mwandishi wa BBC Alice Cuddy ametembelea kijiji cha Amizmiz, katika milima hiyo, sio mbali sana kna mji wa Marrakesh anasema misaada bado inahitajika.

    Ameshuhudia baadhi ya watu wakilala kando ya barabara kusubiri misaada ya ndani na nje.

    Kuna hofu idadi ya vifo kuongezeka kutoka 2,000 ya sasa hasa katika maeneo ya milimani ambapo kufikika imekuwa changamoto huku wengi huko wakihitaji usaidizi.

    Morocco
  4. Moto mlima Kilimanjaro waingia siku ya 7 juhudi za kuuzima zikiendelea,

    MOTO KILI

    Mamlaka nchini Tanzania kwa kushirikiana na wananchi wanapambana kuzima moto uliozuka katika eneo la Indonet-Rongai lililopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA)

    Mpaka sasa chanzo cha moto huo ulioanza Jumapili iliyopita bado haujafahamika ambapo tayari umeteketeza ukanda wa juu mita 3,900 kutoka usawa wa bahari, kaskazini mashariki mwa hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya Rombo.

    Hata hivyo mamlaka zimeeleza kuwa moto huo umedhibitiwa kwa asilimia 90, huku eneo lenye ukubwa wa Kilometa za mraba 17 sawa na asilimia 0.9 ya eneo lote la hifadhi, likidaiwa kuteketea kwa moto.

    Akizungumza kutoka wilayani Rombo, Kaskazini mwa Tanzania, Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa uhifadhi, Angela Nyaki amesema eneo ambalo limeungua lina mimea jamii ya Erika na majani ambayo ikishika moto huwaka kwa kasi.

    Amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana lakini akabainisha kuwa huenda shughuli za kibinadamu zikawa chanzo.

    Hili si mara ya kwanza moto kutokea kwenye maeneo ya Mlima Kilimanjaro. Mnamo 2022, moto uliwaka kwa zaidi ya mwezi mmoja na kuharibu maelfu ya hekta za msitu inayozunguka mlima huo.

  5. Kiongozi wa Upinzani Tanzania, Lissu ashikiliwa na Polisi

    Lissu

    Chanzo cha picha, Lissu

    Makamu Mwenyekiti wa chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania,CHADEMA na mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi mkuu wa 2020, Tundu Lissu anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

    Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, Lissu amekamatwa leo Karatu Arusha, alikokuwa anatarajiwa kufanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mazingira Bora.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Lissu, mbunge wa zamani na mwanasheria, ambaye aliwahi kunusurika kuuawa kwa kupigwa risasi 16 miaka 6 iliyopita anatuhumiwa kwa makosa mawili; kufanya mikusanyiko bila kuwa na vibali na kuzuia Polisi kufanya kazi yao.

    Ruka X ujumbe, 1
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 1

    Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo inaeleza Lissu na viongozi wengine watatu wa chama hicho, watahojiwa na Polisi na utaratibu mwingine wa kisheria kuendelea.

    Kwa mujibu wa viongozi wa CHADEMA, kabla ya kumamatwa kwa Lissu, hoteli aliyofikiwa kiongozi huyo inayoitwa Ngorongoro na nyingine ya Panorama huko Karatu zilizingirwa na Polisi.

    Ruka X ujumbe, 2
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 2

  6. Tetemeko Morocco limeathiri zaidi ya watu 300,000 - UN

    Morocco

    Chanzo cha picha, Getty Image

    Zaidi ya watu 300,000 huko Marrakesh na viunga vyake wameathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Morocco, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inasema.

    OCHA Ilisema: "inafuatilia kwa karibu hali hiyo na iko tayari kuunga mkono juhudi".

    Katika taarifa ya awali, Umoja wa Mataifa ulisema uko tayari "kuisaidia serikali ya Morocco katika juhudi zake za kuwasaidia watu walioathirika".

    Waokoaji wanaendelea kuhangaika kutafuta manusura waliofukiwa na vifusi baada ya tetemeko hilo kubwa la ardhi lililoua zaidi ya watu 2,000.

  7. Ethiopia yakamilisha kujaza maji kwenye bwawa lenye Utata katika Mto Nile

    Ethiopia GERD

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ethiopia inasema imekamilisha awamu yake ya nne na ya mwisho ya kujaza maji bwawa kubwa lenye utata katika eneo la Blue Nile.

    Tangazo hilo lilitolewa leo Jumapili, wiki kadhaa baada ya mazungumzo kati ya Addis Ababa na nchi mbili zinazonufaika na mto Nile- Misri na Sudan. Mazungumzo yalianza tena kwa nia ya kutia saini makubaliano yenye nguvu ya kukabiliana na ukame katika siku zijazo.

    Duru mpya ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika mwezi huu wa Septemba.

    Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) lenye thamani ya dola bilioni 5 limekuwa katikati ya mazungumzo ya kidiplomasia katika muongo mmoja uliopita- kati ya Ethiopia na nchi hizo mbili ambazo zinahofia kwamba upatikanaji wao muhimu wa maji kupitia mto Nile unaweza kutishiwa au kuathiriwa na mradi huo.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter) Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisifu kukamilika kwa ujazo huo kama hatua kubwa ambayo ilifanyika licha ya "changamoto za ndani na shinikizo kutoka nje."

    Habari hizo zinakuja huku kukiwa na ghasia zinazoendelea na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama katika maeneo mengi kote nchini Ethiopia- nchi ambayo bado inakabiliwa na makovu ya vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili, vilivyomalizika mwaka jana kwa makubaliano ya amani.

  8. 'Ukraine imebakiza siku 30 tu za kupambana na Urusi'

    Ukraine

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine imesalia na siku zisizozidi 30 za mapigano dhidi ya Urusi kabla ya hali ya hewa kuzuia mashambulizi yake, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani anasema.

    Akiongea na BBC Jumapili kupitia kipindi cha Laura Kuenssberg, Jenerali Mark Milley alisema hali ya baridi itafanya iwe vigumu zaidi kwa Ukraine kutekeleza mashambulizi.

    Alikiri mashambulizi hayo yalikwenda polepole zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Lakini alisema: "Bado kuna mapigano makali yanayoendelea. "Waukraine bado wanasonga mbele na wamekuwa na maendeleo thabiti."

    Jenerali Milley alisema ni mapema mno kusema kama mashambulizi ya kukabiliana na mashambulizi ya Urusi yameshindwa, lakini akasema Ukraine "inaendelea kwa kasi ya utulivu katika mstari wa mbele wa Urusi".

    "Bado kuna muda wa kutosha, labda takriban siku 30 hadi 45 kabla ya hali ya hewa mbaya kuanza, kwa hivyo Waukraine hawajamaliza. "Kuna vita ambavyo havijafanyika... hawajamaliza sehemu ya mapigano ya kile wanachojaribu kutimiza."

  9. Wakati mkutano wa G20 ukifikia tamati leo, Ukraine yakasirishwa na tamko

    G20

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Uingereza zimepongeza tamko la pamoja la G20, ingawa Ukraine haijafurahishwa sana na tamko la nchi hizo tajiri duniani. Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan aliita taarifa hiyo akisema "hatua muhimu" kwa "kura ya imani kwamba G20 inaweza kuja pamoja kushughulikia masuala kadhaa muhimu".

    Naye Waziri Mkuu Sunak alisema tamko hilo la pamoja lina "lugha kali sana" kuhusu vita vya Ukraine. "Kile utakachoona katika taarifa ni lugha kali, inayoangazia athari za vita kwa bei ya chakula na usalama wa chakula," Sunak alisema.

    Lakini hivyo sivyo Ukraine inavyoliona tamko hilo. Oleg Nikolenko, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, alisema G20 haina “chochote cha kujivunia.” Alionyesha hasa sehemu ya tamko lililosema "vita vya Ukraine" - Kyiv inapendelea kuiita "vita dhidi ya Ukraine".

    India imeshangaza kila mtu kwa kuandaa mkutano huo wa viongozi wa nchi tajiri duniani (G20) na kukubaliana juu ya tamko hilo la pamoja. Lakini wachambuzi hakukuwa na msisito mkubwa kuhusu vita vya Ukraine kama ilivyokuwa kwenye tamko la Bali la mkutano wa mwaka jana.

    Azimio la Delhi haliikosoi Urusi moja kwa moja kwa kuivamia Ukraine na kuendelea na vita. Lakini inazungumzia "mateso ya binadamu na athari mbaya za vita vya Ukraine kuhusiana na usalama wa chakula na nishati duniani". Pia inabainisha kuwa "kulikuwa na maoni tofauti na tathmini ya hali hiyo".

    Tamko la mwaka huu pia linatoa wito kwa mataifa "kujiepusha na tishio au matumizi ya nguvu kutafuta umiliki wa eneo", ambayo inaweza kuonekana kama linaelekezwa kwa Urusi.

    Moja ya mambo yaliyokubalika kwenye tamko ni kujumuishwa kwa Umoja wa Afrika na kuwa mwanachama wa kudumu wa G20. Kwa bara la watu bilioni 1.4, ni uamuzi wa kihistoria kwani sasa watakuwa na uwakilishi mpana kwenye jukwaa la kimataifa kama G20.

  10. Wamorocco wanalala mtaani baada ya tetemeko la ardhi kuua watu 2,000

    Morocco

    Chanzo cha picha, Reuters

    Huko Marrakesh, maelfu ya watu wamekuwa wakitumia usiku wa pili kwenye maeneo ya wazi kulala. Maeneo ya mapumziko, maeneo ya kuegesha magari na viwanja vya umma vimejazwa na idadi kubwa ya watu wa kila rika wakijilaza kwenye mablanketi. Wachache wanaonekana kulala, wengi wako macho wakitafakari na kuhuzunika.

    Kuwa katika usalama wa kiasi wa nje hakuondoi hofu ya kile ambacho tetemeko lingine linaweza kutokea.

    Kuna vifusi katika mitaa mingi ya jiji hili la kihistoria la Marrakesh ingawa jiji hilo limekuwa na haueni kuliko maeneo ya milimani kusini-magharibi.

    Mmiliki wa mgahawa, Safa El Hakym, anajaribu kukubaliana na kilichotokea. "Asante Mungu ni kuta na vifaa ambavyo vimepotea," anasema. "Mambo muhimu zaidi hayapotei. "Na tunamshukuru Mungu tuna nguvu ya ubinadamu nchini Morocco: sote tuko pamoja na kuweka mioyo yetu katika hili na kusaidiana."