Jinsi wahamiaji wa Kiafrika wanavyoishi kwa hofu nchini Marekani

Chanzo cha picha, US Immigration and Customs Enforcement
- Author, Yusuf Akinpelu
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wahamiaji kutoka mataifa ya Kiafrika walio nchini Marekani wanahofia kurejeshwa nyumbani baada ya utawala wa Trump kuimarisha msako dhidi ya wahamiaji haramu.
Baadhi ya wahamiaji hao wanalazimika kujificha kwa sababu wanahofia wanaweza kukamatwa na kurudishwa makwao kwa lazima.
Waliiambia BBC kwamba hawatoki nyumbani, hawaendi kazini, na wanadhibiti shughuli zao za umma, na kuwazuia watoto wao kuenda shule kwa hofu ya kushikiliwa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE).
Mmoja wao ni Kaduli, mhamiaji kutoka Congo aliyeingia Marekani miaka 11 iliyopita.
Kaduli alizaliwa Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, karibu na Goma, ambayo hivi karibuni ilitekwa na waasi wa M23.
Alikuwa daktari mkuu kabla ya kukimbia DR Congo ili kuepuka kukamatwa baada ya kumkosoa Rais wa wakati huo, Joseph Kabila, kwa kubadilisha katiba ili kuongeza muda wake madarakani.
Kaduli ameiambia BBC kuwa sasa amepunguza shughuli zake nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na kuenda kwenye migahawa na maduka, kwa sababu anahofia kuwa atafukuzwa kwa nguvu.
"Shambulio la sasa linatufanya tuishi kwa hofu ya kudumu kwa sababu wanachanganya wahamiaji wote na wahalifu, ambayo si kweli," anasema.
"Ninaogopa kwa sababu Congo inakabiliwa na vita, Congo inaendelea na utawala wa ukandamizaji. Kumrudisha mtu Congo ni kumuweka hatarini."
Sawa na Kaduli, Abdul kutoka Nigeria pia yuko anaishi kwa hofu.
Alikuja Marekani na baba yake akiwa na umri wa miaka kumi, miaka 30 iliyopita.
"Ninajaribu tu kuepuka machafuko na kuwa na imani kwamba kila kitu kitakuwa sawa," anasema mkazi wa Wisconsin.
Abdul amesikia na kuona jinsi maafisa wa ICE wanavyotekeleza operesheni zao katika miji mingine. Anasema anaogopa kwamba atakutana na hatima ileile.
"Ishara ni za kushangaza jinsi wanavyowatendea watu kama vile sisi si wanadamu pia. Sisi sote ni wanadamu, na sote tunadunda damu sawa," anasema.
Wahamiaji wote waliokolewa kwa ajili ya simulizi hii walitaka kujulikana kwa majina yao ya kwanza pekee, kwa hofu ya kulipiziwa kisasi au kufuatiliwa na mamlaka.
Kuondolewa kwa watu

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu kurejea White House mnamo Januari, utawala wa Trump umeongeza kasi ya msukumo wake wa kufukuza wahamiaji kwa wingi, akifanya mashambulizi dhidi ya wahamiaji wasio na hati rasmi katika miji mikubwa.
Umehamasisha rasilimali za kijeshi ili kuipa nguvu Idara ya Uhamiaji kufanya zaidi ya kukamata, ikiwa ni pamoja na katika shule, makanisa na hospitali, jambo linalopokelewa kwa ukosoaji kutoka kwa makundi ya haki za kiraia na wahamiaji.
Maelfu ya watu, wakiwemo wahalifu na wale wasio na historia ya uhalifu, wamekamatwa.
Juma lililopita, maafisa wa ICE waliongeza kasi ya kukamata, wakishikilia watu karibu elfu moja kwa siku.
Kwa kulinganisha, utawala wa Joe Biden ulitekeleza uhamisho wa wahamiaji wastani wa 311 kwa siku, wengi wao wakiwa ni wahalifu, kulingana na ICE.
Serikali ya Trump pia inazingatia kutekeleza Sheria ya Maadui wa Kigeni ambayo inaweza kuruhusu mamlaka kufukuza wahamiaji kwa haraka wanaochukuliwa kuwa sehemu ya " uvamizi wa kinyonyaji, sheria ambayo awali ilitumika tu wakati wa vita.
Pious Ali, mjumbe wa baraza la jiji la Portland katika jimbo la Maine, anasema ingawa kufukuzwa si jambo jipya, mchakato unatumiwa vibaya kwa kushambulia maeneo kama shule, makanisa na sinagogi na "kuoneshwa hadharani watu" kama wahalifu.
Anasema kwa wahamiaji wanaohofia, ni muhimu "kuandika mpango kwa familia yako na kuweka chakula na pesa kando".
"Ikigongwa mlango wako na afisa, hawawezi kuingia bila amri ya mahakama," anasema.
Hali ya ulinzi kwa muda

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wahamiaji wengi kutoka Afrika wanaishi kwa wasiwasi kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu kuanzishwa upya kwa umiliki wa nchi zao chini ya mpango wa Hali Iliyolindwa kwa Muda (TPS).
Programu huwapa ruhusa Wahamiaji haswa wanaotoka katika mataifa – kama vile nchizi zinazokabiliwa na uhalifu wa kivita, majanga au hali nyingine za kipekee kupata hifadhi nchini Marekani na pia kuomba vibali vya kufanya kazi.
Sylvie Bello, mkurugenzi mtendaji wa baraza la Cameroon na Marekani (CAC), shirika la Washington linalowakilisha wahamiaji kutoka Afrika ya Kati, anasema kutokuwepo kwa uhakika huu kunatokana na sera za utawala wa awali wa Biden. Anasema jamii yake ilikuwa na matumaini kuwa Biden angeongeza programu hii yaTPS kwa Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati alipotembelea nchi hizo mwezi Novemba, akiwa ni rais pekee aliyetembelea bara hilo.
"Hata hivyo, alitusahau," anasema. "Wafrika weusi ambao hawakupata kuongezewa muda wa TPS huenda wakakabiliwa na hatari ya kufurushwa Marekani baada ya agizo la rais wa sasa Trump''
Takriban wahamiaji milioni moja kutoka nchi 17 – tano kati ya hizo kutoka Afrika – wanalindwa na programu ya TPS. TPS kwa wahamiaji kutoka Cameroon, Ethiopia, na Sudan Kusini inatarajiwa kumalizika mwaka huu. TPS kwa wahamiaji kutoka Somalia na Sudan itamalizika mwaka 2026.
"Jamii yangu yote inateseka kutokana na hofu ya kufukuzwa," anasema Sylvie Bello.
Kuishi kwa wasiwasi
Katika miaka ya hivi karibuni, Waafrika wamegeukia njia za uhamiaji kwenda Marekani kupitia Amerika ya Kusini na Mexico. Nneka Achapu,mwanaharakati wa sera za Marekani-Afrika anayeishi Texas, anasema hili linatokana na kuwa kuvuka Mediterania kwenda Ulaya kunachukuliwa kuwa hatari sana.
Kulingana na ripoti ya kila mwaka ya ICE ya 2024, takribani watu 1,818 kutoka Afrika walifukuzwa kutoka Marekani, huku Senegal, Mauritania, na Nigeria zikiongoza orodha.
Kati ya wahamiaji milioni 1.4 ambao wanatarajiwa kufukuzwa kutoka nchini Marekani na ICE kufikia Novemba 2024, Waafrika ni asilimia tatu pekee.
Somalia inangoza orodha kwa watu 4,090, ikifuatiwa na Mauritania yenye 3,822, Nigeria 3,690, na Ghana 3,228.
Kujua kwamba kuna maagizo ya mwisho ya kufukuzwa kwa watu hawa kunazidisha hali ya kutokuwa na uhakika na wasiwasi unaozikumba jamii za wahamiaji kutoka Afrika.
"Tutalazimika kupitia hili kwa miaka minne au kadiri hali hii itakavyodumu," anasema Abdul.
Hata hivyo, mwanamkakati wa sera za Marekani-Afrika, Nneka Achapu, anasema hali hii inaweza kuwa fursa kwa jamii ya Waafrika nchini Marekani kuonesha uimara wao.
"Kadiri watu wanavyokutana na mashambulizi dhidi ya wahamiaji, tunakumbushwa kwamba nguvu za jamii za Waafrika zinatokana na kufanya kazi pamoja, kulinda walio hatarini zaidi, na kushiriki rasilimali muhimu," anasema.
Achapu anaamini kwamba kipindi hiki cha kutokuwa na uhakika ni fursa kwa serikali za Afrika kujipanga upya, kukabiliana na sababu za msingi za uhamiaji, na kuunda fursa za kiuchumi kwa watu wao.
"Ikisema Marekani itaendelea kuwafukuza wahamiaji, China, Urusi, na nchi nyingine za kimataifa zinaweza kutumia fursa hii kupanua ushawishi wao barani Afrika, wakitoa njia mbadala za uhamiaji, ushirikiano wa kiuchumi, na makubaliano ya biashara ambayo yanaweza kubadilisha uhusiano wa Marekani na Afrika kwa njia ambazo bado hatujazielewa kikamilifu," anasema.
Kaduli, daktari wa zamani kutoka DRC, pia ana ujumbe kwa Trump.
"Kufanya Marekani kuwa kubwa tena, Marekani inahitaji kusimamia haki za binadamu na kuzingatia vipaji vya wahamiaji ili kuhudumia nchi na kusaidia uchumi," anasema.
"Ningemwambia rais kuweka sababu za kibinadamu mbele ya siasa."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












