Kipi kinachoweza kudhibiti mamlaka ya Rais Trump?

US President Donald Trump holds out his hand in a fist with red and yellow lights behind him during the inaugural parade inside Capital One Arena on inauguration day

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump akinyoosha ngumi wakati wa gwaride la kuapishwa huko Capital One Arena
    • Author, Ángel Bermúdez
    • Nafasi, BBC News Mundo
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kutekeleza mabadiliko makubwa katika muhula wake wa pili kama rais wa Marekani.

Baada ya kuapishwa alitia saini msururu wa hatua za kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kutangaza hali ya dharura ya kitaifa katika mpaka wa Marekani na Mexico, kuyataja makampuni ya madawa ya kulevya kama mashirika ya kigaidi na kuwasamehe waliohusika katika ghasia za tarehe 6 Januari.

Wakati wa kampeni yake, Mrepublican huyo aliapa kuwahamisha maelfu ya wahamiaji wasio na vibali, kuondoa urasimu wa serikali, kupunguza kodi, na kuanzisha ushuru mpya kwa bidhaa za kigeni.

Ili kufikia malengo yake, Trump anategemea wingi wa wawakilishi wa Chama cha Republican katika Congress na majaji wa kihafidhina katika Mahakama ya Juu. Lakini kuna changamoto zingine.

Haya ni mambo sita ambayo wataalam wanasema yanaweza kutatiza mipango yake.

Pia unaweza kusoma

Wawakilishi wa Congress

Mike Johnson, the Speaker of the US House of Representatives, speaks to journalists while wearing a navy suit and a beige tie. Two men stand behind him.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mike Johnson, Spika wa Bunge la Marekani, akizungumza na waandishi wa habari

Wa-Republican wana wingi wa wawakilishi katika mabaraza yote mawili ya Congress. Katika Bunge, kupitia uchaguzi wa Novemba umeipa Republican viti 220 ikilinganishwa na 215 vya Democrats.

Wabunge wawili wa chama cha Republican wamejiuzulu na mmoja anatarajiwa kujiuzulu, na hivyo kupunguza idadi yao - na uchaguzi wa kujaza viti hivyo utafanyika miezi ijayo.

"Ni wengi lakini ni wingi usiotosha katika nyakati za sasa," anasema Prof Mark Peterson, mtaalamu wa sera, sheria na sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Anasema Warepublican "ni wa moja," lakini, ni vigumu kuwaweka pamoja katika masuala magumu.

Katika Seneti, Warepublican wana viti 53, ikilinganishwa na 47 vya Democrats. Hii ina maana wingi wao sio mkubwa sana wa kuepuka mkwamo mara zote.

Hata hivyo, utaratibu unaojulikana kama 'upatanisho' unairuhusu Seneti kuidhinisha bajeti kwa wingi mdogo wa kura 51.

Wanachama wa Republican wanaweza kufikia baadhi ya malengo yao kwa mchakato huu, anasema Prof Peterson, lakini "Democrats wanao uwezo wa kuzuia karibu kila kitu kingine".

Prof Peterson anadokeza, katika nusu ya kwanza ya muhula wake wa kwanza, Trump alikuwa na wingi wa wakilishi katika vyombo vyote viwili, lakini sheria pekee aliyoipitisha ilikuwa ni mswada wa kupunguza ushuru.

Mahakama huru

The nine judges of the US Supreme Court shown in a formal photo, wearing black robes with five seated and four standing behind them

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Majaji tisa wa Mahakama ya Juu ya Marekani kwenye picha rasmi

Mahakama ya Juu ndiyo mahakama kubwa zaidi ya Marekani, na majaji wake huchaguliwa na marais pale nafasi zinapokuwa wazi.

Majaji sita kati ya tisa kwa sasa ni wahafidhina, watatu kati yao waliteuliwa na Trump wakati wa muhula wake wa kwanza. Lakini hilo haitoi hakikisho kwamba maamuzi yote ya mahakama kuhusu mipango ya utawala wake yataungwa mkono.

Mahakama ya Juu ilirejesha mamlaka kwa serikali za majimbo kufanya uamuzi ya ikiwa uavyaji mimba ni ruhusa au la, mwaka 2022 - hukumu hiyo iliungwa mkono na walioteuliwa na Trump - kama alivyoahidi wakati wa kampeni yake ya 2016.

Hata hivyo, mahakama hiyo imeunga mkono baadhi ya mambo ambayo ni kinyume na Republican, kama sheria ya huduma nafuu za afya - inayojulikana kama Obamacare - pamoja na baadhi ya kanuni za ulinzi dhidi ya ubaguzi mahali pa kazi kwa watu wa LGBT.

A 2019 protest in front of the US Supreme Court in favour of migrants, with a protester holding a red sign that reads: Defend DACA #dacahope

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mahakama ya Juu ilihitimisha kuwa jaribio la Trump la kuondoa mpango wa Daca ni kinyume cha sheria

Mahakama ya Juu pia ilikataa jaribio la kutengua matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020 na matakwa ya kusitisha mpango wa Daca, ambao unawalinda wahamiaji walioingia Marekani kinyume cha sheria wakiwa watoto.

Kulingana na Kituo cha Utafiti cha Pew, 60% ya majaji wa mahakama za wilaya walio katika majukumu yao waliteuliwa na marais wa Democratic, wakati 40% pekee waliteuliwa na Republican.

Prof Peterson anabainisha kuwa majaji wanaongozwa na sheria na kanuni zilizowekwa na Mahakama ya Juu, na anasema idara ya mahakama "imesalia kuwa tawi la tatu la serikali lenye uhuru wa hali ya juu."

Serikali za majimbo na za mitaa

Protesters carrying signs including one saying "yes to immigrants" at a march in Los Angeles in December 2024

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji wakiwa wamebeba mabango ya "ndio kwa wahamiaji" kwenye maandamano huko Los Angeles Desemba 2024.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Muundo wa serikali ya shirikisho ya Marekani unaweka kikomo juu ya mabadiliko yanayoweza kuanzishwa na Ikulu ya Marekani kwenda katika majimbo.

Marekebisho ya 10 ya katiba ya Marekani yanatoa mamlaka makubwa kwa serikali za majimbo, ambazo kwa kawaida husimamia usalama, afya, elimu, manufaa ya kijamii, sheria ya jinai, kanuni za kazi na sheria za mali. Kaunti na miji hushughulikia usalama wa umma, mipango miji na matumizi ya ardhi.

Prof Peterson anaamini Wa-Democratic watatumia mamlaka haya kuleta changamoto kwa utawala wa Trump katika ngazi ya majimbo.

Anabainisha kuwa California, ambako anaishi, ndilo jimbo kubwa zaidi la nchi hiyo na lina "uchumi wa tano kwa ukubwa duniani."

Anatarajia, majimbo mengine mengi "kufanya mambo nje ya yale ambayo Utawala wa Trump unataka yafanywe au kupinga utawala wa Trump - kama vile Texas na majimbo mengine yaliyotoa changamoto kwa utawala wa Biden na utawala wa Obama huko nyuma."

Hivi sasa, majimbo 23 kati ya 50 ya Marekani yana magavana wa Democratic.

Baadhi ya mipango ya Trump, kama vile kuwafurushwa wahamiaji wasio na hati, utahitaji usaidizi kupitia majimbo na mpango huo unaweza kutatizika katika ngazi ya serikali za majimbo au ya mitaa.

Miji na majimbo mengi yamejitangaza kuwa "mahali salama" kwa wahamiaji, na hivyo kuzuia ushirikiano na serikali ya shirikisho.

Utumishi wa umma

Sign outside FBI building in Pennsylvania, with office buildings and trees in the background

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Shirika la Upelelezi la FBI ni mojawapo ya mashirika ya serikali ambayo utawala wa Trump unataka kuyafanyia mageuzi.

Wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, Republicans walilalamika kuwa kuna changamoto katika kutekeleza ajenda zao, kutokana na upinzani kutoka kwa maafisa wa umma ndani ya utumishi wa umma.

Kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza, Trump alitia saini amri, ambayo ilimruhusu kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi wa umma na kuwaweka wafuasi wake.

Rais wa zamani Joe Biden alifuta kanuni hiyo, lakini Rais Trump ameirudisha siku ya kwanza ya muhula wake wa pili. Pia amewaamuru wafanyakazi wa shirikisho wanaofanya kazi wakiwa nyumbani warudi katika ofisi zao.

Makundi ya kihafidhina yaliyo karibu na Trump yameunda hifadhidata za wataalamu wanaowaona wanafaa kuchukua nafasi za maafisa wa umma.

One Union, muungano wa wafanyakazi wa Hazina ya taifa, tayari umeanzisha kesi ya kisheria dhidi ya utaratibu huo mpya.

Prof Peterson anasema anatarajia hatua kama hizo za Rais Trump kukumbana na upinzani mkali wa kitaasisi, kisheria, kisiasa na vyama vya wafanyikazi.

Mashirika ya kiraia

A protester dressed in black, wearing sunglasses and a white headscarf, holds up a white sign that reads: "I didn’t need to do this — Donald Trump. #NOTANATIONALEMERGENCY."

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwandamanaji aliyevalia mavazi meusi, miwani ya jua na kitambaa cheupe kichwani.

Trump huenda akakabiliwa na ukosoaji kutoka vyombo vya habari vyenye mwelekeo wa kiliberali na mashirika ya kiraia, kama vile American Civil Liberties Union (ACLU).

Shirika hilo lina wanachama milioni 1.7, ACLU imesema itajaribu kuzuia baadhi ya mapendekezo yake, kwani yatasababisha kutengana familia za wahamiaji, kudhuru afya ya uzazi na kuleta ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na wapinzani wa kisiasa.

Siku ya Jumatatu, ACLU na makundi mengine walifungua kesi kupinga mipango yake ya kukomesha uraia wa kuzaliwa. Mpango ambao unatoa uraia wa moja kwa moja wa Marekani kwa mtu yeyote aliyezaliwa Marekani.

Maoni ya umma

Red, white and blue balloons and glitter are dropped into a crowded arena at the Republican National Convention in July

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Wachambuzi wanaeleza kuwa baadhi ya Warepublican walimpigia kura Trump lakini hawaungi mkono sera zake zote

Prof Peterson anasema sio kila mtu aliyempigia kura Trump anaunga mkono sera zake zote.

Baadhi ni Warepublican ambao hawampendi Trump lakini wanataka ushuru ushuke na kanuni zipungue - huku wengine walimchagua kwa sababu walimwona kuwa chaguo bora zaidi katika kukabiliana na mfumuko wa bei.

Mambo haya yanaweza kutoa shinikizo kwa Trump kufikiria mara mbili mbili juu ya maamuzi yake, ili kudumisha uungwaji mkono wa urais wake na pia kutoa nafasi kwa wana-Republican kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2026.

Pia, baadhi ya wataalamu wanasema ahadi za Rais Trump za kuinua uchumi na kupunguza mfumuko wa bei huenda zikaathiriwa na baadhi ya mipango yake mingine, kama vile ushuru mkubwa wa forodha na uhamisho wa wahamiaji.

Mwanauchumi John Cochrane wa Taasisi ya Hoover anasema swali muhimu ni jinsi Trump atakavyotatua mvutano kati ya watu wake wanao unga mkono biashara na "wahafidhina" ambao wataka tu udhibiti wa mipaka na uadui na China.

"Ni wazi, kambi zote mbili haziwezi kupata wanachotaka kwa wakati mmoja," anasema Cochrane. "Na ndiyo sababu hatuwezi kutabiri nini kitatokea."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah