Kwa nini Urusi inaendelea kukishambulia kiwanda hiki licha ya kuwa tayari kimeshasambaratika?

Chanzo cha picha, Kremenchuk City Hall
- Author, Diana Korishko
- Akiripoti kutoka, BBC Ukrainian
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Urusi imekabiliana na mji wa kati wa Ukraine, Kremenchuk, kwa mashambulizi makali zaidi mwezi Agosti, saa chache tu baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kumaliza mkutano na viongozi wa Ulaya mjini Washington.
Kwa mujibu wa Jeshi la Anga la Ukraine, Moscow ilitumia ndege zisizo na rubani (drones) takribani 270 na roketi kadhaa za aina ya cruise katika mashambulizi haya. Ukraine inadai kuwa imefanikiwa kuzuia ndege nyingi kati ya hizo.
Gavana wa Mkoa wa Poltava, ambapo Kremenchuk ipo, alisema mashambulizi hayo hayakusababisha vifo, lakini yalisababisha umeme kukatika katika nyumba karibu 1,500.
Umuhimu wa kimkakati wa Kremenchuk

Chanzo cha picha, UNIAN
Mji wa Kremenchuk ni kitovu cha viwanda na usafirishaji na ni moyo wa Ukraine. Uko kwenye kando ya mashariki ya Mto Dnieper na kwa miaka mingi umejulikana kama kituo muhimu cha utengenezaji na usafirishaji.
Mji huu una kiwanda kikubwa cha Kerdamash kinachotengeneza mashine za barabara na viwanda vingine kadhaa vinavyounga mkono miundombinu na sekta ya ulinzi ya Ukraine. Kremenchuk pia ni moja ya vituo muhimu vya reli vinavyounganisha mashariki na magharibi mwa nchi.
Pia ni nyumbani kwa kiwanda kikubwa zaidi cha mafuta nchini Ukraine, Kremenchuk Refinery; kiwanda pekee kilichokuwa kikiwaendelea kutoa bidhaa za petroli mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
"Warusi hawakushambulia kiwanda cha mafuta cha Kremenchuk mwanzoni mwa vita. Walidhani wangechukua kila kitu, ikiwemo kiwanda hiki. Lakini operesheni ya 'Kiev kwa siku tatu' iliposhindikana, walilenga kiwanda hiki cha mafuta kwa sababu kilikuwa chanzo cha bidhaa za mafuta," alisema Mykhailo Gonchar, mkuu wa kituo cha utafiti wa kimataifa Strategy 21, kwa BBC Ukrainian.
Mashambulizi ya kwanza kwenye kiwanda hiki yalitokea Aprili 2022, na shambulio jingine lilitokea Mei mwaka huo huo.

Chanzo cha picha, Reuters
Mnamo Juni 2022, roketi ya Urusi ililenga kituo kikubwa cha ununuzi mjini Kremenchuk, ikiwaua zaidi ya watu 20, kulingana na maafisa wa Ukraine.
Urusi imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa haishambulii miundombinu ya raia, na inadai kwamba inalenga ghala zilizo karibu na vituo hivi, ambavyo Moscow inasema vilihifadhi vifaa vya kijeshi vya Magharibi.
Mashambulizi kwenye kiwanda cha mafuta yameendelea mwaka 2023 na 2024. Mnamo Juni 15, 2025, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitangaza kuwa imefanya mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi kwenye kiwanda cha Kremenchuk. Urusi ilidai kuwa kiwanda hiki kilikuwa kikiwapatia mafuta wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Donbass na kwamba shambulio hilo lilikuwa la mafanikio.

Chanzo cha picha, STATE EMERGENCY SERVICE OF UKRAINE / HANDOUT
Sergey Kovin, mkurugenzi wa kikundi cha ushauri wa nishati cha A-95, aliiambia BBC: "Kiwanda hakikuwa kinafanya kazi tena. Wanataka tu kuharibu kile kilichobaki ili iwe ngumu sana au gharama kubwa kukirekebisha. Kwa hakika wanakimaliza kabisa."
Kovin anaongeza kuwa mashambulizi haya yanapaswa kuonekana kama kisasi kwa shambulio la Ukraine kwenye miundombinu ya mafuta ya Urusi, pamoja na kuwa ni hatua ya kisaikolojia, kwa kuwa kiwanda cha Kremenchuk kimekuwa akitoi huduma kwa muda mrefu. Anakadiria kuwa tangu vita vilipoanza, kiwanda hiki kimekuwa kikishambuliwa kwa makumi ya roketi na mamia ya ndege zisizo na rubani (drones).
Je, hali hii itasababisha uhaba wa mafuta nchini Ukraine?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya mashambulizi mara kwa mara, uharibifu wa kiwanda hiki haujathiri hali ya mafuta ya petroli na dizeli nchini Ukraine, kwani bidhaa hizi tayari zinapokelewa kutoka Ulaya kwa kutumia malori ya mafuta.
Kiwanda cha Kremenchuk kina uwezo wa kuchakata tani milioni 19 za mafuta kwa mwaka. Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa kabla ya vita, kilichakata takriban tani milioni 3 tu za mafuta kwa mwaka, kiasi ambacho kilikidhi takriban asilimia 50 ya mahitaji ya petroli nchini Ukraine.
Lakini sasa Ukraine haina uzalishaji wowote wa ndani wa mafuta.
Mwanzoni mwa vita, nchi ilikabiliwa na usumbufu wa usambazaji wa mafuta kwa muda mfupi, lakini mgogoro huu ulitatuliwa haraka kwa njia ya kupata mbadala wa upatikani wa mafuta kutoka Ulaya.
"Usambazaji wa mafuta ulipitia barabarani na reli," anafafanua Mykhailo Gonchar. "Mafuta yaliingizwa kwa malori kutoka Ulaya. Ni ngumu kuharibu mamia ya malori yanayoingia Ukraine."
Anasema kuwa baada ya ufunguzi wa tena wa njia za baharini, uingizaji wa petroli kwa baharini pia ulianza. Hata hivyo, mwezi Agosti, mashambulizi kwa kutumia roketi na drones kwenye njia hii yalianza tena.















