Ukraine & Urusi: Maeneo ya Ukraine yaliyovamiwa na Urusi ambayo ni kitovu cha mazungumzo kati ya Trump na Putin

dfc
Maelezo ya picha, Donald Trump na Vladimir Putin walikutana Alaska siku ya Ijumaa
    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Urusi ilianza kuikalia Ukraine tangu mwaka 2014, wakati Rais Vladimir Putin alipochukua hatua yake ya kwanza ya uvamizi.

Wakati huo, katika muda wa miezi michache, Moscow ilifanya uvamizi wa kumwaga damu na kuikalia peninsula ya Crimea.

Uvamizi huo ulifuatiwa na vuguvugu la wanaotaka kujitenga lililoungwa mkono na Urusi katika eneo la mashariki la Donbas - haswa katika mikoa miwili ya Donetsk na Luhansk.

Vita vilidumu kwa miaka minane huko. Ukraine ilipoteza takriban wanajeshi na raia 14,000 katika kipindi hicho.

Lakini mwezi Februari 2022, Putin alifanya uvamizi mkubwa zaidi. Vikosi vya Urusi vilifika hadi kwenye viunga vya Kyiv na kukamata maeneo makubwa ya kusini, na kuchukua sehemu kubwa za majimbo mawili zaidi, Zaporizhzhia na Kherson.

Na Urusi sasa inadhibiti eneo dogo - kutoka karibu 27% ya Ukraine katika msimu wa joto wa 2022 hadi 20% sasa. Katika eneo la mashariki, majeshi ya Urusi yanaendelea kusonga mbele, lakini polepole sana na kwa gharama kubwa.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine anasema usitishaji mapigano usio na masharti unahitajika. Washirika wa Ulaya pia wanasisitiza kusitisha mapigano. Rais wa Marekani Donald Trump anasema hilo ndilo jambo ambalo amekuwa akijaribu kulifanikisha.

Pia unaweza kusoma

Eneo la Ukraine kwa sasa

Kufikia Agosti 2025, eneo la Ukraine linaonekana kama ifuatavyo:

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Urusi inataka kuwa na udhibiti wa maeneo yote ya Luhansk na Donetsk. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa Putin anaitaka Ukraine kukabidhi eneo lililobaki inalolidhibiti katika majimbo yote mawili.

Lakini hilo litamaanisha kwamba Kyiv inatoa eneo ambalo maelfu ya wanajeshi wa Ukraine wamekufa wakijaribu kulilinda - miji kama Kramatorsk na Sloyansk, na mstari wa mapambano unaolinda eneo la Ukraine la kaskazini na magharibi.

Kwa Kyiv, makubaliano kama hayo litakuwa ni jambo gumu kukubali. Kwa Moscow, ambayo hasara yake imekuwa mbaya zaidi, hilo litaonekana kama ushindi.

Zelensky alisema siku ya Jumanne kwamba Ukraine "haitaondoka Donbas, kwani Moscow itatumia eneo hilo kama njia ya kushambulia nchi nzima.”

Katika siku za hivi karibuni, vikosi vya Urusi vinaonekana kufanya mashambulizi na kusonga mbele, karibu na mji wa Dobropillya. Lakini bado haijabainika iwapo hilo linaashiria hatua muhimu ya kimkakati au ni juhudi tu za kumwonyesha Trump kwamba Moscow bado ina uwezo wa kupigana.

Vipi kuhusu Zaporizhzhia na Kherson, mikoa iliyotekwa mwaka 2022?: Urusi iko tayari kuondoka katika mikoa hiyo?

Siku ya Jumatatu, Trump alizungumza kuhusu Bahari ya Azov au Bahari Nyeusi. Hapa kuna daraja muhimu la kimkakati la Putin linalounganisha Urusi na Crimea inayokaliwa kwa mabavu.

Ni vigumu kuona kiongozi wa Urusi akikubali kuachana eneo hilo. Kama Donetsk na Luhansk, Putin anayachukulia maeneo haya kama sehemu ya Urusi, na aliyatwaa kinyume cha sheria miaka mitatu iliyopita katika kura nne za maoni zinazochukuliwa kuwa za uzushi.

Kwa Ukraine, na Ulaya, kuachia maeneo - katika hatua hii ya mwanzo kabisa ya mazungumzo - sio jambo la kwanza.

Majadiliano kuhusu mipaka ya siku zijazo yanaweza hatimaye kuja, lakini ni wakati ambao vita vimesimama na usalama wa Ukraine umehakikishwa.