Silaha mpya ya kutisha inayobadilisha vita nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Harufu kali imetanda kwenye mji wa Rodynske. Dakika chache baada ya kuingia mjini, tunatazama inatoka wapi.
Bomu lenye uzito wa kilo 250 liliharibu jengo kuu la utawala la jiji hilo na kutandaza vyumba vitatu vya ghorofa. Tumewasili eneo hilo siku moja baada ya bomu kupigwa, lakini moshi bado unaendelea kufuka. Kutoka nje kidogo ya mji, tunasikia sauti ya milio ya risasi : Wanajeshi wa Ukraine wakidungua ndege zisizo na rubani.
Rodynske iko karibu kilomita 15 kaskazini mwa mji uliozingirwa wa Pokrovsk. Urusi imekuwa ikijaribu kuliteka eneo hilo kutoka kusini , lakini vikosi vya Ukraine vimeweza kusitisha harakati za Urusi.
Kwa hivyo Urusi imebadilisha mbinu na kuchagua kuzunguka mji na kukata njia za usambazaji wa silaha na wanajeshi. Katika wiki mbili zilizopita, ikikabiliwa na kushindwa kwa juhudi za kidiplomasia za kufikia usitishaji mapigano nchini Ukraine, Urusi imezidisha mashambulizi yake, na kupiga hatua kubwa tangu mwezi Januari.
Dakika chache baada ya kuwasili jijini, tulisikia ndege isiyo na rubani ya Urusi ikiruka juu. Timu yetu ilikimbilia na kujificha chini ya mti .
Tuliibanana chini ya mti huo ili ili ndege isiyo na rubani isituone. Kisha tukasikia mlipuko mkubwa: droni ya pili ilianguka karibu. Ndege isiyo na rubani iliyokuwa juu yetu iliendelea kuruka. Kwa dakika chache zaidi, tulisikia ndege isiyo na rubani ya kutisha ambayo imekuwa silaha mbaya zaidi katika vita hivi.
Wakati hatukuweza kusikia tena, tulichukua fursa hiyo kukimbilia mahali salama katika jengo lililotelekezwa lililo umbali wa mita 30.
Kutoka kwa makazi hayo, tunasikia sauti nyenegine ya droni. Inawezekana imerudi baada ya kuona tumetoroka.
Ukweli kwamba Rodynske inavamiwa na ndege zisizo na rubani za Urusi inaonyesha kuwa mashambulio hayo yanatoka karibu zaidi kuliko maeneo yanayojulikana ya Urusi kusini mwa Pokrovsk.
Kuna uwezekano mkubwa wanatoka eneo lililotekwa hivi majuzi kwenye barabara kuu inayoelekea mashariki kutoka Pokrovsk hadi Kostyantynivka.
Baada ya nusu saa ya kungoja katika makao hayo, tuliposikia tena ndege isiyo na rubani, tulirudi haraka kwenye gari letu, tukaegesha chini ya vivuli vya miti, na kutoka nje ya Rodynske kwa kasi.
Kando ya barabara, tuliona moshi ukifuka na kitu kinachowaka; pengine ilikuwa ndege isiyo na rubani.

"Wanatumia kila kitu walichonacho"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tunaendesha gari kuelekea Bilytske, mbali na mstari wa mbele . Tunaona nyumba zilizoharibiwa na shambulio la kombora wakati wa usiku. Moja ya nyumba hizo ni ya Svitlana.
"Hali inazidi kuwa mbaya. Hapo awali, tulisikia milipuko; ilikuwa mbali sana. Lakini sasa kijiji chetu kinashambuliwa; tunapitia sisi wenyewe," anasema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 61, anapokusanya baadhi ya mali kutoka kwenye vifusi vya nyumba yake.
Kwa bahati nzuri, Svitlana hakuwa nyumbani wakati shambulio hilo lilipotokea.
"Nenda katikati ya jiji, utaona uharibifu mwingi. Duka la mikate na bustani ya wanyama pia vimeharibiwa," anasema.
Katika makazi, nje ya anuwai ya ndege zisizo na rubani, tulikutana na askari kutoka kitengo cha upigaji risasi cha Kikosi cha 5 cha Mashambulizi.
"Unaweza kuhisi ukubwa wa mashambulizi ya Urusi ukiongezeka. Roketi, kombora, ndege zisizo na rubani... wanatumia kila walichonacho kukata njia za usambazaji katika jiji," Serhii anasema.
Kikosi chake kimekuwa kikisubiri kwa muda wa siku tatu kwenda kushika doria wakitumai kuwa kufunikwa na mawingu au upepo mkali utawalinda dhidi ya ndege zisizo na rubani.

Urusi inaongoza
Katika mzozo unaoendelea kubadilika, wanajeshi wamelazimika kukabiliana haraka na vitisho vipya vinavyoletwa na teknolojia zinazoibuka.
Na tishio la hivi karibuni zaidi linatokana na droni za fiber-optic. Spool ya kebo yenye urefu wa makumi ya kilomita imeunganishwa chini ya droni, na kebo ya fiber-optic inaunganishwa na kidhibiti kinachoshikiliwa na rubani.
"Video na mawimbi ya udhibiti hupitishwa na kutoka kwa droni kupitia kebo, si masafa ya redio. Hii ina maana kwamba haiwezi kuingiliwa na vipokezi vya kielektroniki," anasema askari aliye na ishara ya simu Moderator, mhandisi wa droni wa kikosi cha brigedi ya 68.
Ndege zisizo na rubani zilipoanza kutumika sana katika vita hivi, majeshi yote mawili yaliweka magari yao mifumo ya kivita ya kielektroniki ambayo inaweza kuyapunguza.
Ulinzi huo hathivyo umeyeyuka kufuatia kuwasili kwa droni za fiber-optic, na Urusi kwa sasa inaongoza katika kupeleka vifaa hivi. Ukraine inajaribu kuongeza uzalishaji.
"Urusi ilianza kutumia ndege zisizo na rubani za fiber-optic muda mrefu kabla yetu, tukiwa bado tunazifanyia majaribio. Ndege hizi zisizo na rubani zinaweza kutumika katika maeneo ambayo tunahitaji kuruka chini chini kuliko ndege zisizo na rubani za kawaida. Tunaweza hata kuingia kwenye nyumba na kutafuta shabaha ndani," anasema Venia, rubani wa ndege zisizo na rubani katika Kikosi cha 68 cha Wanajeshi.
"Tulitania kwamba labda tulete mkasi kukata kebo," anasema Serhii, mshika bunduki.
Ndege zisizo na rubani za Fiber-optic zina vikwazo vyake: zinaruka polepole, na kebo yake inaweza kuchanganyikiwa kwenye miti. Lakini kwa sasa, matumizi yao makubwa na Urusi yanamaanisha kuwa kusafirisha askari kwenda na kutoka katika nafasi zao mara nyingi kunaweza kuwa hatari zaidi kuliko uwanja wa vita wenyewe.

Wiki kadhaa katika mahandaki
"Unapoingia kwenye eneo la kushika doria, huwezi kujua ikiwa umegunduliwa au la. Na ikiwa umegunduliwa, unaweza kuwa tayari unaishi saa za mwisho za maisha yako," anasema Oles, Sajini Mkuu wa kitengo cha upelelezi cha Brigedi ya 5 ya mashambulizi .
Tishio hili lina maana kwamba askari wanatumia muda zaidi na zaidi kwenye vituo vyao.
Oles na watu wake wako katika jeshi la vijana wadogo , wanahudumu kwenye mahandaki, kwenye mstari wa mbele wa utetezi wa Ukraine. Siku hizi, ni nadra kwa waandishi wa habari kuzungumza na wanajeshi wachanga kwani kuingia kwenye mitaro hii imekuwa hatari sana. Tulikutana na Oles na Maksym katika nyumba ya mashambani iliyogeuzwa kuwa kituo cha muda, ambapo askari hupumzika wakati hawajatumwa.
"Muda mrefu zaidi ambao nimekuwa kwenye nafasi hiyo ni siku 31, lakini najua watu ambao wametumia siku 90 au hata 120. Kabla ya ujio wa ndege zisizo na rubani, mzunguko unaweza kuwa kati ya siku 3 na 7," anasema Maksym.
"Vita ni damu, kifo, matope mvua, na baridi ambayo inapita kati yako kutoka kichwa hadi vidole. Na hivyo ndivyo unavyotumia kila siku. Nakumbuka wakati mmoja ambapo hatukulala kwa siku tatu, kwa makali kila dakika. Warusi walitushambulia wimbi baada ya wimbi. Hata uzembe mdogo ungetuua."

Chanzo cha picha, Getty Images
Matatizo ya wanajeshi
Licha ya hatua za hivi karibuni zilizopigwa na Urusi, haitakuwa rahisi au haraka kuchukua eneo lote la Donetsk, ambapo Pokrovsk iko.
Ukraine imekabiliana vikali, lakini inahitaji silaha na risasi za kutosha ili kuendeleza mapambano.
Na sasa kwamba vita vinaingia majira ya joto ya nne, matatizo ya wanajeshi wa Ukraine mbele ya jeshi kubwa zaidi la Kirusi pia yanaonekana. Wanajeshi wengi tuliokutana nao walijiunga na jeshi baada ya vita kuanza. Walipata mafunzo ya miezi michache, lakini wamelazimika kujifunza mengi wakiwa kazini, katikati ya vita vikali.
Maksym alifanya kazi katika kampuni ya vinywaji kabla ya kujiunga na jeshi. Nilimuuliza jinsi familia yake inaendelea.
"Ni ngumu, ni ngumu sana. Familia yangu inaniunga mkono sana. Lakini nina mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka miwili, na sioni sana. Ingawa nafanya naye mazungumzo ya video, kwa hivyo kila kitu ni sawa kulingana na mazingira," anasema, macho yake yakijaa machozi.
Maksym ni mwanajeshi anayepigania nchi yake, lakini pia ni baba anayemkumbuka mtoto wake wa miaka miwili.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












