Oreshnik: Tunachojua kuhusu kombora la Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Robert Greenall & Chris Partridge
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Alhamisi wiki hii, mji wa viwanda wa Dnipro nchini Ukraine ulikumbwa na shambulio la anga la Urusi ambalo walioshuhudia walilielezea kuwa lisilo la kawaida kutokana na milipuko iliyoendelea kwa saa tatu.
Shambulio hilo linadaiwa kujumuisha kombora lenye nguvu kubwa, maafisa wa Ukraine walisema huenda kombora la masafa marefu (ICBM) lilitumiwa.
Maafisa wa mataifa ya magharibi walikanusha hilo, wakisema shambulio kama hilo lingeibua tahadhari ya nyuklia nchini Marekani.
Saa kadhaa baada ya shambulio hilo, Rais wa Urusi Vladimir Putin, alisema katika hotuba kupitia televisheni kuwa Urusi ilirusha kombora "jipya la masafa ya kati" aliloliita Oreshnik.
Putin alisema silaha hiyo ina uwezo wa kupaa angani kwa kati ya kilomita 2.5 -3 kwa sekunde (mara 10 zaidi ya kasi ya sauti), akiongeza "kwa sasa hakuna njia za kukabiliana na silaha hii".
Alisema sehemu kubwa ya kituo cha kijeshi na viwanda mjini Dnipro, ambalo linatumiwa kutengeneza makombora na silaha zingine, imeshambuliwa. Alielezea shambulio hilo kama jaribio ambalo "lilifanikiwa" kwa sababu "lengo lilifikiwa".
Akizungumza siku moja baadaye na maafisa wakuu wa ulinzi, alisema majaribio ya kombora hilo yataendelea, "ikiwa ni pamoja na mazingira ya vita".
Licha ya maelezo ya Putin kuhusu silaha hiyo, inaonekana hakuna makubaliano ya wazi kuhusu silaha hiyo.
Ujasusi wa kijeshi wa Ukraine unashikilia kuwa kombora hilo ni aina mpya ya ICBM inayojulikana kama Kedr. Wanasema ilichukua dakika 15 kufika zaidi ya kilomita 1,000 kutoka eneo la Astrakhan nchini Urusi.
Walisema kuwa kombora hilo lilikuwa na vichwa sita, kila moja ikiwa na silaha ndogo sita.
Kauli hii inaendana na uchunguzi wa BBC Verify wa video za shambulio hilo. Uchunguzi unaonyesha wazi miale sita anagani, kila moja ikiwa na kundi la makombora sita mahususi.
Mahali paliposhambuliwa ni eneo la viwanda kusini-magharibi mwa jiji la Dnipro.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwanini kasi ni muhimu?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ikiwa maelezo ya Putin yatakuwa sahihi basi kombora hilo linaendana na sifa ya silaha zilizo na kasi ya juu (Hypersonic)
Kasi ni muhimu kwa sababu kadiri kombora linavyosafiri, ndivyo linavyoelekea kwa shabaha yake haraka.
Kadiri inavyopata lengo haraka, ndivyo inatoa muda mchache kwa jeshi linalolinda linavyopaswa kujibu.
Kombora la balistiki hufikia lengo lake kwa kufuata njia ya kukunja juu ya angahewa na inayofanana na hiyo kuelekea kule inakoenda.
Lakini inapoelekea chini, inaongeza kasi na kupata nishati ya kinetic ambayo inaongeza uwezo wake.
Hali hiyo inaiwezesha kurudi chini kuelekea kwenye shabaha iliyodhamiriwa kushambulia.
Hili si jambo geni kwa wanajeshi ambao wamekuwa wakijilinda dhidi ya vitisho kama hivyo, lakini kadri kasi inavyokuwa kubwa ndivyo inavyokuwa vigumu kudhibiti mashambulizi ya silaha za aina hiyo.
Ndio maana Putin huenda ametilia mkazo kasi yake katika kutangaza aina hii mpya ya kombora.
Asilimia 80 ya makombora yaliyorushwa na Urusi yameharibiwa na Ukraine, idadi isiyo ya kawaida. Lakini kasi hizi za kasi za makombora ya balestiki zinakusudiwa kupunguza asilimia hiyo.
Kombora hili jipya linasafiri umbali gani?
Mtaalamu wa kijeshi wa Urusi Ilya Kramnik ameliambia gazeti la Izvestiya linalounga mkono Kremlin, kwamba huenda kombora hilo jipya kwa sasa ni miongoni mwa silaha za hali ya juu katika safu ya makombora ya masafa ya kati.
"Huenda tunakabiliana na kizazi kipya cha makombora ya masafa ya kati ya Urusi yaliyo na kasi ya kati ya kilomita 2,500-3,000 (maili 1,550-1,860) na ambayo yana uwezekano wa kusafiri umbali wa hadi kilomita 5,000 lakini sio ya kuvuka bara," Anasema.
Hii inamaanisha ku inaweza kufika eneo lolote Barani Ulaya, lakini sio Marekani.
"Ni wazi ina kiungo kinachotenganishwa na sehemu inayotumiwa kuelekeza kombora hilo," Kramnik aliongeza.
Alikadiria kuwa huenda ni toleo Yars-M lililopunguzwa makali, ambalo sasa ni ICBM.
Urusi iliripotiwa kuanza kutengeneza kombora hili jipya linalojumuisha sehemu tofauti mwaka jana.
Mtaalamu mwingine, Dmitry Kornev, aliliambia jarida hilo kuwa Oreshnik inaweza kuundwa kutokana na msingi wa makombora ya masafa mafupi ya Iskander - ambayo tayari yanatumika sana Ukraine - lakini kwa kutumia injini ya kizazi kipya.
Iskander iliyo na injini iliyopanuliwa ilitumika katika majaribio ya Kapustin Yar kusini mwa Urusi msimu wa joto uliopita, alisema, akiongeza kuwa hii inaweza kuwa Oreshnik. Kombora la Alhamisi lilirushwa hadi Ukraine kutoka eneo moja.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Maryam Dodo












