Je, kuna uhusiano upi kati ya mwanamitindo huyu, teknolojia ya Uingereza na vita vya Urusi?

Selfie ya Valeria Baigascina iliyopigwa kwenye kidimbwi cha kuogelea iliyojengwa juu ya paa la nyumba mjini Kuala Lumpur

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha, Mwanamitindo wa muda Valeria Baigascina anaonekana kuwa na mtindo wa maisha wa kutumia ndege
    • Author, Angus Crawford and Tony Smith
    • Nafasi, BBC News Investigations
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Vifaa vya hali ya juu vilivyotengenezwa na kampuni ya Uingereza vyenye thamani ya dola milini 2.1 vimeuzwa kwa makampuni yanayohusiana na jeshi nchini Urusi, nyaraka za forodha zilizoonekana na BBC.

Hati hizo zinaonyesha lenzi za kamera zilizotengenezwa Uingereza zilisafirishwa na kampuni iliyosajiliwa nchini Kyrgyzstan, ambayo inadaiwa kuendeshwa na mwanamitindo wa mavazi ya kuogelea.

Kampuni ya Uingereza, Beck Optronic Solutions, ambayo imefanya kazi kwenye vifaru vya Challenger 2 vya Uingereza na ndege za kivita za F35, alitufahamisha kuwa haijakiuka vikwazo, haikuwa na ushirikiano na Urusi au Kyrgyzstan, na haikufahamu shehena hizo.

Uchunguzi wetu unaibua maswali kuhusu ufanisi wa vikwazo vilivyowekewa Urusi tangu vita vya Ukraine kuanza.

Soma pia:

Uchunguzi huo ulitupeleka kwa Valeria Baigascina, mwenye umri wa miaka 25, mwenye asili ya Kazakhstan lakini sasa anaishi Belarus. Mwanamitindo wa muda, mara kwa mara huweka kwenye mitandao ya kijamii picha kuhusu mtindo wake wa maisha wa kutumia ndege. Katika miaka miwili iliyopita ametembelea Dubai, Sri Lanka na Malaysia.

Mtandao wake wa kijamii haukuonyesha dalili kuwa yeye pia alikuwa mkurugenzi wa kampuni ambayo ilikuwa ikiselekeza vifaa vya thamani ya mamilioni ya dola kwa kampuni zilizoidhinishwa nchini Urusi, jinsi upekuzi wetu wa hati za forodha ulifvyofichua.

Kulingana na maelezo ya usajili wa Belarus, Bi Baigascina alikuwa mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya Rama Group LLC. Ilianzishwa mnamo Februari 2023, imesajiliwa kwa anwani huko Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan - maili 2,300 (kilomita 3,713) kutoka nyumbani kwake huko Belarus.

Nchi zote mbili ni majtaifa ya zamani ya Soviet na viungo vikali vya biashara na Urusi. Belarus inasalia kuwa mshirika mkuu wa Moscow huko Ulaya.

A map showing the locations of Beck Optronic Solutions in Hemel Hempstead, UK, and of Rama Group LLC and Shisan LLC in Bishkek, Kyrgyzstan, as well as Belarus, where Valeria lives, Russia, and Ukraine. The map also shows Crimea, which was annexed by Russia in 2014.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Takwimu za biashara zinaonyesha kuwa tangu vikwazo dhidi ya Urusi vilipoanzishwa Februari 2022, mauzo ya Uingereza kwa Kyrgyzstan yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 300. Wataalam wanashuku kuwa baadhi ya bidhaa zinapelekwa Moscow.

Nyaraka za forodha zilizopatikana na BBC zinaonyesha kuwa Rama Group ilisafirisha hadi Moscow vifaa vya miwani vya hali ya juu ambavyo vinaweza kutumika kwenye makombora, mizinga na ndege.

Vifaa hivyo vimeorodheshwa kwenye fomu ya forodha kuwa vinatengenezwa na Beck Optronic Solutions huko Hemel Hempstead, Hertfordshire. Kampuni hiyo hutengeneza lenzi zenye usahihi wa hali ya juu zinazotumika katika mifumo ya kulenga na ufuatiliaji.

Ingawa baadhi ya lenzi zake hutumika katika huduma ya afya na uhandisi, tovuti ya Beck inaelezea maombi mengi ya kijeshi na ulinzi.

Lenzi na teknolojia ya macho inayouzwa na Beck Optronics zimeorodheshwa kama bidhaa ambazo haziwezi kusafirishwa kihalali kwenda Urusi, au zinazohitaji idhini kutoka kwa mamlaka ya Uingereza kabla ya mauzo yoyote kufanyika.

Sehemu ya maelezo kutoka stakabadhi ya forodha inaonyesha Beck Eptronics Ltd kama mtengenezaji na Urusi kama nchi iliyoagiza
Maelezo ya picha, Sehemu ya maelezo kutoka stakabadhi ya forodha inaonyesha Beck Eptronics Ltd kama mtengenezaji na Urusi kama nchi iliyoagiza

BBC imebaini, kupitia hati za forodha, jumla ya shehena sita za bidhaa zinazosemekana kutengenezwa na Beck zenye thamani ya dola milioni 2.1za Kimarekani zimesafirishwa hadi Moscow kupitia Rama na kampuni nyingine mshirika, Shisan LLC.

Mnamo Desemba 2023 na Januari 2024, Rama Group ilisafirisha bidhaa zake mbili kwenda Moscow ikiziorodhesha kama "sehemu inayozunguka ya kamera". Usafirishaji huu ulienda kwa Sol Group, kampuni iliyoko Smolensk, maili 200 (320km) kusini-magharibi mwa Moscow, ambayo imeidhinishwa na Marekani.

Haijulikani ni njia gani za kimataifa ambazo bidhaa zilichukua - hati zinaonyesha kuwa baadhi ya vifaa hivyo huena vilitoka Thailand.

Shisan LLC, kampuni nyingine ya Kyrgyz, ilishughulikia usafirishaji mwingine wa bidhaa nne za Beck Optronics zenye thamani ya dola milioni 1.5 za Kimarekani.

Shehena mbili kati ya hizo zilihusisha "lenzi ya kamera ya mawimbi mafupi ya infrared" na kwenda kwa Ural Optical & Mechanical Plant, ambayo hutengeneza vifaa vya kulenga bomu na pia imeidhinishwa kwa sababu ya uhusiano wake na jeshi la Urusi.

Rama Group na Shisan zina anwani sawa huko Bishkek - jengo la kisasa la ghorofa tano katika sehemu ya kifahari ya jiji. Hata hivyo, tulipotembelea sehemu hiyo tuliambiwa Valeria Baigascina alikuwa nje ya nchi kwa safari ya kikazi.

Tulipata nambari yake kupitia machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii na kumfahamisha kuhusu madai yaliyotokana na uchunguzi wetu.

Valeria Baigascina akiwa na bunduki

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha, Valeria Baigascina akiwa na bunduki

Bi Baigascina alisema yeye ndiye mwanzilishi wa kampuni hiyo lakini alikuwa ameiuza mwezi Mei. Alikanusha madai hayo, akisema kwamba alipokuwa mmiliki, "hakuna madai kama hayo yaliyotolewa". Kisha akakata simu.

Baadaye, kwa barua pepe, alituambia kuwa tuhuma hizo zilikuwa "za kipuzi" na zilizotokana na "htaarifa za uongo".

Utafiti wetu unaonyesha kuwa Mei mwaka huu aliuza kampuni ya Rama Group kwa rafiki yake mkubwa, Angelina Zhurenko, ambaye anafanya biashara ya nguo za ndani nchini Kazakhstan.

Bi Zhurenko alituambia: "Shughuli za biashara zinafanywa ndani ya mfumo wa sheria ya sasa ya Kyrgyzstan. Kampuni haijakiuka marufuku yoyote. Madai mengine yoyote ni ya uongo.”


Angelina Zhurenko anaendesha biashara ya nguo za ndani huko Kazakhstan na pia husafiri sana

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha, Angelina Zhurenko anaendesha biashara ya nguo za ndani huko Kazakhstan na pia husafiri sana

Mkurugenzi wa kampuni ya Shisan (mshirika) ameorodheshwa kama Evgeniy Anatolyevich Matveev. Tuliwasilisha madai yetu kwake kupitia kwa barua pepe.

Alituambia kwamba taarifa zetu zilikuwa "za uongo" na kwamba aliendesha "biashara ya kusambaza bidhaa za kiraia pekee zilizotengenezwa katika nchi za Asia".

Aliendelea: "Hii haijakiuki sheria za serikali ambayo ninaifanyia kazi, na haina uhusiano wowote na vikwazo vya Marekani, kwa sababu haiwezekani kupiga marufuku biashara huru ya bidhaa za Asia zinazopatikana kwa ajili ya kuuza na kuwasilisha."

Hakuna ushahidi kwamba Beck Optronics alifahamu kuhusu usafirishaji huu au kwamba shehena ya mwisho ya lenzi ilikuwa Urusi.

Kampuni hiyo ilituambia haina uhusiano wowote na usafirishaji huo: "Beck hajasafirisha chochote kinyume na udhibiti wa usafirishaji wa Uingereza au vikwazo vyovyote vinavyotumika nchini Uingereza. Haijajihusisha na chama au kampuni yoyote nchini Urusi, Kyrgyzstan au Thailand, haikujua kwamba usafirishaji wowote unaweza hatimaye kutumwa kwa mojawapo ya nchini hizo na haijasafirisha chochote kwenye maeneo haya."

Inaamini kuwa baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa havikutengenezwa na kampuni na kwamba huenda hati za forodha zilipatikana kwa njia ya ulaghai.

Lakini mauzo haya yanayodaiwa ni sehemu ya sakata kubwa zaidi inayohusisha usafirishaji kutoka kwa vyanzo kadhaa.

Uchambuzi wa hati za forodha na taasisi ya usalama yenye makao yake mjini Washington C4ADS unaashiria kuwa Shisan ilikamilisha usafirishaji 373 kupitia Kyrgyzstan hadi Urusi kati ya Julai na Desemba 2023.

Kati ya hizi, 288 zilikuwa na bidhaa ambazo ziko chini ya kanuni za forodha kwa "vifaa vya kivita vya umuhimu wa hali juu".

Katika kipindi hicho hicho cha miezi sita, Rama Group ilisafirisha jumla ya shehena 1,756 hadi Urusi. Kati ya hizi, 1,355 zilikuwa za vitu vilivyo kwenye orodha ya "vifaa vya vita vya umuhimu wa hali ya juu".

Usafirishaji wake wa hivi karibuni zaidi, pamoja na vifaa vya elektroniki vya kampuni za Marekani na Uingereza, ulienda kwa kampuni ya Urusi inayofahamika kama Titan-Mikro, ambayo imekuwa chini ya vikwazo vya Marekani tangu Mei 2023 kwa kufanya kazi ndani ya sekta ya kijeshi ya Urusi.

"Wanapouza teknolojia hii kwa mteja ambaye anaweza kuwa mtumiaji wa mwisho wa Urusi, wanapaswa kuelewa kikamilifu kwamba hii ni kuua watu," anasema Olena Tregub kutoka NAKO, shirika huru la kupambana na rushwa la Ukraine.

Anaonya kwamba utepetevu wa serikali dhidi ya vikwazo vilivyoweka unagharimu maisha.

"Bila ya teknolojia hizo, silaha hizo haziwezi kufanya kazi. Mifumo ya makombora hayo ya balestiki, ndege hizo zisizo na rubani za kamikaze, zimeundwa kwa kutumia teknolojia ya nchi za Magharibi, "anasema.

Bw Cameron (Kushoto) na Bw. Kulubaev (Kulia) wakisalimiana mbele za bendera ya Uingereza na Kyrgyzstan.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, David Cameron - Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uingereza - alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kyrgyzstan Jeenbek Kulubaev mnamo Aprili na kumtaka aimarishe utekelezaji wa vikwazo vya nchi.

Mamlaka za kimataifa zinafahamu jukumu la Kyrgyzstan katika kukwepa vikwazo.

Mnamo Aprili, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza wakati huo, David Cameron, alisafiri hadi Bishkek na kuwasihi viongozi wa Kyrgystan kuongeza juhudi za kuimarisha utekelezaji wa vikwazo.

Rais wa Kyrgystan alionyesha imani kwamba ziara rasmi ya Cameron nchini mwake "itatoa msukumo mpya kwa ushirikiano wa pande nyingi kati ya Kyrgyzstan na Uingereza".

David O'Sullivan, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Ulaya (EU) kwa Utekelezaji wa Vikwazo alituambia kwamba juhudi zinaendelea kuzima "mitandao haramu ya ununuzi", na kwamba "kampuni zinatakiwa kufanya ukaguzi kwa uangalifu ili kuelewa ni nani mtumiaji wa mwisho na wapi 'vifaa vya vita' huishia hatimaye”.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah