Silaha za Ukraine: Marekani, Uingereza na mataifa mengine yanaipatia Ukraine silaha gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Marekani wanasema Rais Biden ameipa Ukraine ruhusa ya kurusha makombora ya masafa marefu ya ATACMS katika ardhi ya Urusi.
Inafikiriwa kuwa Uingereza na Ufaransa zinaweza kufuata mkondo huo kwa kusema kuwa makombora ya Storm Shadow yanaweza pia kutumika dhidi ya malengo ya mashambulizi ndani ya Urusi.
Mataifa ya magharibi sasa yamechangia zaidi ya dola bilioni 100 (£79bn) za msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Je, ni nani aliyetoa msaada mkubwa zaidi wa kijeshi?
Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na silaha, vifaa na msaada wa kifedha.
Kati ya mwezi Februari 2022 na mwisho wa mwezi Agosti 2024, ilitoa $61.1bn (£48.4bn), kulingana na taasisi ya Ujerumani ya Kiel.
Ujerumani imetoa dola bilioni 11.4 (£9bn) kama msaada wa kijeshi, Uingereza $10.1bn (£8bn), Denmark $7bn (£5.6bn), na Uholanzi $5.5bn (£4.4bn).
Hata hivyo, Taasisi ya Kiel inaonya kuwa huenda kukawa na "kshuka kwa kiasi kikubwa" kwa misaada kwa Ukraine mwaka 2025, ikiashiria kuwa Rais Trump anaweza kupunguza mchango wa Marekani atakaporejea White House mwezi Januari.
Ujerumani inatarajiwa kupunguza msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine mwaka 2025 kwa takriban nusu.
Je, ni silaha gani ambazo nchi za Magharibi zimeipa Ukraine?
Makombora na silaha
Vikosi vyote vya Ukraine na Urusi vimetumia silaha na makombora yaliyoongozwa, kuzuia vikosi vya adui kusonga mbele na kushambulia vituo vya usambazaji na vituo vya amri.
Ukraine imekuwa ikitumia makombora ya ATACMS yanayotengenezwa na Marekani dhidi ya vikosi vya Urusi ndani ya Ukraine. Makombora haya yana uwezo wa kushambulia umbali wa kilomita 190 (300km).
Haikuruhusiwa kushambulia katika ardhi ya Urusi, kwa hofu kwamba kwa kufanya hivyo kunaweza kuitumbukiza Marekani na nchi nyingine za Nato katika vita.
Hata hivyo, maafisa wa Marekani wanasema Rais Biden ameondoa marufuku hiyo, na kuruhusu ATACMS kutumika kuisaidia Ukraine kulilinda eneo inalokalia katika eneo la Kursk la Urusi.

Uingereza na Ufaransa zimeipatia Ukraine makombora ya Storm Shadow au Scalp, ambayo yana kiwango cha juu cha masafa yakiwa na uwezo wa kupiga shabaha zilizopo maili 155 (250km).
Nchi zote mbili zimepiga marufuku vikosi vya Ukraine kuyarusha nchini Urusi, ingawa Ukraine pia imeomba kwa muda mrefu kuruhusiwa kufanya hivyo.

Washirika wa Ukraine pia wametuma zaidi ya mifumo 80 ya roketi ya kurusha makombora, kwa mujibu wa taasisi ya Kiel.
Hii ni pamoja na mfumo wa Himars kutoka Marekani na mfumo wa makombora wa M270 kutoka Uingereza.
Taasisi ya Kiel inasema kuwa pia imetuma zaidi ya vifaru 500 vya kivita, ikiwa ni pamoja na M777 Howitzer kutoka Marekani.
Hata hivyo, Urusi ina faida kwenye uwanja wa vita kwasababu usambazaji wake wa makombora ya silaha umekuwa mkubwa zaidi kuliko wa Ukraine, kulingana na taasisi ya Uingereza Royal United Services Institute (RUSI).
Ndege za kivita (Fighter jet)
Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais wa Ukraine Zelensky alisema jeshi lake la anga limepokea kundi la kwanza la ndege za kivita za F-16 kutoka Magharibi. Alisema kuwa kuna mengi zaidi yanahitajika.
Nchi za Nato zikiwemo Ubelgiji, Denmark, Uholanzi na Norway zimeahidi kuipa Ukraine ndege 65 au zaidi zilizotengenezwa na Marekani, ambazo walikuwa wamepanga kuacha kuzitumia katika majeshi yao ya anga.
Mnamo Agosti 2023, Marekani ilitoa ruhusa ya ndege za kivita aina ya F-16 kutumwa Ukraine. Tangu wakati huo, mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiwafunza marubani wa Ukraine kuziendesha.

Profesa wa Mafunzo ya Mkakati katika Chuo Kikuu cha St Andrews Phillips O'Brien, anasema: "Ukraine itatumia ndege za F-16 zaidi kwa ulinzi dhidi ya mashambulizi ya hewa."
Kituo cha Marekani cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa kinasema hatimaye wanaweza kupewa majukumu ya ziada, kama vile kushambulia mifumo ya ulinzi wa anga wa Urusi, vituo vya amri na vituo vya usambazaji, na kuhusisha ndege za Urusi katika anga ya Ukraine.
Mifumo ya ulinzi wa anga
Ili kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi na makombora katika miji na miundombinu ya Ukraine, mataifa ya magharibi yametuma aina kadhaa za mifumo ya ulinzi wa anga.
Hii ni kuanzia silaha ya Uingereza ya muda mfupi ya kupambana na ndege, Starstreak, hadi mfumo wa kombora la Patriot.

Makombora ya Patriot ni ghali kufanya kazi - kombora moja linagharimu takriban $3m.
Marekani na Norway pia zimetoa Nasams (Mfumo wa hali ya juu ya kukabiliana na mashambuliz ya anga) na Ujerumani imetoa Iris-T.

Risasi
Mnamo Julai 2023, Marekani ilisema kuwa ilisambaza mabomu ya Cluster nchini Ukraine kusaidia kuviondoa vikosi vya Urusi kutoka maeneo ya kujihami.
Silaha hizi, ambazo hutolewa zaidi katika makombora ya silaha, hutawanya mabomu kadhaa, na zimepigwa marufuku na zaidi ya nchi 100 kwa sababu ya hatari zinazosababisha kwa raia.
Mizinga
Mwanzoni mwa mwaka 2023, mataifa ya magharibi yalikubali kupeleka vifaru Ukraine. Ilitarajiwa kuwa wangewezesha vikosi vyake kukiuka mistari ya kujihami ya Urusi katika hatua ya kukabiliana na mashambulizi.
Uingereza ilitoa 14 Challenger 2

Mataifa ya Ulaya yametuma zaidi ya vifaru 200 vya Ujerumani vya Leopard 1 na Leopard 2, kwa mujibu wa takwimu kutoka taasisi ya Kiel.
Marekani ilituma vifaru 31 kati ya vifaru vyake vya M1 Abrams, ambavyo vinaaminika kuwa hali ya juu zaidi duniani.

Silaha za kukabiliana na vifaru
Nchi za Magharibi kwanza zilijibu uvamizi wa Urusi mnamo Februari 2022 kwa kuipatia Ukraine silaha za kujihami ili kukabiliana na brigedi za silaha za adui.
Marekani na Uingereza zilisambaza maelfu ya makombora ya Javelin na Nlaw ya kupambana na vifaru. Hizi zilichukuliwa kuwa muhimu katika kuzuia maendeleo ya vikosi vya Urusi kwenye Kyiv.

Droni
Droni zimetumika sana wakati wote wa vita, kwa ufuatiliaji, kulenga, kuzindua makombora na kama silaha za "kamikaze".
Uturuki ilitoa ndege zisizo na rubani za Bayraktar TB2 mwanzoni mwa mzozo huo, Marekani imetoa ndege zisizo na rubani za "Switchblade" na nchi kadhaa zimetuma ndege zisizo na rubani za kibiashara, kama vile DJI Mavic 3 iliyotengenezwa na China.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












