Hamaki nchini Urusi baada ya 'kuzidishwa kwa mzozo' na hatua ya kutumiwa makombora

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, Russia editor, BBC News
- Akiripoti kutoka, Moscow
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Uamuzi wa Rais Biden wa kuiruhusu Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani umeibua hasira nchini Urusi.
"Rais anayeondoka wa Marekani Joe Biden... amechukua moja ya maamuzi ya uchochezi, ambayo yanatishia kuwa ya matokeo mabaya," ilitangaza tovuti ya gazeti la serikali ya Urusi Rossiyskaya Gazeta Jumatatu asubuhi.
Mbunge wa Urusi Leonid Slutsky, mkuu wa chama kinachounga mkono Kremlin Liberal-Democratic Party, alitabiri kwamba uamuzi huo "bila shaka utasababisha ongezeko kubwa la uhasama, na kutishia madhara makubwa".
Seneta wa Urusi Vladimir Dzhabarov aliitaja kuwa "hatua isiyo na kifani kuelekea Vita vya Tatu vya Dunia".
Ndiyo Hatua hiyo imezua ghadhabu. Lakini hilo sio jambo la kushangaza kwa kweli.
Komsomolskaya Pravda, gazeti la udaku linalounga mkono-Kremlin, liliita "uchokozi wa kutabirika".
Kilicho muhimu sana, hata hivyo, ni jinsi Vladimir Putin atakavyochukulia hatua hiyo na jinsi kiongozi wa Kremlin atakavyojibu.
Mpaka sasa amesalia kimya.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini siku ya Jumatatu msemaji wa Rais Putin, Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari kwamba "ikiwa uamuzi kama huo umechukuliwa inamaanisha hali mpya ya mvutano na hali mpya kuhusu ushiriki wa Marekani katika mzozo huu".
Bw Peskov alishutumu utawala wa Biden kwa "kuongeza mafuta kwenye moto na kuendelea kuzua fujo katika mzozo huu".
Viongozi wa mataifa ya magharibi wanaweza kuhoji kuwa ni Urusi ndio 'inayoongeza mafuta' mzozo huo kwa kupeleka wanajeshi wa Korea Kaskazini hivi karibuni kwenye eneo la vita ili kupigana pamoja na vikosi vya Urusi na kuendelea kuishambulia Ukraine.
Rais Putin mwenyewe huenda hajatoa maoni yake. Lakini rais wa Urusi aliwahi kusema mengi hapo awali.
Katika miezi ya hivi karibuni, Kremlin imeweka wazi ujumbe wake kwa Magharibi: usifanye hivi, usiondoe vikwazo vya matumizi ya silaha zako za masafa marefu, usiruhusu Kyiv kushambulia ndani ya eneo la Urusi kwa kutumia makombora .
Mnamo Septemba Rais Putin alionya kwamba endapo hilo litatokea, Moscow ingeichukulia kama "ushiriki wa moja kwa moja" wa nchi za Nato katika vita vya Ukraine.
"Hii itamaanisha kuwa nchi za Nato ... zinapigana na Urusi," aliendelea.
Mwezi uliofuata, kiongozi wa Kremlin alitangaza mabadiliko ya karibu kwa fundisho la nyuklia la Urusi, hati iliyoweka masharti ambayo kwayo Moscow inaweza kuamua kutumia silaha ya nyuklia.
Hili lilifasiriwa sana kama dokezo lingine lisilo wazi kwa Marekani na Ulaya kutoruhusu Ukraine kushambulia eneo la Urusi kwa makombora ya masafa marefu.
Kukisia hatua zinazofuata za Vladimir Putin si rahisi.
Lakini ametoa vidokezo.
Huko nyuma mwezi wa Juni, katika mkutano na wakuu wa mashirika ya habari ya kimataifa, Putin aliulizwa: Urusi itafanyaje ikiwa Ukraine ingepewa fursa ya kushambulia maeneo ya Urusi kwa silaha zinazotolewa na Ulaya?
"Kwanza, bila shaka, tutaboresha mifumo yetu ya ulinzi wa anga. Tutakuwa tunaharibu makombora yao," Rais Putin alijibu.
"Pili, tunaamini kwamba ikiwa mtu anadhani inawezekana kusambaza silaha kama hizo kwenye eneo la vita ili kushambulia eneo letu na kutuletea matatizo, kwa nini na sisi tusipeleke silaha zetu za kiwango hicho katika maeneo mengine ya dunia na kushambulia miundombinu muhimu katika mataifa yanayoichokoza Urusi?"
Kwa maneno mengine, kuwapa silaha maadui wa Magharibi kushambulia shabaha za Magharibi nje ya nchi ni jambo ambalo Moscow imekuwa ikizingatia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika mahojiano yangu ya hivi majuzi na Alexander Lukashenko, raias wa Belarus, mshirika wa karibu wa Putin alionekana kudhibitisha kuwa Kremlin imekuwa ikifikiria kwa njia hii.
Bwana Lukasjenko aliniambia alikuwa amejadili suala hilo katika mkutano wa hivi majuzi na maafisa wa Magharibi.
"Niliwaonya. 'Jamani, kuweni makini na hayo makombora ya masafa marefu," Bwana Lukashenko aliniambia.
"Wahouthi [waasi] wanaweza kuja kwa Putin na kuomba mifumo ya silaha za pwani ambayo inaweza kufanya mashambulizi ya kutisha kutoka kwenye meli.
"Na kama atalipiza kisasi kwa hatua ya kupeleka makombora ya masafa marefu kwa [Rais] Zelensky kwa kuwapa Wahouthi mfumo wa makombora wa Bastion? Je, nini kitatokea ikiwa chombo cha kubeba ndege kitashambuliwa? Iwe ni ya Uingereza au Marekani. Ni nini kitakachofuata?"
Lakini baadhi ya majibu ya vyombo vya habari nchini Urusi yalionekana kutotilia maanani suala hilo ili kupunguza mambo.
"Vikosi vya jeshi la Urusi tayari [hapo awali] vilinasa makombora ya ATACMS wakati wa mashambulizi dhidi ya ufuo wa Crimea," mtaalam wa kijeshi aliliambia gazeti la Izvestia, ambalo lilipendekeza kwamba Rais Mteule Trump anaweza "kubadilisha" uamuzi huo.
Hii ni, kuishughulikia kwa upole, hali isiyo ya kawaida.
Katika muda wa miezi miwili, Rais Biden atakuwa nje ya ofisi na Donald Trump atakuwa katika Ikulu ya White House.
Ikulu ya Kremlin inajua kuwa Rais mteule Trump amekuwa na mashaka zaidi kuliko Rais Biden kuhusu usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine.
Je! hiyo itakuwa sababu ya hesabu za Vladimir Putin wakati anapoandaa majibu ya Urusi?
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












