Je, makombora ya masafa marefu ya kuishambulia Urusi yatabadilishaje vita?

ol

Chanzo cha picha, shutterstock

Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky aliomba kuruhusiwa kutumia makombora ya ATACMS dhidi ya Urusi
    • Author, Ido Vock
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Marekani kwa mara ya kwanza imeiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu kulenga maeneo ndani ya Urusi.

Utawala unaomaliza muda wake wa Joe Biden umeiambia Kyiv kuwa inaweza kutumia makombora ya ATACMS yaliyotengenezwa na Marekani kufanya mashambulizi ndani ya Urusi, kulingana na chombo cha habari cha CBS.

Ni mabadiliko makubwa ya sera ndani ya miezi miwili kabla ya Rais Joe Biden kukabidhi madaraka kwa Donald Trump, ambaye huenda akazuia msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.

Ukraine imekuwa ikitumia makombora ya ATACMS, kuishambulia Urusi katika eneo linaloikalia ndani ya Ukraine kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Imetumia ATACMS kushambulia kambi za anga katika Rasi ya Crimea inayokaliwa na Urusi na maeneo ya kijeshi katika eneo la Zaporizhzhia.

Lakini Marekani ilikuwa haijawahi kuiruhusu Kyiv kutumia makombora hayo ya masafa marefu kushambulia ndani ya Urusi. Ni makombora yenye nguvu zaidi yaliyotolewa kwa Ukraine, husafiri hadi kilomita 300 (maili 186).

Kwa muda mrefu Ukraine inasema kutoruhusiwa kutumia silaha hizo ndani ya Urusi ni sawa na kupigana huku mkono mmoja ukiwa umefungwa nyuma.

Mabadiliko hayo ya sera yamekuja kutokana na kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini kuisaidia Urusi katika eneo la mpaka wa Kursk, ambako Ukraine imelikalia eneo hilo tangu Agosti.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky bado hajathibitisha hatua hiyo. Lakini alisema siku ya Jumapili: "Mashambulizi hayafanywi kwa maneno. Makombora yatajisemea yenyewe."

Yatakuwa na athari gani?

km

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ukraine imekuwa ikiomba ruhusa ya kutumia makombora ya ATACMS kushambulia ndani ya Urusi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukraine sasa itaweza kulenga maeneo ndani ya Urusi, hasa katika eneo la Kursk, ambapo vikosi vya Ukraine vinashikilia zaidi ya kilomita za mraba 1,000 za eneo hilo.

Maafisa wa Marekani wanasema Kyiv itaweza kutumia ATACMS kujilinda dhidi ya mashambulizi ya wanajeshi wa Urusi na Korea Kaskazini, ambayo huenda yakaanza ndani ya siku chache kwa lengo la kuichukua tena ardhi ya Urusi.

Vikosi vya Ukraine vitaweza kushambulia maeneo ya Urusi huko Kursk, pamoja na wanajeshi, miundombinu na maghala ya silaha.

Makombora ya ATACMS pengine yasitoshe kugeuza wimbi la vita. Vifaa vya kijeshi vya Urusi, kama vile ndege za kivita, tayari vimehamishiwa kwenye viwanja vya ndege ndani zaidi ya Urusi kwa hofu ya uamuzi kama huo.

Lakini makombora hayo huenda yakaipa Ukraine faida fulani wakati ambapo wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele mashariki mwa nchi hiyo.

"Sidhani kama yatakuwa na athari kubwa," mwanadiplomasia wa Magharibi huko Kyiv ameimbia BBC, akiomba kutotajwa jina kutokana na unyeti wa suala hilo.

"Hata hivyo, ni uamuzi wa kiishara kuonyesha kuiunga mkono kijeshi Ukraine. Lakini unaweza kuongeza gharama ya vita kwa Urusi."

Pia kuna maswali kuhusu ni kiasi gani cha makombora kitatolewa, anasema Evelyn Farkas, aliyewahi kuwa naibu Waziri wa ulinzi katika utawala wa Obama.

"Swali ni kwamba wana makombora mangapi? Tumesikia Pentagon ikisema hakuna makombora mengi kama haya ambayo wanaweza kutumwa kwa Ukraine."

Farkas anaongeza kuwa ATACMS yanaweza kuwa na "athari chanya ya kisaikolojia" nchini Ukraine ikiwa yatatumiwa kulenga maeneo kama vile Daraja la Kerch, ambalo linaunganisha Crimea na Urusi bara.

Uidhinishaji wa Marekani pia unaweza kuzifanya Uingereza na Ufaransa kuipa Ukraine ruhusa ya kutumia makombora ya Storm Shadow kushambulia Urusi. Storm Shadow ni kombora la masafa marefu la Ufaransa na Uingereza lenye uwezo sawa na ATACMS la Marekani.

Utawala wa Biden kwa miezi kadhaa ulikataa kuipata ruhusa Ukraine kuipiga Urusi kwa makombora ya masafa marefu, ikihofia kuongezeka kwa mzozo.

Vladimir Putin alionya dhidi ya kuruhusu silaha za Magharibi kutumika kuipiga Urusi, akisema Moscow itaona hilo kama "ushiriki wa moja kwa moja" wa nchi za Nato katika vita vya Ukraine.

"Hatua hiyo itabadilisha kwa kiasi kikubwa kiini cha mzozo," alisema Putin. "Itamaanisha kuwa nchi za Nato, Marekani na mataifa ya Ulaya, zinapigana na Urusi."

Urusi imeweka "mstari mwekundu" hapo awali. Ikiwa ni pamoja na kutotoa vifaru vya kisasa na ndege za kivita kwa Ukraine, lakini mstari huo umevukwa bila kuzusha vita vya moja kwa moja kati ya Urusi na Nato.

Kurt Volker, balozi wa zamani wa Marekani katika Nato, anasema: "Kwa kuzuia matumizi ya baadhi ya silaha za Marekani kwa Ukraine, Marekani inaweka vikwazo vya upande mmoja katika kujilinda kwa Ukraine."

Anasema uamuzi wa kuzuia matumizi ya ATACMS "ulifanywa kwa hofu ya 'kutoichokoza' Urusi."

"Hata hivyo, ni makosa kuweka hadharani mabadiliko kama haya, kwa vile inaipa Urusi taarifa ya mapema kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya Ukraine."

Trump atachukua hatua gani?

k

Chanzo cha picha, Shutterstock

Maelezo ya picha, Baadhi ya washirika wa Trump tayari wamekosoa ruhusa iliotolewa

Biden amebakiza miezi miwili tu madarakani kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Donald Trump.

Haijulikani iwapo Trump ataendelea na sera kama hiyo au la. Lakini baadhi ya washirika wake wa karibu wamekosoa uamuzi huo.

Mwanawe Trump, Donald Trump Jr ameandika kwenye mtandao wa kijamii: "Wazalisha silaha wanaonekana kutaka kuhakikisha wanaanza Vita vya Tatu vya Dunia kabla ya baba yangu hajapata nafasi ya kuleta amani na kuokoa maisha."

Trump hajaeleza ni sera gani atachukua kuhusu vita nchini Ukraine, zaidi ya kuapa kumaliza mzozo huo ndani ya siku moja, ingawa hajawahi kubainisha njia atakazotumia kufanya hivyo.

Wengi wa maafisa wakuu wa Trump, kama vile Makamu wa Rais mteule JD Vance, wanasema Marekani haipaswi kutoa msaada wowote wa kijeshi kwa Ukraine.

Lakini wengine katika utawala ujao wa Trump wana maoni tofauti. Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Michael Waltz amesema Marekani inaweza kuharakisha utoaji wa silaha kwa Ukraine ili kuilazimisha Urusi kufanya mazungumzo.

Rais mteule atapitia njia gani, haijulikani. Lakini raia wengi nchini Ukraine wanahofia kwamba atazuia utoaji wa silaha, ikiwa ni pamoja na makombora ya ATACMS.

"Tuna wasiwasi. Tunatumai [Trump] hatabadilisha [uamuzi]," anasema Oleksiy Goncharenko, mbunge wa Ukraine.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah