Biden airuhusu Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa makombora

Chanzo cha picha, White Sands Missile Range
- Author, Paul Adams & Kathryn Armstrong
- Nafasi, BBC News World
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais wa Marekani Joe Biden ametoa ruhusa kwa Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani kuishambulia Urusi.
Afisa mmoja wa Marekani ameithibitishia CBS kuhusu ruhusa hiyo, ambayo ni mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani, juu ya vita hivyo.
Kwa miezi kadhaa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekuwa akitaka vikwazo dhidi ya makombora hayo yanayojulikana kama ATACMS viondolewe – ili kuiruhusu Kyiv kufanya mashambulizi nje ya mipaka yake.
Akijibu ruhusa hiyo, siku ya Jumapili, alisema "mambo kama hayo hayatangazwi, makombora yanajieleza yenyewe."
Rais wa Urusi Vladimir Putin, siku za nyuma aliyaonya mataifa ya Magharibi dhidi ya hatua hiyo, akisema itamaanisha kuwa muungano wa kijeshi wa Nato "unashiriki moja kwa moja" katika vita vya Ukraine.
Bado Putin hajatoa maoni yake kuhusu ripoti za Jumapili, lakini wanasiasa wengine wakuu wa Kremlin wameelezea hatua hiyo kama ya kukuza vita.
Uamuzi wa Washington juu ya ATACMS unahusiana tu na kushambulia mkoa wa Kursk wa Urusi, ambapo Kyiv ilifanya uvamizi wa kushtukiza mwezi Agosti.
Utawala wa Biden unaiambia Ukraine, kwamba inaunga mkono juhudi zake za kuishikilia sehemu ndogo ya eneo la Urusi ambayo inaikalia hivi sasa, kama mtaji wa mazungumzo yoyote yanayoweza kutokea katika siku zijazo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Serhiy Kuzan, mwenyekiti wa Kituo cha Usalama na Ushirikiano cha Ukraine chenye makao yake makuu mjini Kyiv, aliambia BBC kuwa, uamuzi wa Joe Biden ni "muhimu sana" kwa nchi hiyo.
"Sio jambo litakalobadilisha mkondo wa vita, lakini nadhani litafanya vikosi vyetu kuwa imara."
Makombora ya ATACMS yanaweza kufika hadi kilomita 300 (maili 186). Maafisa wa Marekani ambao hawakutajwa majina wameyaambia magazeti ya New York Times na Washington Post kwamba Biden kutoa ruhusa kwa Ukraine kutumia ATACMS kumekuja kufuatia uamuzi wa Urusi kuruhusu wanajeshi wa Korea Kaskazini kupigana nchini Ukraine.
Bw Kuzan anasema uamuzi huo wa Jumapili umekuja kabla ya shambulio lililofanywa na wanajeshi wa Urusi na Korea, ili kuviondoa vikosi vya Ukraine kutoka eneo la Kursk nchini Urusi.
Ukraine inakadiria kuwa kuna wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini huko Kursk.
Uamuzi wa Rais Biden pia utaziwezesha Uingereza na Ufaransa kuipa Ukraine idhini ya kutumia makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow ndani ya Urusi.
Lakini Uingereza na Ufaransa bado hazijajibu uamuzi wa Biden.

Chanzo cha picha, EPA
Mwezi uliopita, Zelensky alithibitisha kwamba Ukraine imetumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani kwa mara ya kwanza kushambulia maeneo ya Urusi, mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa miezi kadhaa, Ukraine imekuwa ikipambana kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi ambao wamekuwa wakisonga mbele polepole katika eneo la mashariki la Donetsk kuelekea mji muhimu wa Pokrovsk – eneo kuu la usambazaji wa mahitaji kwa vikosi vya Ukraine.
Moscow pia imeongeza mashambulizi ya droni kwa kiasi kikubwa dhidi ya Ukraine. Zaidi ya mashambulizi 2,000 yalifanywa mwezi Oktoba, kulingana na mnadhimu mkuu wa Ukraine.
Usiku wa Jumamosi, Urusi ilifanya shambulio kubwa katika miezi ya hivi karibuni, na kuua watu wasiopungua 10. Karibu makombora 120 na droni 90 zilirushwa, kulingana na Zelensky.
Mashambulizi yaliendelea Jumapili jioni, huku maafisa katika mkoa wa Sumy - karibu na mpaka wa Urusi - wakiripoti kuwa watu wengine wanane wameuawa, wakiwemo watoto wawili, baada ya kombora kupiga jengo la makazi.
Maafisa wa Urusi katika eneo la mpakani la Bryansk waliripoti shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine siku ya Jumapili usiku lakini walisema ulinzi wake wa anga umeangusha droni 26.
Kwa miezi kadhaa Ukraine imekuwa ikisema kuwa washirika wake hawajaipatia msaada wa kutosha kuiruhusu kujilinda vyema.
Joe Biden, ambaye ataondoka Ikulu ya Marekani mwezi Januari, amekuwa akitafuta njia za kuharakisha msaada zaidi kwa Ukraine.
Kuna wasiwasi kwamba mrithi wake, Donald Trump, atapunguza au kusitisha usaidizi wa kijeshi. Anasema kuiunga mkono Ukraine kijeshi ni upotevu wa rasilimali za Marekani na ameashiria kuwa atamaliza vita, bila kueleza kwa njia gani.
Marekani imekuwa mpelekaji mkuu wa silaha kwa Ukraine. Tangu vita vianze na hadi kufikia Juni 2024, imetuma silaha na vifaa vya thamani ya dola za kimarekani bilioni 55.5 (£41.5bn), kulingana na Taasisi ya Kiel, inayohusika na masuala ya utafiti wa Uchumi wa Dunia, kutoka Ujerumani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












