Ukraine yathibitisha kurejea nyumbani kwa watu 115 waliokuwa wametekwa na Urusi

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kurejea kwa wanajeshi 115 wa Ukraine kutoka Urusi, huku Urusi ikitarajiwa kupokea idadi hiyo ya wafungwa kutoka Ukraine

Muhtasari

  • Polisi Tanzania yatoa taarifa juu ya matukio matatu ya watu kutekwa na kuuawa
  • Najutia na kuona aibu baada ya kufutwa kazi na BBC – Jenas
  • Ukraine yathibitisha kurejea nyumbani kwa wanajeshi 115 waliokuwa wametekwa na Urusi
  • Israel na Palestina: Hamas yatuma wawakilishi Cairo kwa mazungumzo
  • Majaribio ya chanjo ya RNA dhidi ya saratani ya mapafu yaanza nchini Uingereza
  • Reuters: Urusi na Ukraine kubadilishana wafungwa siku ya Jumamosi - watu 115 kila upande
  • Polisi Ujerumani wamsaka mshambuliaji wa kisu baada ya watu 3 kuuawa
  • Uchaguzi wa Marekani 2024: Robert F Kennedy Jr asitisha kampeni na kumuunga mkono Trump
  • Justin na Hailey Bieber watangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza
  • Wanafunzi wa vyuo vya tiba waliotekwa nyara Nigeria waachiliwa
  • Mapigano yanaendelea katika eneo la Kursk, huku Urusi ikishambulia kisiwa cha Ukraine

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo, tunakualika kuungana nasi hapo kesho, shukran na alamsiki.

  2. Polisi Tanzania yatoa taarifa juu ya matukio matatu ya watu kutekwa na kuuawa

    h

    Chanzo cha picha, Jeshi la Polisi Tanzania/X

    Polisi nchini Tanzania imetoa taarifa kuhusu watu matukio ya watatu walioteka na kuuawa, katika mazingira ya kutatanisha nchini humo.

    Hii imekuja baada ya hivi karibuni baaadhi ya jamaa wa watu waliopotea nchini Tanzania kuisimulia BBC kuhusu jinsi ndugu zao walivyopoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

    Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo hii leo, inamhusu kijana Samwaja Sifaeli Said, mwanye umri wa miaka 22, aliyetoweka tarehe 8 Agosti, 2024 Singida Tanzania, na mwili wake kupatikana ukiwa umefunikiwa kwenye shimo, huku sehemu zake za siri zikiwa zimekatwa.

    Kufuatia mauji ya Samwaja Sifaeli Said, taarifa hiyo inasema, wameweza kuwakamata vijana wawili ambao walikwenda kunywa pombe na marehemu, na baada ya mahojiano ‘‘waliielezea polisi kwamba ni kweli walikwenda kunywa pombe na marehemu na walipokuwa wanarejea walimuua kwa kumyonga na kisha kumkata sehemu zake za siri’’

    Polisi imeendelea kusema kuwa watuhumiwa waliieleza kuwa walielezwa na mganga wa kienyeji kuwa wakipata sehemu za siri za binadamu watakuwa matajiri.

    Baadaye watuhumiwa waliwaonyesha polisi mwili ambao ulitambuliwa kuwa ni wa Samwaja Said Raphael.

    Polisi imetaja tukio la pili linalomhusu muathiriwa mwanamke kwa jina la Ezenia Stanley Kamana mwenye umri wa miaka 32, Mkazi wa Tandika Magorofani jijini Dar es Salaam, ambaye alitekwa/ kutoweka.

    Imesema baada ya uchunguzi wake ilibaini kuwa marehemu alikuwa na rafiki yake wa kiume kwa jina Abdalla miraji@ mussa ambaye alikana kuwa na marehemu, lakini baada ya polisi kufanya uchunguzi na kupatikana kwa viungo vya marehemu, mshukiwa alikubali kuwa alimuua mpenzi wake.

    Aidha tukio jingine lililotajwa na polisi katika taarifa hiyo ni la mtoto Elia Elfaza @Raymond Mchome mkazi wa wilaya ya Handeni Tanga mwenye umri wa miaka 3 , aliyetoweka tarehe 9 Agosti, 2024 wakati alipokuwa anacheza nje.

    Polisi inasema baada ya uchunguzi wa tukio hilo ilifanikiwa kumkamata mshukiwa Jackson Elisante @ Maeda mkazi Kwadjava Tanga mwenye umri wa miaka 23. Baada ya kuhojiwa mshukiwa akiliri kuwa mtoto huyo kumfukia ndani ya chumba anachoishi, polisi imesema katika taarifa yake.

    Watuhumiwa wengine wawili bado wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

    Polisi imetoa rai kwa viongozi wa kidini, wazee wa kimila , wananchi na wadau mbali mbali kushirikiana kuzuia ‘‘ matatizo haya yanayotokea ndani ya jamii’’

    Polisi imewatahadharisha baadhi ya wananchi wenye tabia ya kujichukuliwa sheria mkononi, kufahamu kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

    Soma zaidi:

  3. Najutia na kuona aibu baada ya kufutwa kazi na BBC – Jenas

    g

    Mchezaji wa kandanda wa zamani na mtangazaji Jermaine Jenas ameliambia gazeti la the Sun kwamba "anajutia" na kwamba "amewaangusha na kuwafeli watu wengi" baada ya kufutwa kazi kama mtangazaji wa BBC.

    Aliambia gazeti hilo kwamba alituma "jumbe zisizostahili" kwa wafanyakazi wenzake wawili katika kipindi cha the One Show, lakini akasisitiza kwamba "hakufanya chochote kilicho kinyume cha sheria" na kwamba alituma jumbe hizo kwa "watu wawili wazima walioridhia".

    Mkataba wa Jenas ambaye alikuwa akitangaza vipindi vya ‘Match of the Day’ na ‘One Show’ ulisimamishwa wiki hii kwa madai ya kutuma ujumbe usiofaa kwa mfanyakazi mwenzake mwanamke.

    BBC haijatoa taarifa zaidi kuhusu madai dhidi yake.

    Jenas alianza rasmi taaluma ya kucheza kandanda akiwa na umri wa miaka 17, ambapo alichezea timu ya Nottingham Forest, ikifuatiwa na Newcastle United na Tottenham Hotspur.

    Alichezea timu ya England mara 21 na kustaafu mwaka 2016, kabla ya kuingia katika utangazaji.

  4. Ukraine yathibitisha kurejea nyumbani kwa wanajeshi 115 waliokuwa wametekwa na Urusi

    g

    Chanzo cha picha, "Ukrainian Truth"

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kurejea kwa wanajeshi 115 wa Ukraine kutoka Urusi.

    Hapo awali wizara ya ulinzi ya Urusi hapo awali ilithibitisha kuhusu mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya nchi hizo.

    "Walinzi wetu wengine 115 wamerejea nyumbani leo. Hawa ni wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Taifa, Vikosi vya Jeshi, Jeshi la Majini, Huduma ya Mpaka wa Jimbo," Rais wa Ukraine alisema.

    Alilishukuru Baraza la Uratibu la Ukraine, ambalo linashughulikia maswala ya kubadilishana kwa wafungwa, na Falme za Kiarabu, ambazo zilifanya kazi kama wapatanishi.

    Kulingana na mamlaka ya Ukraine, wale wote waliorejea nyumbani ni maandishi, ambao baadhi yao walikuwa wamekamatwa na Urusi tangu miezi ya kwanza ya uvamizi wa Urusi mnamo 2022.

    Miongoni mwa walioachiliwa ni mabaharia wa majini, walinzi wa mipakani, na walinzi 82 wa Mariupol, 50 kati yao walipigana kutetea kuchukuliwa kwa jimbo la Azovstal.

    Wawakilishi wa UAE wanasisitiza kuwa hii ni awamu ya 55 ya kubadilishanakwa wafungwa wa vita tangu mwanzo wa vita nchini Ukraine, ambapo nyingizilifanikiwa kwa upatanishi wa Abu Dhabi.

    g

    Chanzo cha picha, "Ukrainian Truth"

    Soma zaidi:

  5. Israel na Palestina: Hamas yatuma wawakilishi Cairo kwa mazungumzo

    f

    Chanzo cha picha, AFP

    Kundi la Hamas limesema kwamba wawakilishi wake wamefika mjini Cairo, Misri siku ya Jumamosi ili kusikia kutoka kwa wapatanishi kuhusu yalipofikia mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza pamoja na hatua ya kubadilishana wafungwa na mateka, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

    Wawakilishi wa Israel walikuwa mjini Cairo siku ya Alhamisi kukutana na wapatanishi kutoka taifa la Marekani, ambalo limewasilisha "pendekezo la muda" linalonuia kutatua mizozo inayoendelea, na ambalo linaangazia uwepo wa Israel katika sehemu kadhaa za Gaza.

    Shirika hilo linaripoti kuwa hakukuwa na ishara ya makubaliano kuhusu baadhi ya masuala muhimu, kama vile hatua ya Israel kusisitiza kwamba lazima idhibiti ukanda wa Philadelphi, katika mpaka wa Gaza na Misri.

    Hamas imeishutumu Israel kwa kutotimiza masuala ambayo ilikuwa imekubali kutekeleza hapo awali katika mazungumzo, madai ambayo Israel inakanusha. Aidha Hamas inadai kwamba Marekani haijaonesha nia njema katika mchakato wa upatanishi.

    Hatua hii inajiri huku Umoja wa Mataifa ukisema kwamba hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya Gaza, ikiwemo ongezeko la utapiamlo na ugonjwa wa Polio.

    Mamlaka za Palestina zilisema kwamba mashambulizi ya Israel katika Gaza yaliua watu 50 siku ya Jumamosi.

    Mazungumzo ya kuleta amani yamekuwa yakianza na kusitishwa kwa miezi kadhaa sasa, na kufikia sasa hayajaweza kumaliza kampeni ya mashambulizi ya Israel katika eneo la Gaza au kupelekea kuachiwa huru kwa mateka waliosalia baada ya shambulizi la Oktoba 7, 2023 ambalo lilisababisha vita vya sasa kuanza.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Majaribio ya chanjo ya RNA dhidi ya saratani ya mapafu yaanza nchini Uingereza

    h

    Chanzo cha picha, PA Media

    Maelezo ya picha, Janusz Racz anasema yuko tayari kujaribu kitu kipya kila wakati

    Janusz Racz, mwenye umri wa miaka 67, alikua mgonjwa wa kwanza wa saratani ya mapafu nchini Uingereza kujaribu tiba mpya yenye matumaii ambayo inaweza kubadilisha kimsingi mbinu ya kutibu ugonjwa huu.

    Chanjo hii ni ya mtu binafsi inayofundisha mfumo wa kinga ya mgonjwa fulani kupambana na ugonjwa huo kwa kuharibu seli za saratani.

    Chanjo hiyo inatokana na teknolojia ya RNA ambayo ilijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani wakati wa janga la Covid-19.

    Hatua ya kwanza ya majaribio ya kliniki ya dawa yoyote daima huangalia usalama wa dawa kwa wagonjwa. Na Janusz alikubali kwa hiari kutumika kupima chanjo hiyo mpya.

    Jumla ya watu i wa kujitolea 130 kama yeye watatumika katika kupima chanjo hii, na uchunguzi utafanywa sambamba na vituo zaidi ya 30 vya utafiti vilivyotawanyika katika nchi saba. Vituo hivi ni pamoja na Chuo Kikuu cha Chuo Kikuu cha London (UCL).

  7. Reuters: Urusi na Ukraine kubadilishana wafungwa siku ya Jumamosi - watu 115 kila upande

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi na Ukraine zitabadilishana wafungwa kufuatia makubaliano hayo yaliyoidhinishwa kupitia upatanishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), limeandika shirika la habari la Reuters, likinukuu chanzo cha UAE.

    Afisa wa Milki za kiarabu aliripotiwa kutoa maoni yake kwa sharti la kutotajwa jina kwa vile maelezo ya mabadilishano hayo bado hayajawekwa wazi.

    Gazeti la RIA Novosti la Urusi liliripoti kuwa Ukraine inatarajiwa kuwarejesha wanajeshi wa Urusi waliokamatwa wakati wa operesheni ya vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine katika mkoa wa Kursk.

    Bado hakuna maoni rasmi kutoka Kyiv na Moscow kuhusu mabadilishano yaliyopendekezwa.

    Kwa mujibu wa maafisa wa UAE, tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, watu 1,788 wamekabidhiwa baina ya pande hizo kupitia upatanishi wa Abu Dhabi.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilithibitisha habari kuhusu kubadilishana kwa wafungwa . Urusi ilirejesha wanajeshi 115 ambao walitekwa katika eneo la Kursk, na kujibu vikosi vya Ukraine vilikabidhi idadi sawa ya watu, idara ya ulinzi iliripoti.

    Soma zaidi:

  8. Polisi wa- Ujerumani wamkamata kijana mwenye umri wa miaka 15 kuhusiana shambulio la kisi lililowauwa watu 3

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Polisi wanasema nchini Ujerumani wamemkamata kijana wa miaka 15 kuhusiana na kisa hicho.

    Watu watatu wamefariki: Wanaume wawili wenye umri wa miaka 67 na 56 na mwanamke mwenye umri wa miaka 56 kufuatia shambulio hilo.

    Watu wengine nane wamejeruhiwa katika shambulio la kisu lililotokea katika mji wa magharibi wa Ujerumani wa Solingen, polisi wamesema.

    Shambulio hilo lilitokea katika tamasha lililokuwa likifanyika katikati mwa mji huo Ijumaa jioni. Watano kati ya watu nane waliojeruhiwa wako katika hali mbaya, kwa mujibu wa vyombo ya habari vya Ujerumani.

    Polisi Jumamosi walisema kwamba bado wanamsaka mshambuliaji huyo, lakini hawakutoa maelezo kuhusu nia ya kutekeleza kitendo hicho.

    Mtu huyo anaripotiwa kuwashambulia wapita njia kwa kisu wakati waakazi walipokuwa wakisherehekea miaka 650 tangu kuanzishwa kwa mji huo.

    Inaaminika kuwa mtu huyo alilenga kuwadunga watu hao kwenye shingo, kwa mujibu wa taarifa za habari nchini humo.

    Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema Jumamosi kuwa mtu huyo lazima akamatwe haraka na kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

  9. Uchaguzi wa Marekani 2024: Robert F Kennedy Jr asitisha kampeni na kumuunga mkono Trump

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi wa urais Marekani Robert F Kennedy Jr ameungana na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, jukwaani katika mkutano wa kampeni huko Arizona baada ya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono rais huyo wa zamani wa Marekani.

    Kennedy, mwenye umri wa miaka 70, aliyekuwa mwanachama wa Democrats kwa kipindi kirefu katika maisha yake na anayetokea kwenye familia kubwa ya Kennedy, alisema kwamba maadili yaliyomfanya aondoke kwenye chama hicho sasa yamemshawishi "kujitosa nyuma ya rais Trump na kumuunga mkono".

    Katika kikao na waandishi wa habari huko Phoenix, Arizona, siku ya Ijumaa, Kennedy alisema kwamba angeanza mchakato wa kuondoa jina lake kwenye karatasi za kura katika majimbo 10 ambayo yana ushindani mkubwa.

    Trump alimsifu Kennedy na kumtaja kama mtu wa "ajabu" na "mwerevu" wakati akimkaribisha jukwaani katika eneo la Glendale. Mpinzani wake wa chama cha Democrats Kamala Harris alisema angejaribu kupata uungwaji mkono wa wafuasi wa Kennedy.

    Kennedy ni mtoto wa Seneta wa zamani wa Marekani Robert F Kennedy na ni mpwa wa rais wa zamani John F Kennedy, akitokea familia yenye ushawishi mkubwa katika siasa za chama cha Democrats.

    Trump aliahidi kuwa iwapo atachaguliwa tena, angefichua kwa umma nyaraka zote zilizosalia kuhusu mauaji ya rais Kennedy ya mwaka 1963.

    Lakini uamuzi wa Bw Kennedy wa kumuunga mkono mgombwa wa chama cha Republican umeghadhabisha jamaa na familia yake, ambao mnamo Februari walikosoa hatua yake ya kutumia jina la familia hiyo katika tangazo katika shindano la Super Bowl.

    Kerry Kennedy, ambaye ni dada yake, alisema kwamba hatua ya kumuunga mkono Trump ni "kusaliti maadili ambayo baba yetu na familia yetu inachukulia kwa thamani kubwa. Huku ni kumalizika vibaya kwa hadithi mbaya."

    “Uamuzi huu unaniumiza sana kwasababu ya ugumu ambao umemsababishia mke na watoto wangu na marafiki zangu,” Bw Kennedy alisema siku ya Ijumaa.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Justin na Hailey Bieber watangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza

    h

    Chanzo cha picha, Bieber/Instagram

    Mwimbaji wa Canada Justin Bieber ametangaza kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza na mkewe Hailey Bieber.

    Katika tangazo kwenye akaunti yake ya Instagram, Bieber aliweka picha ya mguu mdogo wa mtoto wake mvulana.

    "Karibu nyumbani," Bieber aliandika katika ukurasa wake mapema Jumamosi, na kufichua jina la mtoto huyo - Jack Blues Bieber.

    Katy Perry na Kylie Jenner ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao waliwapongeza wawili hao.

    Justin na Hailey Bieber walifunga ndoa katika sherehe ya faragha mjini New York mwaka 2018.

  11. Wanafunzi wa vyuo vya tiba waliotekwa nyara Nigeria waachiliwa

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images Images

    Polisi nchini Nigeria wamethibitisha kuachiliwa huru kwa wanafunzi 20 wa afya waliotekwa nyara Agosti 15 katika jimbo la kati la Benue.

    Msemaji wa polisi Olumuyiwa Adejobi amesema wanafunzi hao waliokolewa kupitia juhudi za pamoja za vyombo vya usalama, wenyeji na ofisi ya mshauri wa usalama wa taifa.

    Wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Maiduguri na Jos walitekwa nyara walipokuwa wakisafiri kwenda kwenye kongamano la kila mwaka kusini mashariki mwa jimbo la Enugu.

    Mkuu wa polisi nchini humo Kayode Egbetokun aliimarisha msako huo wiki iliyopita kwa kuagiza timu maalum za polisi kutumia helikopta, ndege zisizo na rubani na magari ya mbinu kuwaokoa wanafunzi hao.

    Chama cha mafunzo ya tiba nchini Nigeria kimesema kuwa kikombozi kilihitajika kwa ajili ya kuachiwa kwa wanafunzi hao.

    Watekaji nyara hao walikuwa wametishia kuanza kuwaua baadhi ya wanafunzi hao iwapo hawatapata fedha hizo kufikia Jumamosi iliyopita, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.

    Bw Olumuyiwa alisema kuwa waliachiliwa "bila ya fidia yoyote kulipwa. Kwa kweli waliokolewa kwa mbinu na weledi."

    Haijulikani ikiwa kuna kukamatwa kwa watu hao, au kama kulikuwa na majeruhi wakati wa operesheni hiyo. Bw Olumuyiwa aliahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu operesheni ya uokoaji.

    Magenge yenye silaha yanayotajwa na vyombo vya habari vya ndani kama "majambazi" yanaendesha matukio ya utekaji nyara katika hifadhi za misitu zilizotelekezwa katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria.

    Serikali ya shirikisho iliyataja makundi hayo ya uhalifu kama magaidi na kupiga marufuku malipo ya fidia mwaka 2022, lakini uhalifu huo unaendelea.

  12. Mapigano yanaendelea katika eneo la Kursk, huku Urusi ikishambulia kisiwa cha Ukraine kwenye Bahari Nyeusi

    g

    Chanzo cha picha, Telegram

    Kwa mujibu wa Kamandi ya Anga ya kikosi cha kusini cha jeshi la Ukraine, usiku wa Agosti 24, 2024, washambuliaji wa mashambulizi ya makombora ya masafa marefu ya Urusi aina ya Tu-22M3 zilirusha makombora manne ya Kh-22 katika eneo la Kisiwa cha Zmeiny katika Bahari Nyeusi.

    Iliongeza kuwa , shambulio hilo liliongozwa kwa mabomu la angani yaliyodhibitiwa kwenye eneo la Kherson.

    Jeshi la Ukraine halirijapoti kuhusu athari za mashambulizi hayo ya Urusi.

    Taarifa hiyo pia ilisema kuwa katika muda wa saa 24 zilizopita, ulinzi wa anga wa kusini mwa Ukraine uliangusha dronitano za upelelezi ambazo ni : "ZALA" - 2, "Supercam" - 1, "Orlan-10" - 1, "Merlin" - 1, kwa pamoja.

    Wakati huo huo ndege zisizo na rubani za Urusi zimeendeleea kupiga katika wilaya ya Ostrogozhsky ya mkoa wa Voronezh.

    Katika Wilaya ya Ostrogozhsky ya mkoa wa Voronezh, hali ya hatari imetangazwa katika makazi matatu kwa ajili ya kukabiliana na athari za shambulio la ndege zisizo na rubani la usiku, Gavana Alexander Gusev aliripoti.

    Kulingana naye, "kutokana kuanguka kwa bifusi " vya UAV, moto uliwaka, na kusababisha "kulipuka kwa vitu."

    Watu wawili wamejeruhiwa, mmoja wao akiwa katika hali mbaya, gavana alisema. Takriban watu 200 waliokolewa.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza kuwa ndege tano zisizo na rubani zilidunguliwa usiku kucha katika eneo la mkoa wa Voronezh.

    Video kutoka eneo linalodhaniwa kuwa la shambulio la usiku zilizochapishwa kwenye mitandaoya kijami zinaonyesha moto ukiwaka kwenye eneo la tukio.

    Soma zaidi:

  13. Hujambo na karibu kwa matangazo ya mubashara leo ikiwa ni Jumamosi tarehe 24.08.2024