Kwa nini Ukraine imeanzisha mashambulizi ya mpakani dhidi ya Urusi?

g

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin akikutana na wajumbe wa baraza la mawaziri baada ya shambulio la Ukraine huko Kursk
Muda wa kusoma: Dakika 3

Na James Waterhouse

BBC News, Kyiv

Wakati Kyiv ilipoanzisha mashambulizi ya kuvuka mpaka katika eneo la Kursk la Urusi linalopakana na Ukraine, swali kutoka kwa wataalamu fulani wa kijeshi lilikuwa: “Kwa nini?”

Moja ya matatizo makubwa ya uwanja wa vita nchini Ukraine ni uhaba wa wapiganaji. Urusi ina wanajeshi zaidi na wanajeshi wake wanakaribia mji wa Pokrovsk mashariki mwa Ukraine.

Kwa hivyo, kutuma mamia ya askari wa Ukraine nchini Urusi , tuseme, ni jambo ambalo halikutarajiwi kwa maoni ya wengi.

Lakini si wote.

"Haikuwa bahati mbaya," mtaalamu wa vita Kostyantyn Mashovets alisema katika chapisho la Facebook. "Ni wazi ni sehemu ya mpango mmoja kabambe."

Mchambuzi wa kijeshi Mykhaylo Zhyrokhov, anaafiki. Aliiambia BBC kwamba Urusi ililazimika kupeleka tena baadhi ya wanajeshi huko kutoka mstari wa mbele mashariki mwa Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Ukiangalia ripoti rasmi, kulikuwa na mabomu machache sana ya Urusi yaliyorushwa katika eneo la Donetsk," alisema.

"Hiyo inamaanisha kuwa ndege zinazoyabeba sasa ziko mahali pengine nchini Urusi."

Hakuna uwezekano mkubwa kwamba kwa uvamizi huu Ukraine inataka kumiliki eneo la Urusi, lakini iwapo kuvuta vikosi vya Urusi lilikuwa ndio lengo, basi linatekelezwa haraka.

Historia ya hivi karibuni inaweza kuwa sababu pia. Urusi ilianzisha mashambulizi yake ya kuvuka mpaka katika eneo la kaskazini-mashariki la Kharkiv la Ukraine.

Hatua hiyo inaonekana kupungua baada ya Marekani kuipa Ukraine ruhusa ya kutumia makombora yake ya kulenga shabaha ndani ya Urusi.

Hofu ya Ukraine ya shambulio kama hilo katika eneo la kaskazini la Sumy imekuwa ikiongezeka katika miezi mitatu iliyofuata.

Kutokana na wasiwasi wa mara kwa mara wa nchi za Magharibi wa kuongezeka kwa vita, kuna uwezekano wa aina fulani ruhusa ilitolewa kwa operesheni ya ukubwa huu kwenye ardhi ya Urusi.

Kwa ujumla, ni watu wachache waandamizi wa Ukraine wanaosema mengi kuhusu shambulio hili.

Ofisi ya rais ilituambia: "Hakuna maoni, kwa sasa."

Ingawa uvamizi kama huo umetokea hapo awali, ni mara ya kwanza kwa vikosi vya kawaida vya Ukraine kutumika kwa njia hii.

Unaweza pia kusoma:
g

Duru za kijeshi za Urusi ziliripoti haraka shambulio hilo lililohusisha mamia ya wanajeshi na mashambulizi kadhaa ya roketi na ndege zisizo na rubani.

Viongozi wa eneo hilo pia walikuwa wepesi katika kutangaza majeruhi na kuhamishwa kwa watu kutoka eneo la tukio. Mikoa jirani ilionyesha nia ya kukubali wale waliolazimishwa kuzitoroka nyumba zao.

Hali ya hatari imetangazwa huko pia.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi hata ilikiri kuwa wanajeshi walikuwa wakitumwa tena kuelekea Sudzha, mji uliopo katika mkoa wa Kursk.

Rais Vladimir Putin pia alionekana akizungumza na wakuu wake wa usalama kuhusu shambulio hilo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje aliliita shambulio hilo la "kinyama" na "kigaidi".

Hadi jana Urusi ilikuwa ikiliteka eneo hilo kwa kasi huku ikiwazidi nguvu wanajeshi wa Ukraine.

Sasa kuna jambo lingine la kufikiria.

Shambulio hilo tayari linaelezewa na Kremlin kama ushahidi wa kwa nini inapaswa kuendelea na vita vyake - uvamizi ambao bado wanauita kama wa "kujihami".

"Kuna maswali zaidi kuliko majibu yanayotokana na matukio katika eneo la Kursk," anasema mchambuzi wa masuala ya kijeshi Mykhaylo Zhyrokhov.

Ni wazi kwa Ukraine, kwamba iwapo itakwama au hata kuizuia Urusi kufanya mashambulizi kutekeleza makubwa kaskazini mwake, itaona operesheni hii kuwa ya thamani yake.

"Kadiri shinikizo linavyozidi kutolewa kwa mvamizi aliyeleta vita nchini Ukraine," alisema Rais Zelensky katika hotuba yake ya jioni, ndivyo "Amani itakavyokaribia haraka ."

"Amani ya haki kupitia nguvu ya haki."alisema.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah