Mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani yashuhudiwa Ukraine

Takriban watu watatu wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika shambulio kubwa zaidi la drone la Urusi katika mji wa Kharkiv, nchini Ukraine, meya alisema.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo, Kwaheri.

  2. Marekani yamrudisha aliyefukuzwa kimakosa kujibu mashtaka

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kilmar Ábrego García, mwenye umri wa miaka 29 kutoka El Salvador aliyefukuzwa kimakosa mnamo mwezi Machi nchini Marekani, amerudishwa kujibu mashtaka mawili ya jinai.

    Amekuwa akishutumiwa kwa kushiriki katika njama ya usafirishaji haramu wa binadamu kwa miaka kadhaa ya kuwahamisha wahamiaji wasio na vibali kutoka Texas hadi maeneo mengine ya nchi.

    El Salvador ilikubali kumwachilia Bw Ábrego García baada ya Marekani kuwasilisha hati ya kukamatwa kwake, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Pam Bondi alisema Ijumaa.

    Wakili wake alitaja mashtaka hayo kuwa ya "upuuzi".

    Ikulu ya Marekani ilikuwa ikipinga amri ya Mahakama ya Juu ya Marekani kutoka Aprili ya "kuwezesha" kurejea kwake baada ya kusafirishwa hadi jela ya huko El Salvador pamoja na zaidi ya watu wengine 250 waliofukuzwa nchini Marekani

  3. Mwili wa mateka wa Thailand wapatikana Gaza - Israel

    .

    Chanzo cha picha, Israel Katz/X

    Israel imepata mwili wa raia wa Thailand aliyetekwa mateka wakati wa shambulizi lililofanywa na Hamas mnamo Oktoba 2023, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema.

    Alisema mwili wa Nattapong Pinta ulipatikana wakati wa operesheni maalum katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza siku ya Ijumaa. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 35 alikuwa akifanya kazi kama mfanyakazi wa kilimo kusini mwa Israel alipotekwa nyara.

    Bw Nattapong huenda aliuawa wakati wa miezi yake ya kwanza ya kutekwa, afisa wa kijeshi wa Israel alisema. Kabla ya kufanyika kwa operesheni hiyo, haikujulikana ikiwa alikuwa amekufa au yu hai.

    Haya yanajiri baada ya jeshi la Israel kupata miili ya Wamarekani wawili wenye asili ya Israel huko Gaza mapema wiki hii.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mpenzi wa zamani wa Diddy atoa ushahidi kuhusu jinsi alivyoshinikizwa kushiriki ngono

    .

    Chanzo cha picha, Jane Rosenberg/Reuters

    Mpenzi wa zamani wa Sean "Diddy" Combs, alitoa ushahidi kwa siku ya pili katika kesi ya jinai chini ya jina bandia "Jane", na kuelezea jinsi alivyohisi kushinikizwa kushiriki ngono na wasindikizaji wa kiume waliokuwa wakiandamana naye huku akimtazama, licha ya yeye kueleza kuwa jambo hilo lilimkasirisha.

    Pia alidai kuwa mtandao wa wafanyikazi ulimsaidia kupata dawa kukabiliana na matukio ya ngono yaliyopangwa kwa makusudi katika kile kilichofahamika kama "freak-offs", ambako kulimwacha akiwa na maumivu makali na maambukizi ya mara kwa mara.

    Waendesha mashitaka wamemshtaki Bw Combs, 55, kwa kula njama ya ulaghai, ulanguzi wa ngono, na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba.

    Hata hivyo amekanusha mashtaka yote.

    Soma zaidi:

  5. Jeshi la anga la Ukraine linadai kuwa limedungua ndege ya Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine imedai kuidungua ndege ya kivita ya Urusi aina ya Su-35.

    Bado hakuna taarifa iwapo huu ulikuwa makabiliano ya angani wenye kuhusisha ndege za Ukraine, au ni kazi ya mfumo wa ulinzi wa anga ya ardhini - kama vile makombora ya kutoka ardhini hadi angani au mifumo ya kujikinga dhidi ya ndege za kivita.

    Ujumbe wa jeshi la wanahewa la Ukraine linasema: "Asubuhi ya leo, Juni 7, 2025, kama matokeo ya operesheni iliyofanikiwa ya Jeshi la Anga katika upande wa Kursk, ndege ya kivita ya Urusi ya Su-35 ilidunguliwa!"

    Su-35 ni ndege ya teknolojia ya juu ambayo hutumiwa katika vita. Sawa na ndege hii nchini Marekani ni toleo la kisasa zaidi la ndege ya F-15.

    Asubuhi ya leo, jeshi la wanahewa la Ukraine pia liliweka video inayoonyesha ndege ikiungua ardhini. Video hiyo inaonekana kunaswa na vifaa vya ulengaji shabaha juu ya anga - kama vile ndege isiyo na rubani au ndege nyingine.

    Hakuna uthibitishaji huru wa udunguaji huu na vile vile, wizara ya ulinzi ya Urusi bado haijasema lolote.

    Soma zaidi:

  6. Waliohusika na ghasia za Bunge la Marekani waishtaki serikali

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Viongozi watano wa kundi la mrengo wa kulia la Proud Boys, ambao walipatikana na hatia ya kuhusika na ghasia zilizotokea Bungeni za Januari 6, 2021, wameishtaki serikali ya Marekani wakitaka dola milioni 100 (£74m), kwa madai kuwa haki zao zilikiukwa wakati waliposhtakiwa.

    Watano hao walipatikana na hatia ya kupanga njama na kushiriki katika ghasia za kutaka kubadilisha matokeo baada ya Rais Donald Trump kushindwa katika kinyang’anyiro cha mwaka 2020.

    Kuna wale ambao Trump aliwasamehe ama kubatilisha adhabu zao mapema mwaka huu.

    Kesi hiyo, iliyowasilishwa Florida siku ya Ijumaa, inadai kuwa maafisa wa FBI na waendesha mashtaka walikuwa na upendeleo wakati wa kuendesha kesi zao.

    Wanahoji kuwa haki zao za kikatiba zilikiukwa kwa "kuwaadhibu na kuwakandamiza washirika wa kisiasa" wa Trump.

    Soma zaidi:

  7. Wagner wajiondoa nchini Mali baada ya 'kumalizika kwa misheni yake'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kundi la Wagner limetangaza kujiondoa Mali kufuatia kile walichokiita "kumalizika kwa misheni yake kuu" katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

    Kundi la mamluki la Urusi limekuwa likishirikiana na jeshi nchini humo tangu mwaka 2021, kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram, Wagner ilisema "imepambana na ugaidi hatua kwa hatua na watu wa Mali", na kuua "maelfu ya wanamgambo na makamanda wao, ambao waliwatishia raia kwa miaka mingi".

    Tangazo hilo la kujiondoa linawadia siku ambayo kumetolewa ripoti kwamba wanajeshi wa Mali walikuwa wameondoka katika kambi kubwa katikati mwa nchi, baada ya kushambuliwa kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki moja.

    Mali imekuwa ikikabiliana na wanamgambo wa waasi wa Kiislamu kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Wanajeshi wa Ufaransa, ambao awali walitumwa kusaidia serikali ya kiraia, waliondoka nchini humo mwaka wa 2022.

    Kufikia wakati huo, jeshi linalosimamia Mali lilikuwa tayari limeanza kufanya kazi na mamluki wa Kirusi kupambana na wanamgambo.

    Mashambulizi ya wanajihadi yamekuwa yakiongezeka kwenye kambi za kijeshi katika jimbo la Sahel katika wiki za hivi karibuni.

    Soma zaidi:

  8. Mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani yatokea Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Ukraine's state emergencies service DSNS in Kharkiv region

    Takriban watu watatu wameuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulizi kubwa zaidi la ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv nchini Ukraine, meya amesema.

    Ihor Terekhov amesema kwamba usiku kucha Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 48, pamoja na makombora mawili ya kuongozwa kutoka mbali.

    "Tuna kopo mkubwa," amesema, akiongeza kuwa majengo matatu ya ghorofa yalishambuliwa. Kanda za video zimeibuka zikionyesha ghorofa kadhaa za jengo moja kama hilo likiwaka moto.

    Watu sita waliuawa na 80 kujeruhiwa kote Ukraine usiku uliopita , wakati Urusi ilishambulia nchi hiyo kwa zaidi ya droni 400 na karibu makombora 40.

    Urusi ilisema kuwa nishati ya angani ilikuwa yakijibu "vitendo vya kigaidi vya Kyiv", ikidai kuwa maeneo ya kijeshi yalilengwa.

    Hili limejitokeza siku chache baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine zikilenga ndege za kimkakati za Urusi katika vituo vinne vya anga ndani ya nchi hiyo.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja, tarehe ni 07/06/2025