Wagner: Jinsi kundi la mamluki wa Urusi lilivyobadilisha mbinu zake Barani Afrika

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Joe Inwood & Jake Tacchi
- Nafasi, BBC Newsnight & BBC Eye Investigations
Urusi inazipa serikali barani Afrika "njia za kuendelea kusalia madarakani" kwa mabadilishano ya kupata rasilimali muhimu, kwa mujibu wa ripoti mpya.
Nyaraka za ndani za serikali ya Urusi, zilizoonekana na BBC, pia zinaelezea jinsi inavyofanya kazi kubadilisha sheria za madini katika Afrika Magharibi, kwa nia ya kuyaondoa makampuni ya Magharibi kutoka maneo muhimu.
Hii ni sehemu ya mchakato wa serikali ya Urusi kuchukua biashara za kikundi cha mamluki cha Wagner, kilichovunjika baada ya mapinduzi yaliyoshindwa mnamo Juni 2023.
Operesheni hizo za mabilioni ya pesa sasa zinaendeshwa zaidi kama "Kikosi cha Usafiri" cha Urusi, kinachosimamiwa na mtu anayetuhumiwa kupanga jaribio la mauaji ya Sergei Skripal kwa kutumia sumu ya Novichok nchini Uingereza - shtaka ambalo Urusi imekanusha.
"Hili ni taifa la Urusi linajitokeza katika sera yake ya Afrika," kwa mujibu wa Jack Watling, mtaalamu wa vita vya ardhi katika Taasisi ya Huduma ya Royal United (Rusi) na mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo.
Mnamo Juni 2023, Yevgeny Prigozhin alikuwa mamluki wa kuogopwa zaidi na maarufu ulimwenguni. Kundi lake la Wagner lilikuwa linadhibiti makampuni na miradi yenye thamani ya mabilioni ya dola, huku wapiganaji wake wakiwa kiini cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Kisha, akaamua kuandamana kwenda Moscow, akitaka waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi kuondolewa madarakani, lakini kwa kweli alimtishia Rais Vladimir Putin kwa njia ambayo hakuna mtu aliyewahi kufanya hapo awali.
Ndani ya wiki chache alikuwa amefariki katika ajali ya ndege iliyotiliwa shaka sana, pamoja na viongozi wengine wa Wagner. Kulikuwa na uvumi mwingi wakati huo jkuhusu hatma ya kundi la Wagner. Sasa tuna jibu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na Dk Watling, "kulikuwa na mkutano huko Kremlin muda mfupi baada ya maasi ya Prigozhin, ambapo iliamuliwa kuwa shughuli za Wagner za Afrika zingeingia moja kwa moja chini ya udhibiti wa ujasusi wa kijeshi wa Urusi.
Udhibiti ulipaswa kukabidhiwa kwa Jenerali Andrey Averyanov, mkuu wa Kitengo cha 29155, operesheni ya siri ya mauaji na kuvuruga serikali za kigeni.
Lakini inaonekana biashara mpya ya Jenerali Averyanov haikuwa ikivuruga serikali, bali ni kupata mustakabali wao, mradi tu walipe kwa kutia saini haki zao za madini.
Mapema Septemba, akifuatana na naibu Waziri wa Ulinzi Yunus-Bek Yevkurov, Jenerali Averyanov alianza ziara ya shughuli za zamani za Wagner barani Afrika.
Walianza na Libya, wakikutana na mbabe wa kivita Jenerali Khalifa Haftar. Kituo chao kilichofuata kilikuwa Burkina Faso ambapo walilakiwa na kiongozi wa mapinduzi Ibrahim Traoré mwenye umri wa miaka 35.
Baada ya hapo, walitua Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo huenda ndiyo operesheni iliyoimarishwa zaidi ya Wagner barani, kabla ya kuelekea Mali kukutana na viongozi wa serikali ya kijeshi huko.

Chanzo cha picha, AFP
Katika safari iliyofuata pia walikutana na Jenerali Salifou Modi, mmoja wa wanajeshi walionyakua mamlaka nchini Niger mwaka jana.
Mikutano hii inaonyesha kwamba wanaume hao wawili walikuwa wakiwahakikishia washirika wa Wagner katika bara kwamba kufa kwa Prigozhin hakumaanishi mwisho wa mikataba yake ya biashara.
Ripoti za mkutano na Kapteni Traoré wa Burkina Faso zilithibitisha ushirikiano utaendelea katika "kikoa cha kijeshi, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya maofisa katika ngazi zote, ikiwa ni pamoja na marubani nchini Urusi".
Kwa kifupi, kifo cha Prigozhin haikumaanisha mwisho wa uhusiano wa junta na Urusi. Kwa njia fulani, ungekuwa dhabiti zaidi.
Mataifa matatu ya Afrika Magharibi yenye uhusiano wa karibu na Wagner - Mali, Niger na Burkina Faso - yote yamekumbwa na mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Tangu wakati huo wametangaza kujiondoa katika Jumuiya ya Ecowas, na kuunda "Muungano wao wa Mataifa ya Sahel".
Labda iliyohusishwa zaidi na mamluki ilikuwa Mali, ambapo uasi unaoendelea wa Kiislamu, pamoja na mapinduzi mengi, ulikuwa umeacha taifa lililofeli.
Hapo awali, usaidizi wa usalama ulikuja katika mfumo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kama Minusma, pamoja na operesheni ya muda mrefu ya jeshi la Ufaransa kukabiliana na waasi.
Lakini hakukuwa na mapenzi kwa Ufaransa, mamlaka ya zamani ya kikoloni, na hivyo wakati kundi la Wagner lilipojitolea kubadilisha shughuli zao za usalama na kuungwa mkono na Urusi, ofa hiyo ilikubaliwa.
"Wafaransa walivumiliwa, badala ya kukaribishwa," anasema Edwige Sorgho-Depagne, mchambuzi wa siasa za Afrika ambaye anafanya kazi na Amber Advisers.
"Mamlaka ya Wafaransa kusaidia katika mzozo wa ugaidi katika Sahel mara zote yalizingatiwa kuwa ya muda mfupi. Kwa hiyo, ukweli kwamba Wafaransa walikaa kwa muda huo - zaidi ya miaka 10 - bila kutafuta njia ya kumaliza mgogoro huo haikusaidia."

Chanzo cha picha, TELEGRAM
Lakini kwa watawala wa kijeshi wanaoendesha nchi hizi, uwepo wa kijeshi wa Urusi una faida dhahiri.
"Hapo awali, hawa watawala walikuwa viongozi wa mpito. Walitakiwa kuandaa uchaguzi na kurejesha taasisi za kidemokrasia."
"Lakini sasa wanamgambo wa Kirusi wanaletwa kulinda junta ya kijeshi, kuwaruhusu kukaa muda mrefu kama wanataka."
Junta iliamuru vikosi vya Ufaransa kuondoka na Mali sasa inamtegemea Wagner kwa usalama wake wa ndani, mabadiliko ambayo yana athari ya haraka kwa raia wa kawaida wa Mali.
"Kile Warusi wametoa ni kikosi cha kushambulia, na helikopta zenye uwezo wa hali ya juu na nguvu nyingi za moto," anasema Dk Watling. "Wanatumia mbinu za Kisovieti za kupinga upendeleo. Unaona wapiganaji ambao waliuawa, pamoja na raia waliolengwa kuwezesha au kuhusishwa na wapiganaji."
Kumekuwa na madai mengi kwamba vikosi vya Wagner viliendesha ukiukaji wa haki za binadamu katika bara la Afrika, na vile vile huko Ukraine na Syria, ambapo kundi hilo la Prigozhin hapo awali lilikuwa likihudumu.
Moja ya matukio yaliyothibitishwa vyema yalitokea katika mji wa Moura katikati mwa Mali ambapo, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, takriban watu 500 wanaaminika kuuawa na wanajeshi wa Mali na "wazungu wenye silaha", ambao mashuhuda wa tukio hilo wamewaeleza kuwa waliozungumza "lugha isiyojulikana".
Ingawa uthibitishaji huru haujafanyika, Shirika la Human Rights Watch ilitambua washambuliaji wazungu wasiojulikana kuwa mamluki wa Urusi.

Chanzo cha picha, TELEGRAM
Kwa kubadilishana na usaidizi mkubwa, wa kikatili, wa usalama, Wagner walihitaji kitu kama malipo.
Mali, kama mataifa mengi ya Kiafrika, ina utajiri mkubwa wa maliasili - kutoka kwa mbao na dhahabu hadi uranium na lithium. Baadhi ni muhimu tu, wakati wengine wana umuhimu wa kimkakati pia.
Kulingana na Dk Watling, Wagner walikuwa wakifanya kazi katika hali iliyoimarishwa vyema: "Kuna utaratibu wa kawaida wa Kirusi, ambao ni kwamba unalipia gharama za uendeshaji na shughuli za biashara. Katika Afrika, hiyo ni hasa kupitia makubaliano ya madini."
Katika kila nchi ambayo inaendesha shughuli zake, Wagner waliripotiwa kupata maliasili za thamani kwa kutumia hizi sio tu kulipia gharama, lakini pia kupata mapato makubwa. Urusi imechota dhahabu yenye thamani ya dola bilioni 2.5 kutoka Afrika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ambayo huenda ikasaidia kufadhili vita vyake nchini Ukraine, kulingana na ripoti ya Blood Gold.
Mwezi huu, wapiganaji wa Urusi - ambao zamani walikuwa mamluki wa Wagner - walichukua udhibiti wa mgodi wa dhahabu wa Intahaka wa Mali, karibu na mpaka na Burkina Faso. Mgodi huo mkubwa zaidi kaskazini mwa Mali, umekuwa ukizozaniwa kwa miaka mingi na makundi mbalimbali yenye silaha katika eneo hilo.
Lakini kuna jambo lingine, lenye umuhimu wa kijiografia na kisiasa.
"Sasa tunawatazama Warusi wakijaribu kuondoa kimkakati udhibiti wa Magharibi wa upatikanaji wa madini na rasilimali muhimu," anasema Dk Watling.
Nchini Mali, kanuni za uchimbaji madini ziliandikwa upya hivi karibuni ili kuwapa utawala mkubwa udhibiti wa maliasili. Mchakato huo tayari umeshuhudia mgodi wa lithium wa Australia ukisitisha biashara ya hisa zake, kwa sababu ya kutokuwa na uhakika juu ya utekelezaji wa kanuni hiyo.
Ingawa migodi ya lithium na dhahabu ni muhimu, kulingana na Dk Watling kuna uwezekano mkubwa wa hali ngumu inayokuja: "Nchini Niger Warusi wanajaribu kupata makubaliano kama hayo ambayo yatawanyima Wafaransa ufikiaji wa migodi ya uranium nchi humo."

Chanzo cha picha, AFP
Ripoti hiyo inaelezea ilani za ndani za Kirusi zinazolenga katika kujaribu kunafikisha nchini Niger kile kilichofanyika nchini Mali. Iwapo Urusi ingefanikiwa kudhibiti migodi ya urani ya Afrika Magharibi, Ulaya inaweza kuachwa wazi tena kwa kile ambacho mara nyingi kimekuwa kikiitwa "uhasama wa nishati" wa Urusi.
Ufaransa inategemea zaidi nishati ya nyuklia kuliko nchi nyingine yoyote duniani, na vinu 56 vinavyozalisha karibu theluthi mbili ya nishati ya nchi hiyo. Karibu moja ya tano ya uranium yake inaagizwa kutoka Niger. Hapo awali kumekuwa na malalamiko kuhusu masharti ya biashara, na mapendekezo kwamba mamlaka ya kikoloni ya zamani yananyonya mataifa kama Niger.
"Masimulizi ambayo Urusi inasisitiza ni kwamba mataifa ya Magharibi yanasalia kuwa ya kikoloni katika mtazamo wao," anasema Dk Watling. "Inashangaza sana kwa sababu mbinu ya Warusi, ambayo ni kutenga tawala hizi, kukamata wasomi wao na kutafuta maliasili zao, ni ya kikoloni."
Kwa kweli, "Jeshi la Usafiri" linaonekana zaidi kama "Wagner 2.0. Prigozhin ilikuwa imejenga uhusiano wa kina wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi katika bara la Afrika - kuvunja mtandao huu tata ingekuwa vigumu na usio na faida.
Kulingana na Dk Watling, mabadiliko ya kimsingi yanatokana na "uwazi ambao Urusi inafuata sera yake". Kikundi cha Wagner cha Prigozhin kilikuwa kimeipa Urusi namna ya kukana shughuli na ushawishi wake nje ya nchi.
Kufuatia uvamizi kamili wa Ukraine, wengi katika vyombo vya usalama vya Magharibi wanasema kwamba barakoa ya Urusi iliteleza.
"Wanachotafuta kufanya ni kuzidisha mizozo yetu kimataifa. Wanajaribu kuwasha moto mahali pengine, na kuchochea ile mioto ambayo tayari ipo, na kufanya ulimwengu usio salama," Dk Watling.
"Mwishowe, inatudhoofisha katika shindano la kimataifa ambalo tunakabiliana nalo kwa sasa. Kwa hivyo athari hazionekani mara moja, lakini baada ya muda, ni tishio kubwa."
Imetafsiriwa na Jaison Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












