Yevgeny Prigozhin: Jaribio la ustahimilivu wa shughuli za Wagner barani Afrika

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kifo cha mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin, kikithibitishwa, kitajaribu uthabiti wa operesheni za maelfu ya mamluki wanaofanya kazi nchini Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Libya.

Wagner ina ushawishi mkubwa katika bara la Africa ambapo inatoa usalama kwa baadhi ya viongozi wa Afrika kwa kupatiwa madini na makubaliano mengine ya kimkakati ya kiuchumi na kijeshi.

Kundi hilo pia limekuwa muhimu katika kueneza ushawishi wa Urusi kupitia kampeni za vyombo vya habari ambazo kimsingi zinadharau Magharibi.

Huko CAR, ambapo vikosi vya Wagner vilialikwa na Rais Faustin-Archange Touadéra mnamo 2018, mamluki hao wameenea katika sekta ya vyombo vya habari, mbao na hata vodka ili kuunganisha masilahi ya kiuchumi katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini.

Mapema wiki hii, Russia House, kituo cha kitamaduni chenye uhusiano na Wagner kilichoko katika mji mkuu wa CAR, Bangui, kilitangaza maonyesho ya biashara ya miezi mitatu kwa wafanyabiashara wa Urusi wanaotaka kupanua shughuli katika eneo hilo.

Hii inaweza kuwezesha kampuni zinazohusishwa na Wagner kufanya kazi nchini CAR na kukwepa vikwazo vya Magharibi.

Hata hivyo, mamluki wanaofanya kazi nchini CAR wameshutumiwa kwa ukatili wakati wakipigana na waasi nyuma ya nchi hiyo kutokuwa na utulivu.

Serikali inayoongozwa na jeshi la Mali pia imekuwa ikiitegemea sana Wagner baada ya kumaliza makubaliano ya usalama na Ufaransa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, waandamaji wakiwa wamebeba bendera ya Urusi

Angalau mamluki 1,000 walitumwa huko mwishoni mwa 2021, ingawa maafisa wanakanusha uwepo wao.

Mwezi Mei, Marekani ilimuwekea vikwazo kiongozi mkuu wa Wagner huko, Ivan Maslov, kwa kutumia Mali kupata silaha kwa ajili ya juhudi za vita vya Urusi nchini Ukraine.

Aina mbalimbali za shughuli zinasisitiza umuhimu wa Afrika kwa sera ya kigeni ya Urusi.

Walakini, uaminifu wa watendaji wa Wagner kwenye bara itakuwa muhimu katika kuunganisha ushawishi wa siku zijazo wa Moscow.

Yevgeny Prigozhin alikua Afrika mara ya mwisho?

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Video inayoaminika kuwa alikua Afrika

Baada ya zoezi lilofeli la kuongoza uasi, Prigozhin alichapisha video yake ya kwanza, akionekana - inawezekana iliyopigwa barani Afrika - kwenye chaneli za Telegram zinazohusishwa na kundi la Wagner.

Mtu ambaye anaonekana kuwa kiongozi wa mamluki mwenye umri wa miaka 62 anaonekana kwenye video akiwa amesimama katika eneo la jangwa akiwa amejificha na akiwa na bunduki mikononi mwake. Kwa mbali, kuna watu wengi wenye silaha na lori la mizigo.

Mbabe huyo wa kivita anasema kuwa alikua barani Afrika, na kuongeza kuwa "joto ni pamoja na 50 [digrii Selsiasi]".

Alisema Wagner inaendesha shughuli za uchunguzi na utafutaji na "kuifanya Urusi kuwa kubwa zaidi katika mabara yote, na Afrika kuwa huru zaidi".

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wengi wa wagner ni wafuasi wa kiongozi wao

Mustakabali wa Wagner barani Afrika ulikuwa wa shaka hata kabla ya 'kifo' cha Prigozhin?

Hata kabla ya ajali ya ndege ya jana, mustakabali wa Wagner na shughuli zake barani Afrika ulikuwa mashakani.

Vyanzo vilivyo karibu na kundi hilo vinasema kulikuwa na mipango inaendelea, ikiongozwa na naibu mkurugenzi wa kitengo cha kijasusi cha kijeshi cha Urusi GRU, kuchukua nafasi ya sehemu kubwa ya Wagner na kundi sambamba la mamluki.

Prigozhin alisemekana kupinga hili kwa hasira na alikimbia kurudi kutoka Mali hadi Urusi ili kujaribu kulizuia.

Kinachoshumbua kichwa Kremlin sasa ni nini cha kufanya na wapiganaji wa Wagner 25,000, waliotawanyika katika nchi kadhaa, ambao wengi wao waliona uaminifu wao kuwa kwa Prigozhin, badala ya wizara ya ulinzi ya Moscow iliyodharauliwa sana.