Yevgeny Prigozhin: Tunachojua hadi sasa kuhusu ajali ya ndege

Chanzo cha picha, Reuters
Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin anaaminiwa kufariki, baada ya kutajwa kwenye orodha ya abiria ya ndege ya kibinafsi iliyoanguka kaskazini mwa mji mkuu wa Urusi, Moscow.
Mshirika mkuu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, kampuni yake ya kijeshi ya kibinafsi imekuwa na jukumu muhimu nchini Ukraine kufuatia uvamizi wa Moscow mnamo Februari 2022.
Lakini uhusiano wake na Bw Putin ulidorora baada ya Prigozhin kuamuru wanajeshi wake kuandamana mjini Moscow katika uasi wa siku nzima dhidi ya viongozi wa kijeshi wa Urusi mwezi Juni.
Maelezo ya ajali hiyo bado yanaibuka lakini haya ndio tunayojua hadi sasa.
Nini kilitokea kwa ndege?
Maafisa wa anga wa Urusi walithibitisha kuwa ndege hiyo, Embraer Legacy, ilikuwa ikisafiri kati ya Moscow na St Petersburg ilipoanguka katika eneo la Tver, kaskazini mwa Moscow Jumatano jioni.
Lakini kituo cha Telegram kinachohusishwa na Wagner, Gray Zone kiliripoti kuwa ndege hiyo ilidunguliwa na jeshi la Urusi - ingawa hakikutoa ushahidi wowote wa kuunga mkono madai yake.

Ndege hiyo ya kibinafsi ilikuwa imebeba abiria saba na wahudumu watatu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, watu wote 10 waliokuwa ndani ya ndege hiyo waliuawa. Miili yote inasemekana kupatikana.
Ndege hiyo ya Embraer Legacy - iliyosajiliwa na moja ya kampuni za Prigozhin - iliwaka moto ilipogonga ardhi baada ya kuripotiwa kuwa angani kwa chini ya nusu saa.
Picha za video zilizothibitishwa na BBC zilionyesha ndege ikianguka kutoka angani katika eneo la Kuzhenkino, Urusi.
Inaripoti kwamba ndege ya pili ya biashara inayomilikiwa na Prigozhin ilitua salama katika mkoa wa Moscow.
Nani alikuwemo ndani yake?
Ndege hiyo ya kibinafsi iliyoanguka ilikuwa na abiria saba na wafanyakazi watatu.
Shirika la usafiri wa anga la Russia liliwataja abiria hao saba kuwa ni: Prigozhin na mshirika wake wa karibu Dmitry Utkin, Sergei Propustin, Yevgeny Makaryan, Alexander Totmin, Valery Chekalov na Nikolai Matuseyev.
Wafanyakazi hao walitambuliwa kuwa ni Rubani Alexei Levshin, rubani mwenza Rustam Karimov na mhudumu wa ndege Kristina Raspopova.
Tunajua nini kuhusu shughuli za hivi karibuni za Prigozhin?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ndege hiyo ya kibinafsi inaaminiwa kuwa ilikuwa njiani kutoka Moscow kuelekea St Petersburg ilipoanguka karibu maili 60 kaskazini mwa mji mkuu wa Urusi.
Tangu uasi wake wa muda mfupi dhidi ya makamanda wakuu wa kijeshi wa Urusi, ambao alikuwa amewakosoa mara kwa mara kwa mkakati wao nchini Ukraine, Prigozhin alikuwa amekua kimya.
Chini ya makubaliano ya kumaliza uasi, mashitaka dhidi yake yalitupiliwa mbali kwa makubaliano kwamba angehamia Belarus.
Alionekana kufanya hivyo, ingawa kwa ufupi, na kwa masharti yake mwenyewe.
Katikati ya mwezi wa Julai, video ambayo ilionekana kwenye chaneli za Telegraph ilionekana kuonyesha Prigozhin akiwakaribisha wapiganaji huko Belarus.
Lakini baadaye mwezi huo, alipigwa picha katika jiji la Urusi la St Petersburg wakati wa mkutano wa kilele wa Afrika na Urusi.
Katika wiki iliyopita, Prigozhin alitoa taarifa yake ya kwanza ya video tangu uasi wa Juni, ambayo ilimuonyesha kuwa alikuwa Afrika.
BBC haijaweza kuthibitisha ni wapi video hiyo ilirekodiwa.
Baada ya ripoti kuwa amefariki, shirika la usafiri wa anga la Urusi lilitoa kile lilichosema kuwa ni orodha iliyothibitishwa ya waliokuwemo kwenye ndege hiyo iliyoanguka katika eneo la Tver kaskazini mwa Moscow.
Jina la Prigozhin lilikuwa la kwanza kwenye orodha hiyo.
Nini kinachoendelea sasa?
Kwa mujibu wa kamati ya uchunguzi ya Urusi, uchunguzi wa jinai umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo chini ya kifungu cha 263 cha sheria ya makosa ya jinai ya Urusi, kuhusu usalama wa barabarani na usafiri wa anga.
Wakati huo huo, huduma za dharura zimemaliza msako wao katika eneo la ajali.
Gavana wa eneo la Tver, Igor Rudenya, ameripotiwa kuchukua udhibiti wa uchunguzi huo.















