Je, uungwaji mkono wa kimataifa kwa Israel unakufa?

Chanzo cha picha, Reuters
Israel ilianzisha vita huko Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, kujibu mashambulizi ya Hamas, na katika vita hivi, Israel ilitumia silaha ambazo nyingi zilitolewa na Marekani au zilinunuliwa kwa ufadhili wa Marekani.
Washirika wengine wa Israeli wa Magharibi pia waliipatia (Israeli) silaha nyingine zenye nguvu... Na silaha hii ilikuwa msaada kamili wa kimaadili na mshikamano wa Israeli katika vita hivi.
Uungwaji mkono huu kwa Israel kutoka kwa washirika wa Magharibi ulitolewa kama ishara ya kughadhabishwa na vifo vya watu 1,200, wengi wao wakiwa ni raia wa Israel, waliouawa wakati wa shambulio la Hamas.
Lakini sasa inaonekana kwamba uungwaji mkono huu wa kimaadili kwa Israel kutoka kwa washirika wake wa Magharibi umeisha, angalau kutoka kwa Ufaransa, Uingereza, na Canada. Nchi hizi tatu zimeshutumu vikali mbinu ambayo Israel inaendesha vita huko Gaza.
Nchi hizi tatu zimeitaka Israel kusitisha mara moja operesheni yake mpya ya kijeshi huko Gaza, ambayo Waziri Mkuu Netanyahu anadai itapelekea kuondolewa kwa Hamas, kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, na kurejea Gaza yote ili kuelekeza udhibiti wa kijeshi wa Israel.
Uingereza, Ufaransa na Canada zimeukataa mkakati mpya wa Netanyahu na zimetoa wito wazi wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza. Taarifa ya pamoja ya nchi hizo tatu inasema, "Tunapinga vikali upanuzi wa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza." Ukali wa msiba wa mwanadamu huko umekuwa hauvumiliki.

Chanzo cha picha, Reuters
Nchi hizi zilisisitiza matakwa yao ya kuachiliwa mara moja kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, zikikariri kwamba zimetambua haki ya Israel ya kujilinda baada ya "shambulio la kikatili" la Oktoba 7, "lakini kinachoendelea sasa hakina uwiano kabisa."
Ruhusa ya Netanyahu ya kupeleka kiasi "kidogo sana" cha chakula huko Gaza pia imeelezwa kuwa ya "kutoridhisha" na nchi hizo tatu.
Akijibu, Netanyahu alijibu kwa nukali akisema, "Viongozi wa London, Ottawa na Paris wanawatuza wale waliotekeleza shambulio la mauaji ya halaiki nchini Israel tarehe 7 Oktoba na kuandaa njia kwa ukatili zaidi wa aina hiyo."
Netanyahu alisisitiza kwamba vita vinaweza kumalizika ikiwa Hamas itawarudisha mateka, kujisalimisha, uongozi wake kukubali kwenda uhamishoni, na Gaza kuondolewa kijeshi. Netanyahu alisema, "Hakuna nchi inayoweza kutarajiwa kukubaliana na chochote isipokuwa hayo na kwa hakika si Israeli."
Ikumbukwe kuwa Netanyahu anatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai pia imetoa waranti dhidi yake.
Shinikizo la kimataifa linazidi kuongezeka kwa Netanyahu kukoma kuizingira Gaza, hususan baada ya uchunguzi wa shirika linaloheshimika la kimataifa kubaini hatari ya njaa kwa wakazi wa Gaza.
Katika mkutano wa pamoja wa Umoja wa Ulaya na Uingereza mjini London, Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa alielezea hali ya Gaza kama "janga ambapo sheria za kimataifa zinakiukwa kwa ukiukwaji wa wazi na idadi ya watu wote wanakabiliwa na nguvu za kijeshi."
Alisisitiza kuwa "upatikanaji wa haraka wa salama na usiozuiliwa wa utoaji wa usaidizi wa kibinadamu lazima uhakikishwe kwa gharama yoyote."
Uamuzi wa Netanyahu wa kusitasita kuruhusu usambazaji mdogo wa chakula kwa Gaza umelaaniwa na washirika wake wa muungano wenye msimamo mkali nchini Israel.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waziri wa Usalama Itmar Ben-Gweir, ambaye alipatikana na hatia mwaka 2007 kwa kuchochea ubaguzi wa rangi na kuunga mkono kundi la Kiyahudi lenye itikadi kali, alisema uamuzi wa Netanyahu "utawapa Hamas oksijeni wakati mateka wetu wakisalia kwenye mahandaki."
Ni malori matano pekee yaliyobeba chakula yaliingia Gaza siku ya Jumatatu, huku wanajeshi wa Israel wakisonga mbele katika operesheni mpya na mashambulizi ya anga na mizinga huko Gaza yaliwauwa raia zaidi wa Palestina, wakiwemo watoto wengi wadogo.
Watu binafsi na makundi yanayopinga vitendo vya Israel, kama vile kuharibu Gaza na kuwaua maelfu ya raia wa Palestina, watasema kuwa serikali za Ufaransa, Uingereza, na Canada zimechelewa sana kuzungumza dhidi ya Israel.
Wapinzani wa vita hivi kwa muda mrefu wamekuwa wakiandamana kupinga mauaji na uharibifu huko Gaza. Pia wameandamana kupinga mauaji ya kila siku ya raia wa Palestina, kukaliwa kwa mabavu kwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kunyang'anywa ardhi wakati wa operesheni za kijeshi na uvamizi unaofanywa na walowezi wa Kiyahudi wenye silaha na vikosi vya jeshi.
Lakini wakati mwingine katika siasa za vita, tukio huwa na nguvu ya mfano ambayo inaweza kuilazimisha serikali kuchukua hatua au kujibu. Na wakati huu tukio lilikuwa la mauaji ya wahudumu 15 na wafanyakazi wa misaada na vikosi vya Israeli huko Gaza mnamo Machi 23.
Haya yanajiri baada ya Israel kuvunja mkataba wa miezi miwili wa kusitisha mapigano na mashambulizi makubwa ya anga mnamo Machi 18.
Siku ya tano baada ya kumalizika kwa usitishaji mapigano, kikosi cha kijeshi cha Israel kilishambulia msafara wa wafanyakazi wa matibabu na wafanyakazi wa misaada, na kuzika magari ya waliouawa kwenye shambulio hilo chini ya mchanga.
Israel ilitoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, lakini ilithibitishwa kuwa si kweli pale simu ya rununu ilipotolewa kutoka kwa maiti kwenye kaburi la pamoja la watu hao waliozikwa chini ya mchanga.

Mmiliki wa rununu hii alirekodi tukio zima kabla ya mauaji yake. Na kinyume na madai na taarifa za Israel, picha za simu za mkononi zilizopatikana kaburini zilithibitisha kuwa magari na ambulansi kwenye msafara huo sio tu zilikuwa na vimulimuli vya magari ya wagonjwa, lakini pia zilikuwa na alama zote za magari ya dharura. Kikosi cha Israel kilishambulia msafara huo kwa utaratibu na kuua karibu kila mtu katika magari yote ya msafara huo.
Kengele za tahadhari zimekuwa zikilia kwa kasi tangu tukio hilo kujulikana. Sio tu wapinzani wa jadi wa Israel bali pia washirika wake wa Ulaya sasa wanatia ukali kwenye kauli zao. Kauli iliyotolewa na nchi hizo tatu za kutaka kusitishwa uvamizi wa Israel ni ukosoaji mkubwa wa Israel kuwahi kutolewa tangu kuanza kwa vita vya Gaza.
Mwanadiplomasia mkuu wa Ulaya anayefahamu jambo hilo aliniambia kwamba lugha kali inayotumiwa na nchi hizo tatu inaonyesha "hisia halisi ya kuongezeka kwa hasira ya kimataifa katika janga la kibinadamu" huko Gaza, na pia inaonyesha ukandamizaji usio na huruma wa serikali ya Israeli.
Kinachosikitisha zaidi kwa Israel katika kauli hii ya pamoja ni kwamba inasema, "Hatutasimama (na Israel) maadamu serikali ya Netanyahu inaendelea na vitendo hivi viovu." "Ikiwa Israel haitasitisha hatua zaidi za kijeshi na kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, tutachukua hatua zaidi madhubuti kujibu."
Taarifa hiyo haikubainisha hatua hizi madhubuti zitakuwa zipi. Kuiweka vikwazo Israel kunaweza kuwa hatua moja, na hatua kubwa zaidi inaweza kuwa kuitambua Palestina kama taifa huru.
Ufaransa inafikiria kujiunga na umoja wa mataifa mengine 148 ambayo yamefanya hivyo kwenye mkutano uliofanyika New York mapema mwezi Juni. Uingereza pia imefanya mazungumzo na Ufaransa kuhusu kuwatambua Wapalestina.
Israel ilijibu kwa ukali, na kuziambia nchi hizi kwamba kauli yao ilikuwa kielelezo cha ushindi wa Hamas. Lakini sauti iliyopitishwa katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Ufaransa, Canada, na Uingereza inaonyesha kuwa Israel inapoteza uwezo wake wa kutoa shinikizo kwa nchi hizi.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












