Mpango wa kuikalia Gaza unahatarisha kuigawa Israel, kuua Wapalestina na kuushitua ulimwengu

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewaambia Waisraeli kuwa "tuko katika hatua za mwisho za kuingia Gaza kwa nguvu." Amesema, "Israel italikamata eneo hilo lote na kulishikilia." Akiwa na maana hawataingia na kutoka.
Mashambulizi mapya yanaandaliwa, kulingana na msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) Brigedia Jenerali Effie Defrin, ili kuwarudisha mateka waliosalia. Ameiambia redio ya Israel, baada ya hapo, "ni kuukongoa utawala wa Hamas moja kwa moja."
Mashambulizi hayo hayataanza baada ya safari ya ya rais wa Marekani Donald Trump nchini Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar wiki ijayo.
Vita vya Gaza vilivyoanza baada ya mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba 2023, vimepelekea mzozo kati ya Wapalestina na Waisraeli kufikia kiwango cha hatari kuliko wakati wowote katika historia ya mzozo huo. Kuendelea kwa vita hivyo, kunawagawa Waisraeli, kunaua raia wengi zaidi wa Palestina na kuwatia hofu mamilioni ya watu duniani, wakiwemo wanaojiita marafiki wa Israel.
Wakati IDF inaishambulia Hamas huko Gaza, mpango wa serikali ni kwamba wanajeshi wake watawalazimisha baadhi au raia wote milioni mbili wa Palestina huko Gaza kwenda katika eneo dogo lenye magofu upande wa kusini. Misaada ya kibinadamu itapelekwa, labda na makampuni binafsi ya usalama ya Marekani. Kwani mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamesema hayatatoa ushirikiano, yakilaani mpango huo kuwa ni ukiukaji wa kanuni za misaada ya kibinadamu.
Pia mashirika hayo yameonya juu ya baa la njaa huko Gaza kutokana na uamuzi wa Israel wa kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia kwa zaidi ya miezi miwili. Uzuiaji huo wa misaada, ambao bado unaoendelea, umelaaniwa pakubwa, sio tu na Umoja wa Mataifa na pia nchi za Kiarabu.
Ni uhalifu wa kivita?

Chanzo cha picha, EPA
Uingereza na Umoja wa Ulaya wote wanasema wanapinga mashambulizi mapya ya Israel. Wiki mbili zilizopita, Mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, washirika wa Israel ambao wanaichukulia Hamas kama kundi la kigaidi, walionya kwamba kuzuia misaada kinawaweka raia wa Palestina, wakiwemo watoto milioni moja, katika "hatari kubwa ya njaa, magonjwa ya mlipuko na vifo."
Mawaziri hao pia walionya, bila kuficha, kwamba mshirika wao (Israel) anakiuka sheria za kimataifa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Misaada ya kibinadamu kamwe isitumike kisiasa na wakaazi wa eneo la Palestina wasiondoshwe", walisisitiza. "Israel inalazimika chini ya sheria ya kimataifa kuruhusu misaada ya kibinadamu bila vikwazo."
Israel inakanusha kuwa inakiuka sheria za kimataifa na sheria za vita huko Gaza. Lakini maneno ya mawaziri wa Israel, yanaleta utata. Moja ya mifano mingi: Waziri wa Ulinzi, Israel Katz ameelezea kuzuia misaada kama "shinikizo" dhidi ya Hamas." Anaonekana kukiri kwamba zuio hilo ni silaha. Wakati raia wakikumbwa na njaa, hilo linakuwa sawa na uhalifu wa kivita.
Nchi na mashirika ambayo yanaamini Israel inakiuka kimakusudi sheria, kwa kufanya msururu wa uhalifu wa kivita, yatachunguza mashambulizi yoyote mapya ili kupata ushahidi zaidi. Lugha kali zinazotumiwa na Mawaziri wa Israel zitanukuliwa na wanasheria wa Afrika Kusini waliopeleka kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki juu ya madai ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Na watu wenye uzalendo wa hali ya juu ambao wanaiunga mkono serikali ya Netanyahu – wanaouona mpango mpya wa uvamizi kama hatua nyingine ya kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza na kuwaweka walowezi wa Kiyahudi.
Mmoja wa watu wenye msimamo mkali ni Bezalel Smotrich, Waziri wa fedha ambaye alisema katika kipindi cha miezi sita Gaza "itaangamizwa kabisa." Wapalestina katika eneo hilo "watakata tamaa, wakielewa kwamba hakuna matumaini na hakuna kitu kilichobaki huko Gaza, na watatafuta kuhama ili kuanza maisha mapya katika maeneo mengine."
"Kuhama," neno lililotumiwa na Smotrich, ni wazo lililojadiliwa tangu siku za mwanzo kabisa za Uzayuni, yaani kuwalazimisha Waarabu kuondoka katika ardhi kati ya Mto Jordan na Bahari ya Mediterani
Ndani ya Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Wakosoaji wa Netanyahu nchini Israel, wanasema kurefusha vita kwa mashambulizi mapya badala ya kumaliza vita hivyo, kwa kusitisha mapigano ni kwa lengo la yeye mwenyewe kusalimika kisiasa, haihusiani na usalama wa Israel au kurejea kwa mateka.
Siku chache baada ya shambulio la Oktoba 7 kulikuwa na safu za magari yaliyoegeshwa nje ya kambi za kijeshi, Waisraeli wakijiandikisha kujitolea kupigana na Hamas.
Sasa maelfu (baadhi wakisema ni zaidi) wanakataa kujitolea kurudi katika vita kama wanajeshi wa akiba. Wanasema Waziri Mkuu anaendeleza vita kwa sababu asipoendeleza, wanasiasa wa misimamo mikali katika serikali yake wataiangusha serikali na makosa aliyofanya Netanyahu ambayo yaliipa Hamas fursa ya kushambulia yatahesabiwa.
Ndani ya Israel, ukosoaji mkali zaidi wa mashambulizi yaliyopangwa umetoka kwa familia za mateka wanaohofia kuwa wametelekezwa na serikali inayodai inataka kuwaokoa.
Hamas bado ina mateka 24 hai katika Ukanda wa Gaza, kulingana na Israel, na inashikilia miili 35 ambao wamekufa kati ya 251 iliyowachukua tarehe 7 Oktoba. Serikali ya Netanyahu imedai mara kwa mara kwamba shinikizo kubwa la kijeshi litaweza kuwarudisha mateka nyumbani na kurejesha miili ya waliofariki kwa familia zao.
Lakini katika uhalisia, idadi kubwa ya mateka wameachiliwa wakati wa kusitisha mapigano. Makubaliano ya mwisho ya kusitisha mapigano, ambayo Trump aliisisitiza Israel kutia saini katika siku za mwisho za utawala wa Biden – yalivunjika katika awamu ya pili ambayo ilipaswa iwe ya kuwaachilia mateka wote na jeshi lote la Israel kujiondoa Gaza.
Washirika wa Netanyahu wenye itikadi kali walimwambia wataiangusha serikali yake ikiwa atakubali awamu ya pili ya usitishaji mapigano.
Baada ya hapo, Israel ilizuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza ili kuweka shinikizo kwa Hamas, ilisema, Hamas inapaswa kukubaliana na mpango ambao utaipa Israeli fursa ya kurejea vitani hata baada ya mateka kuachiliwa. Hamas ilipokataa, Israel iliendelea na mashambulizi tena makubwa ya anga usiku wa tarehe 18 Machi.
Mashambulizi mapya yatauwa raia wengi zaidi wa Palestina, kuzidisha huzuni kwa walionusurika na kufiwa ndani ya Gaza na kupanua mpasuko ndani ya Israel. Bila ya pango wa kusitisha mapigano, haiwezekani kuilazimisha Hamas kuwaachilia mateka waliosalia.

Chanzo cha picha, Reuters
Mauaji yanayotekelezwa na Israel ndani ya Gaza yamekuwa chanzo cha Hamas na makundi mengine yenye silaha kuajiri wapiganaji wapya, hayo ni kwa mujibu wa utawala wa Rais Joe Biden kabla ya kuondoka madarakani Januari mwaka huu.
Waziri wa mambo ya nje wa Biden, Antony Blinken, katika hotuba yake mjini Washington tarehe 14 Januari, alisema "tathmini yetu ni kwamba Hamas imeajiri wapiganaji wengi wapya kama wale iliowapoteza. Hicho ni kichocheo cha uasi wa kudumu na vita vya kudumu."
Alipozungumza hayo, ulikuwa ni wakati ambao Israel ilidai imewaua wapiganaji wapatao 18,000 wa Kipalestina ndani ya Gaza. Kwa sasa wengi zaidi wameuawa, lakini raia wengi zaidi wameuwawa.
Mashambulizi makubwa ya Israel yaliivunja Hamas kama kundi lililopangwa la kijeshi zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Sasa Israel inakabiliwa na uasi, ambao historia inaonyesha unaweza kuendelea kwa muda mrefu, ikiwa wapiganaji hao wako tayari kupigana na kufa ili kumpiga adui yao.















