Kwa nini Israel imeishambulia Gaza na kipi kifuatacho?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Emir Nader
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ndege za kivita za Israel zilifyatua mabomu katika Ukanda wa Gaza usiku kucha na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400, na hivyo kuvunja mapatano tete ambayo yalianza kutekelezwa tangu mwezi Januari.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, amelitupia lawama kundi la Hamas kwa Israel kuanzisha upya mashambulizi yake mabaya ya anga.
Taarifa ya kiongozi huyo wa Israel ilisema wanajeshi wameagizwa kuchukua "hatua kali" dhidi ya Hamas kufuatia "kukataa kwao kuwaachilia huru mateka wetu" pamoja na kukataa mapendekezo ya Marekani.
Katika vyombo vya habari vya ndani, jeshi la Israeli linasema kumekuwa na ongezeko la shughuli za Hamas za kupanga tena vikosi vyao katika siku za hivi karibuni.
Maafisa wa Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza wamesema zaidi ya watu 140 wameuawa na Israel kabla ya mashambulizi ya jana, katika kipindi cha miezi miwili tangu kuanza kutekelezwa usitishaji wa vita mwezi Januari.
Katika wiki za hivi karibuni, jeshi la Israel limesema limeshambulia maeneo wanayo yataja kuwa ya wapiganaji wa Hamas wanaotoa tishio kwa wanajeshi wake walioko Gaza.
Lakini sababu za uamuzi wa Netanyahu wa kurejea kuishambulia Gaza zina utata.
Jukwaa la Familia za Mateka na Waliotoweka limeishutumu serikali hiyo kwa kujiondoa kwenye makubaliano "ambayo yangeweza kumleta kila mateka nyumbani."
Baadhi ya wakosoaji wakubwa wa Waziri Mkuu wanasema, mashambulizi hayo ni jaribio la Netanyahu kufifisha miito ya kisheria na kisiasa anayokabiliana nayo nyumbani.
Makubaliano ya kusitisha mapigano
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makubaliano ya Januari 19 ya kusitisha mapigano yalipangwa kwa miezi mingi, na upatanishi wa Marekani, Qatar na Misri. Ulikuwa ni mpango wa awamu tatu wa makubaliano hayo.
Awamu ya kwanza ni Hamas kuwaachilia mateka 33 na Israel kuwaachilia wafungwa wapatao 1,900 wa Kipalestina na kuruhusu misaada na bidhaa nyingine kuingia Ukanda wa Gaza.
Huku mapigano yakinyamaza na maelfu ya wananchi wa Gaza waliokimbia makazi yao wakirejea nyumbani. Kisha Hamas na Israel zilipaswa kuanza mazungumzo ya kuanza awamu ya pili.
Awali pande hizo zilikubaliana kwamba mazungumzo ya awamu ya pili yatajumuisha kuachiliwa huru mateka wote waliosalia pamoja na kuondoka kwa wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, na hivyo kupelekea kumalizika kwa vita hivyo.
Awamu ya kwanza ilikamilika tarehe 1 Machi, lakini mazungumzo ya awamu ya pili hayakuwa na maendeleo.
Badala yake, Israel ilisimamisha kabisa misaada yote inayoingia Gaza na kusababisha hofu kubwa ya kimataifa - na kusema inaunga mkono pendekezo jipya la Marekani.
Wajumbe wa Israel wakiwa Qatar wiki iliyopita, na wale wa Hamas, walikutana ili kujadili usitishaji vita utakavyoendelea na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff alitoa "pendekezo lake jipya la kuongeza muda wa awamu ya kwanza ambayo muda wake ulikuwa umeisha."
Mpango huo ulitaka, mateka zaidi warudi nyumbani na kuachiliwa huru wafungwa zaidi wa Kipalestina - lakini mazungumzo ya kumaliza vita moja kwa moja yatakuja baadaye.
Hapa ndio kuna sababu kuu ya kwa nini makubaliano ya amani yamevunjika.
Kiini cha mvutano

Chanzo cha picha, Reuters
Malengo makubwa mawili ya Israel - ni kuwarudisha mateka nyumbani na kuwashinda Hamas - yote mawili hayawezi kufikiwa kwa pamoja kikamilifu.
Hamas ina kadi moja ya kucheza katika mazungumzo; mateka. Hawataki kuwaachilia mateka wote, isipokuwa ihusishe wanajeshi wa Israel kuondoka katika Ukanda wa Gaza, kama ilivyokubaliwa katika mapatano ya awali na Hamas kuendelea kusalia katika Ukanda huo kwa namna fulani.
Israel inapinga hilo. Pendekezo jipya la Marekani ni jaribio la kuwarejesha mateka wote nyumbani, huku Israel ikichelewesha kumaliza vita na kuendelea na mashambulizi ya kuimaliza Hamas.
Katika siku za hivi karibuni, Marekani na Israel imetupilia mbali takwa la Hamas la kutaka kuendelea na makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano – na sio kujadiliana masharti mapya na kuongeza muda wa usitishaji mapigano wa awamu ya kwanza.
Witkoff alishutumu Hamas kwa "kujifanya iko tayari hadharani lakini katika vikao vya ndani, wanatoa matakwa ambayo hayatekelezeki bila usitishaji wa kudumu wa mapigano."
Mwishoni mwa mwezi Februari, maafisa wa Israel walitoa taarifa kwa vyombo vya habari vya ndani kwamba jeshi lake halitaondoka kwenye maeneo muhimu huko Gaza, na hilo linakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Ingawa hatuwezi kujua undani wa mazungumzo yaliyofanyika - tunachojua ni kwamba Israel ilisitisha msaada kuingia Gaza siku 17 zilizopita katika jaribio la kuilazimisha Hamas kukubali makubaliano mapya.
Hilo halijafanya kazi hadi sasa na sasa inaonekana Israel imerejea kwenye mashambulizi ili kujaribu kupata mkataba mpya, ambao unawafaa zaidi viongozi wake wa kisiasa wa Israel, na unaotoa ushindi mdogo kwa Hamas.
Kutoka sasa....
Kuanzia sasa, hali ya Gaza huenda ikaonekana tofauti na miezi miwili iliyopita ya usitishaji wa mapigano.
Asubuhi ya jana jeshi la Israel limechapisha ramani, na kuwaamuru Wapalestina kuondoka katika eneo la Ukanda wa Gaza, ambako maelfu ya wananchi wa Gaza walikuwa wamerejea.
Hamas, kwa upande wake, imetoa wito wa kusitishwa kwa operesheni ya kijeshi ya Israel, lakini bado haijasema ikiwa itarejea katika mapigano.
Mwandishi wa BBC, aliyepo karibu na mpaka wa Israel na Gaza aliambiwa na mwanajeshi, wito umetolewa kwa askari wa akiba 40,000 wa jeshi la Israel kurejea kazini.
Hilo linaonekana kuthibitisha ripoti za vyombo vya habari vya Israel kwamba jeshi linajiandaa kwa mashambulizi mapya ya ardhini katika Ukanda wa Gaza.
Kuendeleza mashambulizi mapya huko Gaza pia kunatoa neema ya kisiasa kwa Waziri Mkuu Netanyahu. Asubuhi ya jana, chama cha mrengo wa kulia cha Jewish Power kimetangaza kitarejea katika muungano wa serikali, wanachama wake akiwemo, Waziri wa zamani Itamar Ben Gvir, walijiuzulu wakipinga kusitishwa kwa mapigano. Ushirikiano huo utakuwa muhimu kwa serikali wakati huu inapojaribu kupitisha bajeti yake.
Operesheni za Israel za jana usiku zinaweza kuwa ni jaribio la kuilazimisha Hamas kukubali mpango wa Israel na Marekani. Au, inaweza kuwa ndio mwanzo wa wimbi jipya la mapigano, na hilo linazitia hofu familia zilizochoka za Gaza na familia za mateka za Israel.















