Idadi ya waliouawa kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza yafikia zaidi ya 400, yasema wizara ya afya ya Hamas

Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imetoa taarifa kuhusu idadi ya waliouawa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Abdalla Dzungu & Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid

  1. tumefika mwisho wa taarifa zetu kwa leo, asante kwa kuwa nasi !

  2. Waisraeli waandamana mjini Jerusalem

    Noga

    Familia za mateka zimekuwa zikikutana na wanasiasa wa Israel katika bunge la Jerusalem, huku umati mkubwa ukiandamana nje.

    Lishi Lavie-Miran, mke wa Omri Miran ambaye alichukuliwa mateka kutoka Kibbutz Nahal Oz tarehe 7 Oktoba, kwa hasira aliwaambia wajumbe wa Knesset kwamba ikiwa mume wake atauawa "hatawajibika kwa matendo yake" ikiwa mmoja wao "atathubutu kumkaribia".

    Nje, Samuel, askari wa jeshi la akiba na mwalimu wa historia, ni miongoni mwa wanaopiga kelele kutaka mateka warudishwe mara moja.

    Anasema anataka kuwa mfano kwa wanafunzi wake. "Wana umri wa miaka 18, watakuwa wanatumikia jeshi katika miezi ijayo na ninaamini hawapaswi kutumikia katika aina hii ya vita," anasema.

    Anaongeza kuwa anaona vita hivi ni vya kisiasa: "Haihusu usalama wa Israel, Benjamin Netanyahu ana sababu zake mwenyewe za vita hivi, na ni fisadi. Tunahitaji kusimamisha vita na kuwarudisha mateka."

    Noga Kaplan, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 katika Chuo Kikuu cha Hebrew, ameshikilia mabango yanayosema "Bibi lazima aende". Anasema kuwa kuanzisha upya vita ni "jambo baya zaidi ambalo linaweza kutokea kwa mateka" na anatoa wito kwa serikali, Hamas, na Marekani kuendeleza makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka.

    Unaweza kusoma;

  3. Iran, Misri, Umoja wa Ulaya na nyinginezo zinasemaje kuhusu mashambulizi ya Israel?

    Wapalestina mjini Beit Lahia, kaskazini mwa Gaza, mapema leo

    Chanzo cha picha, Reuters

    Tunaweza kukuletea hisia zaidi kutoka duniani kote kuhusu mashambulizi ya Israel huko Gaza.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei anasema Marekani ina "ni ya kuwajibika moja kwa moja" kwa "kuendeleza mauaji ya halaiki katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu".

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri Tamim Khallaf anasema mashambulizi ya anga ya Israel yanajumuisha "ukiukaji wa wazi" wa makubaliano ya kusitisha mapigano na yanawakilisha "ongezeko la hatari".

    Jordan imekuwa ikifuatilia "mashambulizi ya kikatili na ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza" tangu jana usiku, shirika la habari la AFP linaripoti, likimnukuu msemaji wa serikali, Mohammed Momani, ambaye anasisitiza "haja ya kukomesha uchokozi huu".

    Saudi Arabia ililaani mashambulizi ya Israel "maeneo yanayokaliwa na raia wasio na ulinzi", bila "kuzingatia hata kidogo sheria za kimataifa za kibinadamu".

    Kamishna wa misaada wa Umoja wa Ulaya, Hadja Lahbib, anatoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia zilizozushwa upya na kurejeshwa kwa usitishaji mapigano, akisema raia wa Gaza "wamevumilia mateso yasiyofikirika".

    Unaweza kusoma;

  4. Takribani watu 12 wapoteza maisha katika ajali ya ndege ya Honduras

    Ajali ya ndege

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani watu 12 wameuawa baada ya ndege kuanguka pwani ya Caribbean ya Honduras Jumatatu jioni, maafisa walisema.

    Ndege hiyo , inayorushwa na shirika la ndege la Lanhsa, ilianguka baharini ndani ya dakika moja baada ya kupaa kutoka kisiwa cha Roatán.

    Polisi wa kitaifa wa Honduras na idara ya zima moto walisema watu watano wameokolewa, huku mtu mmoja bado hajapatikana.

    Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, lakini meya wa Roatán aliviambia vyombo vya habari kuwa haikuwa kwa sababu ya hali ya hewa, kwani ilikuwa ya kawaida.

    Shirika la Aeronautics la Honduras limesema uchunguzi unaendelea.

    Ndege ya Jetstream 32 ilikuwa imepaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juan Manuel Gálvez katika kisiwa hicho saa 18:18 saa za ndani (00:18 GMT siku ya Jumanne), na ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Golosón huko La Ceiba. Afisa wa shirika la ndege la kiraia Carlos Padilla alisema, akinukuliwa na shirika la habari la AFP, kwamba ndege hiyo "ilipinda upande wa kulia wa njia ya kurukia na kuanguka majini".

    Katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii, serikali ilionesha "mshikamano" na familia za waathiriwa. "Serikali ya Honduras inasikitika sana kwa ajali mbaya ya Roatán na inajiunga na maombolezo ya kitaifa," iliongeza.

    Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Honduras Xiomara Castro "aliunda mara moja" kamati ya dharura ya nchi hiyo, inayojumuisha huduma zote za dharura ikiwa ni pamoja na jeshi, polisi, zima moto, Msalaba Mwekundu na Wizara ya Afya.

  5. Idadi ya waliouawa kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza yafikia zaidi ya 400, yasema wizara ya afya ya Hamas

    Majengo yaliyoharibika

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Israel linasema kuwa linafanya "mashambulizi makubwa" katika Ukanda wa Gaza, huku wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas ikiripoti kuwa zaidi ya Wapalestina 400 wameuawa.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema linashambulia kile lilichokiita "maeneo ya ugaidi" ya Hamas.

    Mashambulizi yanaendelea na IDF hivi karibuni ilitoa maagizo mapya ya kuhama kwa maeneo mengi.

    Mahmoud Abu Wafah, naibu waziri wa mambo ya ndani huko Gaza na afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Hamas katika eneo hilo ni miongoni mwa waliofariki.

    Hili ni wimbi kubwa zaidi la mashambulizi ya anga huko Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza tarehe 19 Januari.

    Mazungumzo ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano Gaza yameshindwa kufikia makubaliano.

    Unaweza kusoma;

  6. Hali ya wasiwasi nchini Ukraine kabla ya mazungumzo ya Trump na Putin

    Raia wa Ukraine walihamishwa kwa treni kutoka maeneo ya karibu na mstari wa mbele siku ya Jumatatu

    Chanzo cha picha, EPA

    Kuna hisia ya matarajio iliyochanganyika na woga nchini Ukraine kabla ya simu ya Trump na Putin.

    Rais Volodymyr Zelensky amesema mara kwa mara kwamba mustakabali wa Ukraine usijadiliwe bila Ukraine, na kwamba Kyiv haitakubali kunyakuliwa kwa eneo lake lolote na Urusi.

    Na bado hivi ndivyo marais wa Marekani na Urusi wana uwezekano wa kujadili, kwani Donald Trump anasema mgawanyo wa "mali" utakuwa mezani.

    Sababu nyingine ya wasiwasi kwa Ukraine ni uhusiano unaoendelea kati ya Urusi na Marekani kuhusu masuala kama vile eneo la Kursk la Urusi, ambalo Ukraine imekuwa ikimiliki sehemu zake tangu Agosti mwaka jana.

    Wote wawili wanasema idadi kubwa ya wanajeshi wa Ukraine wamezingirwa huko, lakini Kyiv inakanusha kuzingirwa.

    Unaweza kusoma;

  7. Zaidi ya wafanyakazi 2,000 wako katika siutafahamu baada ya kufungwa kwa kambi za kijeshi za kigeni barani Afrika

    Ndege

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kufungwa kwa kambi za kijeshi za kigeni barani Afrika kunawaacha takribani wafanyakazi 2,000 wa ndani bila ajira, baada ya miongo kadhaa ya kazi katika maeneo haya.

    Leo hii, wanaogopa siku zijazo wanapojitahidi kupata ajira mpya.

    Kambi za kijeshi za Ufaransa zimefungwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, Burkina Faso, Niger, Chad, Senegal na Ivory Coast; nchi ambazo zilidai kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa.

    Lakini nchi nyingine za Magharibi pia zimefunga kambi za kijeshi, ikiwa ni pamoja na kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Niger na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Utulivu nchini Mali (MINUSMA).

    BBC iligundua kuwa wafanyakazi wapatao 859 waliathirika nchini Mali, 400 nchini Chad na 350 nchini Niger.

    Nchini Senegal na Ivory Coast, wafanyakazi 162 na 280 mtawalia wameathirika. Idadi ya wafanyakazi walioathiriwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Burkina Faso haikuwekwa wazi.

  8. Watu 330 wauawa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza

    s

    Takriban watu 330 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yaliyotekelezwa usiku kucha, kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    Jeshi la Israel limesema kuwa lilikuwa likifanya mashambulizi makubwa baada ya mazungumzo ya kuongeza muda wa kusitisha mapigano kushindwa kufikia makubaliano.

    Ni wimbi kubwa zaidi la mashambulizi ya anga tangu Januari 19, wakati zoezi la usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa, anaripoti mwandishi wa BBC Gaza kutoka Cairo.

    "Walifyatua moto wa kuzimu tena Gaza," mmoja wa mashuhuda katika Jiji la Gaza anasema.

    Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu inasema Israel "kuanzia sasa itachukua hatua dhidi ya Hamas kwa kuongeza nguvu zaidi za kijeshi", ikishutumu Hamas kwa "kukataa mara kwa mara kuwaachilia mateka wetu", na kukataa mapendekezo ya kurefusha muda wa usitishaji mapigano.

    Hamas inaishutumu Israel kwa kushambulia "raia wasio na silahai", na inasema wapatanishi wanapaswa kuiwajibisha Israel "kuwajibika kikamilifu" kwa "kukiuka" usitishaji mapigano.

  9. Mzozo wa DR Congo: EU yawawekea vikwazo baadhi ya waasi wa M23 na maafisa wa jeshi la Rwanda,

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Umoja wa Ulaya umewawekea vikwazo watu tisa, wakiwemo wanajeshi wa M23 na askari waRwanda, pamoja na wale ambao umoja huo unasema wana mchango mkubwa katika vita vinavyoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Hayo yamejiri wakati serikali ya Rwanda ikitangaza kukata uhusiano wake kamili na nchi ya Ubegiji ikiishtumu kwa kuchochea vikwazo hivyo.

    Kulingana na tangazo la Umoja wa Ulaya EU, vikwazo hivyo vimewalenga: Meja Jenerali Ruki Karusisi maarufu ‘’Rocky’’aliyekuwa kamanda wa kikosi maalum lakini aliyeondolewa katika wadhifa huo wiki iliyopita na kurudishwa makao makuu ya jeshi.

    Pia maafisa wengine wawili wa jeshi meja jenerali Eugène Nkubito, na Brigedia Jenerali Pascal Muhizi.

    Umoja huo unasema wawili hao waliongoza majeshi ya Rwanda kusaidia waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Upande wa waasi wa M23,waliolengwa hasa na vikwazo vya umoja wa ulaya ni kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo Bertrand Bisimwa, Kanali John Nzenze msimamizi wa idara ya ujasusi na Kanali Joseph Bahati Musanga, anayejulikana kama Kanali Bahati Erasto, aliyeteuliwa hivi karibuni na waasi hao kuongoza jimbo la Kivu Kaskazini.

    Yeye pia ni mshauri wa Général Sultan Makenga ambaye anaongoza jeshi la M23.

    Miongoni mwa wengine waliowekewa vikwazo ni raia wa Kongo wanaohudumu chini ya waasi wa M23 na wengine kutoka Rwanda akiwemo Bwana Francis Kamanzi, mkuu wa Bodi ya Migodi, Petroli na Gesi ya Rwanda.

    Kampuni moja pia iliwekewa vikwazo

    Kampuni ya Gisabo Gold Refinery ya mjini Kigali ,inayochimba na kusafisha dhahabu ni kampuni ya uchimbaji dhahabu yenye makao yake makuu mjini Kigali.

    Umoja wa Ulaya unasema kampuni hiyo inajihusisha na biashara haramu ya madini hususan dhahabu.

    Mali za wahusika zinazopatikana katika mataifa ya sehemu ya umoja huo zitakamatwa na pia kuwapiga marufuku kusafiri barani humo.

    Tangazo hilo limekuja kufuatia Rwanda kutangaza kukata mahusiano yake na Nchi ya Ubelgiji na kuwatimua wanadiplomasia wa nchi hiyo waliokuwa mjini Kigali.

    Kwa kujibu, Ubelgiji pia imechukua hatua kama hiyo.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Rwanda imetuma wanajeshi 4,000 nchini Kongo.

    Serikali ya Rwanda inakanusha kuhusika na vita hivyo, ikisema tu kwamba inachukua hatua za kulinda nchi kutokana na athari za vita.

  10. Trump aionya Iran itakabiliwa na athari 'mbaya' iwapo mashambulizi ya Houthi hayatasitishwa

    Maelezo ya video, Video: Marekani yatekeleza mahambulizi dhidi ya waasi wa Houthi Yemen

    Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran kwamba itakabiliwa na madhara "mabaya" iwapo Wahouthi wa Yemen wataendelea kushambulia njia za meli za kimataifa.

    Alisema uongozi wa Iran utawajibika kwa "kila risasi iliyofyatuliwa na Wahouthi", ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiungwa mkono na Tehran. Kundi hilo baadaye lilisema kuwa lililenga shehena ya ndege ya Marekani mara tatu katika siku mbili zilizopita.

    Waasi wa Houthi walijaribu kwa mara ya kwanza kushambulia meli ya USS Harry S Truman katika Bahari Nyekundu siku ya Jumapili kufuatia mashambulizi mabaya ya Marekani dhidi ya Yemen.

    Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imesema imetekeleza mashambulizi 30 nchini Yemen tangu Jumamosi, katika operesheni kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati tangu Trump arejee Ikulu ya White House.

    Trump alichapisha kwenye jukwaa lake la Ukweli wa Kijamii siku ya Jumatatu: "Kila risasi iliyofyatuliwa na Wahouthi itaangaliwa kuanzia sasa, kama risasi iliyofyatuliwa kutoka kwa silaha ya uongozi wa IRAN. "Na IRAN itawajibika, na itakabiliwa na matokeo, na matokeo hayo yatakuwa mabaya!"

  11. Wanaanga waliokwama kurejea duniani baada ya miezi tisa angani

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Wanaanga wa NASA Suni Williams na Butch Wilmore waliendelea na kile kilichokusudiwa kuwa safari ya siku nane kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga ndani ya Boeing Starliner mnamo 5 Juni 2024.

    Ilikuwa safari ya kwanza ya aina yake ikiwa na ilikuwa jaribio kuona jinsi chombo kipya kitakavyofanya kazi.

    Hata hivyo, masuala ya kiufundi ikiwa ni pamoja na uvujaji wa heliamu na hitilafu za mawasiliano ilimaanisha kuwa Starliner haikuwa salama na chombo hicho kilirudishwa duniani bila wao.

    Mnamo Agosti, baada ya zaidi ya miezi miwili angani, uamuzi ulifanywa kwa wawili hao kurejeshwa Duniani mnamo Machi kwa chombo cha SpaceX.

    Wakati huo huo, Williams na Wilmore wameendelea na kazi yao ndani ya ISS wakifanya utafiti, wakiendelea na safari za anga za juu na kupiga simu shuleni kwa video ili kuelimisha watoto kuhusu maisha angani.

  12. WHO yaonya watu milioni 10 kuambukizwa HIV duniani na vifo milioni 3 kutokana na ukosefu wa dawa

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa dunia inaweza kushuhudia maambukizi mapya ya HIV zaidi ya milioni 10 na vifo vya watu milioni 3 vinavyohusiana na ugonjwa huo, kufuatia kusitishwa kwa msaada wa kigeni wa Marekani unaosaidia upatikanaji wa dawa za HIV.

    Kwa mujibu wa WHO, hatua hiyo imeathiri usambazaji wa dawa katika nchi saba za Afrika, zikiwemo Kenya, Lesotho, Sudan Kusini, Burkina Faso, Mali, Nigeria, na Haiti, ambazo zinaweza kuishiwa dawa ndani ya miezi michache ijayo.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kusitishwa kwa msaada huo kunaweza kufuta mafanikio ya miaka 20 katika kupambana na HIV.

    Pia ameonya kuwa juhudi za kudhibiti magonjwa mengine kama polio, malaria, na kifua kikuu zimeathirika vibaya.

    Ghebreyesus ameihimiza Marekani kuhakikisha kuwa inatoa muda wa mpito kwa nchi zilizoathirika ili ziweze kupata vyanzo mbadala vya fedha badala ya kusitisha msaada kwa ghafla, hatua ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya duniani.

    Marekani kupitia kwa Rais wake Donald Trump ilitangaza mwezi huu kusitisha kutoa fedha za misaada kupitia miradi iliyokuwa chini ya Shirika lake la misaada la USAID, hali iliyoibua taharuki hasa kwa nchi nyingi za Afrika zinazotegemea fedha za ufadhili kushughulika na magonjwa kama Ukimwi.

  13. Israel yatekeleza 'mashambulizi makali' kwenye Ukanda wa Gaza huku 330 wakiripotiwa kufariki

    .

    Jeshi la Israel linasema kuwa linafanya "mashambulio makubwa" katika Ukanda wa Gaza, huku wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas ikiripoti kuwa takriban Wapalestina 330 wameuawa.

    Jeshi la Israel (IDF) limesema linalenga kile ilichokiita "Shabaha ya ugaidi" ya Hamas.

    Mahmoud Abu Wafah, naibu waziri wa mambo ya ndani huko Gaza na afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Hamas katika eneo hilo, ameripotiwa kuuawa katika mgomo.

    Hili ni wimbi kubwa zaidi la mashambulizi ya anga huko Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza tarehe 19 Januari.

    Mazungumzo ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano Gaza yameshindwa kufikia makubaliano.

    Nyumba tatu zilishambuliwa huko Deir Al-Balah katikati mwa Gaza, jengo katika mji wa Gaza, na maeneo ya Khan Younis na Rafah, Reuters iliripoti, ikitoa mfano wa madaktari na mashahidi.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Israel Katz waliamuru mashambulizi hayo siku ya Jumanne asubuhi, kulingana na taarifa kutoka kwa ofisi ya Waziri Mkuu.

    "Hii inafuatia Hamas kukataa mara kwa mara kuwaachilia mateka wetu, pamoja na kukataa kwake mapendekezo yote ambayo imepokea kutoka kwa Mjumbe wa Rais wa Marekani Steve Witkoff na kutoka kwa wapatanishi," ilisema.

    "Israel, kuanzia sasa, itachukua hatua dhidi ya Hamas kwa kuongeza nguvu za kijeshi," iliongeza.

    Mpango wa mashambulizi hayo"uliwasilishwa na IDF mwishoni mwa wiki na kuidhinishwa na uongozi wa kisiasa", ilisema. Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulishauriwa na Israel kabla ya kutekeleza mashambulizi hayo, msemaji wa Ikulu ya White House aliambia Fox News.

    Wapatanishi wamekuwa wakijaribu kutafuta njia ya kusonga mbele baada ya awamu ya kwanza ya mapatano ya muda kumalizika tarehe 1 Machi.

  14. Mzozo wa DRC: M23 yajitoa mazungumzo ya amani ya Angola

    c

    Chanzo cha picha, ge

    Kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limetangaza kuwa halitashiriki tena katika mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika leo mjini Luanda Angola.

    Awali kundi hilo lilithibitisha kuwa litahudhuria kwenye mazungumzo hayo ya kwanza ya ana kwa ana pamoja na serikali ya Kongo, ambayo yenyewe inasema itahudhuria mkutano huo wa Luanda unaosimamiwa na Angola.

    Kujiondoa kwa M23 katika mazungumzo hayo kumekuja baada ya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kwa kiongozi wake na makamanda wa jeshi la Rwanda.

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, Msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka aliandika, "Vikwazo vilivyofuatana vilivyowekwa kwa wanachama wetu, vinaathiri kwa dhati mazungumzo ya moja kwa moja na kuzuia maendeleo yoyote," Kanyuka alisema, akiongeza kuwa kwa sababu hizo, M23 haiwezi "kushiriki tena katika majadiliano".

    Mapema siku ya Jumatatu, Kanyuka aliripoti kuwa wajumbe wa M23 walikuwa wameshakwenda katika mji mkuu wa Angola, Luanda.Wakati M23 wakisusia, ujumbe unaoiwakilisha DRC uko Luanda tayari kwa mazungumzo, msemaji wa Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliambia shirika la habari la AP na kunukuliwa na Aljazeera, kwamba wenyewe watashiriki mazungumzo.

    M23 ni mojawapo ya makundi yapatayo 100 yenye silaha ambayo yamekuwa yakigombea eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC, karibu na mpaka na Rwanda. Mzozo huo umezua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao, huku watu 7,000 wakiripotiwa kufariki tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

    M23 inaungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda, kulingana na Umoja wa Mataifa. Lakini Rwanda inasema kuwa vikosi vyake vinafanya kazi ya kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoishambulia Kigali. Ikulu ya Angola ilitangaza kwa mara ya kwanza mipango ya mazungumzo hayo Machi 11 baada ya mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi.

  15. Trump na Putin kuzungumza leo kuhusu vita vya Ukraine

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump atazungumza na Vladimir Putin wa Urusi leo kuhusu kukomesha vita vya Ukraine, huku kukiwa na makubaliano ya eneo na Kyiv na udhibiti wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia huenda ukahusika katika mazungumzo hayo.

    "Tunataka kuona kama tunaweza kumaliza vita hivyo," Trump aliwaambia waandishi wa habari akipanda ndege ya Air Force One wakati akielekea Washington kutoka Florida. "Labda tunaweza, labda hatuwezi, lakini nadhani tuna nafasi nzuri sana. Nitazungumza na Rais Putin siku ya Jumanne. Kazi kubwa imefanywa mwishoni mwa juma."

    Trump anajaribu kupata uungwaji mkono wa Putin kwa pendekezo lake la kusitisha vita kwa siku 30 ambalo Ukraine ilikubali wiki iliyopita.

    Pamoja na hatua hiyo bado pande zote mbili zinaendelea kufanya mashambulio makali ya angani, huku Urusi ikikaribia kuviondoa vikosi vya Ukraine katika eneo lao Kursk, magharibi mwa Urusi.

    Alipoulizwa ni makubaliano gani yanazingatiwa katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, Trump alisema: "Tutakuwa tunazungumza kuhusu ardhi. Tutakuwa tunazungumza kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme ... Tayari tunazungumza kuhusu hilo, kugawanya baadhi ya mali."

    Trump hakutoa maelezo yoyote lakini kuna uwezekano alikuwa anarejea kuhusu kituo cha Zaporizhzhia kinachokaliwa na Urusi huko Ukraine, ambacho ni kiwanda ama kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya. Urusi na Ukraine zimeshutumiana kila mmoja kwa vitendo vinavyohatarisha usalama katika kinu hicho.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alithibitisha Jumatatu kwamba Putin atazungumza na Trump kwa simu lakini akakataa kuzungumzia matamshi ya Trump kuhusu ardhi na mitambo ya kuzalisha umeme.

    Ikulu ya Kremlin ilisema Ijumaa kuwa Putin amemtumia Trump ujumbe kuhusu mpango wake wa kusitisha mapigano kupitia mjumbe wa Marekani Steve Witkoff, ambaye alifanya mazungumzo mjini Moscow, akielezea matumaini kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa kumaliza mzozo huo wa miaka mitatu.

    Witkoff, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, na Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Trump, Mike Waltz, walisisitiza mwishoni mwa wiki kwamba bado kuna changamoto zinazopaswa kutatuliwa kwanza kabla ya Urusi kukubali kusitishwa kwa mapigano, achilia mbali azimio la mwisho la kupata amani na kumaliza vita.

  16. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya habari zetu leo