Tubaki ama tuhame? Wagaza wako njia panda

vifusi vya jengo lililoporomoka vinaonekana huku mtu akitembea, na majengo mengine karibu naye yameharibiwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jabalia, kaskazini mwa Gaza, wakati mmoja ilikuwa kambi ya wakimbizi yenye shughuli nyingi na iliyojaa sana
    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, BBC News, Jerusalem
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ukitazama eneo la Jabalia, ukiwa angani, inatamausha.

Taswira ambayo inaonyesha uharibifu mkubwa.

Majengo yaliyoporomoka, vifaa vilivyoning'inia na vifusi vilivyogeuka mlima wa taka.

Kutokana na hali hii ya majengo ni vigumu kubaini mandhari halisi ya eneo hilo.

Lakini ukitumia kamera zinazotumia ndege zisizo na rubani utaona mahema ya buluu na meupe ambapo kambi zimeanzishwa katika eneo tambarare.

Na katika pita pita zako utaona masoko yaliyochipuka kando ya vifusi, taka zimetapakaa na watoto wakibembea kwa vyuma vya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

Baada ya wiki sita ya makubaliano yakusitisha mapigano kutekelezwa, eneo hili la Jabalia limeanza kuchipuka upya huku shughuli za kawaida zikianza kurejea.


Nabil akiwa amesimama karibu na vifusi vya nyumba yake aliyoiacha wakati wa vita
Maelezo ya picha, Wengi, kama Nabil, waliorudi makwao wamekuta nyumba zao zimeharibiwa au zimeporomoka

Katika eneo jirani al-Qasasib, Nabil amerejea kwa nyumba yake ya ghorofa nne ambayo kidogo iko katika hali mtu anaweza kuishi, lakini haina madirisha, milango na upande mwingine haina ukuta.

Akiwa na familia yake wamebuni kuta kwa kuweka mbao na kugongelea ili zisianguke.

''Hebu angalia uharibifu huu,'' anasema huku akikagua vifusi vya nyumba yake aliyoienzi.

''Wanataka tuhame bila ya kujenga upya makazi yetu? Tutahama vipi. Kile tunaweza kufanya ni kukarabati upya kwa ajili ya watoto wetu.''

Akianza pilka pilka za mapishi, Nabil anawasha moto katika ngazi yake akitumia mbao zilizoharibika wakati wa majengo kuporomoka.

Laila amekalia kochi la waridi akiwa na msichana mdogo
Maelezo ya picha, Laila, kulia, anahofia vizazi vijazo kutopata elimu ya msingi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika Chumba kingine, Laila Ahmed Okasha anafanya usafi karo ambayo maji ya mfereji yaligoma miezi kadhaa iliyopita.

'' Hakuna maji, stima na pia mabomba yakupitisha maji taka,'' anasema.

''Iwapo tunahitaji maji inatulazimu tusafiri maeneo ya mbali ,''

Anasema alibwaga kilio aliporejea nakupata nyumba yake kuwa gofu .

Analaumu Israel na Hamas kwa kuharibu mahali alipopaita nyumbani.

''Wote ni wa kulaumiwa,''anasema .'' Tulikuwa na makazi mazuri na tuliishi maisha yasio na bughudha''.

Baada ya vita kuanza mwezi Oktoba 2023, Israel iliwaarifu Wapalestina wanaoishi katika ukanda wa Gaza- ikiwemo Jabalia- kuhamia maeneo ya Kusini kwa usalama wao.

Mamia ya maelfu ya watu waliitia wito huo, lakini baadhi walikaidi amri na kuapa kuhimili vita vilivyokuwa vikichacha.

Laila na mumewe Marwan walikuwa wamesalia hadi mwezi Oktoba mwaka jana, ambapo wanajeshi wa Israel walivamia tena Jabalia, kwa madai Hamas walikuwa wakijikusanya upya katika kambi waliokuwa wamejihifadhi.

Baada ya miezi miwili ya kupata uhifadhi katika kambi iliyo karibu ya Shati, Leila na Marwan walirejea Jabalia na kupata hali imegeuka na yakusikitisha.

Marwan ameegemea mbele ya ukuta ulioharibiwa ndani ya ushoroba wa jengo lao
Maelezo ya picha, Marwan na Laila waliweza kukaa nyumbani kwao kwa mwaka wa kwanza wa vita

"Aliporejea na kuona jinsi kulivyoharibiwa, sikutaka kubaki hapa tena," anasema Marwan.

"Nilikuwa na maisha mazuri, lakini sasa ni kama motoni. Ikiwa nitapata nafasi ya kuondoka, nitaenda. Sitakaa hata dakika moja zaidi."

Hili ni jambo ambalo linatoa picha ya hali ngumu inayowakabili watu wa Gaza.

Hatma ya raia wa Gaza imekuwa mada ya mjadala wa kimataifa, huku maswali ya kukaa au kuondoka yakijitokeza kwa dhahiri.

Mnamo Februari, Donald Trump alipendekeza kuwa Marekani inapaswa kuchukua na kudhibiti Gaza, na kwamba wakazi karibu milioni mbili wa Palestina wanapaswa kuondoka, labda kwa kudumu.

Pendekezo hili lilikosolewa vikali, na Trump ameonekana kurudi nyuma, akisema alilipendekeza lakini hatalazimisha mtu yeyote.

Wakati huo, Misri inaongoza juhudi za mataifa ya Kiarabu kutafuta njia mbadala za kutatua mgogoro huu, na inakusudia kuwasilisha suluhu hii kwenye mkutano wa dharura wa Kiarabu utakaofanyika Cairo Jumanne.

Kwa maana muhimu, Misri inasisitiza kuwa watu wa Palestina wanapaswa kubaki Gaza wakati eneo hilo likijengwa upya.

Hata hivyo, pendekezo la Trump limeonyesha upande mwingine wa Gaza – upande unaozikubali changamoto zote na kushikilia msimamo wake.

Laila anasema, "Ikiwa Trump anataka kutufanya tuondoke, nitakaa Gaza. Nataka kusafiri kwa hiari yangu mwenyewe. Sitoki kwa sababu yake."

Hili linatoa picha ya roho ya kupambana na kuendelea, licha ya hali ngumu na ya kutisha.

Kando yake, jengo la ghorofa tisa la rangi ya njano limeharibiwa kwa kiasi kikubwa, na ghorofa za juu zimeanguka kabisa, zikihatarisha ghorofa nyingine.

Hata hivyo, jengo hili linatumiwa na familia nyingine kama makazi yao, huku makoti yakining'inia madirishani na nguo zikikauka chini ya jua la mwishoni mwa majira ya baridi.

Kwa namna isiyotarajiwa, mbele ya mlango wa plastiki wa muda uliojaa kifusi na taka, anasimama sanamu ya mrembo isiyokuwa na kichwa, akiwa amevaa mavazi ya harusi.

Sanaa amesimama nje ya duka lake la kujitengenezea, akiwa ameshikilia sehemu ya vazi jeupe la harusi kwenye sanamu iliyosimama mbele ya rundo kubwa la takataka na vifusi.
Maelezo ya picha, Sanaa alilazimika kuachana na biashara yake ya mavazi ya harusi alipokimbilia kusini mwa Palestina mwishoni mwa mwaka 2023

Hili ni duka la mavazi la Sanaa Abu Ishbak.

Sanaa, mshonaji mwenye umri wa miaka 45 na mama wa watoto 11, alianzisha biashara hii miaka miwili kabla ya vita, lakini alilazimika kuihama alipojikuta akikimbilia kusini mnamo Novemba 2023.

Hata hivyo, alirejea mara tu baada ya mapatano ya kusitisha mapigano kutangazwa.

Kwa kushirikiana na mumewe na binti zake, Sanaa amekuwa akifagia kifusi dukani, akipanga mavazi kwa kiango cha kutundukia mavazi na kujiandaa tena kwa biashara.

"Napenda kambi ya Jabalia," anasema kwa uthabiti. "Na sitahama mpaka nifariki."

Sanaa na Laila wanatoa picha ya wanawake wawili wenye azimio la kubaki Gaza, licha ya changamoto zinazowakabili.

Walakini, wanapozungumzia vizazi vijavyo, sauti zao zinabadilika.

Laila anasema, "Yeye hata hajui kuandika jina lake mwenyewe."

"Hakuna elimu Gaza," anasema, akiwa na huzuni kuhusu mustakabali wa watoto.

Mama wa msichana mdogo aliuawa wakati wa vita. Laila anasema bado anazungumza na mjukuu wake usiku, akijua kuwa alikuwa "kipenzi cha roho yangu" na kwamba alimuacha binti yake mikononi mwake.

"Ikiwa nitapata nafasi ya kusafiri, nitafanya hivyo kwa ajili ya mjukuu wangu," anasema Laila, akionyesha dhamira ya kumtoa mtoto huyu kwenye mazingira magumu.

Simulizi hizi za watu wa Gaza zinaonyesha si tu hali ya kiuchumi na kijamii, bali pia roho ya kudumu na imani ya kuendelea mbele licha ya vita na maafa yanayowakumba.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid