Mpango wa Trump kuhusu Gaza utaonekana kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipoanza kuzungumza kuhusu Gaza siku 10 zilizopita kama eneo linalohitaji kuangaziwa, akitoa wito wa "kusafishwa eneo zima", haikuwa wazi ni kiasi gani alimaanisha kwa kutoa kauli hii.
Lakini kuelekea kwenye ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akizungumza kabla ya mkutano na waandishi wa habari, ni wazi sasa yuko makini sana kuhusu mapendekezo yake.
Walifikia msimamo wa pamoja zaidi uliowekwa na Marekani kuhusu Israeli na Wapalestina katika historia ya hivi karibuni ya mzozo; na itaonekana kama kukiuka sheria za kimataifa.
Pamoja na jinsi tangazo hilo litakavyochukuliwa na watu wa kawaida, linaweza pia kuwa na athari kubwa katika mchakato wa haraka wa kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka.
Trump na maafisa wake wanaandaa wito kama anavyoita kwa lugha yake - "kuwapatia mwanzo mpya" Wapalestina wote nje ya Gaza kama ishara ya kibinadamu, wakisema hakuna mbadala wao kwa sababu Gaza ni "mahali palipobomolewa".
Chini ya sheria za kimataifa, majaribio ya kuhamisha watu kwa nguvu yamepigwa marufuku kabisa, na Wapalestina na mataifa ya Kiarabu wataona hili kama pendekezo la wazi linalolenga kufukuzwa kwao na Wapalestina katika ardhi yao.
Ndiyo maana viongozi wa Kiarabu tayari wamekataa kabisa mawazo yake, yaliyotolewa mara kwa mara katika siku 10 zilizopita,akipendekeza Misri na Jordan kuwa zinaweza "kuwachukua" Wapalestina kutoka Gaza.
Katika taarifa yake ya Jumamosi, Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Mamlaka ya Palestina na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisema kwamba hatua hiyo inaweza "kuhatarisha uthabiti wa eneo hilo, hatari ya kuongeza mzozo zaidi, na kudhoofisha matarajio ya amani na kuishi pamoja miongoni mwa watu wake".
Kwa muda mrefu imekuwa shauku ya wazalendo wenye msimamo mkali huko Israeli kuwaondoa Wapalestina katika maeneo wanayokaa na kupanua makazi ya Wayahudi katika maeneo yao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel, makundi haya - viongozi ambao wamekuwa sehemu ya muungano wa Netanyahu - wamedai vita dhidi ya Hamas kuendelea kwa muda usiojulikana, wakiapa kuanzisha upya makaazi ya Waisraeli katika Ukanda wa Gaza.
Wameendelea na wito wao na kupinga makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House na Waziri Mkuu wa Israel, Trump alienda mbali zaidi hata kuliko wito wake wa hivi karibuni uliokua ukitaka Wapalestina wa Gaza "wahamishwe" hadi Misri na Jordan, akisema kwamba Marekani italichukua eneo hilo na kulijenga upya.
Alipoulizwa ikiwa Wapalestina wataruhusiwa kurejea, alisema "watu wataishi huko, akisema itakuwa "mahali pa kimataifa,ambapo hapakutazamiwa", kabla ya kuongeza "Wapalestina pia".
Mjumbe wake wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff mapema siku hiyo alitoa muhtasari kuhusu pendekezo hilo, akisema kuhusu Trump "jamaa huyu anaelewa kuhusu makazi".
Trump alisema itakuwa "eneo la kuvutia Mashariki ya Kati".
Alipoulizwa iwapo wanajeshi wa Marekani watahusika katika kutwaa Gaza, Bw Trump alisema "tutafanya kinachohitajika".
Mapendekezo yake yanafikia mageuzi makubwa zaidi katika msimamo wa Marekani katika eneo hilo tangu kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948 na vita vya 1967, ambavyo vilishuhudia kuanza kwa utawala wa kijeshi wa Israel katika ardhi hiyo ikiwemo Ukanda wa Gaza.
Gaza ilikuwa tayari makazi ya Wapalestina waliokimbia au kulazimishwa kutoka makwao katika vita vilivyochangia kuimarika kwa Israeli.
Wao na vizazi vyao wanaunda idadi kubwa ya wakazi wa Gaza hadi leo.
Mapendekezo ya Trump, yakipitishwa kuwa sheria yangehusisha idadi hiyo ya watu, ambayo sasa ni zaidi ya watu milioni mbili, wanaolazimishwa kwingineko katika ulimwengu wa Kiarabu au hata kwingineko, anasema Trump, "kupata makazi upya ... ya kudumu".
Mapendekezo hayo yatafutilia mbali uwezekano wa suluhu ya baadaye ya serikali mbili kwa maana yoyote ile ya kawaida na yatakataliwa kimsingi na Wapalestina na ulimwengu wa Kiarabu kama mpango wa kuwaondoa.
Sehemu kubwa ya kambi ya kisiasa ya Netanyahu na vuguvugu la walowezi lenye msimamo mkali nchini Israel litatetea kauli ya Rais Trump, wakiyaona kama utimilifu wa hatua kama Netanyahu anavyoiweka kukomesha "Gaza kuwa tishio kwa Israeli".
Kwa Wapalestina wa kawaida, itakuwa sawa na kitendo cha adhabu ya pamoja.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Lizzy Masinga












