Je, ni eneo gani la amani la Syria lililotekwa na Israel?

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Jeshi la Israel lilisema siku ya Jumapili kwamba vikosi vyake vimewekwa katika eneo la amani kati ya Syria na Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, kufuatia "kuingia kwa watu wenye silaha kwenye eneo la amani".
Hapo awali, Redio ya Jeshi la Israel iliripoti, ikinukuu chanzo cha kijeshi, kwamba vikosi vya Israel vinadhibiti eneo la kijeshi katika Mlima Hermon nchini Syria baada ya kuondoka kwa vikosi vya jeshi la Syria katika eneo hilo.
Haya yanajiri baada ya matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambapo alisema kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria, kumeondosha makubaliano ya kutoingia eneo hilo yaliyotiwa saini mwaka 1974, na akaamuru "kushikiliwa" kwa eneo la amani.
Eneo la amani ni lipi?
Netanyahu ameeleza kwamba "kila mtu anatambua umuhimu wa Israel wa kudhibiti Milima ya Golan." ambayo amesisitiza "milele itabaki kuwa sehemu muhimu ya Israel."
Tangu mwisho wa Vita vya Kwanza vya Dunia 1918, maeneo ambayo yalidhibitiwa na Dola la Ottoman, ambayo ni Syria ya leo, Lebanon, Israel na maeneo ya Palestina, yalikuwa chini ya jeshi la Washirika baada ya kushinda vita, na maeneo hayo yakagawanywa kati ya Uingereza na Ufaransa.
Mwaka 1923, mipaka iliwekwa na Mamlaka ya Ufaransa huko Syria na Lebanon, na Mamlaka ya Uingereza huko Palestina - ambayo ni pamoja na maeneo ambayo leo yanaunda Israel na Maeneo ya Palestina.
Kisha Paris na London zilikubali kuweka mipaka ili Miinuko yote ya Golan iwe ndani ya maeneo ya Mamlaka ya Ufaransa, na Ziwa lote la Tiberias liwe ndani ya Mamlaka ya Uingereza.
Mamlaka ya Ufaransa juu ya Syria yalimalizika mwaka 1946, na Milima ya Golan ikawa sehemu ya Jamhuri ya Syria.
Lakini kufuatia kuanzishwa kwa Taifa la Israel mwaka 1948, Vita vya Waarabu na Waisraeli vilianza, ambapo Syria ilishiriki vita hivyo.
Kisha Syria na Israel zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano 1949 na kuweka mipaka ya kusitisha mapigano kati yao, na kuanzishwa kwa maeneo yasiyotakiwa kuwa na wanajeshi karibu na Ziwa la Galilaya na Uwanda wa Hula.
Katika vita vya 1967, Israel iliikalia sehemu kubwa ya Milima ya Golan, ukiwemo mji wa Quneitra, pamoja na miteremko ya Mlima Hermoni (Mlima Hermoni) upande wa kaskazini wa Golan. Syria na Israel zikafikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuunda eneo linalojulikana kama Mstari wa Zambarau.
Mkataba wa Israel na Syria
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika vita vya mwaka 1973, wanajeshi wa Syria waliishambulia milima ya Golan na kuweza kusonga mbele katika baadhi ya maeneo, hasa katika maeneo ya kusini mwa miinuko hiyo, lakini majeshi ya Israel yalianzisha mashambulizi na kufanikiwa kudhibiti tena milima hiyo.
Vikosi vya Israel vilipenya mashariki hadi kaskazini mwa Milima ya Golan, na kuteka maeneo mengine ndani kabisa ya Syria ambayo hawakuwa wameyakalia kabla ya 1973, pamoja na maeneo ya barabara kati ya Miinuko ya Golan na mji mkuu, Damascus, na kilele cha Mlima Hermoni.
Kisha ukaja mwaka 1974, Syria na Israel zilipofikia makubaliano ya kusitisha mapigano, ambapo Israel ilijiondoa katika maeneo yote iliyokuwa imeyanyakua katika vita vya 1973, pamoja na maeneo machache ambayo iliyanyakua mwaka 1967, ikiwa ni pamoja na mji wa Quneitra.
Pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha eneo la amani, kati ya sehemu ya Milima ya Golan inayokaliwa na Israel na Syria. Sehemu hii itakuwa ndani ya Syria - mashariki mwa mstari wa zambarau, Mlima Hermoni upande wa kaskazini, hadi katika mpaka kati ya Syria na Jordan upande wa kusini.
Syria iliweka utawala wa kiraia ndani ya eneo hilo, huku jeshi la Syria likisalia nje ya mipaka ya eneo hilo.
Makubaliano hayo pia yalijumuisha uwepo wa jeshi uwe ni mdogo kwa pande zote mbili. Makubaliano hayo pia yalijumuisha vifungu vingine kama vile kubadilishana mateka wa vita na miili ya askari waliokufa kati ya pande hizo mbili.
Eneo la amani lina urefu wa kilomita 75 kutoka kaskazini hadi kusini, na kwa upana kati ya mita 200 na kilomita 10.
Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha waangalizi wa amani (UNDOF) kiko ndani ya eneo hilo, ambacho kina jukumu la kufuatilia usitishaji vita kati ya pande hizo mbili.
Kikosi hiki - ambacho kina wanajeshi wapatao 1,200, kutoka nchi 13 - kiliundwa kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama, na mwishoni mwa Juni 2024, Baraza la Usalama liliongeza uwepo wake hadi mwisho wa 2024.
Makubaliano hayo yamedumu kwa miaka 50, licha ya "ukiukaji" uliotokea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, ikiwemo "ongezeko la shughuli za kijeshi katika eneo la amani," kulingana na Umoja wa Mataifa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla












