Maswali 8 kuuelewa mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mzozo kati ya Wapalestina na Waisraeli unazidi kupamba moto. Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi makali huko Gaza Jumamosi hii, Oktoba 7.
Ni baada ya Hamas, kundi la wapiganaji wa Kiislamu linalodhibiti eneo hilo, kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa kurusha mamia ya makombora na wanamgambo kupenya kusini mwa Israel.
Kuna mamia ya vifo kati ya pande zote mbili katika mapigano ambayo wachambuzi wanaona kuwa hayajawahi kutokea kabla. Ni mapigano ya hivi karibuni katika mzozo wa miongo kadhaa Mashariki ya Kati.
Mgogoro ulianza vipi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwa sababu ya chuki dhidi ya Uyahudi na Wayahudi huko Ulaya, mwanzoni mwa karne ya 20, kulipelekea harakati ya Wazayuni kupata nguvu, ikitafuta kuanzisha taifa la Wayahudi.
Eneo la Palestina, kati ya Mto Jordan na Bahari ya Mediterania, linachukuliwa kuwa takatifu na Waislamu, Wayahudi na Wakristo, lilikuwa chini ya milki ya Dola la Ottoman katika miaka hiyo na lilikaliwa zaidi na Waarabu na jamii zingine za Kiislamu.
Kuhamia kwa Wayahudi kwa wingi katika eneo hilo, wakichochewa na itikadi ya Kizayuni, kulichochea kuleta mvutano miongoni mwa za kiarabu na kiyahudi.
Kufuatia kusambaratika kwa dola la Ottoman katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Uingereza ilitakiwa kusimamia eneo la Palestina kwa ruhusa ya Umoja wa Mataifa.
Kabla na wakati wa vita, Waingereza walitoa ahadi mbalimbali kwa Waarabu na Wayahudi ambazo baadaye hawakuzitimiza, kwa sababu tayari nchi hiyo na Ufaransa zilikuwa zimejigawanyia Mashariki ya Kati.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mvutano kati ya wazalendo wa Kiarabu na Wazayuni ulisababisha mapigano kati ya vikundi vya wanamgambo wa Kiyahudi na magenge ya Waarabu.
Baada ya Vita vya Pili vya Dunia na mauaji ya Holocaust, shinikizo liliongezeka la kuanzishwa taifa la Kiyahudi. Mpango wa awali ulikuwa ni kugawa eneo kwa Wayahudi na Wapalestina.
Baada ya kuanzishwa kwa taifa la Israeli Mei 14, 1948, mvutano huo ulitoka kuwa suala la Palestina na Israel hadi suala la kikanda.
Siku iliyofuata, Misri, Jordan, Syria na Iraq zilivamia eneo hili. Vikawa vita vya kwanza vya Waarabu na Israeli, ambavyo pia vinajulikana na Wayahudi kama vita vya uhuru au ukombozi. Baada ya mzozo huo, eneo lililopangwa hapo awali na Umoja wa Mataifa kwa Nchi ya Kiarabu lilipunguzwa kwa nusu nzima.
Kwa Wapalestina, Nakba , kinachojulikana kama "janga" lilianza: mwanzo wa janga la kitaifa. Wapalestina 750,000 walikimbilia nchi jirani au walifukuzwa na wanajeshi wa Kiyahudi.
Vita vya Siku Sita kati ya Juni 5 na 10, 1967. Ulikuwa ushindi wa kishindo kwa Israel dhidi ya muungano wa Waarabu. Israeli iliteka Ukanda wa Gaza na Rasi ya Sinai kutoka Misri, Ukingo wa Magharibi (pamoja na Jerusalem ya Mashariki) kutoka Jordan, na Milima ya Golan kutoka Syria. Wapalestina nusu milioni walikimbia.
Mzozo wa mwisho wa Waarabu na Waisraeli ulikuwa Vita vya Yom Kippur mnamo 1973, ambavyo vilizikutanisha Misri na Syria dhidi ya Israeli na kuruhusu Cairo kurudisha Sinai.
Kwa nini Israeli ilianzishwa Mashariki ya Kati?

Chanzo cha picha, HULTON ARCHIVE
Mapokeo ya Kiyahudi yanadai kwamba eneo ambalo Israeli ipo ni nchi iliyoahidiwa na Mungu kwa Abrahamu na watoto wake.
Eneo hilo lilivamiwa huko nyuma na Antiquity, Waashuri, Wababeli, Waajemi, Wamasedonia na Warumi. Roma ilikuwa dola iliyoita eneo hilo Palestina. Miongo saba baada ya Kristo, iliwafukuza Wayahudi baada ya harakati zao za utaifa zilizotafuta uhuru.
Uislamu ulipopata nguvu katika karne ya 7 BK, Palestina ilitekwa na Waarabu na kisha kutekwa na wapiganaji wa vita vya msalaba kutoka Ulaya. Kisha utawala Ottman ulichukua hadi Vita vya Kwanza vya Dunia, wakati agizo la Uingereza lilipowekwa.
Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina (UNSCOP) ilisema katika ripoti yake kwa Baraza Kuu Septemba 3, 1947, sababu za kuanzishwa kwa taifa la Kiyahudi katika Mashariki ya Kati zilijikita katika "hoja zinazotokana na vyanzo vya Biblia na kihistoria.
Pia Azimio la Balfour 1917, serikali ya Uingereza ilitangaza ingependa kuona taifa la Wayahudi huko Palestina.
Kufuatia mauaji ya Nazi dhidi ya mamilioni ya Wayahudi huko Ulaya kabla na wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, shinikizo la kimataifa liliongezeka kutambuliwa kwa serikali ya Kiyahudi.
Haikuweza kutatua mgawanyiko kati ya Waarabu na Uzayuni, serikali ya Uingereza ilipeleka suala hilo kwenye Umoja wa Mataifa.
Novemba 29, 1947, Baraza Kuu liliidhinisha mpango wa kugawanywa kwa Palestina, ambao ulipendekeza kuundwa kwa nchi huru ya Kiarabu na dola ya Kiyahudi na utawala maalumu wa mji wa Jerusalem.
Mpango huo ulikubaliwa na Waisraeli lakini sio Waarabu, ambao waliona ni kupoteza eneo lao. Ndiyo maana haukutekelezwa kamwe.
Siku moja kabla ya Mamlaka ya Uingereza ya Palestina kuisha, Mei 14, 1948, Wayahudi walitangaza uhuru wa Israeli. Siku iliyofuata Israeli iliomba uanachama katika Umoja wa Mataifa, iliupata mwaka mmoja baadaye.
Kwa nini kuna maeneo mawili ya Wapalestina?

Chanzo cha picha, HULTON ARCHIVE
Maeneo mawili ya Palestina ni Ukingo wa Magharibi (ambao ni pamoja na Jerusalem Mashariki) na Ukanda wa Gaza, ambao uko umbali wa kilomita 45.
Ukingo wa Magharibi upo kati ya Jerusalem, unaodaiwa kuwa mji mkuu na Wapalestina na Waisraeli. Wakati Gaza ni ukanda wa kilomita 41 na upana wa kati ya kilomita 6 na 12.
Gaza ina mpaka wa kilomita 51 na Israeli, kilomita 7 na Misri na kilomita 40 za ukanda wa pwani kwenye Bahari ya Mediterania.
Ukanda wa Gaza ambao awali ulikuwa ukikaliwa na Waisraeli ambao bado wanadumisha udhibiti wa mpaka wake wa kusini, ulitekwa na Israel katika vita vya 1967 na uliachwa mwaka 2005, ingawa Israel inashikilia kizuizi cha anga, baharini na nchi kavu.
Ukanda huo kwa sasa unadhibitiwa na Hamas, kundi kuu la Kiislamu la Palestina ambalo halijawahi kutambua makubaliano yaliyotiwa saini kati ya makundi mengine ya Palestina na Israel.
Ukingo wa Magharibi, unatawaliwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina, serikali ya Palestina inayotambulika kimataifa ambayo kundi lake kuu, Fatah, si la kidini.
Je, kuna mkataba wa amani kati yao?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kufuatia kuundwa kwa Taifa la Israel na maelfu ya watu waliopoteza makaazi yao, vuguvugu la Palestina lilianza kujikusanya tena katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Misiri, na katika kambi za wakimbizi zilizoundwa katika mataifa mengine ya Kiarabu.
Muda mfupi kabla ya vita vya 1967, mashirika ya Palestina kama vile Fatah - likiongozwa na Yasser Arafat - liliunda Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO) na kuanzisha operesheni dhidi ya Israeli kwanza kutokea Jordan na kisha kutoka Lebanoni.
Mashambulizi haya pia yalijumuisha mashambulizi dhidi ya Israel katika ardhi ya Ulaya ikiwemo ndege, balozi au wanariadha.
Baada ya miaka mingi ya mashambulizi ya Wapalestina na mauaji ya yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya Israel. PLO na Israel zikatia saini makubaliano ya amani ya Oslo mwaka 1993.
PLO iliacha mashambulizi na kutambua kuwepo kwa Israel na kuishi kwa amani na usalama. Hamas hawakutambua makubaliano hayo.
Kufuatia makubaliano hayo Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina iliundwa, ambayo inawakilisha Wapalestina katika majukwaa ya kimataifa.
Rais wake huchaguliwa kwa kura ya moja kwa moja na yeye huchagua waziri mkuu na wajumbe wa baraza lake la mawaziri. Mamlaka yake zinadhibiti maeneo ya mijini na wawakilishi wake wa kiraia wanadhibiti maeneo ya vijijini.
Jerusalem Mashariki, ambayo inachukuliwa kuwa mji mkuu wa kihistoria na Wapalestina, haijajumuishwa katika makubaliano haya. Jerusalem ni moja eneo lenye mgogoro kati ya pande zote mbili.
Ni mambo gani yanayozozaniwa?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kucheleweshwa kuanzishwa kwa Taifa huru la Palestina, ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kizuizi cha usalama kuzunguka eneo hilo - kinacholaaniwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague - kumetatiza maendeleo ya mchakato wa amani. .
Vikwazo, ni pamoja na kushindwa kwa mazungumzo ya mwisho ya amani yaliyofanyika Camp David, Marekani, mwaka 2000, wakati Bill Clinton aliposhindwa kufikia makubaliano kati ya Arafat na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel wakati huo, Ehud Barak.
Maeneo yanayozozaniwa:
Jerusalem: Israel inadai mamlaka juu ya mji huo (mtakatifu kwa Wayahudi, Waislamu na Wakristo) na inadai kuwa ni mji mkuu wake baada ya kuchukua Jerusalem Mashariki mwaka 1967. Hili halitambuliki kimataifa. Wapalestina wanataka Jerusalem Mashariki kuwa mji mkuu wao.
Mipaka na ardhi : Wapalestina wanadai serikali yao ya baadaye ifuate mipaka kabla ya Juni 4, 1967, kabla ya kuanza kwa Vita vya Siku Sita, jambo ambalo Israeli inakataa.
Makazi : Hizi ni nyumba, kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa, zilizojengwa na serikali ya Israel katika maeneo yaliyotwaliwa na Israel baada ya vita vya 1967. Katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki kuna walowezi wa Kiyahudi zaidi ya nusu milioni.
Wakimbizi wa Kipalestina: Idadi ya wakimbizi inategemea nani anahesabu. PLO inasema kuna milioni 10.6, ambapo karibu nusu yao wamesajiliwa na UN.
Wapalestina wanashikilia kuwa wakimbizi wana haki ya kurejea katika eneo ambalo sasa ni Israel, lakini kwa Israel kufungua mlango kungeharibu utambulisho wake kama taifa la Kiyahudi.
Je, Palestina ni nchi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Umoja wa Mataifa uliitambua Palestina kama "nchi mwangalizi isiyo mwanachama" mwishoni mwa 2012.
Mabadiliko hayo yaliwaruhusu Wapalestina kushiriki katika mijadala ya Baraza Kuu na kuboresha nafasi zao za uanachama katika mashirika ya Umoja wa Mataifa na vyombo vingine.
Mwaka mmoja kabla Wapalestina walijaribu kutambuliwa lakini hawakupata uungwaji mkono wa kutosha katika Baraza la Usalama.
Zaidi ya asilimia 70 ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (138 kati ya 193) wanaitambua Palestina kama Taifa.
Nani anaifadhili Israel na nani Palestina?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwanza, lazima tuzingatie kuwepo kwa ushawishi mkubwa na wenye nguvu wa kuunga mkono Israel nchini Marekani na ukweli kwamba maoni ya umma kwa kawaida yanapendelea Israel, hivyo kwa rais kuondoa uungaji mkono kwa Israel ni jambo lisilowezekana .
Israeli ni mojawapo ya wapokeaji wakubwa wa misaada ya Marekani na mingi yao huja katika mfumo wa ruzuku kwa ununuzi wa silaha.
Disemba 2016, chini ya Rais Barack Obama, hatua isiyo ya kawaida ilichukuliwa katika sera ya Marekani kuelekea Israel; kutopinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalolaani sera ya Israeli ya makazi.
Lakini kuwasili kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House kulitoa nguvu mpya kwa uhusiano kati ya Merika na Israeli. Uhamisho wa ubalozi kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem, na kuifanya Marekani kuwa nchi ya kwanza duniani kutambua kama mji mkuu wa Israeli.
Mrithi wa Trump, Rais Joe Biden, alichukua madaraka kwa nia ya kukwepa mzozo hatari wa Israel na Palestina, kwa kuuona kuwa ni tatizo linalohitaji mtaji mkubwa wa kisiasa. Utawala wa Biden unaendelea kuunga mkono kutambuliwa kwa Israeli.
Kwa upande wa Wapalestina hawana uungwaji mkono wa wazi. Misri iliacha kuunga mkono Hamas, kufuatia kuondoshwa madarakani na jeshi la Rais Mohamed Morsi, wa Muslim Brotherhood.
Syria na Iran na kundi la Lebanon Hezbollah ni waungaji mkono mkubwa wa Hamas.
Kipi kitokee amani ipatikane?

Waisraeli watalazimika kuunga mkono taifa huru la Wapalestina ambalo linajumuisha Hamas, kuondoa vizuizi vya Gaza na vizuizi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.
Makundi ya Wapalestina yanapaswa kuachana na ghasia na kulitambua Taifa la Israel.
Na makubaliano ya busara yatapaswa kufikiwa kuhusu mipaka, makazi ya Wayahudi na kurejea kwa wakimbizi.
Wakati katika medani ya vita mambo yanazidi kupamba moto katika Ukanda wa Gaza, kuna aina ya vita vya kimya kimya katika Ukingo wa Magharibi na kuendelea kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi, ambavyo, kwa hakika, vinapunguza eneo la Wapalestina.
Pengine suala gumu zaidi kutokana ni Jerusalem, mji mkuu wa Wapalestina na Waisraeli.












