Bashar al-Assad: Kutoka kuwa daktari wa macho hadi rais mwenye mamlaka Syria

Picha ya rais wa Syria Bashar al-Assad

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya rais wa Syria Bashar al-Assad
Muda wa kusoma: Dakika 8

Kuna matukio muhimu katika maisha ya rais wa Syria Bashar al-Assad,lakini iliyojulikana sana ni ajali ya gari iliyotokea mbali na alikoishi.

Bashar Assad hakupangiwa kumrithi babake.

Hii ilianza tu pindi kaka yake mkubwa ,Bassel,kufariki katika ajali ya gari karibu na Damascus mwaka wa 1994.

Wakati huo,Bashar alikuwa akisoma taaluma ya udaktari wa macho nchini Uingereza.

Kufuatia kifo cha Bassel ,mipango ilianzishwa rasmi ya kumrithisha kaka yake mdogo kuchukua madaraka nchini Syria.

Baadaye,angeongoza nchi kupitia vita ambavyo viliangamiza maelfu ya watu na kuwakosesha wengi makaazi.

Lakini vipi Bashar al-Assad alivyobadilika kutoka kuwa daktari hadi kuwa kiongozi wa kiimla ambaye anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita?

Urithi wa baba yake Assad

Baba wa Assad,anayefahamika kama Hafez al-Assad alikuwa rais kwa takriban miaka 30

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baba wa Assad,anayefahamika kama Hafez al-Assad alikuwa rais kwa takriban miaka 30

Bashar al-Assad alizaliwa mwaka 1965 na wazazi wake Hafez al-Assad na Anisa Makhlouf.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuzaliwa kwake kulilingana na matukio ya kutamausha nchini Syria, mashariki ya kati na kwingineko.

Wakati huo ,utaifa wa waarabu ulijikita zaidi katika siasa za mikoa nchi nyingi katika eneo hilo na Syria haikuwa tofauti.

Chama cha Ba'ath kilichukua madaraka baada ya kuanguka kwa muungano wa muda kati ya Misri na Syria(1958-1961) na kuhamasisha uzalendo wa waarabu.

Kama vile nchi zingine za kiarabu wakati huo,Syria haikuwa na demokrasia na ilikosa uchaguzi wa vyama vingi.

Jamii ya Alawite, ambayo ni chimbuko la Assad, ilikuwa miongoni mwa jamii ambazo zilitelekezwa nchini Syria na kutokana na uchumi duni uliowaandama wengi walijipata wakijiunga na wanajeshi wa Syria.

Hafez al - Assad alijiunga kama mwanajeshi na mfuasi sugu wa chama cha Baa'th ,na kuwa waziri wa ulinzi mwaka 1966.

Hafez al-Assad alijenga ushawishi na kuwa rais mwaka 1971, wadhifa alioushikilia hadi kifo chake mwaka 2000.

Ulikuwa wakati wa kipekee katika historia ya Syria baada ya uhuru ambao uliona mapinduzi ya kijeshi mara kadhaa.

Alitawala taifa hilo kwa njia ya udikteta ,akiwakandamiza wapinzani wake na kukataa uchaguzi wa kidemokrasia.

Hatahivyo alionyesha busara katika siasa za nje, akishirikiana na umoja wa kisovieti lakini akajiunga na muungano ulioongozwa na Marekani katika vita vya Ghuba mwaka 1991.

Udaktari nchini Uingereza

Asma al-Akhras

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bashar alikutana na mkewe Asma al-Akhras, nchini Uingereza

Bashar Assad alichagua mkondo tofauti,mbali na siasa na uanajeshi.Aliamua kusoma taaluma ya sayansi.

Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha Damascus, akihamia Uingereza mwaka 1992 kusomea kiundani zaidi udaktari wa macho katika hospitali ya Western Eye nchini Uingereza.

Kulingana na makala maalum mwaka 2018 'A Dangerous Dynasty': Familia ya Assad, Bashar alifurahia maisha ya Uingereza.

Alivutiwa na mwimbaji wa Uingereza Phil Collins na akakumbatia utamaduni wa Magharibi.

Ni wakati huo akiwa Uingereza Bashar alikutana na mkewe , Asma al-Akhras.

Asma alikuwa akisoma sayansi ya Kompyuta katika tasisi ya King's College nchini Uingereza na baadaye akajiunga na Chuo kikuu cha Havard kwa shahada ya uzamili. Asijue maisha yake yatachukua mkondo tofauti.

Akiwa mtoto wa kiume wa pili wa Hafez al -Assad , Bashar alikuwa amefunikwa zaidi na kaka yake mkubwa Bassel, mbaye alikuwa ameaminika kumrithi baba yake.

Kifo cha Bassel mwezi Januari 1994 kiliathiri maisha ya Bashar moja kwa moja.

Aliitwa mara moja kutoka Uingereza , na kuanza rasmi kutayarishwa kuwa kiongozi mtarajiwa wa Syria.

Bashar alijiunga na jeshi na kuanza kuunda upya umaarufu wake akijiandaa kwa majukumu yaliyokuwa yanamuangalia siku za usoni.

Ndoto ya mabadiliko

Picha ya familia ya Assad

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Familia ya Assad imetawala Syria kwa nusu karne

Hafez al-Assad alifariki mwezi juni mwaka 2000 na Bashar akiwa na umri wa miaka 34 akachukua usukani kuendeleza utawala wa baba yake baada ya katiba ya Syria kufanyiwa marekebisho na kuweka miaka ya kuwa rais kupunguzwa hadi chini ya miaka 40.

Bashar Assad alikula kiapo cha urais majira ya joto mwaka 2000 akizindua siasa mpya nchini humo.

Alizungumzia sana kuhusu uwazi ,demokrasia, maendeleo,u sasa ,uwajibikaji na fikra za kisera.''

Miezi baada ya kuchukua mikoba ya uongozi , Bashar alimuoa Asma al-Akhras.

Wamebarikiwa na watoto watatu: Hafez, Zein, and Karim.

Mwanzoni, msimamo wa Bashar kuhusu mabadiliko ya kisiasa na uhuru wa wanahabari uliwapa matumaini wakaazi wengi wa Syria.

Mtindo wake wa uongozi ukishirikiana na elimu ya mkewe Asma iliashiria mwanzo mpya.

Syria iliingia kipindi cha mjadala wa umma na uhuru wa kuongea kinachojulikana kama ''Damascus Spring", lakini mwaka 2001 maafisa wa usalama walianza msako wa kuwakamata wakosoaji wa serikali.

Huku Bashar akizindua mabadiliko ya kiuchumi ambayo yalilenga kukuza ukuaji wa sekta za kibinafsi, miaka ya awali ya utawala wake pia ulipatia umaarufu binamu yake Makhlouf.

Makhlouf alijenga milki iliyokuwa pana ya kiuchumi ambayo wakosoaji waliitaja kama ulimbikizi wa mali na mamlaka.

Iraq na Lebanon

Picha ya Rafik Hariri ikiw aimening'inia katika daraja mjini Lebanon

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuuawa kwa aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri kulimtia tumbo joto Bashar al - Assad

Vita vya Iraq vya 2003 vilileta mzozano na kutia doa uhusiano kati ya Bashar al -Assad na serikali za magharibi.

Rais wa Syria alipinga vikali kuvamiwa kwa Iraq kulikoongozwa na Wamarekani, ambapo kunaaminika alihofia Syria kutekwa na Marekani.

Washington, kwa upande wao, walishutumu Damascus kwa kufumbia macho ulanguzi wa zana za vita kwa waasi ambao walikuwa wakipinga Marekani kuteka Iraq na pia kuruhusu walio na msimamo mikali kuvuka katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Mwezi Disemba ,mwaka 2003 ,Marekani iliweka vikwazo nchini Damascus kwasababu kadhaa, ikiwemo mikakati ambayo hailingani zaidi na Iraq lakini kwa Syria kusaidia Lebanon.

Mwezi Februari mwaka 2005 aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri -aliyekuwa mpinzani mkali wa Syria nchini Lebanon aliuawa katika shambulizi la kombora katikati mwa Beirut. Lawama yote iliangukia Syria.

Maandamano yalizuka mjini Lebanon ikilingana na msukumo wa kimataifa kwa Damascus, ambapo yalipelekea Syria kujiondoa kutoka Lebanon baada ya miaka 30 ya kuwa na wanajeshi wake nchini humo.

Hata hivyo, Assad na marafiki wake wa karibu wa Lebanon kama vile Hezbollah, walikataa katakata kuhusika na mauaji ya Hariri, hata baada ya mahakama spesheli ya kimataifa kumpata hatiani mwanachama wa Hezbollah kujihusisha na uhalifu 2020.

Mapinduzi ya 'Arab Spring'

Waandamanaji walirarua mabango ya picha ya Assad na baba yake

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, "Arab Spring"maandamano yalifika Syria mwaka 2011

Muongo wa kwanza wa utawala wa Bashar al- Assad uliona kuimarika kwa uhusiano wa Syria na Iran na kuongezeka kwa uhusiano wa Qatar na Uturuki, Uhusiano ambao baadaye ungebadilika.

Mahusiano na Saudi Arabia yalikuwa na pandashuka zake, licha ya Riyadh kumuunga mkono rais Bashar.

Rais Bashar al-Assad alifuata nyayo za baba yake katika sera za mataifa ya nje ,akiwa makini kuepuka mapigano ya kijeshi ya moja kwa moja.

Baada ya miaka kumi, utawala wa Assad unaweza kuelezewa kama mtindo wa kiimla, kwani sauti za upinzani zilikuwa zikiendelea kudhibitiwa.

Mnamo Disemba 2010, Asma al-Assad alifanya mahojiano na jarida la Vogue, ambapo alidai kuwa nyumba yao inasimamiwa "kwa demokrasia".

Katika siku hiyo hiyo, muuzaji mboga wa Tunisia, Mohamed Bouazizi, alijiteketeza kwa moto baada ya kupigwa na polisi, jambo lililochochea maandamano ya umma nchini Tunisia ambayo yalimng'oa rais Zine El Abidine Ben Ali.

Maandamano ya Tunisia yalichochea harakati za mapinduzi katika ulimwengu wa Kiarabu, na kufikia nchi za Misri, Libya, Yemen, Bahrain, na Syria.

Mahojiano na Vogue, yaliyochapishwa kwa mada "A Rose in the Desert" mwezi Machi 2011 (na baadaye kutupiliwa mbali), yalielezea Syria kuwa nchi isiyokumbwa na milipuko ya mabomu, ghasia na utekaji nyara''.Sifa hiyo ilikuja kuwa na dosari miezi iliyofuata.

Kufikia katika mwezi Machi ,maandamano yalifanyika Damascus na siku kadhaa baadaye maandamano yakaenea hadi kusini mwa mji wa Daraa, baada ya watoto kukamatwa kwa kuandika maneno ya kumpinga Assad ukutani.

Assad alisubiri wiki mbili kabla ya kuhutubia Syria.

Akiwa bungeni aliwahakikishia kupambana vikali na mahasimu wa Syria aliodai walijaribu kuingilia siasa zao huku akikiri kuwa matarajio ya wengi hayajaafikiwa na serikali.

Maafisa wa usalama waliwamiminia risasi waandamanaji mjini Daraa na kuzidisha sokomoko ,iliyopelekea raia kumtaka Assad ajiondoa mamlakani.

Mamlaka ilijibu mandamano hayo na vita ,ikilaumu mahasimu ambao walidai wametumwa na mataifa mengine.

Baada ya miezi kadhaa, ghasia hizo zililipuka na kuwa mvutano kati ya serikali na upande wa upinzani ambao ulienekea kote nchini.

Mikakati ya kimataifa, kampeni kali na vita

Raia wa Syria wakikagua majengo yaliyoharibiwa kufuatia shambulizi la kombora la serikali yao nakulipua Aleppo,mwezi juni tarehe 26 2014.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maeneo mengi Syria yameharibiwa baada ya muongo mmoja wa vita za wenyewe kwa wenyewe

Kadri mgogoro ulivyoongezeka, makadirio ya Umoja wa Mataifa kuhusu vifo yaliongezeka kutoka maelfu hadi mamia ya maelfu huku ushiriki wa nguvu za kimataifa ukiwa unaongezeka.

Urusi, Iran, na makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran walishirikiana na vikosi vya Assad, huku Uturuki na nchi za Ghuba zikisaidia makundi ya upinzani yenye silaha.

Ingawa maandamano ya kupinga Assad yalikuwa yakitaka demokrasia na uhuru kwa wote, mgawanyiko wa madhehebu ulijitokeza mapema na baadhi ya makundi ya upinzani yalilaumu serikali kwa kuteua Alawites kuliko Waislamu wa madhehebu ya Sunni.

Uingiliaji wa kanda ulizidisha mgawanyiko wa madhehebu.

Makundi ya Kiislamu yalitumia kauli za kibaguzi dhidi ya Alawites, huku wanamgambo wa Shia waaminifu kwa Iran, wakiwa chini ya uongozi wa Hezbollah, wakimiminika nchini Syria kumuunga mkono Assad.

Katika Iraq nchi jirani, kikundi cha kigaidi kilichokuwa kinatafsiri sheria za Kiislamu kwa njia kali zaidi kilikuwa: Dola la Kiislamu (IS).

Kikundi hicho kilitumia vita vya wenyewe kwa wenyewe kuchukua ardhi nchini Syria, na kutangaza mji wa mashariki wa Raqqa kuwa mji wake mkuu.

Mnamo Agosti 2013, watu kadhaa waliuawa katika shambulio la kemikali huko Ghouta Mashariki, eneo lililoongozwa na upinzani karibu na Damascus.

Nguvu za Magharibi na makundi ya upinzani ya Syria yalilaumu utawala wa Assad kwa shambulio hilo.

Ingawa Damascus ilikataa kujihusisha, ilikubali kutenganisha silaha zake za kemikali chini ya shinikizo la kimataifa na vitisho.

Hata hivyo, hili halikuweka mwisho uhalifu wa kivita nchini Syria, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kemikali zaidi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yalilaumu pande zote za mgogoro kwa kutenda uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, na ubakaji.

Kufikia 2015, serikali ya Assad ilionekana kuwa karibu kuanguka, baada ya kupoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi.

Hata hivyo, uingiliaji wa kijeshi kutoka Urusi uligeuza mwelekeo wa vita, na kumwezesha Assad kurejesha maeneo muhimu.

Vita vya Ghuba

Wanajeshi waliovalia sare kwenye gari la kijeshi wakipita kwenye maelekezo ya kuelekea miji tofauti ya Syria

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maafisa wa upinzani vimeanza maendeleo katika siku za hivi karibuni

Kati ya 2018 na 2020, makubaliano ya kanda na kimataifa yalizua hali ambapo vikosi vya serikali vilikuwa vikisimamia sehemu kubwa ya Syria, huku makundi ya upinzani ya Kiislamu na wanamgambo wa Kikurdi wakishirikiana kudhibiti kaskazini na kaskazini-mashariki.

Makubaliano haya yalipiga jeki wadhifa wa Assad na akarejea katika jukwaa la kidiplomasia la kiarabu: Syria ilirudishwa katika jumuiya ya nchi za kiarabu zikafungua balozi zao mjini Damascus.

Licha ya uchumi wa Syria kudorora katika muongo wa tatu wa utawala wa Assad, rais alionekana kuhimili changamoto yake kubwa zaidi.

Hata hivyo, mwezi Oktoba 2023 ,Hamas ilishambulia kwa kushutukizia Israel,i kichochea vita Gaza, ambavyo vilienea haraka hadi Lebanono, hasa kuathiri mshirika wa Assad, Hezbollah.

Mgogoro huo ulisababisha hasara kubwa kwa Hezbollah ,ikiwa ni pamoja na kifo cha kiongozi wao Hassan Nasrallah.

Katika siku hiyo hiyo ambapo makubaliano ya kusitisha mapigano Lebanon ,wapinzani wa Syria wakiongozwa na kundi la kiislamu la Hayat Tahrir al- Sham(HTS) walivamia kwa kushtukizia na kuuteka mji wa Aleppo.

Kisha Hama na siku kadhaa baadaye ,kitongoji kikuu cha Homs kilitekwa. Baadaye Damascus ilitekwa na rais wa Syria amedaiwa kutorokea mjini Moscow.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla