Kwanini kuanguka kwa Rais Assad wa Syria ni pigo kubwa kwa Urusi?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Bashar al Assad wa Syria na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa takriban muongo mmoja ilikuwa ni uwezo wa kijeshi wa Urusi ambao ulimuweka Bashar al-Assad madarakani.

Hadi matukio ya ajabu ya saa 24 zilizopita.

Serikali ya Damascus imeanguka, rais wa Syria amepinduliwa na inasemekana ametorokea nchini Moscow.

Wakinukuu chanzo kimoja huko Kremlin, mashirika ya habari ya Urusi na Televisheni ya serikali iliripoti kwamba Urusi imempa Assad na familia yake hifadhi "kwa misingi ya kibinadamu".

Katika muda wa siku chache, mradi wa Syria wa Kremlin umefumbuliwa katika hali ya kushangaza zaidi, huku Moscow ikishindwa kumtetea .

Katika taarifa yake wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilitangaza kuwa Moscow "inafuatilia matukio makubwa nchini Syria kwa wasiwasi mkubwa."

Kuanguka kwa utawala wa Assad ni pigo kwa heshima ya Urusi.

Kwa kutuma maelfu ya wanajeshi mwaka 2015 kwenda kumsaidia Rais Assad, moja ya malengo makuu ya Urusi ilikuwa ni kujitangaza kuwa nchi yenye nguvu duniani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ilikuwa changamoto kuu ya kwanza ya Vladimir Putin kwa mamlaka na utawala wa Magharibi, mbali na nafasi ya zamani ya Soviet.

Na ilionekana kuwa na mafanikio. Mwaka wa 2017 Rais Putin alitembelea kambi ya wanahewa ya Urusi ya Hmeimim nchini Syria na kutangaza kuwa kazi hiyo imekamilika.

Licha ya ripoti za mara kwa mara kwamba mashambulizi ya anga ya Urusi yalikuwa yakisababisha vifo vya raia, wizara ya ulinzi ya Urusi ilijiamini vya kutosha kupeleka vyombo vya habari vya kimataifa hadi Syria kushuhudia operesheni ya kijeshi ya Urusi.

Katika safari moja kama hiyo nakumbuka afisa mmoja aliniambia kwamba Urusi ilikuwa Syria "kwa muda mrefu".

Lakini hii ilikuwa zaidi ya ufahari tu.

Kwa kurudisha usaidizi wa kijeshi, mamlaka ya Syria iliikodishia Urusi kwa miaka 49 kambi ya anga ya Hmeimim na kambi ya wanamaji huko Tartous.

Urusi ilikuwa imepata eneo muhimukatika Bahari ya Mediterania. Vituo hivyo vikawa vitovu muhimu vya kuhamisha wakandarasi wa kijeshi ndani na nje ya Afrika.

Swali muhimu kwa Moscow: Je, nini kitatokea sasa kwa kambi hizo za Kirusi?

.
Maelezo ya picha, Kambi za Kijeshi za Urusi nchini Syria

Taarifa iliyotangaza kuwasili kwa Assad huko Moscow pia ilitaja kwamba maafisa wa Urusi walikuwa wakiwasiliana na wawakilishi wa "upinzani wa Syria wenye silaha".

Mtangazaji huyo wa televisheni ya taifa alisema viongozi wa upinzani wamehakikisha usalama wa vituo vya kijeshi vya Urusi na balozi za kidiplomasia katika eneo la Syria.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi inasema kuwa kambi hizo nchini Syria zimewekwa "katika hali ya tahadhari", lakini inadai kuwa "hakuna tishio kubwa kwao kwa sasa."

Bashar al-Assad alikuwa mshirika mkuu wa Urusi katika Mashariki ya Kati. Kremlin ilikuwa imewekeza sana kwake. Mamlaka ya Urusi itajitahidi kukubali kupinduliwa kwake lakini kama pigo kubwa kwa upande wa Moscow.

Bado, wanajaribu… na kutafuta visingizio.

Siku ya Jumapili usiku kipindi cha televisheni cha taifa cha Urusi cha kila wiki kililenga jeshi la Syria, kikililaumu kwa kutopigana dhidi ya waasi.

"Kila mtu aliweza kuona kwamba hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya kwa mamlaka ya Syria," mtangazaji Yevgeny Kiselev alisema.

"Lakini huko Aleppo, kwa mfano, maeneo yaliachwa bila vita vyovyote . Maeneo yenye ngome yalisalimishwa moja baada ya jingine na kisha kulipuliwa, licha ya [wanajeshi wa serikali] kuwa na vifaa bora zaidi na kuwazidi washambuliaji mara nyingi. Inashangaza "

Mtangazaji huyo alidai kwamba Urusi "daima ilikuwa na matumaini ya upatanisho [kati ya pande tofauti] nchini Syria."

Kisha hoja yake ya mwisho:

"Bila shaka hatujali kile kinachotokea Syria. Lakini kipaumbele chetu ni usalama wa Russia yenyewe - kile kinachotokea katika ukanda wa Operesheni Maalum ya Kijeshi [vita vya Urusi nchini Ukraine]."

Kuna ujumbe wazi hapa kwa umma wa Urusi.

Licha ya miaka tisa ya Urusi kumwaga rasilimali katika kumweka Bashar al-Assad madarakani, Warusi wanaambiwa wana mambo muhimu zaidi ya kuhangaikia.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla