Ni nini kinachotokea kaskazini magharibi mwa Syria, na kwanini sasa?

Chanzo cha picha, Reuters
Makundi ya upinzani yenye silaha yalianzisha mashambulizi yao makubwa dhidi ya serikali ya Syria miaka kadhaa iliyopita na kuyateka maeneo makubwa kaskazini magharibi mwa Syria, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, baada ya jeshi la Syria kuondoa haraka majeshi yake kutoka eneo hilo.
Makundi hayo yanapigana vita dhidi ya jeshi la Syria karibu na mji wa Hama katikati mwa Syria, huku Urusi, mshirika mkuu wa serikali ya Syria, inafanya mashambulizi ya anga dhidi yao.
Kwa nini kuna vita nchini Syria?
Maandamano ya amani ya kuunga mkono demokrasia dhidi ya rais wa Syria Bashar al-Assad mwaka 2011 yaligeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoiharibu nchi hiyo na kuyahusisha mataifa yenye nguvu ya kikanda na kimataifa.
Zaidi ya watu nusu milioni wameuawa na wengine milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, karibu milioni tano kati yao wakiwa wakimbizi au kutafuta hifadhi nje ya nchi.
Kabla ya mashambulizi ya upinzani, ilionekana kana kwamba vita vilimalizika kwa ufanisi baada ya serikali ya Assad kurejesha udhibiti wa miji kwa msaada wa Urusi, Iran na vikosi vyao vya wakala, hata hivyo, sehemu kubwa ya nchi hiyo bado iko nje ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali.
Sehemu hizi ni pamoja na maeneo ya kaskazini na mashariki yanayodhibitiwa na muungano wa wapiganaji wa Kikurdi unaoungwa mkono na Marekani.
Ngome ya mwisho iliyobaki ya upinzani ni katika mikoa ya kaskazini magharibi ya Aleppo na Idlib, ambayo inapakana na Uturuki na ni makazi ya watu zaidi ya milioni nne, wengi wao wakiwa wameachwa bila makao.
Kundi la wanamgambo wa Kiislamu Hayat Tahrir al-Sham linadhibiti eneo la kaskazini magharibi, na jeshi la Syria linaloungwa mkono na Uturuki pia linashikilia eneo hilo kwa msaada wa vikosi vya Uturuki.
Hayat Tahrir al-Sham ni nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hayat Tahrir al-Sham lilianzishwa mwaka 2012 chini ya jina tofauti, Jabhat al-Nusra, na kutangaza utiifu kwa al-Qaeda mwaka uliofuata.
Jabhat al-Nusra lilichukuliwa kuwa moja ya makundi yenye ufanisi na hatari yanayompinga Rais Assad, lakini badala ya nguvu ya mapinduzi itikadi yake ya jihadi ilionekana kuwa sera yake, na ilionekana wakati huo kama kinyume na muungano mkuu unaojulikana kama Jeshi Huru la Syria.
Mwaka 2016, Jabhat al-Nusra ilivunja uhusiano wake na al-Qaeda na kuchukua jina la Hay'at Tahrir al-Sham wakati lilipoungana na makundi mengine mwaka mmoja baadaye. Hatahivyo, Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza, na nchi nyingine kadhaa bado zinalichukulia kundi la Hay'at Tahrir al-Sham kuwa na uhusiano na al-Qaeda na mara nyingi hulitaja kama Jabhat al-Nusra.
Hayat Tahrir al-Sham limeimarisha nguvu zake katika mikoa ya Idlib na Aleppo kwa kuwasambaratisha wapinzani wake, ikiwa ni pamoja na al-Qaeda na Islamic State, na kuunda serikali ya wokovu ya Syria kusimamia eneo hilo.
Lengo kuu la HTS ni kumpindua Assad na kuanzisha aina ya utawala wa Kiislamu, lakini haijaonyesha ishara ya kujaribu kutawala mgogoro kwa kiwango kikubwa na weka changamoto yake kwa utawala wa Assad hadi sasa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa nini upinzani ulianzisha mashambulizi hayo?
Kwa miaka kadhaa, Idlib imekuwa uwanja wa mapambano, huku vikosi vya serikali ya Syria vimejaribu kurejesha udhibiti.
Lakini mwaka 2020, Uturuki na Urusi zilikubaliana kusitisha mapigano ili kusitisha majaribio ya serikali ya kuukomboa mji wa Idlib, na usitishaji mapigano kwa kiasi kikubwa umeendelea licha ya mapigano ya hapa na pale.
Mnamo Oktoba 2024, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria alisema Hayat Tahrir al-Sham lilifanya mashambulizi makubwa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Syria, Urusi ilianza tena mashambulizi ya anga kwa mara ya kwanza katika miezi kadhaa, na vikosi vinavyoiunga mkono serikali vimeongeza kwa kiasi kikubwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya makombora ya vikosi vya upinzani.
Siku ya Jumatano, Hayat Tahrir al-Sham na makundi washirika walisema walianzisha mashambulizi ya "kuzuia uchokozi," wakiishutumu serikali na vikosi vinavyoungwa mkono na Iran kwa kuongezeka kwa mashambulizi kaskazini magharibi.
Lakini kile kilichotokea kilikuja wakati ambapo serikali ya Syria na washirika wake walipokuwa wakikabiliana na migogoro mingine.
Hezbollah ya Lebanon, ambayo ilikuwa na jukumu muhimu katika kumsaidia Assad kuondokana na upinzani katika miaka ya mapema, hivi karibuni imeteseka kutokana na mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon, huku mashambulizi ya Israeli yakiwaondoa viongozi wa kijeshi wa Iran nchini Syria na ku dhidi ya vuruga usambazaji wa vifaa kwa vikosi vya serikali huko, na Urusi kuzidiwa na vita nchini Ukraine.
Serikali ya Syria na washirika wake walijibu vipi?
Rais Assad ameapa kile alichokitaja kama "kuyaponda" makundi ya upinzani, akiyataja kama "magaidi."
Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran Masoud Pezeshkian siku ya Jumatatu, aliilaumu Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa shambulio hilo, akisema wanajaribu "kuchora ramani" ya eneo hilo.
Pezeshkian alisisitiza kuwa Iran inasimama imara na serikali ya Syria na watu wake, na kwamba kuhifadhi uhuru wa Syria na uadilifu wa eneo ni msingi wa mkakati wake wa kikanda.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Urusi pia inachukulia hali inayoendelea Aleppo kama "shambulio dhidi ya uhuru wa Syria" na kwamba "inaunga mkono mamlaka ya Syria kurejesha hali ya utulivu katika eneo hilo na kurejesha hadhi ya kikatiba haraka iwezekanavyo."

Chanzo cha picha, EPA
Je, mataifa ya magharibi na Uturuki yanasema nini?
Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani - nchi zinazompinga Assad - zilitoa taarifa ya pamoja Jumatatu zikihimiza "kuia kuongezeka kwa mashambulii na kuimarishwa kwa ulinzi wa raia na miundombinu ili kuzuia kutoroka zaidi kwa raia na upatikanaji rahisi wa kibinadamu."
Pia wametoa wito wa "suluhisho la kisiasa linaloongozwa na Syria katika mgogoro" huo kama ilivyoainishwa katika azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2015.
Msemaji wa Baraza la usalama la Taifa la Ikulu ya Marekani (White House )Sean Savitt alisema Jumamosi kwamba kukataa kwa Assad kushiriki katika mchakato wa kisiasa na "kuitegemea kwake Urusi na Iran kunatengeneza mazingira ambayo sasa yanajitokeza."
Pia alisisitiza kuwa "Marekani haina uhusiano wowote na shambulio hili."
"Itakuwa makosa wakati huu kujaribu kuelezea matukio nchini Syria kwa uingiliaji wowote wa kigeni," Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan alisema, akitoa wito kwa serikali ya Syria "kuwapatanisha watu wake na upinzani halali."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












