Kwa nini milima ya Golan, eneo linalokaliwa na Israel ni chanzo kikuu cha mzozo na Syria?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo 1981, Israeli iliamua kwa upande mmoja kunyakua Milima ya Golan.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Shambulio la hivi majuzi la roketi kwenye Majdal Shams, mojawapo ya vijiji vinne katika Milima ya Golan, ambapo watoto 12 waliuawa, linaweka angalizo katika eneo hili ambalo, ingawa dogo, lina umuhimu mkubwa wa kisiasa na kimkakati katika eneo la Mashariki ya Kati.

Milima ya Golan ni uwanda wa miamba unaopatikana kusini-magharibi mwa Syria, takriban kilomita 60 kusini-magharibi mwa Damascus, na unachukua eneo la takriban kilomita 1,000 mraba.

Israel iliiteka Milima ya Golan kutoka Syria katika hatua za mwisho za Vita vya Siku Sita vya 1967.

Wakati wa vita, Waarabu wengi wa Syria walikimbia eneo hilo.

Mstari wa eneo la kutoruhusu silaha ulianzishwa na eneo hilo likawa chini ya udhibiti wa kijeshi wa Israel.

Na mara moja baada ya hatua hiyo Israel ikaanza kuitawala milima ya Golan.

Wakati huo huo, Syria ilijaribu kuteka tena eneo hili wakati wa Vita vya Yom Kippur mwaka 1973 katika shambulio la kushtukiza ambalo, licha ya kuleta hasara kubwa kwa majeshi ya Israel, lilizuiwa.

Nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka mmoja baadaye, ambayo yalilenga zaidi kutangaza eneo lisilotawaliwa na nchi yoyote kati yao lenye kilomita 70 kati ya maeneo yanayodhibitiwa na nchi zote mbili huku askari wa UN wakishika doria kama waangalizi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hatahivyo, nchi zote mbili zilisalia kwenye vita baridi.

Mwezi Desemba 1981, Menachem Begin akiwa Waziri Mkuu, Israeli iliamua kunyakua Milima ya Golan.

Jumuiya ya kimataifa haikuitambua na ikashikilia kuwa Milima ya Golan ambayo ni ardhi ya Syria ilikaliwa kwa mabavu na Israel.

Azimio nambari 497 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza uamuzi wa Israel kuwa "batili na usio na athari za kisheria za kimataifa."

Kwa miongo kadhaa, Marekani na sehemu kubwa ya dunia imepinga hatua ya Israel kuikalia kwa mabavu Milima ya Golan.

Mnamo Machi 2019, Donald Trump alitambua milima hiyo kama ardhi ya Israel.

Inakadiriwa kuna makazi 30 ya Wayahudi katika eneo hili, ni nyumbani kwa watu wapatao 20,000.

Wanaishi pamoja na Wasyria wapatao 20,000, wengi wao wakiwa Waarabu wa Druze, ambao hawakutoroka wakati Milima hiyo ilipotwaliwa.

Makaazi hayo yanachukuliwa kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel inakanusha hilo.

Syria imekuwa ikisisitiza kwamba haitakubali makubaliano ya amani na Israel iwapo haitajiondoa katika milima hiyo.

Kwa nini milima hiyo ni muhimu sana?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ili kuelewa umuhimu wake wa kisiasa na kimkakati, mtu akiwa juu ya milima hiyo yenye urefu wa mita 2,800, anaweza kuona wazi eneo la kusini mwa Syria na mji mkuu, Damascus, yapata kilomita 60 upande wa kaskazini. .

Hali hiyo inalifanya kuwa eneo zuri la kimkakati.

Kutoka milima hiyo, kwa mfano, Syria ilifanikiwa kutumia silaha dhidi ya kaskazini mwa Israeli kutoka 1948 hadi 1967, wakati bado walikuwa wikiidhibiti.

Ramani ya eneo hilo ni faida kubwa kwa Israel, ambayo ina nafasi nzuri ya kufuatilia mienendo ya Syria.

Vilevile milima hiyo ni kizuizi cha asili dhidi ya shambulio lolote la kijeshi la Syria.

Milima ya Golan pia ni chanzo kikuu cha maji kwa eneo hilo ambalo ni kame tangu jadi.

Maji ya mvua yanayoanguka katika bonde la Golan hutiririka hadi kwenye Mto Yordani na eneo hilo ni chanzo cha theluthi moja ya maji ya Israeli.

Imedaiwa kwamba pia ardhi ya eneo hilo ina rutuba na udongo wake wa volkeno unafaa kwa kukuza mizabibu, bustani na kufuga mifugo.

Miongoni mwa mambo mengine, milima hiyo pia ni mahali pekee ambapo Israeli ina hoteli.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sehemu kubwa ya kushikilia

Syria inataka kurejeshwa kwa milima ya Golan kama sehemu ya makubaliano yoyote ya amani.

Mwishoni mwa mwaka 2003, Rais wa Syria Bashar al-Assad alisema yuko tayari kurejesha mazungumzo ya amani na Israel.

Kwa Israeli, kanuni ya kurudisha eneo kwa lengo la kuleta amani tayari imeanzishwa.

Wakati wa mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Marekani mwaka 1999-2000, Waziri Mkuu wa wakati huo nchini Israel Ehud Barak alikuwa amejitolea kurudisha sehemu kubwa ya milima ya Golan nchini Syria.

Syria, kwa upande wake, inataka Israel ijitoe kikamilifu katika mpaka wa kabla ya 1967.

Hilo lingeipa Damaskus udhibiti wa pwani ya mashariki ya Bahari ya Galilaya, chanzo kikuu cha maji safi ya Israeli.

Kwa upande mwingine, Israel inataka kubakia na udhibiti wa Galilaya na inasema mpaka huo uko mita mia chache mashariki mwa pwani.

Kwa kuongezea, makubaliano yoyote na Syria yatahusisha pia kuvunjwa kwa makazi ya Wayahudi katika eneo hilo.

Maoni ya umma nchini Israel kwa ujumla hayajaunga mkono uondoaji huo, ikisema milima ya Golan ni muhimu kimkakati kuweza kurejeshwa.

Mazungumzo ya mara kwa mara

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Syria yalianza tena mwaka 2008, kupitia waamuzi kutoka serikali ya Uturuki, lakini yalisitishwa kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert kutokana na uchunguzi wa ufisadi.

Serikali ya kwanza ya Israel ya Benjamin Netanyahu, iliyochaguliwa Februari 2009, ilionyesha kuwa ilikuwa imedhamiria kuchukua msimamo mkali zaidi kwenye milima ya Golan, na Juni 2009 Syria ilisema hakuna mshirika wa mazungumzo kwa upande wa Israel.

Utawala wa Marekani wa Rais Barack Obama (2009-2017) ulitangaza kuanza tena kwa mazungumzo kati ya Israel na Syria kuwa mojawapo ya malengo yake makuu ya sera za kigeni, lakini ujio wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mwaka 2011 ulikomesha hatua zozote.

Mapigano ya Syria yalifikia mstari wa kusitisha mapigano wa Golan mwaka 2013, lakini serikali iliyofufuka ya Syria ilihisi kuwa salama vya kutosha kufungua tena kivuko chake cha Golan kwa waangalizi wa UN mnamo Oktoba 2018.

Mwaka 2019, chini ya Rais Donald Trump, Marekani ilitambua rasmi uhuru wa Israeli juu ya Milima ya Golan.

Syria imekosoa hatua hiyo na kusema ni "mashambulizi ya wazi dhidi ya mamlaka yake".

Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla