Moja kwa moja, Trump asema Marekani inatafakari uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu Greenland

Rais wa Marekani Donald Trump alisema hatatumia nguvu kuichukua Greenland baada ya kile alichokiita mkutano uliofanikiwa pakubwa na kiongozi wa Jumuiya ya kujihami ya nchi za magaribi NATO.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Mwandishi wa habari wa Ufilipino akutwa na hatia ya kufadhili ugaidi

    Kesi ya mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 26 imeelezewa kama 'dhuluma kubwa' na watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwandishi wa habari kutoka Ufilipino amekutwa na hatia ya kufadhili ugaidi na kuadhibiwa kifungo cha miaka isiyopungua 12 gerezani, jambo ambalo mashirika ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyataja kama “kukiuka haki”.

    Frenchie Mae Cumpio, mwenye umri wa miaka 26, alikamatwa mnamo Februari 2020 baada ya wanajeshi kuchunguza nyumba yake ya kulala usiku na kudaiwa kupatikana handgrenadi, silaha, na bendera ya kikomunisti kitandani mwake.

    Mashirika ya haki za binadamu yalisema kuwa mashtaka hayo yalitengenezwa kwa uongo na Cumpio alitambuliwa kama hasimu wa serikali kwa kazi yake ya uandishi, ambayo ilikosoa polisi na jeshi.

    Waangalizi wanasema kuwa kutajwa huko dhidi ya waandishi wa habari na wanaharakati kuliongezeka chini ya utawala wa Rodrigo Duterte, ambaye aliendesha vita vya kikatili dhidi ya madawa ya kulevya kuanzia 2016 hadi 2022.

    Alhamisi, baada ya miaka sita gerezani bila kesi kuanza, Cumpio alifutiwa mashtaka yanayohusiana na umiliki haramu wa silaha na milipuko, lakini alikutwa na hatia ya kufadhili ugaidi.

    Anakabiliwa na kifungo cha miaka 12 gerezani. Mwenzake waliokuwa wakiishi chimba kimoja, Marielle Domequil, naye alikutwa na hatia na kupewa hukumu sawa na yake.

    "Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo ya hukumu hii, ikizingatiwa kwamba kuna kesi nyingine nyingi, na ningesema, kesi zilizobadilishwa, za kufadhili ugaidi ambazo bado zinaendelea kote nchini," Mwanasheria Josa Deinla, mmoja wa mawakili wa Cumpio, aliiambia BBC.

    Unaweza kusoma;

  2. Mo Salah arejea kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool

    Salah alianza Liverpool kwa mara ya kwanza tangu kushindwa na PSV mnamo Novemba

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Salah aliichezea Liverpool kwa mara ya kwanza tangu waliposhindwa na PSV mwezi Novemba

    Winga matata wa Liverpool Mohamed Salah hatimaye alirejea kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool na akapiga mechi yake ya kwanza tangu alipotoka kuiwakilisha Misri katika michuano ya soka ya bara la Afrika AFCON.

    Mshambuliaji huyo wa Misri alianzishwa kwenye kikosi cha Liverpool kilichoichabanga Olympic Marseille ya Ufaransa mabao matatu kwa nunge katika mechi ya klabu bingwa ulaya iliyosakatwa uga wa ugenini Velodrome.

    Mashabiki wengi duniani hawakuamini macho yao kumshuhudia sogora huyo wa Liverpool uwanjani ikiwa ishara kamili kumalizika mvutano baina yake na kocha Arne Slot na sasa amerudi kuitumikia Liverpool.

    Katika mtanange huo,Salah alipoteza fursa ya kufunga bao katika dakika ya 83 lakini Liverpool ilicheza vizuri na aliisaidia kushinda kiurahisi huku nyota wa mchezo huo akiwa Dominik Szoboszlai.

    Baadhi ya mashabiki na wachambuzi wa soka kutoka England walihofia kuwa safari ya Mo Salah Liverpool ilifikia mwisho mwezi Disemba baada ya mchezaji huyo kuelezea vyombo vya habari kuwa kuna watu Fulani hawakumtaka kwenye timu hiyo na hivyo walimlaumu yeye kwa matokeo mabovu ya timu wakati huo.

    Hata hivyo, kocha Arne Slot alisema kabla ya mechi hiyo ya jana na hata baada, kuwa amemaliza tofauti zake na Salah na amemrejesha kwenye kikosi cha kwanza kwa ajili ya kutafuta matokeo bora.

    Mo Salah aidha upande wake aliomba radhi kwa wachezaji wenzake wa Liverpool uongozi Pamoja na mashabiki nah atua hiyo inaonekana kufuta mzizi wa fitina baina ya Salah na Liverpool.

    Liverpool inacheza mechi ijayo dhidi ya Bournemouth katika mechi ijayo ya Ligi kuu ya Premier nchini England.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Marekani kuwahamisha wafungwa wa Islamic State kutoka Syria hadi Iraq

    Vikosi vya usalama vya serikali ya Syria mbele ya kambi ya al-Hol katika jimbo la Hasakeh

    Chanzo cha picha, EPA

    Jeshi la Marekani limeanza uhamisho wa hadi wafungwa 7,000 wa kundi la Islamic State (IS) kutoka gerezani kaskazini-mashariki mwa Syria kuelekea Iraq, huku serikali mpya ya Syria ikichukua udhibiti wa maeneo ambayo kwa muda mrefu yalidhibitiwa kwa uhuru na vikosi vya Wakurdi.

    Kamandi ya Kati ya Marekani (US Centcom) imesema tayari imehamisha wapiganaji 150 wa IS kutoka mkoa wa Hassakeh kwenda "eneo salama" nchini Iraq.

    Imesema kuwa hatua hii inalenga kuzuia wafungwa kutoroka na kujiunganisha upya.

    Uhamisho huu unafuatia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yameweka sehemu kubwa ya kaskazini-mashariki mwa Syria chini ya udhibiti wa Damascus, baada ya Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria vinavyoongozwa na Wakurdi (SDF) kuondoka katika maeneo muhimu, ikiwa ni pamoja na vituo vya wafungwa vinavyoshikilia maelfu ya washukiwa wa IS na familia zao.

    Kundi la haki za binadamu la Reprieve lilionya kwamba wafungwa waliohamishwa hadi Iraq wanaweza kukabiliwa na mateso na kunyongwa na kuihimiza serikali ya Uingereza kubaini kama raia wowote wa Uingereza walikuwa miongoni mwa wale wanaohamishwa.

    Shirika hilo la hisani lilisema linaamini kwamba hakukuwa na zaidi ya wanaume 10 wa Uingereza walioshikiliwa katika magereza, ingawa idadi kamili haikuwa wazi.

    Takribani raia 55 hadi 60 wa Uingereza, wengi wao wakiwa watoto, bado wamefungwa katika kambi na magereza katika eneo hilo, lilisema.

  4. Shambulio la Israel huko Gaza laua waandishi wa habari watatu, kwa mujibu wa maafisa wa uokoaji

    Mwili wa mmoja wa waandishi wa habari ulibebwa na waombolezaji katika hospitali ya Nasser huko Khan Younis.

    Chanzo cha picha, EPA

    Waandishi wa habari watatu wa Kipalestina wameuawa katika shambulio la Israel katikati mwa Gaza, kwa mujibu wa wahudumu wa uokoaji.

    Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza linaloendeshwa na Hamas lilisema gari lao lilipigwa katika eneo la al-Zahra, na likawataja waliouawa kuwa ni Mohammed Salah Qashta, Anas Ghneim na Abdul Raouf Shaat. Inaelezwa kuwa walikuwa wakifanya kazi kwenye shirika la misaada kutoka Misri.

    Jeshi la Israel lilisema lilishambulia “washukiwa kadhaa waliokuwa wakiendesha droni inayohusishwa na Hamas kwa namna iliyotishia askari wake,” na kuongeza kuwa tukio hilo bado linachunguzwa.

    Watu wengine wanane, wakiwemo watoto wawili, pia waliuawa na mizinga na risasi za Israel katika maeneo mbalimbali ya Gaza siku ya Jumatano, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

    Takribani Wapalestina 466 wameuawa huko Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hamas kuanza tarehe 10 Oktoba, kulingana na wizara ya afya.

    Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake watatu wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha ya Kipalestina katika kipindi hicho hicho.

    Unaweza kusoma;

  5. Nchi saba zaidi zakubali kujiunga na Baraza la Amani la Trump

    Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, alitembelea Ikulu ya White House mwezi Novemba.

    Chanzo cha picha, EPA

    Nchi saba, zikiwemo Saudi Arabia, Uturuki na Misri, zimesema zitajiunga na Baraza la Amani la Rais wa Marekani Donald Trump, kulingana na taarifa ya pamoja.

    Nchi hizo zitajiunga na Israel, ambayo tayari ilithibitisha hadharani ushiriki wake mapema.

    Jioni ya Jumatano, Trump alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin pia amekubali kujiunga, lakini Putin alisema nchi yake bado inachunguza mwaliko huo.

    Hapo awali, ilidhaniwa kuwa baraza hilo lililenga kusaidia kumaliza vita vya miaka miwili kati ya Israel na Hamas huko Gaza pamoja na kusimamia ujenzi upya.

    Hata hivyo, rasimu ya katiba iliyopendekezwa haijalitaja eneo la Palestina, na inaonekana kubuniwa ili kuchukua nafasi ya baadhi ya majukumu ya Umoja wa Mataifa (UN).

    Bado haijabainika ni nchi ngapi zimealikwa kujiunga na chombo kipya cha Trump, Canada na Uingereza ni miongoni mwa nchi zilizoalikwa, lakini bado hazijatoa majibu yao hadharani.

    Hata hivyo, Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Albania, Armenia, Azerbaijan, Belarus, Hungary, Kazakhstan, Morocco na Vietnam tayari zimekubali kujiunga.

    Siku ya Jumatano, Vatican pia ilithibitisha kuwa Papa Leo amepokea mwaliko. Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo, Katibu wa Serikali wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, alisema Papa atahitaji muda wa kutafakari kabla ya kuamua iwapo atashiriki.

    Unaweza kusoma;

  6. Trump asema Marekani inatazama uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu Greenland

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Donald Trump amesema Marekani inachunguza uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu Greenland baada ya mazungumzo na NATO, huku akiondoa mipango ya kuweka ushuru kwa washirika wa Ulaya waliopinga mpango wake wa Marekani wa kumiliki kisiwa hicho.

    Kupitia mitandao ya kijamii, Trump alisema kuwa “mkutano wenye mafanikio makubwa” na kiongozi wa NATO ulisababisha kuwepo kwa “mfumo” wa makubaliano yanayoweza kufikiwa kuhusu Greenland na eneo la Arctic, ingawa hakutoa maelezo mengi.

    NATO nayo ilielezea mkutano huo kuwa “wenye tija kubwa” na kusema kuwa majadiliano kuhusu mfumo huo uliotajwa na Trump yatalenga kuhakikisha usalama wa eneo la Arctic.

    Hapo awali, Trump aliliambia Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) huko Davos kwamba hatatumia nguvu za kijeshi, lakini anataka mazungumzo ili kufanikisha umiliki wa eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo